Udumavu wa kilimo ni hatari kwa usalama wa nchi

“Katika nchi kama yetu ambayo Watanzania walio wengi bado wanategemea sekta ya kilimo katika kujiendeleza kimaisha, udumavu huu wa ukuwaji na uchangiaji wake katika pato la taifa ni hatari kwa usalama wa nchi. Tukumbuke kuwa, katika dunia yetu hii ya sasa, suala la kilimo na chakula si suala la ustawi wa wananchi kijamii na kiuchumi tu, bali pia ni suala la kiusalama.”

mananasiHotuba ya msemaji mkuu wa Kambi ya Upinzani Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2008/09

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika.

Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama leo hii kwa ajili ya kuwasilisha mawazo ya Kambi ya Upinzani katika Wizara hii ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Mheshimiwa Spika,

Pili kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, napenda kukushukuru wewe binafsi na Naibu wako kwa kunipa fursa ya kuweza kuwasilisha mawazo ya upinzani Kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hii kwa mwaka wa fedha 2008/09 Kwa mujibu wa la kanuni za Bunge, kanuni ya 99(7) toleo la mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika,

Pia napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru viongozi wangu wa Kambi ya Upinzani Mhe. Hamad Rashid Mohamed na Dkt. Wilbord Slaa kwa kunipa ushirikiano mkubwa mwanzo hadi mwisho wa maandalizi ya hotuba hii.

Mheshimiwa Spika,

Nitakuwa mkosefu wa fadhila ikiwa sitowashukuru wanachama wa chama changu cha Wananchi- CUF hasa wa jimbo langu la Chambani ambao kwa msaada wa M/Mungu na kura zao ndio sababu ya mimi kuwepo hapa leo. Nawaahidi nitakuwa nao na nitasimama kidete katika kutetea haki zao. Pia na mwisho lakini si kwa umuhimu namshukuru naibu Waziri Kivuli kwa wizara hii Mhe. Juma Said Omar, mbunge wa Jimbo la Mtambwe kwa ushirikiano mkubwa alionipa katika maandalizi ya hotuba hii.

Mheshimiwa Spika,

Wote tunafahamu kuwa kilimo ndio sekta mama nchini kwani ndiyo sekta inayotegemewa na watanzania zaidi ya asilimia 65% kwa kipato chao na karibu watanzania milioni 40 kwa kuendeleza maisha yao ya kila siku. Sekta hii ni miongoni mwa sekta muhimu zenye kutoa mchango mkubwa katika jitihada za kunyanyua uchumi wa nchi yetu na imeendelea kuwa sekta muhimu inayochangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa. Hivyo kuwa na umuhimu mkubwa katika juhudi zetu za kuondoa umaskini, kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Mheshimiwa Spika,

Licha ya umuhimu wa sekta hii kwa wananchi na taifa kwa ujumla, bado ukuaji wake haufanani na mahitaji yake kwa jamii. Kwa mujibu wa Ripoti ya Umasikini na Maendeleo ya Binadamu nchini ya 2007, takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2000 na 2006 kulikuwa na ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 4.7%. Wakati ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2007 inaonyesha kuwa katika mwaka 2000 sekta ya kilimo kwa maana ya mazao ilikuwa kwa asilimia 4.7%, mwaka 2004 asilimia 6.6% na mwaka 2007 ilikuwa kwa asilimia 4.5%. Hii inaonyesha ukuaji wa sekta hii nyeti umedumaa na pia kushuka kwa kasi kubwa.

Mheshimiwa Spika,

Katika hali ya ongezeko la idadi ya watu la zaidi ya asilimia 3%, ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 4.7% ni hatari kubwa kwa taifa. Ukitilia maanani kuwa sekta hii ni muhimu kama chanzo cha kujitosheleza kwa chakula na wakati huohuo kusaidia ukuaji wa kiuchumi.

Mheshimiwa Spika,

Takwimu za zamani zilionyesha kuwa mwaka 2004 sekta ya kilimo iliweza kuchangia pato la taifa kwa 46.2% wakati mwaka 2005 ilichangia kwa asilimia 46.1%. Hata hivyo kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2007, takwimu zinaonyesha kuwa kwa kutumia kizio cha mwaka 2001, katika mwaka huo huo wa 2004 sekta ya kilimo kwa maana ya mazao imechangia asilimia 22.4% tu na huku mchango wa sekta hii kwa mwaka 2007 ni 19.0% tu.

Mheshimiwa Spika,

Katika nchi kama yetu ambayo Watanzania walio wengi bado wanategemea sekta ya kilimo katika kujiendeleza kimaisha, udumavu huu wa ukuwaji na uchangiaji wake katika pato la taifa ni hatari kwa usalama wa nchi. Tukumbuke kuwa katika dunia yetu hii ya sasa, suala la kilimo na chakula si suala la ustawi wa wananchi kijamii na kiuchumi tu, bali pia ni suala la kiusalama. Vilevile kwa hali kama hii ni wazi Tanzania haitaweza kufanikiwa kufikia malengo ya MKUKUTA ya kuwa na kilimo endelevu kinachokua asilimia 8 – 10 na kuwezesha kufikia ukuaji wa uchumi wa asilimia 6 – 8 ifikapo mwaka 2010.

Mheshimiwa Spika,

Udumavu huu wa ukuaji wa sekta ya kilimo unaonyesha wazi kuwa kamwe serikali ya awamu ya nne ambayo ilingia madarakani kwa Ilani ya uchaguzi iliyowaahidi watanzania kuwa kilimo kitakuwa kwa asilimia 20, haitaweza kufikia lengo hilo ifikapo mwaka 2010. Ni wazi ilani hii ilikuwa ama ya kilaghai ama ya kusadikika kwani wachumi waliobobea wanadai ukuaji wa kasi ya aina hii haujawahi kutokea kwa nchi yeyote duniani.

Mheshimiwa Spika,

Tatizo kubwa linalodumaza kilimo chetu ni pamoja na bajeti ndogo ya Serikali katika kilimo. Leo hii, badala ya kuongeza fedha za bajeti katika wizara ya kilimo, Serikali imepunguza kutoka bajeti ya Tshs.131, 912, 102, 600/= 2007/2008 hadi Tshs.113, 737, 050, 400/= mwaka 2008/09.

Mheshimiwa Spika,

Japokuwa Serikali imetoa sababu za upungufu huo, lakini Kambi ya Upinzani haikubaliani na sababu hizo kwa msingi kuwa, bajeti ya umwagiliaji maji iliyopelekwa kwenye wizara ya maji na umwagiliaji kwa mwaka 2008/09 ni Shilingi 13,185,574,000/, Fedha hizi zikijumlishwa na za bajeti ya wizara ya kilimo ya mwaka huu zinakuwa Shilingi 126,922,624,400/-. Hata hivyo bado bajeti ya mwaka huu ni pungufu kwa Shilingi 4,989,478,200/- sawa na 3.78% kulinganisha na bajeti ya wizara ya kilimo kwa mwaka 2007/08.

Mheshimiwa Spika,

Inasikitisha kuwa wakati duniani kote wenzetu wanajipanga kupambana na tishio la upungufu wa chakula, sisi ndio kwanza tunapunguza bajeti ya wizara ya kilimo. Hii sio tu inatuingiza katika hatari ya janga kubwa la njaa lakini pia inatulazimu kuendelea na tabia ya kuombaomba chakula ambacho tulipaswa kukizalisha sisi wenyewe.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani kwa kuona umuhimu wa sekta hii katika kuongeza ajira, pato la taifa na kuweza kuyalinda maisha ya watu ambayo yanaweza kupotea wakati wowote kutokana na uhaba wa chakula, tulipendekeza kiasi cha Tsh. Bilioni 959.2 ikiwa ni mara saba na nusu (7.5) ya bajeti ya Wizara ya kilimo ya Serikali kwa mwaka huu wa 2008/09.

Mheshimiwa Spika,

Sambamba na hilo, katika Ilani ya CCM Ibara ya 31(l) inatamka bayana kuwa, nanukuu, “CCM inazitaka Serikali kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo inatengewa si chini ya asilimia 10 ya uwekezaji unaofanywa na Serikali, sambamba na lengo la Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).” Kambi ya Upinzani inajiuliza hivi Serikali hii inafuata na kutekeleza sera na ilani za nani? Serikali hii ya CCM haijui kuwa ilani ya uchaguzi ni ahadi takatifu kwa wananchi na ni lazima kuheshimiwa?

Mheshimiwa Spika,

Kilimo cha Watanzania kinafanywa na wakulima wadogo wadogo ambao mashamba yao ni madogo sana kati ya hekta 0.5 na 2.5 lakini hadi sasa suala la kuwasaidia kikamilifu wakulima hawa limekuwa ni la hadithi za alfu lela ulela. Inashangaza kuwa serikali ya nchi iliyomasikinishwa kama Tanzania, inadharau udogo wa mashamba ya watanzania, wakati inajulikana wazi kuwa suala si udogo au ukubwa wa eneo la kulima, bali ni tija inayopatikana kwa maeneo hayo (production per area or productivity).

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inatambua na kuthamini mchango wa wakulima wadogowadogo kuwa ndio injini ya kilimo hapa nchini na ndio wanaolisha watanzania takriban milioni 40.

Mheshimiwa Spika,

Katika nchi za mashariki ya mbali, mfano; China, Taiwan, Vietnam na nyingize, wakulima wadogo wadogo wenye wastani wa mashamba chini ya hekta moja ndio wazalishaji na wasafirishaji wa chakula cha nafaka inayotumika duniani kote. Wakulima hawa wamejengewa mazingira mazuri na serikali zao kwa kuweza kupata mbolea, utaalamu wa kilimo, mbegu bora, miundombinu ya umwagiliaji maji na barabara bora za vijijini zinazosaidia kufikia masoko.

Mheshimiwa Spika,

Serikali inapaswa kutambua kuwa ukuwaji wa haraka wa idadi ya watu unaweza kuchochea uzalishaji kwa kutanua soko kwa ajili ya bidhaa na huduma, kutengeneza nafasi za uwekezaji wa uzalishaji na pia inachochea uwekaji wa akiba.

Mheshimiwa Spika,

Na sisi Watanzania tukiwa makini katika mipango yetu, inawezekana siku moja tukafika huko.

Mheshimiwa Spika,

Sekta ya kilimo ni moja ya sekta yenye miradi mingi sana ambayo inatokana ama kwa ufadhili ama mikopo kutoka kwa mataifa na asasi mbalimbali duniani. Hata hivyo, kama ilivyo katika miradi mingi ya nchi hii, suala la ushiriki ama ushirikishwaji wa wanajamii katika kupanga, kutekeleza na kusimamia miradi hii halijatiliwa mkazo ipasavyo.

Mheshimiwa Spika,

Wakati serikali inapenda kudai kuwa inajenga utamaduni wa kuwashirikisha wananchi katika miradi kadhaa inayotekelezwa hivi sasa chini ya wizara ya kilimo kama vile mradi wa ASDP kwa njia ya ‘D By D’ (DECENTRALIZATION BY DEVOLUTION). Tafiti mbalimbali za asasi za kiraia zinaonyesha kuwa utaratibu huu umeelelezwa hadi ngazi ya Halmashauri za wilaya tu. Hauzavuka kwenda katika ngazi ya kata, vijiji, vitongoji hadi kwenye mitaa.

Matokeo yake hali hii inatengeneza mazingira ya ufisadi miongoni mwa watendaji wanaokabidhiwa majukumu ya uratibu na usimamizi na vilevile kukosekana kwa mwamko wa kutosha miongoni kwa upande wa walengwa ili kujihusisha vyema katika miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika,

Katika nchi ya Malawi, kwa mfano, wameweza kupata mafanikio makubwa ya kilimo yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikishwaji wa moja kwa moja wa jamii. Ni muhimu kwa Wizara kufahamu na kuheshimu falsafa ya kuwa hakuna maendeleo bila ya jamii kupewa kipaumbele (Community Base).

MFUKO WA PEMBEJEO (Agricultural Inputs Trust Fund -AGITF)

Mheshimiwa Spika,

Mfuko huu wa pembejeo ulianzishwa rasmi kwa sheria ya Bunge mwaka 1994 na kuanza kazi rasmi mwaka 1995 ukiwa na jukumu kuagiza na kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakulima. Sambamba na hilo, mfuko unajishughulisha na kutoa mikopo ya kusambaza pembejeo kupitia kwa mawakala wa pembejeo, wakulima binafsi, vyama vya wakulima na kuanzisha vituo vya kukodisha matrekta.

Mheshimiwa Spika,

Toka kuanzishwa kwake mwaka 1995 hadi mwaka jana (2007), taarifa zinaonyesha kuwa Mfuko wa Pembejeo ulikuwa umetoa mikopo ya jumla shilingi billioni 18.5 na kukusanya asilimia 46 ya fedha hizo, ambazo ni sawa na shillingi bilioni 8.5 tu.

Mheshimiwa Spika,

Utekelezaji wa shughuli za mfuko huu umekumbwa na majanga mbalimbali ya uzembe na ufisadi. Moja ya janga lililoukumba mfuko huu ni lile la kufaidisha watu wasio walengwa ambao kunatetezi kuwa wengi wao ni watu wenye nafasi kubwa katika chama na Serikali. Taarifa zinaonyeshaa kuwa wengi wao waliweka dhamana hewa ya mikopo hiyo na kuilaghai serikali.

Mheshimiwa Spika,

Janga lingine ni lile la mfuko huu kutowasaidia sana wakulima wadogo wadogo walio wengi na wenye uhitaji mkubwa wa mbolea za ruzuku. Kwa kiasi kikubwa wakulima waliofaidika na mfuko huu ni wale wakubwa wakubwa na mawakala wa kilimo (rural agro dealers/stockist) wakiwaacha wakulima walio wengi kununua pemebejeo hizo za ruzuku kwa bei ya soko au zaidi ya hapo.

Kambi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri kulieleza bunge lako Tukufu:

  • Ni hatua gani zimechukuliwa kwa wakopaji ambao hadi sasa wanadaiwa kiasi cha Shilingi billioni 10?
  • Ni hatua zipi zimechukuliwa kwa wale waliotumia vifaa hivi kwa udanganyifu na wala trekta hazikununuliwa na au hazikukarabatiwa.

Kambi ya Upinzani inataka taarifa ya kina itolewe katika Bunge lako tukufu ili waheshimiwa wabunge katika majimbo yao waweze kuthibitisha kama kweli matrekta hayo yapo.

Mheshimiwa Spika,

Kila mwaka Serikali hutenga kasma kwa ajili ya mfuko wa pembejeo ili kutoa mikopo ya kununulia na kusambaza pembejeo na zana za kilimo. Pamoja na kwamba Serikali imejitoa katika kuhudumia mfuko wa pembejeo mwaka huu na kuiachia sekta binafsi lakini imetenga shilingi billioni 7.16 kwa bajeti hii ya 2008/09. Kati ya fedha hizo shilingi billioni 5 ni zile zinazotegemewa kurejeshwa toka kwa waliokopeshwa miaka ya nyuma.

Mheshimiwa Spika,

Hili ni jambo la kubahatisha kwani wadeni hao wanaweza kushindwa kulipa madeni yao kama ambavyo imejitokeza katika miaka iliyopita. Ikiwa hilo litajitokeza tena basi mfuko huo hautokuwepo. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza itatumia kasma gani kufidia fedha za mfuko wa pembejeo kwani dhana ya wakopaji wengi hapa nchini ni kuwa fedha za Serikali ni fedha za bure. Kama wanavyoamini katika fedha za mfuko wa JK.

Mheshimiwa Spika,

Matumizi ya mawakala wa kilimo (rural agro-dealers) ambao wengi inasemekana wengi wao ni watu wenye maslahi serikalini na pia katika sekta ya kilimo imesababisha tatizo kubwa la ulanguzi wa mbolea ya ruzuku na kuifanya kuuzwa kwa bei kubwa sana. Taarifa zinaonyesha kuwa katika mkoa wa Iringa, kwa mfano, mbolea ya ruzuku inauzwa kati ya Tsh 70,000/= hadi 90,000/= kwa mfuko wa Kilo hamsini (50) badala ya bei halali ya serikali ya shilingi 23,000/=. Kambi ya Upinzani inaitaka Waziri atueleze ni kwanini Serikali inashindwa kuthibiti bei ya mbolea ya Ruzuku na kuwafanya wakulima washindwe kuinunua.

KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Mheshimiwa Spika,

Nchi yetu imebahatika kuwa na eneo kubwa na la kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji la zaidi ya hekta milioni 29.4, kati ya hizo hekta milioni 2.3 zinauwezo mkubwa wa kuendelezwa na hekta milioni 4.8 zinauwezo wa wastani na hekta milioni 22.3 zina uwezo mdogo wa kuendelezwa. Hadi sasa eneo lililoendelezwa kwa umwagiliaji ni hekta milioni 0.29 tu.

Mheshimiwa Spika,

Tanzania haina uhaba wa maji. Kati ya eneo lote la Tanzania lenye ukubwa wa hekta millioni 94.5, hekta milioni 5.5 zimefunikwa na maji ya mito na maziwa. Tanzania ina ziwa la pili kwa ukubwa duniani la Victoria, ziwa lenye kina kirefu kuliko yote duniani la Tanganyika na vilevile mito mikubwa kama Malagalasi, Rufiji, Ruvu, Kilombero, Kagera, Ruvuma, Pangani, Wami n.k inayofaa kabisa kwa kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika,

Tunapenda kumkumbusha mheshimiwa Waziri kuwa alitoa ahadi hapa Bungeni katika bajeti ya mwaka 2006/07 kuendeleza hekta milioni 1 kwa kipindi cha miaka mitano (2006/07- 2009/2010). Lakini kwa masikitiko makubwa mpaka sasa eneo la umwagiliaji ni hekta 275,388 tu, ambalo ni kiasi cha asilimia 27.5 tu ya lengo hilo na imebakia miaka miwili tu kufikia 2010. Je itawezekana?

Mheshimiwa Spika,

Mkoa wa Morogoro peke yake una mito ipatayo 176 isiyokauka mwaka mzima, kama vile Mto kilombero, Ruaha kuu, Kihansi, Mpanga, Mgeta, n.k Mkoa wa Mbeya umebahatika pia kuwa na jumla ya hekta 82,000 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini cha kushangaza ni kwamba kiasi cha hekta 17,000 tu ambazo ni sawa na asilimia 20.7 ndizo zinazotumika kwa kilimo hicho. Vile vile jumla ya eneo lote la mkoa huu linaloweza kutumika kwa kilimo ni hekta milioni 5.7 lakini eneo linalolimwa ni hekta 712,558 tu ambalo ni sawa na asilimia 12.5. Hii yote inatokea wakati Mikoa hii yenye vyanzo vingi vya maji vinavyoweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji havitumiki. Zaidi ya yote hayo, mikoa hii miwili iliyobarikiwa na rasimali zote hizo, ni miongoni mwa mikoa iliyokuwemo katika orodha ya mikoa iliokumbwa na njaa katika mwaka 2007/08. Kambi ya Upinzani inaiuliza Serikali kuwa itawezaje kuleta mapinduzi ya kijani ikiwa kilimo cha umwagiliaji hakipewi nafasi inayostahili?

Mheshimiwa Spika,

Katika Mpango Shirikishi wa Kilimo cha Umwagiliaji (PIDP), serikali ilishauriwa na kukubali ushauri wa kuvuna maji ya mvua katika mikoa yenye matatizo ya ukame ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza na Arusha. Hadi sasa bado utekelezaji wake haujaonekana na maji ya mvua yanaendelea kuachwa yapotee baharini.

BENKI YA KILIMO

Mheshimiwa Spika,

Jambo ambalo ni muhimu sana kwa ukuwaji wa sekta hii ni upatikanaji wa Benki ya kilimo. Katika bajeti iliyopita ya wizara hii Serikali iliahidi kubadilisha benki ya Rasilimali (TIB) kuwa Benki ya Kilimo. Lakini hadi sasa maamuzi hayo bado hayajatekelezwa kwa madai kuwa serikali haina mtaji wa kuanzisha benki hiyo.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inapingana kabisa na dhana ya kubadilisha TIB kuwa benki ya kilimo na pia sababu ya kwamba Serikali haina fedha za mtaji wa kuanzisha benki ya Kilimo. Tunaamini kuwa endapo serikali ingetumia fedha ilizotoa kwa Benki ya Exim na CRDB kwa ajili ya kuwakopesha wakulima kama mtaji wa kuanzisha benki ya kilimo ingewezekana, badala ya kuendelea kuzinufaisha benki hizo kibiashara ambazo ki-ukweli zinaendelea kukwepa jukumu la kuwasaidia wakulima wadogo.

Pia tunashauri serikali kutumia kiasi fulani cha ushuru wa mazao mbali mbali kama vile Pamba, Kahawa, Korosho, Miwa n.k. kuwa kama nyongeza ya mtaji kwa ajili ya uanzishwaji wa Benki ya Kilimo. Vilevile serikali ingetumia kiasi cha shilingi bilioni 2.8 ilizozitoa mnamo July 2003 kukopesha wakulima binafsi na kupitia vyama vya msingi ushirika pamoja na SACCOS kuanzisha benki hiyo.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inaamini ili kupiga hatua ya maendeleo ya kweli tunahitaji kufanya maamuzi magumu na kama kweli serikali iko makini na tayari kuachana na utamaduni wa maneno tu, Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi bora katika kilimo.

KILIMO CHA MAZAO MBALI MBALI

Mheshimiwa Spika,

Katika hotuba ya Mhe.Waziri wa Kilimo ya mwaka 2007/2008 alisema kuwa, nanukuu “hakuna njia ya mkato ya kuinua kipato cha wananchi walio wengi na kufikia azma ya maisha bora kwa kila Mtanzania bila ya kuleta mapinduzi katika kilimo.” Suala la mapinduzi ya kilimo limekuwa kama kauli mbiu ya kudumu kwa serikali tangu enzi za TANU hadi sasa. Lakini suala hili limebaki kuwa nadharia ya kuwapa Watanzania matumaini yanayoendelea kupotea bila ya utekelezaji wake kuonekana. Maana ya mapinduzi ni mabadiliko ya haraka yenye kuonyesha mafanikio yake kwa muda mfupi. Sasa sijui ndugu zetu hawa wanaongelea mapinduzi gani yasioyonekana hata baada ya miaka 46 ya Uhuru na miaka 44 ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Tumekuwa na uzalishaji usioridhisha kwa mazao ya kilimo mwaka hadi mwaka. Mfano, kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika Mwaka 2007, uzalishaji wa wa mazao mengi makuu umeshuka kwa kiasi kikubwa.

Zao

2006

2007

Badiliko la asilimia

Sukari kwa (tani)

290,863,000

279,494,000

-4%

Kahawa (tani)

45,534,000

33,708,000

-25.08%

Pareto (tani)

2,046,000

1,000,000

-51.6%

Mahindi (tani)

3,423,000

3,302,000

-3.53%

Ngano (tani)

109,500

83,000

-24.2%

Muhogo (tani)

2,049,800

1,733,000

-15.57%

Ndizi (tani)

1,169,200

1,027,000

-12.16%

Mheshimiwa Spika,

pamoja na kushuka huko kwa uzalishaji kwa zao moja moja, lakini kuna tatizo la msingi la kushuka kwa uzalishaji kwa mikoa ya nyanda za juu kusini. Kwani basi Serikiali haitumii ipasavyo vyuo vyetu vya tafiti kama vile Mlingano Tanga, Serian Arusha na SUA Morogoro kubaini aina na ukubwa wa tatizo kwa maeneo husika ili kuwanusuru wakulima na hasara wanayoipata mwaka hadi mwaka.

Mheshimiwa Spika,

Kama ambavyo tumesema kuwa uzalishaji ni ule wenye tija, na tija inatokana na huduma makini na sahihi ya utaalam wa kilimo. Katika kijitabu cha mwelekeo wa utekezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha mwaka 2005-2010 kinasema uzalishaji wa pamba utapanda toka kg.100 kwa ha. hadi kg.1000 kwa ha.

Mheshimiwa Spika,

kwa sasa mikoa inayolima pamba inazalisha kg 250 kwa ha., huu ni uzalishaji mdogo sana kwa kulinganisha na lengo la ilani ya CCM. Lakini licha uzalishaji huu mdogo bado wakulima hivi sasa wanakosa soko na bei ya uhakika. Kambi ya Upinzani inataka Serikali ilieleze Bunge lako tukufu, ikiwa kwa uzalishaji huu mdogo pamba haina soko wala bei nzuri, je hali itakuwaje pale uzalishaji utakapofikia kilo 1000 kwa hekta?

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inashauri serikali kuacha mtindo wa kutenganisha mazao ya biashara na chakula kama ilivyoainishwa katika Sera ya Kilimo ya 1997. Tafiti zinaonyesha kuwa jambo hili ndilo linalowazidishia wakulima wetu kuzama kwenye lindi la umaskini. Kambi ya upinzani inaamini kuwa kila zao ambalo linaweza kuingizwa sokoni na kuuzwa ni zao la biashara, nalinapaswa kupewa umuhimu ulio sawa na mazao mengine.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya upinzani inakemea vikali tabia ya viongozi wa serikali kuingilia uhuru wa wakulima kuuza mazao yao yaitwayo ya chakula. Hili linapelekea wakulima hao kuuza mazao yao kwa bei ya chini ambayo inawaletea umasikini badala ya kuwakomboa kiuchumi. Tunaitaka serikali iache mara moja mtindo huu wa kuwapangia wakulima jinsi ya kuuza mazao yao vinginevyo iwe tayari kuwalipa fidia kwa kiasi kile wanachoingia hasara kutokana na utekelezaji maamuzi hayo ya kisiasa.

ONGEZEKO LA BEI YA VYAKULA DUNIANI

Mheshimiwa Spika,

Kwa kutambua upungufu na kuongezeka kwa bei ya wa chakula Duniani, Serikali inadai inaandaa mikakati ya kuongeza uzalishaji wa chakula. Mikakati hiyo ni ya muda mfupi na muda mrefu. Mfano, mikakati ya muda mfupi:

  • Kusitisha uuzaji wa mazao makuu ya chakula nje ya nchi.
  • Kutoa msamaha wa kodi wa uingizaji mahindi kutoka nje ya nchi (tax waiver)
  • Kuhamasisha na kuhimiza matumizi mazuri ya chakula katika ngazi zote.

Mheshimiwa Spika,

Ni wazi kuwa mikakati ya aina hii haikufanyiwa utafiti wa kutosha na kamwe haitoweza kuongeza uzalishaji wa chakula nchini. Inashangaza kuwa wakati wenzetu wanajipanga kutumia vyema rasilimali walizonazo kuzalisha chakula sisi tunajipanga kusamehe kodi za uagizaji wa mazao toka nje, na kumzuia mkulima asiuze mazao yake nje kwa faida. Kinachotakiwa ni Serikali kujipanga Kimkoa na kiwilaya kuzalisha chakula kwa wingi na kuwapunguzia wakulima mzigo wa kodi unaowaelemea wakulima wetu ambao wanalipa mara 17 (5% Vs 0.3%) zaidi ya kodi anayolipa mwenye kiwanda.

UWEKEZAJI KATIKA KILIMO

Mheshimiwa Spika,

Taarifa zinaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko la wawekezaji binafsi katika sekta ya kilimo kutoka 77 mwaka 2001 hadi 219 mwaka 2007, sawa na ongezeko la wastani la asilimia 7.9%. Kwa mwaka 2007 kilimo kilikuwa na miradi 27 yenye thamani ya dola za kimarekani 142.45million.

Mheshimiwa Spika,

Hadi sasa Tanzania haina sera ya makini zenye vishawishi vya kuwavutia wawekezaji wakubwa kwenye kilimo, wala aina Sera makini za matumizi bora ya ardhi. Huu ni udhaifu mkubwa kwa Serikali. Serikali inaandaa Sera wakati huu ambapo wawekezaji tayari wanaendela kuhodhi maeneo yenye rutuba kwa kilimo cha mazao ya chakula ili wazalishe mazao ya nishati mbadala.

Mheshimiwa Spika,

Katika suala la wawekezaji Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ihakikishe kunakuwepo na uhusiano wa moja kwa moja kati ya viwanda na kilimo (foward and backward linkage). Ili wawekezaji wakubwa waweze kuvipatia viwanda vyetu vya ndani malighafi ili pasiwepo na haja kwa viwanda hivyo kuagiza malighafi toka nje ya nchi. Bidhaa za viwanda hivyo zitosheleze soko la ndani kwanza na ziada iuzwe nje.

PROGRAMU YA KUENDELEZA SEKTA YA KILIMO (ASDP)

Mheshimiwa Spika,

Mpango huu wa ASDP ambao unapaswa kutekelezwa kwa miaka saba kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2014 kwa kutumia jumla ya shilingi trilioni 2.5, una fedha nyingi sana ambazo kama tungelikuwa makini zingeliweza kabisa kuinua sekta ya kilimo kwa kiasi kikubwa kabisa.

Mheshimiwa Spika,

Taarifa ya wizara inaonyesha kuwa kazi zitakazofanyika chini ya programu hii katika mwaka huu wa fedha ni pamoja na kuimarisha timu za wawezeshaji katika ngazi ya taifa, wilaya hadi kata, kuendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa DADPS katika ngazi za wilaya na vijiji, kuboresha utangazaji na uenezi wa matokeo ya kazi na ASDP na kuendelea kujenga uwezo wa watendaji katika ngazi zote.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inajiuliza kama kweli Serikali iko makini na kilimo badala ya kutumia programu hii kwa kuingiza nchini matrekta ya kutosha, mbolea na madawa, kuwapa maofisa ugani wachache tulionao vitendea kazi na motisha mbali mbali, tunatumia fedha nyingi za programu kwa watendaji katika semina, makongamano na warsha mambo ambayo hayaongezi tija ya moja kwa moja katika uzalishaji kwa mkulima. Kambi ya Upinzani inahoji pia ni kwa nini kiasi fulani cha fedha hizi kisitumike katika uanzishwaji wa benki ya kilimo.

USHIRIKA

Mheshimiwa Spika,

Tanzania ilikuwa ni nchi ya mfano katika vyama vya ushirika. Wasomi wengi wamesomeshwa na vyama vya ushirika vya mikoa yao. Swali la kujiuliza kwa kiwango hicho kilichofikiwa ni kwanini ushirika ulikufa?

Mheshimiwa Spika,

Ushirika wa wakati huo haukuwa ni wa kununua mazao tu kama ilivyo hivi sasa, bali ulikuwa ni wa kumsaidia mkulima katika hatua zote za kuzalisha hadi kumtafutia soko kwa bei stahili.

Mheshimiwa Spika,

Ushirika uliopo sasa ni wa kibiashara mno badala ya kutoa huduma kwa mkulima, kwa sababu SACCOS ndizo zinazochukua nafasi ya vyama vya ushirika. SACCOS zimeanzishwa kwa misingi isiyo thabiti yenye utashi wa kutengeneza faida zaidi kuliko kutoa huduma, SACCOS zina mapungufu makubwa ya uongozi na utaalam katika kuziendesha. Misingi ya ushirika sio mikopo kama zinavyofanya SACCOS za leo kwa kuziendea taasisi kama PRIDE,SELF,na BENKI bali msingi mkuu wa ushirika ni michango ya wanachama wake. Kambi Upinzani inaona kwa kuwa SACCOS msingi wao ni mikopo na kupata faida, mwisho wake utakuwa ni kuiingiza Serikali kwenye mtego wa kulipa madeni, kwani SACCOS hizo zitakufa kifo cha mende kutokana na kukosa misingi imara.

Mheshimiwa Spika,

Maafisa ushirika wilayani ndio wasimamizi waelekezi wa SACCOS, lakini nao wanakumbwa na matatizo makubwa ya kutokuwa na fani ya ushirika pamoja na vitendea kazi.

Jambo la kusikitisha ni kuwa hata vile vyama vya ushirika vilivyobaki kwa kusuasua bado vinakabiliwa na matatizo makubwa ya uongozi na ubadhirifu wa mali za ushirika.

COASCO

Mheshimiwa Spika,

Bunge lako tukufu lilipitisha sheria ya kuundwa kwa chombo ambacho kitakuwa na mamlaka ya kukagua mahesabu ya vyama vya ushirika nacho ni COASCO. Jambo la kusikitisha ni kuwa vyama vingi vya ushirika havijakaguliwa kwa muda mrefu na COASCO ipo. Jambo la ajabu zaidi ni kuwa vyama vya ushirika vinapeleka vitabu vyao vya mahesabu COASCO badala ya COASCO kwenda vilipo vyama vya ushirika na kuona hali halisi na ikibidi kukutana na wanaushirika. Kambi ya Upinzani inauliza kwa utaratibu huu ni kweli tutaweza kushinda ubadhirifu ndani ya vyama vya ushirika?

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inaitahadharisha Serikali kutorudia makosa yaliyosababisha vyama imara vya ushirika kufa kwa kuchanganya siasa na ushirika. Hivyo basi, ushirika uongozwe na katiba zilizounda ushirika huo na ziwe huru katika utekelezaji wa majukumu yao.

  • Mabadiliko ya mara kwa mara ya Muundo wa Wizara

Mheshimiwa Spika,

Mabadiliko ya mara kwa mara ya muundo wa wizara inayohusika na kilimo chakula na ushirika yamekuwa yakileta mkangayiko mkubwa wa kiutekelezaji na kifedha kwa watendaji wa sekta hii.

Mkanganyiko huu wa mara kwa mara kwa sekta nyeti kama hii unatoa taswira mbaya. Serikali inashindwa kufanya maamuzi ya kitaalamu kama vile muundo wa serikali bila ya kutumia na kuthamini ushauri wa wataalamu wetu. Hali ambayo inapelekea kulingiza taifa letu katika matumizi ya ziada ya kodi za watanzania pasipo na ulazima na kusababisha mkanganyiko mkubwa wa kisera na kiutekelezaji miongoni mwa watendaji wetu, kiasi cha kuathiri utekelezaji wa mipango mingi ya kuendeleza sekta ya kilimo.

  • Mamlaka ya Maendeleo ya Kilimo Nchini

Mheshimiwa Spika,

Kutokana na ukubwa wa nchi yetu na wingi wa asasi na miradi iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, tunashauri serikali ichukue hatua za haraka za kuanzisha Mamlaka ya Maendeleo ya Kilimo Nchini (National Agriculture Development Authority-NADO) ambayo itakuwa na majukumu ya kusimamia bodi zote za mazao mbalimbali, miradi yote ya kilimo na kuhakikisha utekelezaji wa mikakati na mipango yote ya kilimo nchini. Mamlaka hii ambayo inapaswa kuwa chini ya wizara husika itakuwa ndio kiungo muhimu cha usimamizi wa utekelezaji wa mikakati, mipango na miradi yote ya kilimo nchini inayotekelezwa na ama ndani ya wizara husika ama asasi na bodi mbalimbali za mazao ya kilimo nchini.

Ni muhimu sana kuanzisha mamlaka hii ili kuhakikisha nafasi ya wataalamu wetu katika kuendeleza sekta hii nyeti na vilevile kupunguza mzigo mzito wa majukumu uliopo katika wizara. Tukifanya hivi ni wazi tutakuwa tunatengeneza mazingira bora ya kuendesha kilimo chetu kitaalamu zaidi na kupunguza athari za maamuzi ya kisiasa yanayoendelea kuidumaza sekta hii siku hadi siku.

  • Sheria ya Kilimo

Mheshimiwa Spika,

Vilevile, Kambi ya Upinzani inaamini wakati umefika wa kuwa na sheria maalumu ya kilimo nchini ambayo itaweka wazi haki na wajibu wa wakulima kwa upande mmoja na serikali na asasi zingine kwa upande mwengine kama ilivyo katika sheria ya madini. Ni muhimu kuwa na sheria hii ya kilimo ambayo itaonyesha wazi masuala ya kodi za shughuli za kilimo, masuala ya umiliki na mamlaka ya maamuzi ya uuzaji na matumizi ya mazao ya kilimo.

Na vilvile kuonyesha wazi ni vipi serikali inapaswa kuwezesha sekta hii kama ambavyo inafanya katika sekta za madini na ujasiriamali.

Mheshimiwa Spika,

Uwepo wa sheria ya kilimo utawezesha kuondoa matatizo mbalimbali yanayowakumba wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla. Vilevile sheria hii itaweza kubainisha nafasi ya mazao ya kilimo haswa yale ya chakula katika muktadha mzima wa maendeleo na usalama wa Taifa letu. Ni muhimu sana kuanzisha sheria hii ambayo itaondoa ukiritimba wa maamuzi na kuweka bayana mipaka ya mamlaka mbalimbali zinazohusika katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kilimo. Sheria hii inapaswa kuweka wazi ushiriki wa wizara mtambuka katika sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

…………………………………

Salim Hemed Khamis (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI-WIZARA YA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA

22.07.2008

Advertisements

One thought on “Udumavu wa kilimo ni hatari kwa usalama wa nchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s