Ni ipi hatma ya demokrasia Tanzania baada ya ‘Tsunami’ ya CCM

Makamo Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali

Makamo Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali

“Tanzania iliingia katika mfumo wa vyama vingi baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin na kusambaratika kwa ukomunisti Ulaya Mashariki na Urusi. Nchi za magharibi zinazotoa misaada ziliweka “sharti la demokrasia” ili Tanzania iendelee kupata misaada. Kwa kuwa serikali ya Tanzania ni tegemezi kwa misaada ililazimika ijitoe kimasomaso kuwa nayo imo katika wimbi la ujenzi wa demokrasia ya vyama vingi. CCM iliukubali mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kwa shingo upande na si kwa ridhaa yake bali kutokana na shindikizo kutoka nchi wahisani pamoja na vikundi vilivyokuwa vikipigania mageuzi ya kisiasa ndani ya nchi. Matokeo yake yakawa ni kwa nchi kuingia katika mfumo huo mpya wa siasa bila ya marekebisho ya msingi ya taasisi zinazosimamia maongozi ya nchi. Kama zilivyo nchi nyingi za Kiafrika, chama kinachotawala Tanzania kilikubali mfumo wa vyama vingi pasina kukubali kuwa matokeo ya mfumo huo yanaweza kuwa ni kupoteza madaraka na kuyakabidhi kwa chama kingine kitakachoridhiwa na wananchi wenyewe. Upinzani utavumiliwa ikiwa tu utakubali kubakia katika upinzani.”

Mada iliyotayarishwa na CUF kwa ajili ya Mkutano wa Tanzania Center for Democracy (TCD) kuponyesha majeraha ya Uchaguzi Mkuu wa 2005, Machi 24 2006

Utangulizi

Mwaka 2005 Watanzania tulishiriki katika uchaguzi mkuu wa kuchagua madiwani, wawakilishi, wabunge na Rais. Upande wa Zanzibar uchaguzi ulifanyika tarehe 30 Oktoba 2005. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilimtangaza Aman Abeid Karume kuwa mshindi wa Urais. Chama cha CUF hakikuafiki kutangazwa kwa Amani Karume kuwa Rais halali kwa sababu kutangazwa kwake hakukutokana na kura halisi za Wazanzibari walizopiga katika vituo vya kupigia kura. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilitangaza matokeo ya kupika. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar pia ilitangaza kuwa CCM wameshinda viti 31 vya uwakilishi – vyote vikiwa ni vya Unguja na CUF imeshinda viti 19, viti vyote 18 vya Pemba na kimoja tu cha Unguja.

Uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano ulifanyika tarehe 14 Desemba 2005 baada ya kuahirishwa kutokana na kifo cha Mgombea mwenza wa CHADEMA. Tume ya Uchaguzi ya Taifa ilitangaza ushindi wa tsunami wa CCM. Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Mheshimiwa Jakaya Kikwete alipata asilimia 80 ya kura zote halali. Kati ya viti 182 vya Ubunge Tanzania Bara, CCM walikomba viti 175. CHADEMA walijitutumua wakapata viti 5, TLP kimoja na UDP kimoja. CUF ikaangamizwa na tsunami na kufundishwa adabu na wanamtandao kwa kutoka na nunge. Upande wa Zanzibar matokeo ya uchaguzi wa Wakilishi yalijirudia katika uchaguzi wa Wabunge. CUF ilipata Wabunge wote 18 wa majimbo ya Pemba na mbunge mmoja tu wa Mjimkongwe kwa upande wa Unguja. CCM ikanyakua viti 31 vya Unguja.

Katika chaguzi tatu zilizopita ushindi wa CCM umekuwa unaongezeka uchaguzi mmoja baada ya mwingine. Ikiwa uchaguzi wa Tanzania ni huru na wa haki, vyama vya upinzani havikubaliwi na wananchi Tanzania Bara na Unguja. Ni Pemba peke yake ndio kwenye upinzani. Kwa Tanzania kwa ujumla tunaweza kujenga hoja kuwa baada ya chaguzi tau za vyama vingi, Watanzania wanapendelea kuwa na mfumo wa Chama kimoja. CCM inaweza kuweka mgombea yeyote na wananchi watampigia kura mgombea wa CCM. Lakini kwa nini Watanzania waipende CCM kiasi hiki?

Baada ya miaka 45 chini ya utawala wa CCM, Tanzania ni nambari wani kwa ujinga, umaskini na maradhi. Vijana hawana ajira, wakulima hawana huduma, zahanati hazina dawa. Tanzania inaongoza kwa vifo vya kinamama wajawazito. Pamoja na madhira yote haya bado Watanzania wanaihusudu CCM.

Jee? Watanzania ni mazezeta na hamnazo wa mwisho? Hawapigi hata kura ya kulalamika (protest vote)? Au matokeo ya uchaguzi ni ya kupanga? CCM ni chama dola. Vyombo vya dola na hasa usalama wa taifa, tume ya uchaguzi na jeshi la polisi ndivyo vinavyotumiwa kuhakikisha CCM inabaki madarakani na kupata ushindi wa tsunami. CCM kupitia vyombo vya dola wamekuwa magwiji wa wizi wa kura na mabingwa wa kuwatumia watazamaji wa kimataifa kuhalalisha wizi wao.

Demokrasia na Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii

Katika ulimwengu wa leo, demokrasia ni muhimu katika kulinda na kuendeleza haki za binadamu. Demokrasia pia ni nyenzo ya kukuza uchumi na kuboresha huduma za jamii. Wataalam wa historia ya uchumi wa ulimwengu wamejenga hoja kuwa ukuaji wa uchumi endelevu kwa muda mrefu unategemea sana mfumo mzima wa kiutawala na kiuchumi. Kama nchi ina mfumo ambao maamuzi ya watawala yanafuata taratibu zinazoeleweka na kutabirika, mfumo wa utawala una uhalali machoni kwa wananchi, utawala unafuata sheria na haki za kumiliki mali zinalindwa na kutoa motisha kwa wananchi kuchapa kazi kwa bidii, kuwa wabunifu kwani wana uhakika kuwa matunda ya jasho lao na ubunifu wao hayataporwa na dola au watu wenye nguvu au silaha basi uchumi unaweza kukua kwa haraka na kwa muda mrefu.

Demokrasia ya kweli inajenga mazingira ya kuwepo ushindani wa kisiasa. Wanasiasa na vyama vyao wanaeleza sera na mipango itakayoboresha maisha wananchi. Wapiga kura wanapata fursa ya kuyapima maelezo ya wanasiasa na kuchagua wale wanaoamini watkidhi mahitaji yao. Ikiwa watashindwa kufanya hivyo watawaangusha katika uchaguzi unaofuata.

Uchaguzi kila baada ya muda uliopangwa ni sehemu muhimu ya demokrasia. Lakini uchaguzi peke yake hautoshi kuifanya nchi kuwa na demokrasia. Nchi yenye demokrasia ya kweli lazima iwe na utawala wa sheria, iheshimu na kulinda haki za binadamu, pawepo na uhuru wa kujieleza na kujumuika, uhuru wa vyombo vya habari vya kusambaza taarifa na ukosoaji wa haki. Uchaguzi utakuwa na kasoro kubwa ikiwa washindani katika uchaguzi hawana fursa sawa ya hoja zao kuziwasilisha kwa wananchi na wapiga kura ili waweze kuzipima na kufanya maamuzi ya kuwapigia au kutowapigia kura.

Kuna watu wanafikiri kuwa demokrasi ni jambo la anasa linalopatikana wakati nchi imekuwa tajiri. Mheshimiwa Mkapa alisema ” Kwa asiye na chakula, demokrasia ni anasa.” Hii ni kauli ya viongozi wa kimla na kidikteta. Ukweli ni kwamba watu maskini wanahitaji kuwepo kwa demokrasi inayowapa sauti na kuvilazimisha vyama vya siasa na wanasiasa kuwasikiliza wapiga kura maskini.

Mtaalam wa mambo ya uchumi wa India aliyepata Tuzo ya Nobel (Nobel Prize) katika mambo ya uchumi ya 1999 baada ya kufanya utafiti unaoonyesha kuwa hakuna nchi yenye demokrasi na uhuru wa vyombo vya habari ambayo imekumbwa na baa la njaa mpaka watu wakafa kwa njaa. Katika miaka ya 1958-60, wakati wa utawala wa Mao, watu milioni 30 walikufa kwa njaa China lakini serikali iliweza kuficha ukweli huu uliokujakujulikana baada ya Deng Hsiao Ping kushika madaraka mwishoni mwa miaka ya sabini. India pamoja na kuwa na masikini wengi ina utaratibu wa kuhakikisha kuwa watu masikini wanapata chakula cha msingi hata katika miaka ambayo mavuno siyo mazuri na kuna uhaba wa chakula. Ikiwa watu watakufa kwa njaa, vyombo vya habari vitapiga kelele. Serikali iliyoko madarakani itapoteza kura wakati wa uchaguzi.

Katika Bara la Afrika nchi mbili tu ndizo zilizopata maendeleo makubwa ya kiuchumi katika miaka 30 mpaka 40 iliyopita. Nchi hizo pia ndizo pekee zenye mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa vyombo vya habari kwa muda wote huu. Nchi hizo ni Botswana na Mauritius. Watanzania tusikubali dhana ya kidikteta kuwa demokrasi ni anasa. Demokrasi ya kweli inalinda haki za msingi za binadamu. Demokrasi pia ni nyezo ya kuleta maendeleo endelevu. Sera mbovu za uchumi kama vile Operesheni Vijiji ambayo ilwahamisha wananchi kwa nguvu, kuwavunjia nyumba na kuwapa umaskini au Operesheni Maduka na kamata kamata ya Wahujumu uchumi zisingetekelezwa kama nchi yetu ingekuwa na uhuru wa vyombo vya habari na demokrasi ya kweli yenye uchaguzi ulio huru na wa haki.

Baada ya miaka 44 ya utawala wa CCM Tanzania, maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanasikitisha. Watanzania walio wengi ni miongoni ya watu masikini wa kutupwa ulimwenguni, hawana elimu bora, huduma za afya ni duni, ajira imetoweka na rushwa kukithiri. Katika mwaka 2005 Watanzania walikuwa na kila sababu ya kutaka mabadiliko.

Demokrasia ya Vyama vingi Tanzania

Tanzania iliingia katika mfumo wa vyama vingi baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin na kusambaratika kwa ukomunisti Ulaya Mashariki na Urusi. Nchi za magharibi zinazotoa misaada ziliweka “sharti la demokrasia” ili Tanzania iendelee kupata misaada. Kwa kuwa serikali ya Tanzania ni tegemezi kwa misaada ililazimika ijitoe kimasomaso kuwa nayo imo katika wimbi la ujenzi wa demokrasia ya vyama vingi. CCM iliukubali mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kwa shingo upande na si kwa ridhaa yake bali kutokana na shindikizo kutoka nchi wahisani pamoja na vikundi vilivyokuwa vikipigania mageuzi ya kisiasa ndani ya nchi.

Matokeo yake yakawa ni kwa nchi kuingia katika mfumo huo mpya wa siasa bila ya marekebisho ya msingi ya taasisi zinazosimamia maongozi ya nchi. Kama zilivyo nchi nyingi za Kiafrika, chama kinachotawala Tanzania kilikubali mfumo wa vyama vingi pasina kukubali kuwa matokeo ya mfumo huo yanaweza kuwa ni kupoteza madaraka na kuyakabidhi kwa chama kingine kitakachoridhiwa na wananchi wenyewe. Upinzani utavumiliwa ikiwa tu utakubali kubakia katika upinzani.

CCM haikuwa na nia ya dhati ya kujenga miingi imara ya demokrasia. Mapendekezo ya msingi ya Tume ya Jaji Nyalali ikiwa ni pamoja na kutunga katiba mpya yenye misingi imara ya demokrasia na kufutwa sheria 40 za ukandamizaji hayakutekelezwa mara moja. Badala yake katiba ya ukiritimba wa Chama kimoja kushika hatamu imewekewa viraka kuhalalisha kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi. Taasisi za dola na hasa Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Vyombo vya Habari vya Umma vimekuwa na utendaji kazi wa kupendelea Chama tawala. Tume ya Uchaguzi ya Taifa siyo huru. Sekretariati ya Tume ya Uchaguzi inaendeshwa na mashushu wa Usalama wa Taifa.

Katika kipidi chake chote cha Uongozi Rais Mkapa hakuwa na agenda ya kuendeleza demokrasia. Hakuwa na utaratibu wa kukutana na kubadilishana mawazo na viongozi wa upinzani. Hata baada ya mauaji ya Zanzibar ya tarehe 26 na 27 Januari 2001 na Muafaka wa CCM na CUF wa Oktoba 2001 ambao ulihimiza “na kusisitiza kuendelea na mpango wa kuleta maridhiano na maelewano ya kitaifa kwa msingi wa mazungumzo na kujenga imani miongoni mwa vyama vya siasa hapa nchini.” Na ibara ya 17 ya Muafaka ikaeleza

“Ili kufanikisha azma hii ya kuwa na mashauriano ya kudumu baina ya viongozi wa vyama vya siasa, vyama vya CCM na CUF vimekubaliana kuwa ipo haja ya kuwa na Kamati ya Pamoja ya Mashauriano ya Vyama vya Siasa hapa nchini ambayo itakuwa ni ya kudumu na itakayowajumuisha viongozi wa kitaifa wa vyama vyote vya siasa vilivyopo nchini katika mfumo ambao utaamuliwa na vyama husika baadaye. Kamati hii itakuwa ndiyo jukwaa la kubadilishana mawazo na kujenga maelewano juu ya masuala mazito yanayoihusu nchi yetu.”

Rais Mkapa alikutana na Viongozi wa vyama vya siasa mara moja tu. Vikao hivi vilikuwa vya kila kiongozi wa Chama cha siasa na ujumbe wake. Vilikuwa vikao vya kufahamiana. Jitihada za Bob Makani aliyekuwa Mwenyekiti wa Vyama vya Upinzani kuandaa Mkutano wa pamoja wa vyama na Rais Mkapa haikufanikiwa. Rais Mkapa alipenda kuuonyesha Ulimwengu kuwa Tanzania ina mfumo wa demokrsia ya vyama vingi. Alikuwa mkarimu wakati wa ziara ya Viongozi kutoka nje alitukaribisha katika chakula na viongozi hao hata kuandaa mazungumzo tubadilishane mawazo na Marais waliotembelea nchi yetu. Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa walipewa fursa ya kusafiri na Rais katika zira zake za nje. Hata hivyo hakujenga mazingira ya kuhakikisha mfumo wa vyama vingi unashamiri nchini.

CCM iliridhia mfumo wa vyama vingi siyo kwa nia thabiti ila iweze kuonekana vizuri katika macho ya nchi zinazotoa misaada kwamba Tanzania pia imo katika mchakato wa ujenzi wa demokrasia. Viongozi wa CCM hawajakubali mantiki ya mfumo wa demokrasia ya vyama kuwa ukishindwa uchaguzi uachie madaraka na utoe fursa kwa Chama kilichochaguliwa na wapiga kura kuendesha serikali. Ushahidi wa ubabe wa CCM kuiminya demokrasi unadhihirishwa na matumizi ya vyombo vya dola katika chaguzi zote Zanzibar kuhakikisha CCM inabakia madarakani.

USALITI WA MATUMAINI YA UMMA ZANZIBAR

Mbinu za CCM za wizi wa kura Zanzibar zimebadilika katika kila uchaguzi. Katika uchaguzi wa kwanza wa Oktoba 1995, CCM walishindwa pamoja na mbinu walizotumia kuzuia baadhi Wazanzibari wanaoaminiwa kuunga mkono CUF kukataliwa kuandikishwa. Uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika tarehe 22 Oktoba 1995. Kwa kuwa wapiga kura wote walikuwa chini ya 350,000, matokeo yalitarajiwa kutangazwa usiku wa tarehe 22 au asubuhi tarehe 23. Baada ya kimya kirefu hatimaye tarehe 24 Oktoba 1995 katika milango ya saa 8.00 mchana Mkurugenzi wa uchaguzi aliwaita mawakala wa Wagombea Urais, Bwana Mwinyi Mzee wakala wa Dr. Salmin Amour, Mgombea Urais wa CCM, Bwana Nassor Seif Amour wakala wa Maalim Seif Shariff Hamad, Mgombea Urais wa CUF. Pia alikuwepo Bi Judith Thompson, raia wa Canada, aliyekuwa mshauri wa mambo ya uchaguzi wa ZEC. Mkurugenzi wa Uchaguzi aliwapa nakala ya matokeo ya uchaguzi yaliyoonyesha Mgombea wa CUF Seif Shariff Hamad ameshinda kwa kupata kura 166,522 sawa na asilimia 51.4 ya kura zote halali zilizopigwa ukilinganisha na kura 157,351 alizopata mgombea wa CCM Dr. Salmin Amour Juma. Kituo cha televisheni cha DTV na gazeti la Majira kiliyapata matokeo haya na kuyatangaza. Baada ya taarifa ya Mkurugenzi wa ZEC kupokelewa na CCM, Naibu Katibu Mkuu wa CCM upande wa Zanzibar Bwana Ali Ameir Mohamed aliandika barua ZEC tarehe 25 Oktoba 2005 kupinga matokeo na kudai uchaguzi urudiwe kwa sababu haukuwa huru na wa haki.

ZEC ilishinikizwa na CCM na vyombo vya dola kumtangaza Dr. Salmin Amour Juma ndio mshindi wa uchaguzi wa Rais. Balozi Kari Karanko wa Finland aliyekuwa anaongoza United Nations Election Observation Team aliieleza ZEC kuwa kuna makosa ya wazi kati ya matokeo toka kwenye vituo vya kupigia na kuhesabia kura na yale yaliyotangazwa na ZEC. Alishauri uapishaji wa Rais usifanyike mpaka hapo hitilafu hii itarekebishwa. ZEC walikataa kata kata.

Baada ya matukio hayo, Zanzibar iliingia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa ambao uliathiri kiasi kikubwa sana umoja na amani ya nchi yetu. Jumuiya ya Madola (The Commonwealth) iliingilia kati na hatimaye Juni 9, 1999 vyama vya CCM na CUF vikatia saini Muafaka wa I katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi. Muafaka huu uliitaka CUF ifumbie macho madai ya ushindi wake halali na wajumbe wake wa Baraza la Wawakilishi warejee na kushiriki kikamilifu katika shughuli za Baraza. CUF iliyatekeleza hayo mara tu baada ya kutiwa saini Muafaka huo.

Kwa upande wake, CCM na Serikali yake walitakiwa kufanya marekebisho ya msingi ya taasisi za maongozi ya nchi ili kuzifanya chaguzi zinazofuata ziwe zinazokubalika na zisizo na utatanishi. Hayo hayakufanyika; na CCM na Serikali zake waliubeza Muafaka huo huku wakikataa kutekeleza kifungu chochote cha Muafaka.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 ulipowadia sio tu ulifanyika katika mazingira yale yale ya 1995 bali zaidi uliambatana na joto kali la kisiasa lililotokana na vyama vya CCM na CUF kutoaminiana na hivyo kusababisha chuki na uhasama wa hali ya juu miongoni mwa viongozi na wafuasi wake. Hali hiyo ilisababishwa kwa kiasi kikubwa na CCM kutoheshimu makubaliano ya Muafaka wa I.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000, CCM Zanzibar waligawanyika. Mgombea Urais Mhe. Amani Abeid Karume aliyewekwa na CCM mwaka 2000 alikuwa hatakiwi hata na CCM Zanzibar. Katika kura za maoni za Wajumbe wa Zanzibar wa Halmashauri Kuu ya CCM Mhe. Karume alikuwa mtu wa tatu na alipata kura 9 tu akiwa ameshindwa vibaya na kutupwa mbali na Dk. Mohamed Gharib Bilal aliyezoa kura 44. Mheshimiwa Karume alipewa nafasi ya kugombea Urais na wajumbe wa Halmashauri ya CCM wa Tanzania Bara. Wana CCM wa Zanzibar waliamini Karume sio tu hakubaliki miongoni mwa Wazanzibari bali hata miongoni mwao wana CCM wa Zanzibar.

Vyombo vya dola vilitumiwa kuukandamiza upinzani. Viongozi na wafuasi wa upinzani walinyanyaswa na kuadhibiwa, vipigo na mateso dhidi ya wapinzani vilikuwa ni mambo ya kawaida, risasi za moto zilitumiwa kujeruhi wafuasi wa CUF ndani ya mikutano ya kampeni, sheria za uchaguzi na katiba zilipuuzwa; mikutano ya kampeni ya CUF ilivurugwa; na baada ya yote hayo kushindwa kumhakikishia ushindi mgombea wa CCM, vikosi vya ulinzi na usalama vikaamriwa kuuteka nyara uchaguzi na kuyachukua masanduku ya kura kwa mtutu wa bunduki.

CCM walipogundua kuwa wanashindwa vibaya katika uchaguzi wa mwaka 2000 wakaamua kutumia askari kwenda kubeba visanduku vya kura kwa nguvu. ZEC ikaamuru uchaguzi wa majimbo 16 ya Mkoa wa Mjini Magharibi urudiwe, wakati uchaguzi ulivurugika nchini kote. Taarifa ya watazamaji wa uchaguzi wa ndani na wa nje ulieleza uchaguzi haukuwa huru na wa haki na unapaswa urudiwe wote baada ya kuunda upya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Wana-CUF walipoamua kufanya maandamano ya amani Januari 27, 2001 kudai kurudiwa kwa Uchaguzi kama yalivyokuwa madai ya Watazamaji wote wa ndani na nje wa uchaguzi, Dola ikitumia vikosi vya ulinzi na usalama iliyazima kwa mtutu wa bunduki maandamano hayo na kuwaua raia wasio na hatia wasiopungua 65. Tanzania kwa mara ya kwanza ikazalisha wakimbizi pale wananchi wapatao 2,000 walipokimbilia Shimoni, Kenya kunusuru maisha yao.

Muafaka wa II ulipatikana baada ya miezi minane ya majadiliano makini na yaliyokuwa na machungu makubwa kwa washiriki kutokana na hali ya kisiasa ya nchi yetu ilivyokuwa baada ya mauaji ya Januari 26 na 27. Pamoja na ahadi ya Rais Mkapa aliyeitoa katika sherehe za kusaini Muafaka aliposema:-

“Nikiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi natamka wazi kuwa chama changu ni sehemu ya muafaka huu, na chama changu kimeuridhia muafaka huu kwa dhati na kwa moyo mweupe. Kwa hivyo, tunaahidi mbele ya Watanzania wote kuwa tutautekeleza kwa ukamilifu kwa kila sehemu inayotuhusu.

Nikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nathibitisha pia kuwa nitatekeleza kwa ukamilifu yale yote yanayonihusu mimi na Serikali yangu katika muafaka huu.”

Rais Mkapa na Karume hawakuutekeleza Muafaka wa II kama walivyoahidi hadharani tarehe 10 Oktoba 2001. Ibara ya 5 ya utangulizi wa Muafaka inatanabahisha:

“KWAMBA vyama vyetu viwili vimejifunza kwamba kuna haja ya kutekeleza makubaliano yanayofikiwa kwani kinyume cha hayo ni wananchi kupoteza imani na njia ya mazungumzo kama ndiyo njia sahihi ya kutatua migogoro katika jamii.”

Vifungu vingi ambavyo vinagusa maeneo ya msingi kabisa yakuhakikisha uwanja ulio sawa wa ushindani wa haki katika siasa (level playing field for fair competitive politics) havikutekelezwa. Sekretarieti ya Tume haikufanyiwa marekebisho, vyombo vya habari vya Serikali vilikataa kabisa kutangaza habari za Upinzani na wakati mwingi vinachochea chuki, hasama, ukabila, vurugu na fujo katika jamii, Mahkama hazikufanyiwa marekebisho na zilfanya kazi sawa na maskani za CCM, Vyombo vya Dola na hasa Polisi na Vikosi vya SMZ vinafanya kazi kukilinda chama kinachotawala (CCM) na uajiri wake unafanywa kupitia matawi ya CCM, sheria zinazoviza demokrasia na kukandamiza haki za bianadamu bado zingalimo katika vitabu vya sheria za nchi, uhuru wa kufanya shughuli za siasa unaingiliwa, Daftari la Kudumu la Wapiga Kura liliandikishwa kwa misingi ya ubaguzi wa kuwakataa wana-CUF na hasa Wapemba.

Azma ya Muafaka II ya kujenga mazingira ya uchaguzi huru na wa haki mwaka 2005 haikufikiwa badala yake taasisi zote za dola Zanzibar zimetengenezwa na kufumwa ziwatumikie sehemu tu ya raia na ziwanyanyase na kuwakandamiza sehemu nyengine ya raia hao hao na kuzuia sauti ya umma kupitia visanduku vya kura kutoheshimiwa.

Uchaguzi wa Oktoba 2005 Zanzibar haukuwa huru na wa haki na kwa mara nyingine Wazanzibari walisalitiwa kwa kutangaziwa Rais ambaye siyo chaguo lao. Mbinu za wizi wa kura zilibadilishwa. Safari hii CCM walihakikisha hawarudii uporaji wa masanduku ya kura kama walivyofanya mwaka 2000. Hata hivyo Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30 Zanzibar ulitawaliwa na kasoro nyingi na kubwa pamoja na hujuma za makusudi, tokea wakati wa uandikishaji hadi upigaji, uhesabuji wa kura, majumuisho na utangazaji wa matokeo.

Uandikishaji na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) halikusambazwa kwa vyama vyote kabla ya uchaguzi kama ilivyokuwa imekubaliwa, pamoja na maombi kadhaa. CUF iliingia katika uchaguzi huu bila ya kuwa na nakala ya Daftari ambalo tokea awali ilishaweka wazi msimamo wake kwamba isipopewa mapema na kujiridhisha, haitayakubali matokeo ya uchaguzi utakaoendeshwa kwa kutumia daftari hilo.

Nakala ya DKWK ilipotolewa Novemba 7, ilidhihirika kwamba daftari hilo lilikuwa limejaa kasoro na limechafuliwa kwa makusudi. DKWK lilikuwa ndio kiini cha wizi wa kura na msingi mkuu wa mkakati wa CCM na Serikali wa kuiba kura. Dosari kadhaa ambazo CUF ilizieleza kuhusiana na DKWK mwezi Agosti 2005 bado hazijarekebishwa, hata baada ya hicho kinachoitwa ‘uhakiki’ ambao uligharimiwa na nchi wahisani. Miongoni mwa mambo yanayofichuliwa katika ripoti hii ni pamoja na:

  • Uandikishaji wa zaidi ya mara moja kwa mtu mmoja
  • Uandikishaji haramu wa watu wasio wakaazi katika maeneo wakiwemo askari wa vikosi vya ulinzi na usalama
  • Uandikishaji wa watoto wadogo wa chini ya umri wa miaka 18
  • Uandikishaji uliothibitishwa wa ziada ya majina hewa yasiyopungua 30,000
  • Kukataliwa kuandikishwa kwa wapiga kura halali wasiopungua 12,000

CUF ililalamikia watu walioandikishwa zaidi ya mara moja mwezi Agosti 2005 pale Daftari lilipobandikwa kwa wananchi kujiridhisha. Watu wale walioajiandikisha angalau mara mbili bado wamegunduliwa kuwemo katika daftari hilo hadi hii leo, baada ya huo unaoitwa ‘uhakiki’. CUF iliweza kuwagundua watu wenye shahada za kupigia kura zaidi ya moja zikiwa na picha yao ile ile lakini majina tofauti.

Watoto wadogo wa chini ya miaka 18 waliogunduliwa na CUF mwezi Agosti na taarifa zao kuwasilishwa ZEC bado wangalimo katika DKWK.

Takwimu za mwisho za ZEC kwa walioandikishwa kupiga kura zinaonyesha kwamba kwa mikoa ya Kusini Unguja na Kaskazini Unguja, idadi ya walioandikishwa imezidi idadi ya watu kwa mujibu wa sensa za mwaka 2002 kwa watu 31,197; ikiwa ni asilimia 34% zaidi kuliko idadi ya wakaazi halisi.

Bila ya uhakiki wa kina na ulio huru utakaojumuisha majina, picha na alama za vidole za walioandikishwa, DKWK lililoandaliwa na ZEC litabaki kuwa si la kuaminika na hivyo kutokubalika kwa CUF. Na kwa msingi huo, halina maana yoyote na wala halipaswi kutegemewa kama msingi wa chaguzi huru au mapatano ya kisiasa visiwani Zanzibar. DKWK kama ilivyo sasa inaamaanisha Daftari la Kudumu la Wizi wa Kura.

CUF imeshtushwa na hatua za CCM, Serikali na ZEC kuchezea na kupuuza Muafaka na pia kuchezea na kupuuza nia njema pamoja na msaada wa kiasi kikubwa cha fedha uliotolewa na nchi wahisani. Baada ya juhudi kubwa za Wazanzibari, vyama vya siasa, UNDP, na marafiki wa Tanzania katika jumuiya ya kimataifa kuanzisha dafrari la wapiga kura linaloheshimika, matokeo haya ya kulivuruga siyo tu hayakubaliki kisiasa, na yanahatarisha amani ya nchi na utulivu wa kisiasa Zanzibar, bali pia ni kuwatukana wote walioshiriki katika juhudi hizi.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar

Tukizungumzia utawala, ZEC iliweza kusimamia vyema ugawaji wa vifaa vya uchaguzi na upangaji wa vituo vya kupigia kura kote Zanzibar, na kwa jumla kisiwani Pemba uendeshaji wa uchaguzi haukuwa na matatizo makubwa. Hata hivyo, Unguja kuliripotiwa matatizo kadhaa katika utendaji wa ZEC yakiwemo:

  • Maafisa wa ZEC kushirikiana na hata kupokea amri kutoka kwa mawakala wa CCM na vikosi vya ulinzi na usalama
  • Maafisa wa ZEC kusaidia au kupuuza upigaji kura haramu au wa zaidi ya mara moja
  • Maafisa wa ZEC kutotia alama majina ya waliokwisha piga kura au kutowatia wino usiofutika
  • Maafisa wa ZEC kuzuia na kutotoa fomu za mtokeo ya uchaguzi
  • Maafisa wa ZEC kuwazuia mawakala wa CUF wasifanye kazi zao na kukataa kufuata sheria za uchaguzi

Isitoshe, kama ilivyoelezwa na CUF mwezi Oktoba 2004, maafisa wa ZEC waliajiriwa kwa kuzingatia maelekezo ya CCM na Serikali, ikiwa ndiyo sifa pekee. Wasimamizi wa Uchaguzi na wasaidizi wao takriban wote walikuwa ni maafisa au wanachama wakereketwa wa CCM au watumishi wa serikali waliokuwa na historian na rekodi ya kuchafua chaguzi zilizopita, kuvunja sheria na kuvuruga taratibu za demokrasia.

Baada ya matokeo, Makamishna wa ZEC kutoka CUF walitangaza kukataa kuhusishwa na Tume na wizi wa kura iliousimamia. Walisema hawakuhusishwa katika kufanya maamuzi ya msingi ya Tume na walizuiwa kufanya kazi zao na maafisa pamoja na makamishna wengine wa Tume ambao walionekana wazi wakipokea maagizo kutoka nje ya ZEC.

Utendaji wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama na Uvunjwaji wa Haki za Binadamu

Idadi kubwa ya askari kutoka vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar – JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa, KMKM, JKU, Valantia, Mafunzo na Zimamoto – viliwatisha wapiga kura na katika maeneo mengi vilishiriki hasa katika kuwazuia wasitekeleze haki zao za kidemokrasia. Katika maeneo kadhaa, waliwapiga raia, kupiga mabomu ya machozi na kurusha maji ya kuwasha na hata kupiga risasi za moto ili kuwazuia Wazanzibari wasifike katika vituo vya kupigia kura.

Lakini lililo kubwa zaidi, vikosi hivi vilishiriki kikamilifu katika kuwasafirisha wapiga kura haramu na wale waliopiga kura zaidi ya mara moja kutoka kituo kimoja hadi kingine na pia katika kuwalinda ili wavunje sheria bila ya kuingiliwa au kuhojiwa. Katika maeneo mengi, askari wenyewe walipiga kura zaidi ya mara moja, huku wakiwa na sare zao na wakibeba silaha.

Hata baada ya uchaguzi na hadi wiki moja baada ya kuapishwa kwa Amani Karume, vikosi hivi vya ulinzi viliendesha operesheni ya unyanyasaji na mateso dhidi ya wanachama na wafuasi wa CUF. Wakaazi wa Pemba waliathirika zaidi katika vitendo hivi. (Katika uchaguzi wa Muungano, kampeni ya aina hii iliendeshwa katika maeneo ya Mji Mkongwe na Tumbatu kisiwani Unguja.)

Maelfu ya wafuasi na viongozi wa CUF walizuiwa na kuzingirwa katika eneo la Makao Makuu ya CUF kwa siku 3 mfululizo baada ya uchaguzi wakiwa hawana chakula wala maji, mamia walipigwa na kuteswa wakiwa rumande na wawili walifariki kutokana na vipigo hivyo. Huko Pemba, wakimbizi 200 walikimbilia Kenya kutokana na operesheni hiyo ya mateso na udhalilishaji, Wabunge na Wawakilishi wa CUF walipigwa, wanawake kadhaa walibakwa, na kijana mmoja alipigwa risasi na kuuawa papo hapo. Baadhi ya watazamaji wa kimataifa wa uchaguzi waliokuwepo Zanzibar na ambao wameshuhudia pia uchaguzi wa Palestina wamelinganisha idadi na unyanyasaji wa vikosi vya ulinzi Zanzibar wakati wa uchaguzi kuwa sawa kama si zaidi ya ule wa vikosi vya Israel katika Ukanda wa Magharibi na Gaza.

Utendaji wa vikosi hivi vya ulinzi kwa ujumla umeishushia hadhi Tanzania mbele ya ulimwengu wa kimataifa lakini zaidi mbele ya raia wake wenyewe, na umefuta wasiwasi wowote uliokuwepo juu ya mwenendo wa kikandamizaji na kidikteta wa tawala zetu Zanzibar na Tanzania Bara.

Upigaji Kura Haramu na Zaidi ya Mara Moja

Huku wakiwa wanalindwa na kusaidiwa na vikosi vya ulinzi na maafisa wa ZEC, idadi kubwa ya vijana wa CCM (maarufu kwa jina la Janjaweed) walipiga kura katika vituo zaidi ya kimoja na pia mara nyingi ndani ya kituo kimoja. Wafuasi wengi wa CCM waliandikishwa zaidi ya mara moja na hata wale wasioandikishwa, walishiriki katika njia kadhaa za wizi wa kura. Njia hizo ni pamoja na:

  • Kupiga kura wakiwa tayari wana wino usiofutika katika vidole vyao (kuashiria wameshapiga kura)
  • Kupiga kura zaidi ya mara moja ndani ya kituo kimoja cha kupigia kura
  • Kupiga kura zaidi ya kituo kimoja cha kupigia kura
  • Kupiga kura kwa kutumia shahada za kujiandikisha za watu wengine
  • Kupiga kura bila ya kuwa na shahada yoyote ya kujiandikisha
  • Watoto wadogo wa chini ya miaka 18 kupiga kura
  • Wasio wakaazi kupiga kura

Watu Walionyimwa Haki ya Kupiga Kura

CCM na ZEC walikuwa na mkakati maalum na wa makusudi wa kuyavuruga majina ya wapiga kura wa CUF ili yasitambulikane. Hii ilipelekea matatizo kadhaa:

  • Watu wengi wakiwa na shahada za kupigia kura walikwenda kupiga kura na kuambiwa majina yao hayamo katika orodha
  • Baadhi walikuta majina yao katika orodha zilizobandikwa nje ya vituo lakini hayakuonekana ndani ya Daftari lililowekwa ndani ya vituo
  • Watu walioshikilia haki yao ya kupiga kura walitolewa nje ya vituo na askari wa vikosi vya ulinzi
  • Wapiga kura halali walipofika vituoni waliambiwa na maafisa wa ZEC kwamba rekodi zinaonyesha walishapiga kura

Matokeo Yaliyotangazwa na ZEC

Kisiwani Pemba, ZEC imedhihirisha kwamba ikitaka inaweza kufanya uchaguzi mzuri na usio na matatizo. Mawakala wote wa CUF walitia saini fomu na kuthibitisha matokeo ya Pemba. Lakini kisiwani Unguja, fomu nyingi zilizuiwa, nyengine zilijazwa kimakosa, na matokeo ‘rasmi’ yanatofautiana kimsingi na matokeo yaliyorekodiwa katika vituo na ZEC na mawakala wa CUF.

Kufuatia shindikizo za jumuiya ya kimataifa na waangalizi wa uchaguzi, hatimaye ZEC ilitoa nakala ya kile ilichokiita matokeo ya uchaguzi wa Rais kutoka vituo vya kupigia kura. Matokeo haya yameanika hadharani ukweli kwamba matokeo ya uchaguzi huo ni ya kupikwa. Kuna tofauti nyingi na za msingi kati ya matokeo hayo, yale yaliyotangazwa awali na ZEC hapo Novemba 2, 2005 na yale yaliyomo kwenye fomu za matokeo kutoka vituoni ambazo CUF inazo. Wakati matokeo yaliyotangazwa na ZEC yenyewe Novemba 2, 2005 yanaonyesha Amani Karume alipata idadi ya kura 239,832 sawa na asilimia 53.02% na Maalim Seif Sharif Hamad alipata idadi ya kura 207,733 sawa na asilimia 46.1%, matokeo ya sasa yanayopatikana kutokana na majumuisho ya kile kinachodaiwa matokeo ya vituoni yanaonyesha Amani Karume alipata idadi ya kura 241,899 sawa na asilimia 53.6% na Maalim Seif Sharif Hamad alipata idadi ya kura 205,872 sawa na asilimia 45.6%. Inakuwaje ZEC hiyo hiyo inakuwa na matokeo tofauti, ni ZEC yenyewe tu inayoweza kujibu lakini huu ni ushahidi wa wazi wa matokeo ya kupikwa.

Hitimisho na Hatua za Kuchukuliwa

CUF imeshtushwa na dharau na kebehi iliyoonyeshwa na CCM na Serikali zake kwa Muafaka na zaidi kwa nia njema na mpango wa kuleta usuluhishi na mageuzi ya kidemokrasia Zanzibar.

Pamoja na utawala na uendeshaji wa uchaguzi kuonekana afadhali (uchaguzi mara hii haukusimamishwa na masanduku ya kura hayakuondolewa vituoni kwa mtutu wa bunduki), uchaguzi mkuu wa 2005, kama zilivyo chaguzi za 1995 na 2000, hauwakilishi matakwa ya wananchi wa Zanzibar. Lakini zaidi, ukitafakari athari za jumla na za kisaikolojia kwa jamii, kwa misingi ya demokrasia na kwa dhamira ya dhati ya wananchi ya kupigania mabadiliko kwa njia za amani, uchaguzi wa tatu uliovurugwa kwa wizi wa kura utakuwa na taathira mbaya kwa Zanzibar. Taifa letu linaingia katika awamu nyengine ya giza katika historia yake.

Njia ya kuelekea kujenga tena imani kwa serikali, kwa mfumo wa uchaguzi na kwa uadilifu wa utawala wa sheria Zanzibar ni vigumu kuonekana katika wakati huu. Hatua za awali kwa serikali inayojali heshima yake kwa wananchi wake na kwa jumuiya ya kimataifa; inayojali uadilifu; na inayodhamiria kikweli kujenga mazingira mema ya kisiasa, ni lazima zijumuishe:

  1. Uchunguzi huru na wa kina utakaokuwa na uwakilishi wa jumuiya ya kimataifa kuhakiki mwenendo mzima wa uchaguzi na matokeo yake na kusikiliza na kupokea ushahidi kutoka pande zote na kisha kutoa mapendekezo muafaka.
  2. Uhakiki huru na wa kina wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuondoa watoto wadogo, wapiga kura hewa na wale waliojiandikisha zaidi ya mara moja.
  3. Uchapishaji wa majina ya wale wote walioondolewa katika Daftari la Wapiga Kura.
  4. Uandikishaji wa watu takriban 12,000 walionyimwa haki ya kujiandikisha na kasha majina yao kuingizwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
  5. Uchunguzi na mashtaka kufunguliwa dhidi ya maafisa na askari wa vikosi vya ulinzi waliohusika na uporaji, upigaji, ubakaji na mauaji ya raia wasio na hatia.
  6. Ulipwaji wa fidia kwa raia waliopoteza mali zao na jamaa zao katika fujo na ghasia zilizosimamiwa na kufanywa na dola katika kipindi chote cha uchaguzi wa 2005.

Sasa imefahamika wazi kwamba CCM haitaki wala haiheshimu demokrasia na itatumia nguvu na uwezo wake wote kuwazuia Wazanzibari wasichague viongozi wanaowataka. Katika mazingira hayo, ni vigumu kufikia hitimisho jengine zaidi ya kusema kwamba njia pekee ya kufanyika uchaguzi ulio huru na wa haki ni kuwa uchaguzi huo usimamiwe na chombo kingine kama vile Umoja wa Mataifa kupitia Sekretarieti yake ya Uchaguzi. Hili limefanyika katika nchi kadhaa zenye matatizo katika ujenzi wa demokrasia kama ilivyoshindwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia haki hiyo kwa Wazanzibari.

Hata hivyo, na pamoja na hayo, uchaguzi huu uliovurugika unatoa fursa nyingi za kujifunza. Hatua muhimu za kuepusha uchafuzi wa uchaguzi na ukandamizaji wa demokrasia katika siku zijazo ni lazima zijumuishe:

  1. Kuifanyia mabadiliko Katiba ili kuruhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais kupingwa Mahkamani.
  2. Kuimarisha uhuru wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) katika katiba na sheria ili uteuzi wa maafisa na watumishi wake na taratibu za uendeshaji wake zitokane na maafikiano ya vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi.
  3. Kufuta utaratibu wa askari wa vikosi vya ulinzi kujiandikisha katika maeneo wanakohamishiwa kwa muda; wanapaswa wajiandikishe kama wakaazi katika maeneo yao wanayoishi kama ilivyo kwa raia wengine. Majina ya askari wote waliopelekwa katika maeneo maalum kwa lengo la uchaguzi tu na kuandikishwa huko yafutwe kutoka katika DKWK.
  4. Kuwekwa utaratibu wa kuchapisha matokeo kutoka vituo vyote vya kupigia kura, na pia ZEC kutangaza matokeo ya uchaguzi kadiri yanavyopokelewa kutoka majimboni, kama ilivyo kwa nchi nyengine nyingi.

Nimeelezea kwa urefu wizi wa kura katika uchaguzi wa Zanzibar kwa sababu ndiyo kielelezo kamili cha ukosefu wa dhamira ya dhati ya watawala wa Tanzania katika suala la ujenzi wa demokrasia nchini. Katika chaguzi tatu CCM wametumia vyombo vya dola kuhakikisha wanabakia madarakani. Kama CCM wamekataa kuheshimu matakwa ya Wazanzibari, hawawezi kuheshimu matakwa ya Watanzania.

UCHAGUZI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Kura za kambi ya upinzani zimekuwa zinapungua kila baada ya uchaguzi mmoja. Katika uchaguzi wa mwaka 1995, kura za wagombea ubunge wote wa kambi ya upinzani zilikuwa asilimia 41, mwaka 2000 asilimia 35 na mwaka 2005 asilimia 29 (jedwali 1). Viti vya upinzani katika Bunge la Jamhuri ya vinavyotokana na majimbo ya uchaguzi vimepungua toka viti 46 kati ya viti 232 mwaka 1995, viti 29 kati ya viti 231 mwaka 2000 na viti 26 kati ya viti 232 mwaka 2005. Kwa upande wa bara peke yake viti vya upinzani vimepungua toka viti 22 kati ya viti 182 mwaka 1995, viti 14 kati ya viti 182 na kufikia viti 7 kati ya viti 182. Kama tungekuwa na utaratibu wa uwakilishi wa uwiano, vyama vya upinzani vingekuwa na uwakilshi mkubwa zaidi ndani ya bunge kuliko ilivyo sasa haidhuru ungekuwa unapungua kila baada ya uchaguzi. Kwa upande wa Tanzania Bara CHADEMA ndiyo imeweza kuongeza alau mbunge mmoja kila baada ya uchaguzi. Ilipata wabunge watau mwaka 1995, ikapata wabunge wanne mwaka 2000 na mwaka 2005 imepata wabunge watano. CUF haikupata hata mbunge mmoja Tanzania Bara mwaka 1995, mwaka 2000 ikapata wabunge wawili na mwaka 2005 ikakumbwa na tsunami na kuambulia nunge pamoja na kwamba karibu nusu ya kura zote za wagombea wa upinzani walipigiwa wagombea wa CUF.

Kura za Wagombea Urais wa kambi ya upinzani pia zimekuwa zinapungua. Mwaka 1995 kambi ya upinzani ilipata asilimia 38 za kura zote. Mwaka 2000 zikapungua kufika asilimia 28. Mwaka 2005 zimeporomoka kufikia chini kidogo ya asilimia 20. Hata kama uchaguzi ungekuwa huru na wa haki matokeo haya lazima yangemstusha Mtanzania yeyote ambaye anataka demokrasia ishamiri nchini. Hasa ukizingatia kuwa baada ya utawala wa chama kimoja kwa muda wa miaka 44 Watanzania hawana maendeleo ya kuridhisha ya kiuchumi na kijamii. Suala la kujiuliza ni kwa nini matokeo ya uchaguzi yamekuwa mabaya kwa kambi ya upinzani kiasi hiki?

Udhaifu na ukosefu wa umoja wa vyama vya upinzani

Wadadisi wengi hutoa hoja ya udhaifu wa vyama vya upinzani. Hata Rais Mkapa alikuwa bingwa wa kububujika machozi ya mamba na kudai kuwa linalomsikitisha sana ni udhaifu wa vyama vya upinzani. Kuungana vyama vya upinzani na hasa vile vinavyofanya kazi ya kisiasa ndani ya umma vitaimarisha kambi ya upinzani. Hata hivyo matokeo ya uchaguzi hayaonyeshi kuwa kambi ya upinzani imepoteza viti vingi kwa sababu havikuweka mgombea mmoja.

Viti ambavyo kambi ya upinzani ingevipata kama wapiga kura wote wa upinzani wangempigia mgombea wa upinzani aliyeongoza ni Arusha Mjini (TLP), Kigoma Kusini (NCCR) na Kisesa (CHADEMA). Lakini pia tuelewe kuwa sheria ya vyama imetungwa makusudi kuzuia vyama kuungana. Vyama vilivyosajiliwa haviwezi kuungana na kuanzisha Chama kimoja bila kujisajili upya na kujitoa katika vyama vyao vyenye usajili. Vyama vinaweza kushirikiana, lakini makubaliano yao hayatambuliwi rasmi kisheria. Mathalani CUF na CHADEMA tulikubaliana kushirikiana katika uchaguzi wa mwaka 2000 lakini wagombea wetu wa Urais na katika majimbo tuliyoweka mgombea mmoja hawakutambuliwa rasmi na Tume kuwa ni Wagombea wa CUF na CHADEMA kwa pamoja.

Hoja ya udhaifu wa vyama pia lazima ilinganishwe kihistoria. Ni kweli vyama vyote vya upinzani havina fedha za kutosha, havina mtandao wa matawi nchi nzima, havimiliki vyombo vya habari vya kutosha na havina watendaji wengi wenye uwezo wa hali ya juu. Hata hivyo maendeleo ya mtandao wa CUF kati ya 1995 mpaka kabla ya uchaguzi wa 2005 yalikuwa makubwa mno. Chama kiliamua kuwa kata yeyote haiwezi kutambuliwa kuwa ina uongozi wa chama mpaka iwe na alau matawi matatu ya chama yenye wanachama 50-400.

Wilaya haiwezi kutambuliwa kuwa ina uongozi wa chama mpaka alau nusu ya kata za wilaya zimekamilisha masharti ya kutambuliwa kuwa ni kata za chama zenye uhai. Mpaka Aprili 2005 CUF ilikuwa na wilaya 80 Tanzania Bara zenye mtandao wa Chama uliohakikiwa. Viongozi wa kitaifa na hasa Mwenyekiti wa Chama alitembelea karibu mikoa yote ya Tanzania Bara kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura. Ilani ya uchaguzi wa sera za Chama zilisambazwa na kufahamika mwaka 2005 kuliko mwaka 2000. Mgombea Urais wa CUF ilifahamika vizuri mwaka 2005 kuliko mwaka 2000. CUF ilikuwa na nguvu za kisiasa zilizodhihirika wazi katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Kagera, sehemu za mkoa wa Mara hasa Musoma Mjini, wilaya yote ya Kondoa na Tunduru. Tulitegemea kushinda viti 50 vya uhakika na vingine 20-40 tulikuwa na mategemeo ya nusu kwa nusu.

Baada ya kazi ya kujenga chama na kuboresha maandalizi ya kuingia katika uchaguzi, CUF haikupata kiti kimoja bara. Dar es Salaam ambayo ndiyo iliyokuwa ngome yetu hatukupata hata diwani mmoja hata kwenye kata ambazo CUF ilishinda serikali nyingi za mitaa kuliko CCM. Hata katika majimbo ambayo wagombea wetu na chama chetu kilikuwa nguvu sana kama vile Kigamboni, Temeke, Ukonga, Tanga, Mkinga, Pangani, Bukoba Mjini, Bukoba Vijijini, Musoma Mjini, Serengeti, Sumve, Kwimba, Geita, Nyang’wale, Buchosa, Magu Mjini, Maswa, Solwa, Tabora Mjini, Igalula, Tabora Kaskazini, Sikonge, Urambo magharibi, Kondoa Kusini, Kondoa Kaskazini, Mchinga, Lindi Mjini, Liwale, Tandahimba, Newala, Mtwara Vijijini na Tunduru hatukuambulia kitu.

Kwa upande wa kura za Rais siyo tu tumepata asilimia ndogo mwaka 2005 (11.7) ukilinganisha na mwaka 2000 (16.3) lakini hata idadi ya kura zimepungua kutoka 1329077 mwaka 2000 na kufikia 1327125 mwaka 2005. Kabla na wakati wa kampeni, wananchi wengi walivutiwa na hotuba za mgombea na mgombea mwenza na wanachi wengi walihudhuria mikutano ya kampeni bila kupewa motisha ya kapelo, fulana au usafiri wa bure. Je? Watanzania wote hawa walikuwa wanatuhadaa?

Mvuto wa Mgombea Urais wa CCM

Kuna wanaodai kuwa tsunami ya CCM ni matokeo ya mvuto kwa wapiga kura ya mgombea Urais wa CCM. Inawezekana Mhe. Jakaya Kikwete ana mvuto maalum. Hata hivyo hali ya kisiasa ilivyokuwa ndani ya CCM siyo mvuto bali kampeni nzito zikiwemo kampeni za kuchafuliana majina ndizo zilizofanikisha uteuzi wake. Aliyekuwa Waziri alitamka hadharani na kulalamika kuhusu kutumia kalamu kuchafua jina lake. Vile kura za maoni ndani ya CCM zilisababisha mtafaruku mkubwa miongoni mwa wanachama wa CCM. Wagombea wengi wa Ubunge wa CCM walikuwa hawakubaliki kabisa na wengine walizomewa hadharani wakati Mgombea Urais wa CCM alipowanadi. Imekuwaje wagombea hawa pia wamepata ushindi wa tsunami?

Hujuma na Wizi wa Kura

Mchakato wote wa uchaguzi unasimamiwa na vyombo vya dola ambavyo dhamira yake ni kuhakikisha kuwa kwa vyovyote vile CCM inabaki madarakani. Rais Benjamin Mkapa alitamka hadharani kwamba atatumia hata vyombo vya dola kuhakikisha CCM inabaki madarakani. Kabla na wakati wa kampeni viongozi wa CCM walikuwa wakitutambia kuwa hatutapata serikali Zanzibar na hatutapata hata kiti kimoja Tanzania Bara. Mwaka 2005 ndio mwisho wa CUF na Lipumba. Baadhi yetu tukawapuuza tukadhani hizo ni kauli za mfamaji haachi kutapatapa. IGP Mahita alithibitisha hujuma ya jeshi la Polisi dhidi ya CUF pale alipokishutumu Chama cha CUF kuwa kinaendeleza ujambazi kuhujumu jeshi la polisi kama njia ya kulipiza kisasi kwa jeshi hilo kutokana na CUF kushindwa vibaya kwenye uchaguzi mkuu. Alisisitiza kuwa Chama cha CUF hakitatawala mpaka kiama na yeye ni mwiba mkubwa dhidi ya CUF. Katika moja ya hotuba yake, Rais Kikwete alivieleza vyama vya upinzani visitafute Mchawi aliyesababisha vishindwe vibaya kwenye uchaguzi mkuu. IGP Mahita amejitokeza hadharani kuwa yeye na Jeshi la polisi ndiye “mchawi” (mwiba mkubwa) dhidi ya CUF. Hotuba ya IGP imeonyesha wazi kuwa yeye na jeshi la polisi analoliongoza limefanya kazi ya ziada kufanikisha ushindi wa tsunami wa CCM. Tarehe 13 Desemba siku moja kabla ya siku ya kupiga kura Mahita alionekana kwenye vyombo vya habari akionyesha visu na skafu yenye picha ya mgombea urais wa CUF na kuwaeleza wananchi chama cha CUF kimepanga kuvuruga uchaguzi na kwamba jeshi lake limebaini hali hiyo kuwa umma wa Watanzania usiwe na wasi wasi atapambana na hali hiyo.

Mpaka hivi leo hakuna kiongozi wa CUF aliyeulizwa na kumfunguliwa mashtaka na jeshi la polisi juu ya visu vile vilivyoonyeshwa siku moja kabla ya uchaguzi. Ni wazi jeshi la Polisi likiongozwa na IGP Mahita walichangia kutuhujumu wakati wa uchaguzi mkuu. Katika kipindi chote cha mchakato mzima wa uchaguzi wanachama wetu, viongozi na wagombea walishambuliwa na polisi, kukamatwa na kubambikiziwa kesi.

Mgombea wetu wa jimbo la Ukonga Mchungaji Heko Pori alibambikiziwa kesi ya kuvuruga kampeni ya Mgombea mwenza wa CCM wakati CCM ndiyo waliovuruga mkutano wake wa kampeni uliokuwa unafanyika eneo tofauti na kampeni ya Dr Shein. Mchungaji Pori alifungwa na kunyimwa dhamana. Hakuweza kupiga kura Wakati wa uchaguzi kwa sababu alikuwa yuko jela. Mkurugenzi wetu wa vijana Said Miraj aliyekuwa anaratibu shughuli zote za ofisi kuu wakati wa kampeni alibambikiziwa kesi za kumpiga Mwandishi wa Habari nje ya ofisi za CUF wakati yeye ndiye aliyetoka ofisini kwake kwenda kutuliza vurugu hizo. Alinyimwa dhamana na kuwekwa ndani mpaka uchaguzi ulipomalizika.

Nina wasiwasi kuwa hata tukio la kupigwa kwa waandishi wa habari nje ya ofisi za CUF yalipangwa na vyombo vya dola kuchafua jina la chama chetu mbele ya umma na kujenga mahusiano mabaya kati ya CUF na vyombo vya habari ili habari zetu zisitolewe ipasavyo. Katika mwaka 2005 CUF imeshughulikia zaidi ya kesi za kubambikiziwa zaidi ya 180. Wanachama na wapenzi wa CUF wanapohujumiwa jeshi la Polisi halishughuliki. Wakati wa sakata ya uchaguzi wa serikali za mitaa, katika mtaa wa Mbagala Kiburugwa wilaya ya Temeke, mwanafunzi wa shule, Khalid Omar Mfaume aliuawa kwa kupigwa risasi na vyombo vya dola. Kijana mwingine Abdallah Ramadhan alipigwa risasi ya pajani na kuumizwa vibaya.

Taarifa toka ndani ya jeshi la polisi zinaeleza kuwa risasi iliyomuua Khalid Omar Mfaume haikupigwa na polisi bali ilipigwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke. Hata hivyo polisi hawajamkamata aliyeua kwa sababu ya shinikizo za CCM kuwa Wakurugenzi wa manispaa na wilaya ni makada muhimu wa CCM katika utaratibu wao wa wizi wa kura. Mpaka leo mtu huyo hajakamtwa na kufikishwa pamoja na jeshi la polisi kuwa na ushahidi wa risasi iliyomuua kijana huyo.

Tume ya Uchaguzi ya Taifa

Vyama vya Upinzani havishirikishwi kwa namna yeyote ile katika uteuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa. Tume ya Taifa ya Uchaguzi siyo Tume huru ni chombo cha kuhalalisha wizi wa kura wa CCM. Mwaka 1995 inahisiwa hakuna Mgombea Urais aliyepata zaidi ya asilimia 50. Ilibidi uchaguzi wa Rais urudiwe na Mkapa apambane na Mrema. Tume ikapangua matokeo ya Dar es Salaam na kudai uchaguzi wa Dar urudiwe ili kupata nafasi ya kupika matokeo na kuipa ushindi CCM. Watendaji wengi wa sekretariati ya Tume ni maafisa wa Usalama wa Taifa na wanafanyakazi kwa karibu na kitengo hicho kuhakikisha ushindi wa tsunami wa CCM. Wengi wa wasimamizi wa uchaguzi wilayani na kwenye kata ni makada wa waziwazi au wa kujificha wa CCM. Kazi yao ni kuhakikisha CCM inashinda.

Uchaguzi wa mwaka 2005 ulitegemewa kuwa bora zaidi kwa kutumia daftari la kudumu la wapiga kura. Hata hivyo kwa makusudi serikali ilichelewesha uandikishaji wa daftari. Mpaka kufikia tarehe 30 Oktoba 2005, daftari lilikuwa halijasambazwa kwenye vyama vya siasa au kubandikwa kwenye tovuti ya Tume ya Uchaguzi kama vyama vya siasa vilivyoahidiwa wakati wa maandalizi ya uandikishaji wa wapiga kura. Nakala ya elektroniki ya daftari la kudumu lilipelekwa katika vyama vya siasa wiki moja kabala ya tarehe 14 Desemba 2005, tarehe mpya ya uchaguzi. Kwa muda huo mfupi, vyama visingeweza kulitumia kwa maandaliza ya uchaguzi.

Uchaguzi wote uliahirishwa baada ya kifo cha mgombea mwenza wa CHADEMA. Uchaguzi uliostahiki kuahirishwa ulikuwa ni wa Rais. Uchaguzi wa Wabunge na madiwani ungeendelea. CCM na Tume ya Uchaguzi ilikuwa na wasiwasi kuwa mbinu za wizi wa kura zikifichuka katika uchaguzi wa wabunge na madiwani, uchaguzi wa Rais hautafanyika kwa hiyo chaguzi zote zikaahirishwa kwa kisizingizio za kupunguza gharama.

Kuna wasiwasi mkubwa kwamba karatasi za kupigia kura zilichezewa katika uchaguzi wa 2005. Katika chaguzi mbili zilizpita za 1995 na 2000 majina ya wagombea yalipangwa katika karatasi za kupigia kura kufuatana na alphabet ya majina ya wagombea. Mwaka 2005, tume ya uchaguzi bila kushauriana na vyama vya siasa ikabadilisha utaratibu na kupanga wagombea kufuatana na vifupisho vya majina ya vyama. Kwa hiyo katika kila karatasi ya kupigia kura za Rais, Mbunge na Diwani jina la mgombea wa CCM lilikuwa la kwanza. Utaratibu huu ulirahisisha uchezeaji wa karatasi za kupiga kura.

Inaaminika lakini haijathibitishwa kuwa katika maeneo mengi karibuni nusu ya karatasi ya kupigia kura zilikuwa karatsi maalum ambazo tayari zimeishapigwa kura katika visanduku vya CCM. Karatasi hizo zinapochorwa sehemu nyingine alama hizo hufutika baada ya muda mfupi. Mawakala wengi wa CUF walipigwa na butwaa walipokuwa wanahesabu kura na kushuhudia kuwa CUF ina kura chache sana wakati wanachama na wapenzi wengi wa CUF walipiga kura. Alama za vema zilizowekwa katika kisanduku cha CCM zilifanana sana kama vile zimechorwa na mtu mmoja au mashine.

Mbinu za wizi wa kura zilibadilika eneo hadi eneo. Katika majimbo ambayo chama chetu kina nguvu sana kama Bukoba mjini, nguvu za dola zilitumiwa ikiwa ni pamoja na kumkatalia mgombea wetu ubunge kuingia katika baadhi ya vituo wakati kura zinahesabiwa. Baadhi ya mawakala walinunuliwa. Baadhi ya vituo havikuwa na mawakala na CCM na Tume walitoa matokeo waliyoyataka.

Watanzania wengi hawaamini matokeo yaliyotangazwa. Wanakubali kuwa Rais Kikwete ameshinda uchaguzi lakini siyo kwa asilimia 80. Kambi ya upinzani ingeweza kupata wabunge 90 – 120 wa kuchgulwa katika bunge la Jamhuri ya Muungano.

Lipi tufanye kujenga demokrasia ya kweli Tanzania

Demokrasia ni mfumo wa serikali unawahakikishia wananchi wote ulinzi wa haki zao za binadamu na ujenzi wa uchumi utakaowaltea neema na wananchi wote. Chaguzi zilizo huru na za haki ni muhimu katika karne hii kuhakikisha kuna amani na mshikamano wa kitaifa ulio madhubuti.

Alipoingia madarakani mwaka 1995, Rais Mkapa hakujiwekea agenda ya kujenga demokrasia. Hakuwa na muda wa kubadilishana mawazo na viongozi wa vyama vya siasa na taasisi zisizokuwa za kiserikali zenye malengo ya ujenzi wa demokrasia nchini. Rais Kikwete airekebishe kasoro hii kwa kujiwekea agenda na malengo ya ujenzi wa demokrasia ya kweli Tanzania. Katika Jumuiya ya nchi zenye misingi imara ya demokrasia kwa chama kinachotawala kwa muda wa miaka 44 iliyopita kujivunia kuwa kimeshinda uchaguzi kwa asilimia 80 wakati wananchi wake ni masikini wa kutupwa. Pia miongoni mwa wanademokrasia Rais hawezi kujisifia kuwa vyama vya upinzani ni dhaifu. Wanademokrasi watahisi kuwa serikali yako ni ya kidikteta au imekubuu katika wizi wa kura.

Hotuba ya Rais Kikwete katika kufungua Bunge ilitoa matumaini kuwa anayo agenda ya ujenzi wa demokrasia na ya kutatutua migogoro ya kisiasa. Sehemu ya kuanzia ni Zanzibar kwani huko CCM imeiba kura mara tatu bila haya. Kuna mpasuko mkubwa wa kisiasa. Suala la Zanzibar lisipushughulikiwa haraka kunaweza mlipuko mkubwa utakaoathiri maendeleo ya kisiasa na kiuchumi ya Tanzania yote. Rais Kikwete amezungumzia nia yake ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro wa Zanzibar. Ufumbuzi wake ni kuwa na chaguzi zilizo huru na za haki na kuheshimu matakwa ya Wazanzibari. Kauli ya Rais Kikwete kuhusu Zanzibar inastahiki kutafsiriwa kwa vitendo kuwapa matumaini Watanzania kuhusu azma yake ya kujenga demokrasia.

Katiba mpya yenye misingi imara ya demokrasia

Watanzania hatujapata fursa ya kushiriki kutunga katiba yetu itakayokuwa na misingi imra ya demokrasia. Wakati umefika wa kufanya hivyo. Tunaweza kuanzia ilipomalizia Tume ya Jaji Nyalali na mapendekezo ya kamati ya Jaji Kisanga. Rais kwa kushirikiana na wadau wengine vikewemo vyama vya siasa na taasisi sizizokuwa za kiserikali kutatibu mapendekezo ya wananchi kuhusu katiba mpya na kupendekeza utaratibu muafaka wa kufikia makubaliano ya katiba mpya. Katiba hiyo izipe nguvu za kisheria haki za msingi za raia wa Tanzania (Bill of Rights), itoe fursa kwa kila Mtanzania mtu mzima mwenye akili kuwa na haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika ngazi yeyote ya uongozi bila kuweka sharti la kuwa mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa. Mfumo wetu wa uchaguzi uzingatie uwakilishi wa uwiano ili kila kura iwe na uzito wa uwakilisha ndani ya Bunge. Katiba iliyojadiliwa na kukubaliwa na Watanzania wote itakuwa ndiyo dira ya taifa letu bila kujali itikadi na sera za vyama vyetu.

Kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi

Pamoja na katiba ya nchi kuainishi kuwepo kwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa iliyo huru, ni muhimu uteuzi na utendaji wa Tume uonekane wazi kuwa ni huru. Tume inastahiki kuwa na fedha za kutosha kufanya kazi zake kwa ufanisi, watendaji wenye uwezo na wasiopendelea Chama chochote. Tume iwe taasisi ya kudumu yenye mtandao nchi nzima na watendaji wachache wa muda mrefu na wengine wanaajiriwa bila upendeleo nyakati za uchaguzi. Tume ijengewe wa kuendesha uchaguzi bila migogoro. Tume ijijengee sifa ya kuaminiwa na vyama vya siasa bila upendeleo. Wananchi kwa ujumla na vyama vya siasa vijijengee utamaduni wa kidemokrasia wa kushindana bila kupigana na kukubali matokeo ya uchaguzi ulio huru na wa haki.

Vyombo vya dola kutopendelea chama tawala

Vyombo vya dola hasa Usalama wa Taifa na jeshi la polisi visiwe taasisi za kuhakikisha CCM inabaki madarakani kwa njia yeyote ile. Vifanye kazi bila ya upendeleo wa kisiasa. Kazi za Usalama wa Taifa zieleweke na zihakikiwe na kudhibitiwa na Bunge.

Kamati ya Pamoja ya Mashauriano ya Vyama vya Siasa

Ili kufanikisha kuwepo kwa mashauriano ya kudumu baina ya viongozi wa vyama vya siasa, kuna haja ya kuwa na Kamati ya Pamoja ya Mashauriano ya Vyama vya Siasa hapa nchini ambayo itakuwa ni ya kudumu na itakayowajumuisha viongozi wa kitaifa wa vyama vyote vya siasa vilivyopo nchini katika mfumo tutakaokubalian. Kamati hii itakuwa ndiyo jukwaa la kubadilishana mawazo na kujenga maelewano juu ya masuala mazito yanayoihusu nchi yetu.

Vyombo vya Habari

Ni vizuri vyombo vikubwa vya habari vijiwekee malengo na maadili ya ujenzi wa demokrasi nchini kwa kuwatendea haki washiriki wote katika medani ya ushindani wa kisiasa.

JEDWALI 1- IDADI YA KURA ZA WAGOMBEA UBUNGE WA KILA CHAMA KATIKA CHAGUZI TATU

1995

2000

2005

Idadi ya kura

Asilimia

Idadi ya kura

Asilimia

Idadi ya kura

Asilimia

CCM

3814206

59.22

4628127

65.19

7613516

70.37

CHADEMA

396825

6.16

300567

4.23

880281

8.14

CHAUSTA

37675

0.35

CUF

323432

5.02

890044

12.54

1537957

14.22

DP

11386

0.11

FORD

1625

0.02

JAHAZI ASILIA

20755

0.19

MAKINI

2102

0.02

NCCR-MAGEUZI

1406343

21.83

256591

3.61

209986

1.94

NLD

26666

0.41

2507

0.04

6042

0.06

NRA

60707

0.94

70

0.00

3459

0.03

PONA

18155

0.28

11731

0.17

PPT-MAENDELEO

13532

0.13

SAU

6041

0.06

TADEA

76636

1.19

9647

0.14

6904

0.06

TLP

27963

0.43

652504

9.19

305061

2.82

TPP

15335

0.24

10206

0.14

UDP

213547

3.32

315303

4.44

154809

1.43

UMD

41257

0.64

7550

0.11

1501

0.01

UPDP

19841

0.31

14789

0.21

6462

0.06

Jumla Upinzani

2626707

40.78

2471509

34.81

3205578

29.63

JUMLA

6440913

100.00

7099636

100.00

10819094

100.00

JEDWALI 2: IDADI YA VITI VYA BUNGE VYA KILA CHAMA KATIKA CHAGUZI TATU

1995

2000

2005

CCM

186

202

206

CHADEMA

3

4

5

CUF

24

17

19

NCCR-MAGEUZI

16

1

0

TLP

0

4

1

UDP

3

3

1

Jumla Upinzani

46

29

26

Jumla

232

231

232

JEDWALI 3: IDADI YA VITI VYA BUNGE VYA KILA CHAMA KATIKA CHAGUZI TATU TANZANIA BARA

1995

2000

2005

CCM

160

167

175

CHADEMA

3

4

5

CUF

0

2

0

NCCR-MAGEUZI

16

1

0

TLP

0

4

1

UDP

3

3

1

Jumla Upinzani

22

14

7

Jumla

182

181

182

JEDWALI 4: IDADI YA KURA ZA WAGOMBEA URAIS WA KILA CHAMA KATIKA CHAGUZI TATU

1995

2000

2005

Idadi ya kura

Asilimia

Idadi ya kura

Asilimia

Idadi ya kura

Asilimia

CCM

4026422

61.82

5863201

71.74

9123952

80.28

CHADEMA

668756

5.88

CUF

418973

6.43

1329077

16.26

1327125

11.68

DP

31083

0.27

MAKINI

17070

0.15

NCCR-MAGEUZI

1808616

27.77

55819

0.49

NLD

21574

0.19

PPT – Maendeleo

18783

0.17

SAU

16414

0.14

TLP

637115

7.80

84901

0.75

UDP

258734

3.97

342891

4.20

Jumla Upinzani

2486323

38.18

2309083

28.26

2241525

19.72

Jumla

6512745

100.00

8172284

100.00

11365477

100.00

Leave a comment