CUF Wawakilishi

WAWAKILISHI WAIONYA CCM KUIGAWA Z’BAR

Mwakilishi wa Jimbo la Mkanyageni, Haji Faki Shaali (CUF), alisema anazo taarifa kuhusu mpango wa CCM wa kutafuta ushindi katika uchaguzi ujao kwa kupunguza idadi ya watu waliofikia umri wa kuandikishwa katika daftari la wapiga kura kunyimwa haki hiyo. Alisema viongozi wa serikali lazima waheshimu viapo wanavyokula kwa vile kitendo hicho kinakwenda kinyume cha kifungu cha pili cha katiba ya mwaka 1984, ambayo inatoa haki kwa kila Mzanzibari mwenye umri, kuanzia miaka 18 kuwa na haki ya kushiriki uchaguzi mkuu. Endelea kusoma habari hii…

MSIMAMO WA CUF: MAFUTA SI YA MUUNGANO

ZAKIA OMAR JUMA

ZAKIA OMAR JUMA

“…Suala la mafuta si suala la Muungano, kwanza. Na katika masuala haya, Articles of Union ni International Agreement ambayo kiilivyo Mkataba huu ni mkubwa kuliko hiyo Katiba ya Jamhuri ambayo imeambiwa isitiwe mkono au katiba nyengine yoyote katika nchi husika kwa ule Mkataba wake. Kwa hivyo, ninaamini kabisa ingelikuwa ni vyema ukaangaliwa ule Mkataba – ambao bado unawekwa siri, sijui kwa sababu zipi – akapewa huyo mshauri, akajuwa kwamba hayo mambo yenyewe yakoje katika suala hili, ili akaona kazi yake inarahisika vipi. ..” ZAKIA OMAR JUMA – CUF NAFASI MAALUM

KUVITUMIA VIKOSI KISIASA KUTAVUNJA AMANI YA NCHI HII

Hivi ndivyo SMZ inavyovitumia vikosi vyake, kufanya unyanyasaji dhidi ya raia wasio hatia. CUF inaonya kuwa kuna siku raia hawa watachoka na kuamua kupambana na vikosi hivi

Hivi ndivyo SMZ inavyovitumia vikosi vyake kufanya unyanyasaji dhidi ya raia wasio hatia. CUF inaonya kuwa kuna siku raia hawa watachoka na kuamua kupambana na vikosi hivi

“Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani na wananchi kwa ujumla, naomba niitumie fursa hii kuihadharisha SMZ kwa mara nyengine tena iache mara moja mpango wake huo  kwani sio tu unaidhalilisha demokrasia . lakini pia ni hatari, sio tu kwa wananchi wa jimbo la Chonga pekee lakini ni kwa Zanzibar nzima. Mimi, na kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, siko tayari hata siku moja kuona pesa za walipa kodi wa nchi hii zinateketezwa kwa kurundika vijana wa maskani katika makambi haya kwa ajili ya kuipigia kura CCM na kwa mantiki hiyo ni vyema tukaziba ufa kabla hatujalazimika kujenga ukuta.” – Abdallah Juma Abdallah (MBLW), Msemaji wa Upinzani kuhusu Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ

SMZ INAPOBAGUA HADI KWENYE MATIBABU

Rashid Seif Suleiman, Mwakilishi wa Ziwani (CUF)

Rashid Seif Suleiman, Mwakilishi wa Ziwani (CUF)

“Wakati wagonjwa wote waliohudumiwa na hospitali 7 hizi hadi kufikia Machi 2008 ni  84,661, Pemba ambayo ilihudumia wagonjwa 70,066 ambayo ni asilimia 83% ya wagonjwa wote, ilipangiwa kutumia milioni 84 na zile hospitali 2 za Unguja ambazo zilihudumia wagonjwa 14,595 asilimia 17% ya wagonjwa wote ilipangiwa milioni 196 zaidi ya mara mbili ya ile ya Pemba.” Rashid Seif Suleiman, Msemaji wa Upinzani barazani kuhusu Afya na Ustawi wa Jamii

KUNA HARUFU KALI YA UFISADI KWENYE SMZ

Said Ali Mbarouk, Mwakilishi wa Gando (CUF)

Said Ali Mbarouk, Mwakilishi wa Gando (CUF)

“Ni kwa vipi Wizara hii ilizembea au niulize kulikuwa na ufisadi katika shughuli nzima wa mkataba na Prismo hata Prismo akapata nafasi ya kuvunja mkataba? Kwa sababu  hiyo, naomba  Tume ya Baraza lako iundwe kuchunguza  utaratibu wa usimamizi wa zabuni  katika Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, na Tume ijikite katika zabuni za Uwanja wa Ndege na Kampuni ya Kichina, zabuni ya  Gati ya Malindi na Kampuni ya Phil na zabuni ya Barabara  ya Mazizini – Fumba, Amani – Dunga, Mfenesini – Bumbwini na Kampuni ya Prismo.” – Said Ali Mbarouk (MBLW), Msemaji wa Upinzani barazani kuhusu Mawasiliano na Uchukuzi

VIJANA WA JUA KALI HAWAKUTENDEWA HAKI

Aziza Nabahan, Mwakilishi wa CUF

Aziza Nabahan, Mwakilishi wa CUF

“Kitendo cha Serikali kuwahamisha (vijana wa Jua Kali) bila ya kukamilisha majenzi katika sehemu hizo za Saateni, hakikubaliki licha ya kuwa ni kitendo cha ajabu na aibu kufanywa na Serikali inayojinadi kwa kuwa na utawala wa sheria na utawala bora. Haiwezekani hata kidogo umma wote wa Jua Kali upangiwe sehemu ndogo kama ile banda moja la Saateni. Kumbe kama Serikali ingekuwa na nia njema ingeweza tu kuwapatia viwanja hivyo ili wajijengee wenyewe. Hata hivyo, kama kawaida inasikitisha kuwa viwanja vingi vimechukuliwa na baadhi ya watu wenye uwezo kwa maslahi yao ya kibinafsi kuliko kuzingatia jamii inayoisaidia Serikali katika vita dhidi ya umasikini. Baada ya hayo, kinachoshuhudiwa ni matumizi ya nguvu yanayofanywa na askari wa Manispaa katika kuwahamisha. Hii si njia nzuri hata kidogo na zaidi ni njia ya vitisho ambayo kwa kawaida haitumiwi na Serikali inayojinadi kwa demokrasia.” – Aziza Nabahan (MBLW), Msemaji wa Upinzani barazani kuhusu Vijana, Wanawake na Watoto

SMZ IMEUPUUZA MKARAFUU

Muhiddin Mohammed Muhiddin, Mwakilishi wa Mtambile (CUF)

Muhiddin Mohammed Muhiddin, Mwakilishi wa Mtambile (CUF)

“Mkarafuu unakabiliwa na hatari ya kupotea kutokana na matatizo yanayoukabili ikiwa hatua za haraka za kuhami hazikuchukuliwa. Lakini kwa bahati mbaya Serikali bado inafanya utani juu ya kuliokoa zao la karafuu. Hivyo ni kweli kama serikali imekusudia kuuhami mkarafuu ingetenga shs 40 milioni kwa mradi wa kuimarisha mikarafuu, huu ni utani na serikali haistahiki kufanya utani na maendeleo ya Nchi.” Muhiddin Mohammed (MBLW), Msemaji Mkuu wa Upinzani barazani kuhusu Utalii, Biashara na Uwekezaji

BADO SMZ INACHEZA NA HAKI ZA WATU

Haji Faki Shaali, Mwakilishi wa Mkanyageni (CUF)

“…bado vyombo vya dola havijajirekebisha ipasavyo, kwani bado Polisi inaendelea na utamaduni wa kukamata watu na kuwaweka kizuizini muda mrefu bila kuwapeleka Mahkamani. Pamoja na Mheshimiwa Waziri kutueleza kwamba Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka  imeanza hatua ya kukamilisha lengo la kuimarisha mfumo wa Uendeshaji Mashtaka kwa utaratibu wa kukamilisha Upelelezi  kabla ya kufungua Mashtaka na kwamba mwezi Machi mwaka huu imekutana na wahusika wa upelelezi kukamilisha azma hii, matendo hayaonyeshi mabadiliko makubwa.” – Haji Faki Shaali (MBLW), Msemaji wa Upinzani barazani kuhusu Katiba na Utawala Bora

Advertisements