Ilani ya Cha Chama Cha Wananchi CUF, juu ya upatikanaji wa Maji safi na Salama kwa Wananchi wa Zanzibar

UPATIKANAJI WA MAJI SAFI
Tatizo la upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama limeendelea kuathiri maeneo mengi ya visiwa vyetu. Wananchi wanalazimika kulipa Serikalini kupitia Mamlaka ya Maji ada za michango ya utoaji wa huduma ya maji lakini bado hawajaona tija ya michango hiyo wala huduma kuimarika.

a) Uvunaji mdogo wa maji ya mvua
Chanzo pekee cha upatikanaji wa maji safi Zanzibar ni maji ya ardhi (Groundwater). Tofauti na visiwa vingine vya ukanda huu, Zanzibar haina mito wala maziwa ya kuhifadhi maji ya juu. Tafiti mbali mbali zinaonyesha kuwa visiwa vya Zanzibar vinapoteza takriban asilimia 83% ya maji yote ya mvua ambayo huachiwa bila jitihada za kuyavuna, kutiririkia baharini.Mamlaka ya Maji (ZAWA) kwa sasa ina uwezo wa kuvuta kiasi cha wastani wa mita milioni 33 za ujazo kwa mwaka au sawa na asilimia 9% ya maji yote yanayoweza kufikiwa chini ya ardhi.

b) Uvutaji wa Maji Ardhi
Ni ukweli usiofichika kutokana na hali hii kuwa bado hatujaweza kuyavuna maji ya mvua kwa wingi ipasavyo, na kwamba bado hatujawa na miundombinu bora au teknolojia ya uhakika ya kuvuna na kuvuta maji ardhi ya kutosha tuliyo nayo kwa matumizi ya binadamu, kilimo, umwagiliaji, na maendeleo mengine.

c) Misaada, Sera Mbovu, na Ukosefu wa Haki ya Maji Safi na Salama
Pamoja na juhudi mbali mbali za washirika wa maendeleo wa kimataifa kama Finland, Umoja wa Ulaya, Japan, n.k. katika kuisadia Zanzibar kujikwamua kutokana na shida ya maji safi, bado suala la upatikanaji wa maji safi na ya uhakika kwa wananchi wengi wa visiwa hivi limekuwa ni jambo sugu lililokosa mpango kazi wa kweli wa kitaifa kulimaliza.
Serikali ya CCM imeshindwa kutumia fursa zilizopo za ndani na nje ya nchi kumaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na ya uhakika kutokana na sera zake mbovu na zilizopitwa na wakati za usimamizi endelevu wa sekta hii. Vipaumbele vya uwekezaji katika miundombinu vimewekwa kibiashara zaidi bila ya kujali uwiano wa jamii (Social Equity).Unyonge huu wa mwananchi wa Zanzibar hauwezi kuachwa kuendelea kama ulivyo na ni wajibu wa kila Mzanzibari kuhakikisha kuwa maji safi ni haki ya kila mtu.

d) Wawekezaji na Maji Safi kwa Wanavijiji
Wananchi wengi vijijini hususan katika kanda za Pwani za mashariki wamelazimika kuviacha visima vyao vinavyokabiliwa na tatizo la ukame na kuingia kwa maji ya chumvi na kutegemea maji yanayotolewa na wenye mahoteli. Shida kubwa hutokezea pale ambapo maji yanapofungwa au panapotokea suitafahamu kati ya wananchi na wenye mahoteli. Hakuna maji ya kutosha na vyanzo vya maji safi vilivyobaki kama visima na mapango ya maji hufungwa ili kuzuiwa watu kwenda kuchukua maji huko. Hali hii imezidi kuwatia unyonge wananchi wa vijijini na kujihisi kuwa hawana haki ya maji safi ndani ya nchi yao wenyewe.

e) Kamati za Maji na Uongozi Mbovu
Kamati za maji pia zinalalamikiwa kuwa hazitendi haki na hazifanyi kazi zake kwa njia za kidemokrasia. Siasa za kupendelea CCM zinaonekana kuongeza zaidi kamati hizi. Hakuna uwakilishi wa kweli kutoka kwa wananchi katika kutafuta ufumbuzi wa maji safi. Mamlaka ya ZAWA inalalamikiwa kutosikiliza vilio vya wananchi. Sheria au kanuni au sheria ndogo za huduma ya maji safi zipo katika kulinda maslahi ya wawekezaji zaidi kuliko kutafuta njia za kumaliza kabisa tatizo la ukosefu wa maji safi kwa jamii visiwani. Sekta ya maji safi Zanzibar inaonekana kuongozwa katika misingi ya faida na kusahau kabisa malengo ya Mapinduzi ya kuhakikisha kuwa maji safi ni haki ya kila Mzanzibari popote pale alipo, mjini na vijijini.

f) Ukosefu wa Maji Safi na Salama Mijini na Hatari ya Afya
Halikadhalika, mfumo wa usambazaji maji kutoka kwenye vyanzo vya maji umechakaa na kupelekea kiasi cha theluthi nzima ya maji yanayotoka kwenye vyanzo hivyo kupotea bure kutokana na tatizo la uvujaji ovyo wa mabomba. Ujenzi holela na uvujaji ovyo wa mabomba yanayosambaza maji safi mijini umepelekea kuathirika kwa sekta nzima ya maji katika maeneo hayo. Hatari ya maji safi kuchanganyika na maji machafu imekuwa ni jambo la kawaida kwa wakaazi wa maeneo mbali mbali ya mjini wakiwemo wale wanaoishi katika nyumba za maendeleo. Maradhi ya mripuko kama kipindupindu huja kwa sababu kuu moja nayo ni ukosefu wa maji safi na ya kutosha kwa matumizi ya binadamu.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF itatekeleza hatua zifuatazo:
 Tutahakikisha tatizo la upatikanaji na usambazaji wa huduma ya maji safi na salama, Mjini na vijijini, Unguja na Pemba, linamalizwa katika kipindi cha miaka mitano na linakuwa historia.

 Itaupitia upya muundo wa usimamizi, usambazaji, ugawaji na utoaji wa huduma za maji safi ikiwemo mfumo mzima wa kitaasisi inayohusika na huduma za maji safi.

 Itapitia upya upya muundo, malengo na operesheni za kamati za maji na kuhakikisha kuwa kamati hizi zipo kwa kuwahudumia wananchi na si kwa kuwabughudhi au kuwachonganisha kisiasa.

 Itaanzisha mfumo wa usimamizi shirikishi wa maliasili ya maji (Integrated Water Resources Management) katika uongozaji wa sekta nzima ya maji safi ikiwemo uhifadhi wa vyanzo vya maji safi.

 Itahakikisha kuwa haki ya huduma ya maji safi kwa wananchi kama ilivyoahidiwa na wawekezaji wa mahoteli (Corporate Social Responsibility) haichezewi na kwamba wananchi wanapata maji yao safi kama kawaida na bila ya madhila na kufungiwa kiholela.
 Itashughulikia mara moja na kwa vitendo mpango kazi wa kitaifa wa ujenzi wa miundombinu ya uvutaji, uhifadhi, na usambazaji maji safi na salama kwa wananchi wote, mijini na vijijini.

 Itashajiisha uwekezaji katika miundombinu ya huduma za maji safi, ikiwemo kupitia mifumo ya kodi, ushuru, na gharama nyingine zinazokwamisha mipango ya taifa ya kufanikisha upatikanaji wa maji mijini na vijijini.

 Itaendelea kushirikiana na washirika wa kimaendeleo wa kimataifa katika kusaidia Zanzibar kufikia lengo lake la uhakika wa maji safi.

 Italinda vianzio vya maji na kuzuia ujenzi unaoathiri vianzio vya maji.

 Itaweka mfumo wa usambazaji maji katika maeneo mapya yanayokusudiwa kwa makaazi kabla ya viwanja kugawiwa.

 Itajenga matangi ya maji katika maeneo mengi yenye matatizo ya maji ili kuhakikisha kuwa upatikanaji wa maji ni wa uhakika.

 Itaunda mpango kazi wa kitaifa wa kushajiisha wananchi kutumia mbinu za kisasa na bora za kuvuna maji ya mvua (Rain Water Harvesting).

 Itajenga maabara ya kisasa kwa ajili ya uchunguzi wa maji Unguja na Pemba ili kuhakikisha usambazaji wa maji kwa wananchi ni safi na salama.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s