Ajenda ya CUF kwa Maendeleo ya Zanzibar: Manifesto kwa Uchaguzi Mkuu 2005

Maalim Seif Sharif Hamad

Maalim Seif Sharif Hamad

 

NAFASI PEKEE YA KULETA MABADILIKO YA KWELI

 

Mpendwa Mzanzibari mwenzangu,

 

Jumapili ya Oktoba 30, 2005 tutapiga kura kwa mara nyengine tena kuchagua Serikali itakayotuongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Wengi wenu mtakao kuwa mnapiga kura siku hiyo, hamkuwahi kushuhudia kitu kingine zaidi ya serikali ya CCM. Nyote mmeshuhudia kibri cha utawala ambao umekulia huku ukiamini kuwa kutawala ni haki yao tu na kwamba maslahi ya umma maana yake ni maslahi yao wao. CCM imepoteza uhalali wa kuongoza. Kuichagua CUF ni nafasi pekee ya mabadiliko ya kweli.

 

CCM imajiweka mbali na dhana ya uongozi wa heshima uadilifu na kusahau kwamba uongozi ni dhamana. Kwa miongo na miaka kadhaa sasa imekuwa ikisaliti imani na kudharau heshima iliyopewa na wananchi wa Zanzibar. Wakuu wake sasa hawana tena uwezo wa kuongoza. Kuichagua CUF ni nafasi pekee ya mabadiliko ya kweli.

 

Viongozi wa CCM wametugawa na kutudhoofisha na wameshindwa kutanabahi kuwa jamii iliyoungana huwa na nguvu na huweza kufanya mambo mengi mazuri na makubwa. Wanashindwa kufahamu na kuthamini umoja wa watu wetu hata wakiwa na tofauti ya mawazo. Sasa hawana tena uwezo wa kuongoza. Kuichagua CUF ni nafasi pekee ya mabadiliko ya kweli.

 

CCM imeshindwa kulinda uhuru, haki na usalama wetu. Kwa CCM, utawala wa sheria maana yake ni kuzivunja na kuzitumia vibaya sheria. Kwao wao, maana yake ni kutumia sheria kwa upendeleo na kwa mabavu dhidi ya raia wasio na hatia kwa sababu tu wamethubutu kuhoji utawala wao lakini wanasiasa wala rushwa, wababaishaji, waporaji na wauaji wanaendelea kulindwa na sheria hizo. Viongozi wake wameua uchumi wa nchi yetu kwa kushindwa kupambana na rushwa.hawa hawana tena uwezo wa kuongoza.kuichagua CUF ni nafasi pekee ya Mabadiliko ya kweli.

 

Viongozi wa CCM wametufukarisha na kupoteza maisha watoto wetu wengi kutokana na kushindwa kuwapatia elimu bora na ya maana na huduma za uhakika za afya. Wamesimamia miradi iliyofeli wanayoiita ya maendeleo na kutuletea njaa, ukosefu wa ajira na ongezeko la uhalifu. Kutokana na hali hii, haishangazi kuona Wazanzibari wengi wenye uwezo na vipaji wameikimbia nchi. CCM haina tena uwezo wa kuogoza. Kuichagua CUF ni nafasi pekee ya mabadiliko ya kweli.

 

Mfumo wetu wa kisiasa unahitaji upepo mpya wa mabadiliko wenye nguvu ya kuisafisha jamii yetu na kuleta mawazo na fikra mpya, kuleta Viongozi na watu walioungana na wenye dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko ya maana, na ambao wanathamini utu na heshima ya binaadamu,wanaofahamu maana hasa ya utumishi wa umma na uwajibikaji. Ni CUF pekee inayoweza kuyaleta haya.

 

Mtazamo wetu ni kwamba Wazanzibari tutakuwa na nguvu na sauti licha ya udogo wetu ikiwa tutakuwa na mfumo shirikishi baada ya tenganishi na kwamba tunaweza kuyafikia, kwa umoja wetu, mengi ambayo hatukuweza kuyafikia kwa kugawanyika kwetu. Ni CUF pekee inayoweza kuyaleta haya.

 

Muafaka wetu na mafahamiano yetu juu ya malengo na dhamira zetu ni kuamini kwamba tunaweza kuingiza shauku na hamu mpya katika utungaji wa sera bora zenye nia ya kuleta mabadiliko ya haraka na ya maana yenye tija na neema kwa wananchi wote.Changamoto pekee itakayobaki itakuwa ni kusimamia na kufuatilia utekelezaji wake. Ni CUF pekee inayoweza kuyaleta haya.

 

Nchi yetu ina utajiri mkubwa.Ikiwa tutaziruhusu na kuziachia nguvu, vipaji na taaluma za watu wetu,na kuthamini na kuheshimu utajiri mkubwa wa mchanganyiko wa makabila na asili za watu wetu badala ya kuzitumia kuwagawa watu, basi kuna mambo mengi makubwa tunayoweza kuyafikia na kuushangaza ulimwengu. Ni CUF pekee inayoweza kuyaleta haya.

 

Katika kurasa hizi, tunakuelezeni kwa muhtasari tu baadhi ya yale mambo muhimu yanayowagusa Wazanzibari wenzetu na ambayo tunakusudia kuwatekelezea katika kipindi cha miaka mitano ijayo kupitia ridhaa yenu takayotukabidhi Oktoba 30, 2005. Ni CUF pekee inayoweza kuleta haya.

 

Nayaleta kwenu, kwa niaba ya wenzangu, muyapokee. Hatuwaombi kingine chochote zaidi ya nafasi ya kuwatumikia.

 

Tukiwa tumeungana, tunakupeni Wazanzibari nafasi pekee ya kuleta mabadiliko ya kweli.

 

Seif Sharif Hamad

Kujenga Uongozi Mwema kwa Kuimarisha Misingi ya Uhuru, Haki na Maelewano

 

Leave a comment