CUF yataka Muungano ujadiliwe upya

Maalim Seif Shairf Hamad, Katibu Mkuu wa CUF

Maalim Seif Shairf Hamad, Katibu Mkuu wa CUF

  • Yasema mazingira yanalazimisha hivyo
  • Usiri wa muda mrefu umeongeza matatizo
  • Yaonya vitisho dhidi ya Wazanzibari havitafaulu

Na Ripota Wetu, Mauwa Mohammed, Zanzibar

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema Wazanzibari wanataka suala la Muungano wa Zanzibar na Tanganyika lijadiliwe upya kwa kuwa mkataba wake umegubikwa na mambo mengi yasiyokubaliwa na wananchi wengi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama chake uliofanyika Chaani, Kaskazini A, Unguja mwishoni mwa wiki. Maalim Seif alisema kwamba Wazanzibari hawaridhiki na muundo wa sasa wa Muungano na wala hawautaki muundo huu na ndio maana kumekua na mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi juu ya suala hilo.

“Wazanzibari wanapojadili na kusema Muungano ulivyo sasa hawataki, haina maana kwamba hatutaki Muungano, lakini kuna mambo yanayohitaji makubaliano yenye manufaa kwa pande zote.” Alisema Muungano unaohitajika sasa ni ule wa makubaliano na ridhaa za pande zote kwa kuainishwa  rasmi  maeneo na masuala yaliyo ya Muungano na yale yasiyokuwa.

“Tukifanya hivyo, lazima  tutakubaliana, ni mambo gani, sura gani na mamlaka gani kwa upande wa Tanganyika na kwa upande wa Zanzibar ni hivyo hivyo.”

Akipingana na kauli ya Rais Kikwete Bungeni juu ya njia za kuumaliza mgogoro uliojitokeza hivi karibuni kuhusu suala la hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano, ambapo Rais Kikwete alitaka suala hilo waachiwe wanasheria wa serikali mbili kulitolea ufafanuzi kama vile ilivyokwishasemwa awali na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Maalim Seif alisema hili sio suala la kuachiwa wanasheria hao tu, bali “hali ya Muungano ilivyo sasa inaonesha dhahiri kuwepo mgogoro wa kikatiba ambapo suluhu yake haiwezi kupatikana bila Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kuunda Mahakama ya Katiba” ambayo itapewa jukumu la kutafuta jawabu linalofaa kwa suala hilo.

“Ni lazima watu wa kuujadili Muungano huo watoke pande zote mbili na wawe na uwezo wa kuandika rasimu ya katiba rasmi. Sio waseme vikao vya mawaziri ndio vijadili mambo ya Muungano na kuamua.”

Katika hotuba yake Bungeni mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Kikwete alijaribu kutoa ufafanuzi kuhusiana na kadhia hii ya hadhi ya Zanzibar lakini Maalim Seif alibainisha kwamba Rais huyo wa Jamhuri hakutoa jibu lolote la maana juu ya suala hilo, maana kauli yake ya kushangazwa na kuwepo kwa watu ambao hawaelewi dhamira ya waasisi wa Muungano ikiwa sasa ni miaka 44, si mpya wala si jibu.

“Wa kuwashangaa si wananchi wanaohoji dhamira ya Muungano. Hali ilivyo sasa ya Muungano huwezi kuwalaumu wananchi kwa kuwa ni kweli Muungano huu haueleweki na kwa kuwa bado wananchi hawajaelezwa dhamira za Mzee Abeid Amani Karume na Mwalimu Nyerere, kuunganisha nchi. Na kwa kuwa kipindi chote cha utawala wa Mwalimu Nyerere ukizungumzia Muungano unaambiwa haini. Kwa hali hiyo Muungano utaeleweka vipi?”

Maalim Seif, ambaye anafahamika kwa kuwa mtetezi mkubwa wa Zanzibar tangu katika zama za kuwa ndani ya serikali na CCM, aliuambia umma uliokusanyika kwenye mkutano huo wa aina yake kwamba Muungano huo ulifanywa  kwa siri kubwa wakati wa kuasisiwa kwake mwaka 1964,  kwa vile ni Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Karume tu, watu  wawili, ndio waliozungumza na kukubaliana. Hata Baraza la Mapinduzi, ambalo kwa wakati huo lilikuwa linasimama kama Baraza la Mawaziri na Bunge kwa wakati mmoja kwa upande wa Zanzibar, halikuarifiwa.

“Kuna mawaziri kadhaa wa Zanzibar ambao kwa mara ya mwanzo walisikia kuhusu Muungano April 26, 1964 kwenye redio.”

Aliwataja miongoni mwa watu muhimu ambao ingelibidi kuwashirikisha katika mashauriano na mazungumzo ya Muungano, na ambao hata hivyo hawakushirikishwa kuwa ni pamoja na aliyekua Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wa wakati huo, Wolfgang Dourado. Mara kadhaa Dourado amewahi akinukuliwa akitamka wazi wazi kuwa yeye hakushirikishwa, na hakuambiwa lolote kuhusu  kufanyika kwa Muungano huo.

Mwengine ni aliyekuwa msaidizi wa karibu wa mzee Karume na ambaye alikuja kuchukua nafasi yake baada ya kuuawa, Mzee Aboud Jumbe, ambaye naye anazungumza katika kitabu chake cha The Partnership kuwa hakuweza kushirikishwa na kushiriki kwenye suala hilo. Hata hivyo, kwa upande wa pili wa Muungano, yaani Tanganyika, Mwalimu Nyerere alihakikisha kuwa anapata ushauri ulio bora kabia kutoka kwa wanasheria wakiwemo wale wa dola ya Uingereza, ambao walikuwa ni wakoloni wa zamani wa Tanganyika na Zanzibar.

Na katika hatua ya kushangaza na iliyoibua hamasa kali katika mkutano huo wa Chaani, ni pale Maalim Seif alipoweka wazi kuwa hadi sasa Muungano huu haujaidhinishwa Zanzibar kama ambavyo ilitakiwa iwe kisheria. Maalim Seif alisema kuwa hata Baraza la Mapinduzi halikuidhinisha Muungano huo kwa kuwa hawakupelekewa na hadi leo hii haujatangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali kama ilivyo kawaida ya sheria. Badala yake, Maalim Seif alifichua, kumbe Mwalimu Nyerere alimtumia mwanasheria wake wa Kiingereza kuandika kwenye Gazeti la Serikali ya Tanganyika kwamba Muungano umeridhiwa na Baraza la Mapinduzi (jambo ambalo si la kweli) na kisha kuutangaza rasmi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Sera ya CUF kuelekea Muungano ni ya serikali tatu, na Maalim Seif alisema kwamba kila siku zikienda mbele ushahidi unazidi kuibuka kwamba hilo ndilo suluhisho la kudumu kwa mgogoro wa muda mrefu wa Muungano, kwani kimsingi hivyo ndivyo ilivyotakiwa iwe tangu mwanzoni.

“Rais (Kikwete) anaposema Zanzibar ni nchi ukiwa ndani, lakini ukiwa nje si nchi inajulikana Tanzania, anafanya usanii tu. Mkataba wa Muungano haujafuta nchi ya Tanganyika wala ya Zanzibar kwa kuwa unasema shughuli za Bara zitaongozwa na Katiba ya Tanganyika na za Zanzibar zitaongozwa kwa sheria za Zanzibar.”

Vile vile Maalim Seif aliitupilia mbali hoja ya Rais Kikwete katika hotuba yake ya Bungeni kwamba hapakuwa na sababu ya mjadala uliozuka wa Zanzibar si nchi kufikia ulipofikia na kuhoji kwamba wale wanaouendeleza mjadala huu ni kwa sababu wana ajenda zao binafsi na akafikia umbali wa kuwaita machakubimbi.

“Mimi nataka nimwambie ndugu yangu, Rais Kikwete, kwamba kama anakusudia uchakubimbi ni pale Wazanzibari wanapodai haki yao ndani ya Muungano, kwa hilo anakosea. Sisi tutaendelea kusema na kutetea maslahi ya nchi yetu. Chakubimbi ni yeye mwenyewe!” Alisema Maalim Seif huku akishangiliwa na maelfu ya Wazanzibari waliokusanyika hapo katika mkutano wa kihistoria.

Maalim Seif alisema kuwa ni haki ya wananchi kuujadili Muungano na kusema nini hasa wanataka na nini hawakitaki kwenye Muungano huu, ikiwa ni kweli huu ni Muungano wa wananchi na sio wa viongozi tu. Alisisitiza haja ya wananchi kuendelea kujadili Muungano hivi sasa kwa kuwa walizibwa midomo kwa miaka mingi na akaonya juu ya kutaka kurejewa kwa tabia hiyo ya kidikteta

“Sasa mazingira yamebadilika ni sasa ‘ruksa’ kuzungumza Muungano. Kikwete asitumie vitisho dhidi ya Wazanzibari. Eti watachukuliwa hatua. Nani achukuliwe hatua hapa?”

Katika siku za karibuni, tangu Waziri Mkuu Pinda aseme Bungeni kwamba Zanzibar si nchi, takribani viongozi wote wa Zanzibar kutoka vyama na taasisi tafauti wameonekana kusimama pamoja kutetea hoja yao kuwa Zanzibar ni nchi na itaendelea kubakia hivyo milele. Kauli zinazofanana kuhusiana na hili zimetolewa na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), wabunge na wawakilishi wa CUF na CCM, viongozi wa vyama vingine vya kisiasa na viongozi wa taasisi za kidini, huku wananchi kwa ujumla wakisimama nyuma ya viongozi wao.

Katika mkutano huo, Maalim Seif aliwasifu akina Ali Juma Shamhuna (Mwakilishi wa Donge kwa tiketi ya CCM na Naibu Waziri Kiongozi), Mansour Yusuf Himidi (Waziri wa Nishati na Mazingira), Hamza Hassan (Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi), Hafidh Tahir (Mbunge wa CCM Dimani) kwa upande wa CCM na pia kuwasifu viongozi wa CUF, wakiwemo Aboubakar Khamis Bakar (Kiongozi wa Upinzani kwenye Baraza la Wawakilishi) na Hamad Rashid Mohammed (Kiongozi wa Upinzani Bungeni) kwa msimamo wao wa kuitetea Zanzibar.

<!– /* Style Definitions */ p.MsoNormal, li.MsoNormal, div.MsoNormal {mso-style-parent:””; margin:0in; margin-bottom:.0001pt; mso-pagination:widow-orphan; font-size:12.0pt; font-family:”Times New Roman”; mso-fareast-font-family:”Times New Roman”;} @page Section1 {size:8.5in 11.0in; margin:1.0in 1.25in 1.0in 1.25in; mso-header-margin:.5in; mso-footer-margin:.5in; mso-paper-source:0;} div.Section1 {page:Section1;} –>
/* Style Definitions */
table.MsoNormalTable
{mso-style-name:”Table Normal”;
mso-tstyle-rowband-size:0;
mso-tstyle-colband-size:0;
mso-style-noshow:yes;
mso-style-parent:””;
mso-padding-alt:0in 5.4pt 0in 5.4pt;
mso-para-margin:0in;
mso-para-margin-bottom:.0001pt;
mso-pagination:widow-orphan;
font-size:10.0pt;
font-family:”Times New Roman”;}

(c) 2008, Kurugenzi ya Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma, CUF

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s