Hali tete Pemba: CUF wataka JK aingilie kati

Wednesday, 12 August 2009 06:59
Na Reuben Kagaruki

CHAMA cha Wananchi (CUF),kimemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw.Jakaya Kiwete, kuhakikisha anasitisha mpango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wa kutaka kutumia vikosi vyote vya ulinzi na usalama kusimamia duru ya pili ya uandikishaji wapiga kura, vinginevyo uchaguzi wa 2010 hautafanyika.

Kauli ya CUF imekuja siku moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Bw. Hamza Hassan Juma, kunukuliwa na vyombo vya habari, akisema SMZ itatumia vikosi vyote vya ulinzi na usalama wakati wa awamu ya pili ya uandikishaji wapiga kura itakapoanza ili kuthibiti vurugu.

Alienda mbali zaidi na kusema kuwa; “Wananchi wa Pemba wasishangae kuona vifaru kwa vile Tanzania tupo makini katika suala la ulinzi wa nchi, ndiyo maana tumeamua kupeleka askari wa majini katika maeneo ya Kaskazini ya Pemba.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Bw. Salim Biman, alisema; “Raia hawana chochote tunawakaribisha (askari) na vifaru vyao wawaswage na kama Rais Kikwete hatazuia mpango huo uchaguzi wa 2010 hautafanyika.”

Alisema Pemba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, hivyo uchaguzi kama hautafanyika visiwani humo basi hata wa Jamhuri hautakuwepo.

Bw. Biman alisema vitisho ambavyo vimeanza kutolewa na SMZ haviwatishi wananchi wa Pemba bali vinazidi kuwaongezea ari zaidi.

Alisema kauli iliyotolewa na Bw. Juma inaonesha wazi kuwa SMZ imedhamiria kuendeleza mauaji kama yale yaliyotokea mwaka 2001 wakati wa vurugu za kupinga matokeo ya uchaguzi uliompa ushindi Rais Amani Abeid Karume wa mwaka 2000 watu 21 waliuawa na wengine kukimbilia Mombasa.

“Kama wanataka kuleta vikosi vyote vya ulinzi na usalama na vifaru pia, basi hayo ni maandalizi ya mauaji mabaya zaidi ya yale ya mwaka 2001,” alisema Bw. Biman.

Alisema kama Rais mtaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, angekuwa amekamatwa na kushitakiwa kwa mauaji ya mwaka 2001, maandalizi yanayoendelea sasa yasingekuwepo kwani hata Rais Kikwete angeogopa.

“Watu hawana fujo wanachotaka ni haki yao, na wataidai hadi mwisho,” alisema na kuongeza kuwa nia yao ni kutaka kuona watu wote wenye sifa wanaandikishwa katika daftari la wapiga kura.

Alitoa mwito kwa wananchi wa Pemba wasiogope vitisho kwani ni haki yao ya kikatiba kujiandikisha kupiga kura. Alipoulizwa hatua ya SMZ kupeleka vikosi vya majini ili kudhibiti watu wanaoingia kwa ajili ya kuvuruga uandikishaji, Bw. Biman alijibu;

“Hakuna mtu anayeingia hiyo ni aina nyingine ya ufisadi, wanatumia fedha za walipa kodi vibaya.”

Alisema madai hayo yanatolewa ili kuhalalisha hatua ya Serikali ya kupeleka vikosi vingi vya ulinzi na usalama kisiwani Pemba kwa lengo la kukandamiza demokrasia wakati wa uchaguzi mwakani.

Aliongeza kuwa pamoja na hatua hiyo wananchi bado wapo ngangari.Ameiomba Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati suala hilo kwa kuwa alidai Tanzania ni moja ya nchi ambazo haziheshimu haki za binadamu. “Jumuiya ya Kimataifa iitazame Tanzania kwa jicho jingine vinginevyo uchaguzi hautakuwa huru na wa haki,” alisema.

Akizungumzia vifaru ambavyo tayari vimepelekwa Pemba na kuonekana vikirandaranda, Bw. Biman alisema;

“Ni kweli vinaonekana na kimoja kimepinduka lakini yote hayo ni maandalizi ya vitisho.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini pemba, Bw. Said Marekano, alinukuliwa na vyombo vya habari jana akithibitisha vifaru hivyo kuonekana mitaani, lakini alisema askari hao wa JWTZ wapo katika mazoezi ya kawaida ya kulenga shabaha kwa ajili ya kujiweka tayari katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aliwataka wananchi kuondoa wasiwasi kwa vile mazoezi hayo ni ya kawaida kwani wanajeshi kuonekana na vifaru ni sawa na mvuvi kuonekana na nyavu.

Chanzo: http://www.majira.co.tz

Leave a comment