Mafuta ya Zanzibar ni mali ya Wazanzibari – Maalim Seif

"Bila ya idhini ya Zanzibar, mafuta hayachimbiki!"

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad: "Bila ya ruhusa ya Wazanzibari, mafuta hayachimbiki!"

Na Ripota Wetu, Zanzibar

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amemtaka Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, kuunda wizara maalumu itakayoshughulikia mafuta na gesi asilia visiwani Zanzibar.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Kibanda Maiti jana, Maalim Seif alisema kwamba ikiwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina dhamira ya dhati ya kuliondoa suala la mafuta katika Orodha ya Muungano ni vyema wizara hiyo ikaundwa kwa kuwa Shirika la Maendeleo la Mafuta Tanzania (TPDC) sio la Muungano.

Maalim Seif alisema mbali na kuunda wizara hiyo, pia SMZ iunde Shirika Maalumu la Maendeleo ya Mafuta Zanzibar liweze kutoa vibali vya uchimbaji wa mafuta na gesi katika vitalu namba 9, 10, 11 na 12 vilivyopo katika ukanda wa bahari kuu ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika mkutano huo mkubwa uliohudhuriwa na maelfu ya Wazanzibari, Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema kwamba kuna fununu ya makampuni makubwa ya uchimbaji wa mafuta katika Nchi za Ghuba zikieleza kuwa Zanzibar kuna gesi nyingi kama ilivyo katika nchi ya Qatar ambapo makampuni hayo yako tayari kuanza mchakato wa uchimbaji wa mafuta na gesi kupitia Serikali ya Muungano lakini wamekuwa na khofu juu ya Kambi ya Upinzani, Zanzibar

“Makampuni hayo yameleta ujumbe kwangu kwamba wao hawana shaka kuwa serikali itakubali suala la uchimbaji mafuta na gesi, lakini khofu yao ni Upinzani. Mimi nikawaeleza kupitia kwa mjumbe wao kuwa, ikiwa watachimba chini ya Serikali ya Muungano hatukubali na iwapo watachimba kwa kibali cha SMZ tutawaunga mkono,” alisema Maalim Seif huku akishangiriwa na maelfu hayo ya watu waliokusanyika maalum kwa ajili ya kusikiliza msimamo wa CUF kuhusu mafuta ya Zanzibar.

Kiongozi huyo alisema kwamba wakati makampuni hayo yakiwa katika mchakato wa kutafuta ufumbuzi wa suala hilo, wameelezwa na upande wa Tanzania Bara kuwa sio vyema kuweka mitambo ya usafishaji wa mafuta katika visiwa vya Zanzibar kwani itasababisha uchafuzi mkubwa wa kimazingira na badala yake kushauri kuwa mitambo hiyo ijengwe Bara.

“Jamani hawa ndio ndugu zetu wanaotuonea huruma kila siku. Wanasema mitambo ya usafishaji wa mafuta ikijengwa Zanzibar itachafua mazingira kwa hivyo ni bora ijengwe Tanzania Bara,” amesema Katibu Mkuu huyo.

Aidha Katibu Mkuu huyo wa CUF amesema kwamba msimamo wa Wazanzibari hadi sasa bahari kuu yote na inayopakana nayo ni mali ya Zanzibar na rasilimali zake ikiwa pamoja na kumiliki kilomita 50 kutoka ufukweni mwa bahari ambapo Zanzibar upande wa mashariki inajumuisha kisiwa cha Pemba na bahari kuu wakati Tanzania Bara na Zanzibar inagawana nusu kwa nusu kwa upande wa kaskazini.

Alisisitiza kuwa Zanzibar ni nchi kwani ina sifa zote zinazotakiwa ikiwa ni pamoja na kuwa na ukanda maalumu kiuchumi, exclusive economic zone, upatao kilomita 200.

Kutokana na hali hiyo, Maalim Seif alisisitiza kuwa ni busara ikabaikia kuwa mali ya Zanzibar kwa sababu Wazanzibari wengi hawapendi kuwa ya Muungano. Hivyo ni lazima kuepusha kama yale yanayotokea nchini Nigeria ambapo kumekuwa na ugomvi wa mafuta.

Katika hatua nyengine Maalim Seif alishangazwa na matamshi yaliotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatib, kuwa matamshi ya wajumbe wa Baraza la Wawakislihi sio msimamo wa Serikali ya Zanzibar. Alisema kwamba waziri huyo amekuwa akitoa matamshi yanayotofautiana na yale ya SMZ kupitia kwa Waziri wake, Mansour Yussuf Himid, kuwa hakujakuwa na ufumbuzi wa ama mafuta kubaki katika Orodha ya Muungano au kuondolewa.

Chanzo: http//:www.zanzinet.net

Advertisements

One thought on “Mafuta ya Zanzibar ni mali ya Wazanzibari – Maalim Seif

  1. Wazanzibar Hawana lao kazi yao kuvaa vikoi msilete longolongo twajua kuwa mafuta hayapo katiak muungano ila tunataka tuwakomeshe tutakula wote na nyinyi hamu gusi Madini kwa sababu hayapo katika muungano

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s