Mauaji ya 2001: Ujio wa Mfumo wa Vyama Vingi

SURA YA TATU

MAJIO YA MFUMO WA LEO WA VYAMA VINGI, TANZANIA

Mfumo wa leo wa siasa za vyama vingi ulipokewa kwa hisia tafauti.  Wakati vyama vya upinzamo kwa uchanga na uzoefu wao mdogo vikitumia mazingira magumu kujiimarisha, CCM chama chenye uzoefu wa miaka 40 ya siasa kilijizatiti kuhakikisha kwamba vyama vya upinzani haviimariki na kujitangaza.  CCM ilitumia mbinu nyingi za kuupaka matope upinzani kwa jamii.  Kwa msaada mkubwa wa vyombo vya dola na vile vya habari vinavyomilikiwa na Serikali na hata baadhi ya vile vya taasisi binafsi vilijitahidi kumwaha propaganda ya kuwatisha na yakitekelezwa kwa kasi, vyombo vya ukandamizaji vya dola hasa jeshi la polisi, usalama wa Taifa, KMKM vilikuwa vikisaidiana ‘kutesa kwa zamu’ na kuendeleza unyanyasaji wa wafuasi wa upinzani.  Hivyo ilichukuwa muda kwa wananchi kuamino usalama wao ndani ya upinzani.  Leo, zipo hoja zinazotagulizwa na wachambuzi wa mambo ya siasa kwamba mfumo huu ulipokelewa vibaya na wafuasi wa upinzani na hivyo kusababisha kasoro nyingi katika uendelezaji wa demokrasia.  Ukweli ni kwamba mfumo huu haukupokelewa vibaya na wananchi, isipokuwa uliletwa vibaya na Serikali.

Sehemu ya 1: Kupokelewa kwa Mfumo wa vyama vingi

Ulipovuma upepo wa mabadiliko ya mfumo wa siasa duniani na kuzusha wimbi lililoikumba Afrika, Tanzania kwa kuwa si kisiwa kilichojitenga na ulimwengu, nayo ililazimika kuwemo ndani ya mkondo wa mabadiliko.  Hali hii ilizifanya nchi nyingi za Afrika na zile za Ulaya Mashariki kutoka katika mfumo wa siasa ya chama kimoja na kuingia katika mfumo wa siasa za vyama vingi.

Ilikuwa mwaka 1992 ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania iliunda Tume kuratibu maoni y a Watanzania juu ya mfumo gani wa siasa ufuatwe Tanzania.  Tume hii iliongozwa na Jaji Mkuu mzoefu wa Tanzania, Fransis Nyalali.  Baada ya Tume kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi katika sehemu mbali mbali za nchi, ilipeleka ripoti yake Serikalini.  Tuliambiwa na Serikali katika ripoti hiyo kwamba, ingawaje ni asilimia ndogo tu ya Watanzania ndio iliyokubali mageuzi ya kutaka mfumo wa vyama vingi badala ya ule wa wakati ule wa chama kimoja, kwa huruma zake, Serikali iliona iwakubalie wachache hao na kwamba kukubali huku kwa Serikali kufuata mageuzi kulikuwa ni kwa “hiari na huruma tu” wala hakukutokana na shindikizo kutoka Mataifa ya Nje.  Maneno haya yalikuwa yakisemwa na wakuu wa Serikali na wa Chama cha Mapinduzi mara kwa mara, na kwa hivyo kuashiria tokea mwanzo kuwa iwapo Serikali haikubali kuwa uhalisi wa mabadiliko ya mazingira nje na ndani ndio sababu ya mageuzi basi bila shaka mfumo huu utakuwa umeletwa ‘shingo pegani na Serikali’.  Hivyo, mwanzo wa safari ya kuelekea demokrasia ya kweli ulifanywa uwe mgumu na hivyo hata safari yenyewe ni ya kusuasua.

Hoja hii ya “hiari na huruma” ni ya nguvu sana na pia inapingana na ukweli kwamba kuibuka tena na kushamiri kwa mfumo wa vyama vingi kwa nchi za Afrika na Ulaya Mashariki ni matokeo ya sababu za ndani na nje ya nchi hizo zilizolazimika bila hiari kuufuata.  Ama kwa upande wa hali ya ndani ya nchi hizo ni kwamba kulijidhihirisha wazi kuzorota kwa utekelezaji wa sera za uchumi na maendeleo ya jamii licha ya umilikaji wa nyenzo zote za uzalishaji mikononi mwa umma.  Na kwa upande wa nje, ushindi wa vita baridi kwa Mataifa ya Magharibi dhidi ya Mashariki yalipelekea kuporomoka kwa Umoja wa Mataifa ya Urusi (USSR) ambayo ilikuwa na ushawishi mkubwa kwa nchi nyingi za Mashariki na Afrika.

Matokeo ya sababu zote ni kuongezeka kwa mvuto na ushawishi wa sera na masharti ya vyombo vya kiuchumi vya Mashariki ndani ya malengo, mipango, sera na mikakati ya maendeleo kwa nchi za Mashariki na Afrika ikiwemo Tanzania.  Haikuwa hiari, ndio maana Tanzania haikuwa mstari wa mbele duniani kuanzisha na pengine kushawishi nchi nyengine zifuate mfumo huu kama ilivyofanya katika jitihada zake za kiukombozi.  Hali hii ilipelekea kiasi kikubwa cha fedha kutumika kuunda kamati za siri na dhahiri sio tu karatibu maoni ya watu juu ya mfumo upi ufuatwe bali hata kushawishi wananchi waukatae ili iwe ni kichecheo mbeleni na kisingizio cha uhalali wa kujenga hoja za kuzorotesha maendeleo ya demokrasia ya kweli nchini.  Matokeo ya kuzorota kwa hali ya kisiasa inayoendelea ni uthibitisho wa kwamba Tanzania iliukubali mfumo huu ‘shingo begani’.

Kwa hivyo majio yake yameufanya uonekane kama ni mfumo wa vyama vingi ulio maalum kwa Tanzania na unaonesha utafauti na nchi nyengine katika maadili na misingi ya uendeshaji na usimamizi wake.  Shabaha ya yote ni kufanya mazingira yake yaonekane kwamba uchanga wa mfumo huu unahitaji muda zaidi kuzoeleka na kufahamika hasa kwa wanaokusudia kujiunga na upinzani.  Ama kwa maana nyengine ilikusudiwa ionekane kwamba kwa wale asilimia kubwa waliotangazwa kuupinga, wao wana ufahamu bora na wamehitimu zaidi nadharia na uzoefu wa mfumo huu na kwamba walifahamu matatizo yake ndio maana wakaukataa.  Hata hivyo, haikuelezwa na Serikali iwapo mazingira yetu yalikuwa kipingamizi kikubwa mno cha ustawishaji wa mfumo huu basi kuanzishwa kwake katika muda huu kulikuwa kwa faida ya nani! Maoni ya kuuza uhalisi wa sababu na mazingira ya majio mfumo wa vyama yalitumiwa zaidi na Serkali na vyombo kandamizi vya dola ingawa kidogo kidogo wadadisi na wachunguzi wa hali ya siasa walianza japo si kwa kasi kuwaelimisha watu uhalisi wa mambo.

Kutokana na kasoro hizo za Serikali ambayo ndio msimamizi mkuu wa mfumo wenyewe, basi majio ya mfumo wa mpya wa siasa haukutilia maanani hata kidogo umuhimu wa elimu na taaluma ya kuhusu haki za kiraia.  Hali ya ukosefu wa taaluma wa maarifa kuhusu haki za kiraia ilikuwa mbaya zaidi katika miaka yote 30 ya mfumo wa ukiritimbo wa chama kimoja.  Mjadala juu ya mambo ya haki za kiraia ulizusha woga na hata kwa baadhi ya watu kufikiria ni kitendo cha dhambi kubwa.  Kutokana na hali hiyo basi, mijadala juu ya mfumo upi wa siasa ufuatwe uliwakuta watu wengi wakitoa maoni yasiozingatia ufahamu wa mfumo mpya wa siasa.  Zaidi ya hayo, maoni yalikumbwa na kasoro kubwa ya uwazi miongoni mwa watoa maoni ili kupata matokeo yatakayosaidia kujenga hoja na uhalali wa kuendelea kupendwa kwa mfumo wa cham kimoja ili kuiburuza na kuilemaza demokrasia ya vyama vingi.

Ingawa si kosa, kama kuna nia njema, kwa Serikali kufanya huruma kwa wananchi wake lakini baya ni kwa Serikali yenyewe kuitumia huruma hiyo kuuficha ukweli na uhalisi wa mambo hata pale ambapo yako wazi.  Ndio maana hata kama tutachukulia kuwa ilikuwa ni hiari na huruma kama Serikali ilivyodai basi pia ni lazima tujuwe kwamba hakuna kitu kibaya zaidi kwa waungwana wanaojithamini kama kwenda kinyume na mambo waliyoyakubali wenyewe, au kufanya vitendo ambavyo vitadhihirisha kupingana na maamuzi yao waliyokubaliana nayo na kuyatangaza huku umma ukishuhudia na dunia ikisikia.  Kufanya hivyo, waswahili wanaita, “kutia ulimi puani”, jambo ambalo huwaondolea wafanyai hivyo ile sifa na heshima ya uungawa waliokuwa wakifikiriwa na wengine kuwa wanao.

Pamoja na CCM kutoa wito wa kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, kwa maneno ya hekima ya wahenga wa zamani inaonesha ni kweli kuwa, “cha mfu hufa, na cha nchami huchama” wakiwa na maana kuwa kila amali aliyokuwanayo mtu katika uhaii wake huondoka wakati akifa, na kila kitu anachokimiliki mtu pahala alipo huondoka nacho wakati akihama.  Katika kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere aliyoitoa mbele ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, mwaka 1992 alisema, “hata wapinzani wakitoka ndani ya CCM ni haki yao, na wasionekane maadui wa Taifa hili”.  Haijulikani iwapo warithi wa siasa wa CCM waliipokea kauli hii kwa utii au waliitikia kwa unafiki tu!.

Hatua ya kuanzishwa kwa mfumo wa siasa ya vyama vingi Tanzania ilikuwa ni uamuzi wa busara kwani ndani ya mfumo huu hupatikana ushindani wa fikra, mawazo na hatimae sera na taratibu mbadala za kuongoza nchi kwa misingi madhubuti ya demokrasia yenye kuheshimu utu na kulinda haki za binaadamu.  Hali hio huleta msukumo katika harakati za kimaendeleo, ustawi wa maisha na kundosha umaskini ingawa kuzidisha umoja wa haki kwa watu.  Zaidi, tulidhani kutokana na mchango wetu katika harakari za kusaidia kuondosha udhalimu na ukandamizaji wa kikoloni kwa nchi ambazo zilichelewa kujitawala.

Mbele ya nchi kama hizo, Tanzania ilionekana kama ni chuo cha siasa za kiukombozi dhidi ya manyanyaso ya Wakoloni ambapo matokeo ilikuwa ni kupatikana kwa uhuru wa Angola, Msumbiji, Zimbabwe, Mauritius na Afrikaya Kusini, kwa kutaja baadhi.  Kwa hivyo basi, kwa dhana hiii ya kupevuka kwake kisiasa, Tanzania ilichukuliwa kama kwamba mfumo huu wa demokrasia ya vyama vingi umefika kwao.  Hata hivyo, kinyume na matarajio ya wengi, mfumo wa vyama ulianza na umekuwa ukikua sambamba na kushamiri kwa vitendo vya ukandamizaji, unyanyasaji na hatimae mauwaji ya raia wasio hatia.  Chaguzi na mabadilishano ya madaraka ambayo ni vipimo vikubwa vya ustawi wa demokrasia ndio kwanza vinaendelea kuwa vikwazo vya kuheshimu haki za binaadamu vinavyoendeleza kebehi ya utawala wa sheria pamoja na kudumaza demokrasia na maendeleo.

Sehemu ya 2: Kigeugeu cha Serkali katika Mfumo wa vyama vingi

Baada ya Serikali kusema imewafanyia huruma wachache waliokubali mfumo mpya wa siasa Watanzania hatukufikiria kuwa Serikali ingewacha ile tabia njema ya kuwahuruma wananchi wake na badala yake ikaanzisha ukatili kwa kuwanyanyasa.  Serikali ilizidi kuwajengea chuko na uhasama kwa wananchi ili wawaone wapinzani kama vile ni maaadui, hawana haki na zaidi hawastahiki kupewa dhamana ya uongozi katika nchi yao.  Zaidi ni kuwa utawala wa CCM umejenga dhana miongoni mwa baadhi ya viongozi na watendaji wa vyombo vya Serikali kwamba viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani ni watu waliopotoka na kupotea na kwamba siasa safi imo ndani ya CCM tu.  Hisia hizi sio tu zimezidisha chuki ndani ya jamii, lakini pia imepunguza kasi ya mashirikiano miongoni mwa raia wanaoangalia kwa hofu na kuogopa hali ambayo mwishowe hupunguza kasi ya maendeleo.

La kushangaz ni kule kuona kuwa, pamoja na kukubali wenyewe mfumo wa siasa ya demokrasia ya vyama vingi, CCM bado kabisa wana mawazo na mzubao wa mfumo wa chama kimoja (mono – party hangover) ya kwamba chama ndicho chenye kauli na nguvu za mwisho, “party supremacy” katika maendesho ya nchi.  Kutokana na kujenga dhana na hisia hizi Serikali imekuwa ikiendelea kufanya vitendo vinavyopingana kabisa na kauli ya kukubali mfumo wa mageuzi.  Chamungwana (1994), katika kuelezea uhondo wa mawazo ya chama kimoja anasema, “watu wale wale ndio wanaopitisha sera, wale wale ndio wanazipeleka katika bunge la chama kimoja na kutoa amri zipitishwe kama sheria na baada ya hapo ni watu wale wale ndio wanaokwenda kwa watendaji ili kusimamia zitekelezwe”.  CCM kwa kutumia mbinu mbali mbali ili kuhakikisha upinzani ni finyu katika bunge maana yake ni kutaka kuendelea na mazoea haya ambayo hayatoi hatma nora kwa uhai na umadhubuti wa ushindani katika siasa.  Kwa hivyo, fahari ya upinzani Tanzania imebaki kuwa na Mabunge yenye sura ya upinzani usioweza kuzuia sheria ambazo hutungwa kwa ajili ya maslahi ya watawala kuliko yale ya Taifa.

Kilichodhihirika tokea kusajiliwa vyama vya upinzani kwa hivyo, ni ule ubabu wa chama kimoja unaofanywa na viongozi wa chama tawala, CCM na wafuasi wake dhidi ya vyama na wafuasi wa upinzani badala ya kuonesha ustaarabu wa demokrasia ya kweli.  Hali hii imesababisha mageuzi ya kisiasa Tanzania kuwa na mazingira machafu, yalioambatana na madhila, mateso na unyanyasaji kwa wananchi wanaoonekana tu wana maoni ya kiupinzani.  Haya yakitokea utawala uliolelewa katika fikra za chama kimoja unazidi kujizatiti kukaa madarakani kwa hila na wakati mwengine mabavu, hata kama kufanya hivyo kutaondosha raia wasio hatia duniani.  Fedha nyingi hutumiwa na Serikali katika kuhuisha chama tawala huku uchumi ukizorota.  Kwa kuwa unyanyasaji unahitaji kutumia vyombo vya dola, hivi vimetumika sana kuzuia maendeleo ya siasa na wakati wote vimekuwa ndio chanzo cha maafa kwa raia.  Taratibu za ubadilishanaji wa madaraka kwa njia za kiungwana (conventional method of handing over power to others) zinaendelea kutoheshimiwa.  Hali hii yaufanya mfumo wa vyama vingi bado kuwa katika kiza kizito Tanzania.

Sehemu ya 3: Taswira ya CCM na Dola kwa Wapinani

Pamoja na kuwapotosha watu wasiunge mkono upinzani, pia viongozi na makada wa CCM wakisaidiwa na vyombo vya dola na vile vya habari (hasa vya Serikali) walijenga hofu kwa wananchi wawaone na kuwahesabu wapinzani kama watayarishaji wa fujo  na vita.  Kwa mfano TV Zanzibar ilikuwa ikihofisha upinzani mbele ya umma kwa kuonesha kanda za video za vita vya wenyewe kwa wenyewe kama vile vya nchi za Rwanda na Burundi.  Kwa mkakati wao huo, watawala wamekuwa wakijenfa hofu kwamba wapinzani ni watu wakutengwa na kuogopwa.  Hii ndio maana ubaya wa mpinzani humaliza mara tu akikubali kushawishiwa na kurejea au kujiunga na CCM.  Mpinzani yule yule ambae jana alikuwa mbaya mara tu anapojiunga na CCM hung’ara na kusifiwa kuliko mwanachama yeyote.  Iko mifano ya viongozi wa upinzani kama vile Dr. Masumbuko Lamwai (alietoka NCCR), Chifu Abdalla Fundikira na Abbas Mtevu ambao mara tu waliporejea CCM ubaya waliokuwa nao uligeuka na kuwa  sifa za kuaminika kiasi cha kupewa dhamana za Ubunge kupitia Chama walichowakikilani muda mfupi kabla ya kuhamia.

Kwa bahati mbaya, ufahamu mdogo wa watu juu ya masuala ya siasa na maendeleo ndio unaotumiwa na Serikali kwa uwezo wake wa kumiliki vyombo vya habari na mtandao wa utawala ili kuwazidishia watu upotofu kuhusu vyama vingi.  Halikadhalika, wataalamu wanaoipendelea na kuitumikia CCM hawaelezi kwamba ni ufahamu mdogo huu huu ndio uliopelekea watu wengi kuhiari kubakia katika mfumo wa chama kimoja hata kama dunia na watawala wanalazimika kugeuka.  Baadahi ya wataalamu wa siasa wamekuwa wakitoa maoni kwamba ufahamu mdogo katika jamii umekuwa ukiathiri zaidi upinzani tu, na sio vyengine.  Hii ndio maana popote ambapo pametokea hitilafu katika utekelezaji wa demokrasia, ni wapinzani ndio ambae wamekuwa wakihusishwa moja kwa moja.  Hali hii sio tu kwamba imekuwa ikiviza upinzani, lakini pia imekuwa ikiongeza matatizo na mizozo kwa suluhisho la kudumu.  Zaidi ya yote, ilijitokeza wazi kuwa wataalamu na wadadisi wengi wa masuala ya siasa walipendelea kutumia kalamu zao kuisifu CCM na kuuponda upinzani.  Hivyo, hili pia lilipunguza kiwango cha ukuaji uwelewa wa mfumo.  Kwa hivyo, kutoeleweka kwa mfumo kulikuweko lakini pia kuliongezwa kwa matumizi mabaya ya vyombo vya dola, vyombo vya habari vya serikali pamoja na wataalamu.

Sehemu ya 4: Kusakamwa Wapinzani

Pamoja na wapinzani kunyimwa fursa na haki mbali mbali za uhuru wa kujumuila, pia chama tawala kimekuwa kikitumia vyombo vya serikali zake kuchafua mazingira ya ushindani ulio huru na wa haki huku vile vile, chama tawala kikisaidiwa kubuni na kupanga njama za kuwasakama wapinzani.  Hila na propaganda za vyombo hivyo hufanywa mpaka kufikia pahala pa kupendekeza kufutwa kwa vyama vya upinzani.  Muda na fedha zinazotumika kwa mikakati wa aina hii hugharimu sana maendeleo ya nchi.  Makali ya umasikini yanayoongezeka siku hadi siku yamechangiwa na sababu hizi.  Kwa kweli umasikini huongezeka mara tu baada ya chaguzi kutokana na fedha nyingi zinazotumika kiholela ili kuwashawishi wananchi wairejeshe Serikali ambayo siku zote huwa na hofu ya kushindwa.  Hofu hii hutokana na ukweli kwamba katika miaka mitano iliyopita wananchi hawaoni mabadiliko ya matatizo yao ambayo Serikali huahidi kuyashughulikia baada ya kuchaguliwa.  Katika kila hali, ili Serikali ijihakikishie kurudi madarakani, haina budi kuzidisha kasi za shutma kama sehemu ya mkakati.  Baadhi ya shutuma nzito ambazo zimekuwa zikielekezwa kwa CUF ni kama zifuatazo:

?          CUF ni Chama cha Ukabila

?          CUF ni chama cha Udini

?          CUF inataka kuvunja Muungano

?          CUF inataka kuleta vita vya wenyewe kwa wenyewe

?          CUF ni chama cha vibaraka wa Mataifa ya nje

?          CUF inataka kurejesha utawala wa Kisultani Zanzibar

?          CUF ni chama cha Wapemba

?          CUF pia sasa ni chama cha Magaidi, n.k

Wakati vyoombo vingine vya dola hufanya propaganda, na hila mbali mbali huku vingine hasa Polisi na Usalama wa Taifa vikiwa na kandarasi ya kuhakikisha kuwa upinznia unasambaratika kwa kufanya juhudi kuzuia vyama vya upinzani kufanya mikutano na kutembeza mkong’oto kwa wale wasiotii.  Sambamba na yote hayo yanayofanywa na CCM dhidi ya vyama vya upinzani kwa nia ya kuwa visambaratike, migogoro ndani ya vyama vya upinzani ulipandikizwa tena kwa kutumia fedha nyingi kuwanunua viongozi wa vyama vya upinzani.  Utashangaa unapomuona kiongozi wa chama cha upinzani anaetoa madhambi na shutma nzito kwa Serikali na CCM lakini mara tu anaponunuliwa kwa tama za kibinafsi huvigeuka vyama vya upinzani kwa matusi bila aibu.  Mara nyengine anaenunuliwa akishitukiwa na kufukuzwa kwa mujibu wa Katiba za Vyama vyao, CCM hugeuka kwenye vyombo vya Sheria na hata vya kutunga sheria ili kumlinda na eti kumrejeshea ile wanayoiita haki yake.

Kimsingi, chombo cha sheria ni cha kufanya haki, lakini hutumiwa na CCM na Serikali zake kupinga haki bila aibu.  Mahkama zimeifedhahesha sana Tanzania kwa hili.  Mfano hai ni ule wa Naila Majid ambae alikuwa Mbunge wa viti maalum vya upendeleo wa wanawake kwa tiketi ya CUF.  Baada ya CUF kubaini kuwa Mbunge huyo anakwenda kinyume na maadili ya Katiba ya chama hicho Mkutano Mkuu uliamua kumuengua Kikatiba, lakini kwa kuwa CCM ndiyo waliompandikiza kuwatumikia akiwa ndani ya CUF, waliiamuru Serikali kupitia Spika  wa Bunge la Jamhri ya Muungano kumbakisha na kumlipa akiwa Mbunge hewa.  Huu ni mkakati unaotumiwa na CCM hadi leo na wengi wetu hushangaa sana vyombo ya kutunga sheria hapa nchi vinaposhutumu wafanyakazi hewa huku wakati vyombo wenyewe vinashadidia wanasiasa hewa.

Kashfa hizi ambazo zimekuwa zikielekezwa kwa CUF ni kubwa sana lakini kwa vile zinafanywa na Waafrika kuwatendea Waafrika wenzao, basi hii huonekana ni jambo dogo linalokubalika katika nchi na pengine hata linalovumilika mbele ya mabwana wa mfumo wa vyama vingi ambao  mi Mataifa ya Magharibi na Jumuiya za Kimataifa.  Hata hivyo, Waswahili wanasema wimbo mbaya haimbiwi motto, na vivyo hivyo jina baya hapewi motto.  Majina hayo yaliyonasibishwa na CUF hayakuivuruga, lakini kufanya hivyo, Serikali iliibua siasa za zamani na ingawa vijana wengi leo hawazikumbatii kwa kuwa hawazifahamu lakini CCM imekuwa ni darasa la kuwakumbusha yaliyopita.  Huku mambo ya kale yakiamshwa kitaalamu, wataalamu hao hao wanatumia kalamu kuupotosha ulimwengu kuwa Zanzibar haiwezi kurekebisha matatizo yake kutokana na siasa za zamani.  Hivi kwa muhtasari ndivyo mazingira ya vyama vingi yalivyoanzishwa na kukuzwa, na hapana shaka, hakuna aliyetarajia kuwa haki na usawa vingetawala katika chaguzi kuanzia ule wa 1995 hadi wa 2000 zilirusha cheche zilizozaa moto tarehe 26 na 27 Januari, 2001.

SURA YA NNE

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s