Maalim Seif: Wananchi tuungane kutetea Maslahi ya Zanzibar

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewashauri wananchi kuweka mbele maslahi ya Zanzibar na kuacha kushabikia utashi wa kisiasa katika kutetea maslahi ya nchi na wananchi wake.

Akihutubia mkutano wa kampeni za Chama hicho katika viwanja vya Mkokotoni jimbo la Tumbatu, Maalim Seif amesema suala la uwepo wa Zanzibar na mamlaka yake sio la kulifanyia mchezo, na badala yake wananchi wanapaswa kuungana kuhakikisha kuwa maslahi ya Zanzibar yanalindwa baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Amesema katika kulinda maslahi ya Zanzibar, ni vyema wananchi hasa wapiga kura kupima sera za wagombea, ili kubaini sera zipi zinalenga kuikomboa Zanzibar, na kufanya maamuzi sahihi siku ya uchaguzi itakapofika.

Akizungumzia katiba inayopendekezwa, Maalim Seif amesema haijatoa mamlaka kwa Zanzibar kuendesha mambo yake ikiwa ni pamoja na kushughulikia suala la uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.

Amefahamisha kuwa mamlaka yote bado yako chini ya Serikali ya Muungano, na kwamba bila ya CUF kupewa ridhaa ya kuongoza nchi, Zanzibar itazidi kupoteza mamlaka yake na kuwepo uwezekano wa kugeuzwa kuwa Mkoa au sehemu ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Hivyo amewaomba Wazanzibari kukichagua Chama Cha CUF ili kiweze kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano, na hatimaye kupigania mamlaka kamili ya Zanzibar.

Aidha amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha kuwa huduma zote za msingi zikiwemo elimu na afya zinatolewa bila ya malipo katika ngazi zote.

Ameeleza kuwa iwapo atachauguliwa atawatumikia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote na kwamba wananchi wote watakuwa na fursa sawa katika upatikanaji wa huduma hizo.

Amesema chini ya uongozi wake sekta ya elimu itapewa kipaumbele katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ili kuufanya Mkoa huo kwenda sambamba na Mikoa mengine ya Zanzibar.

Amesema kwa kipindi kirefu Mkoa huo umekuwa ukishikilia nafasi za mwisho katika mitihani ya kitaifa, jambo ambalo amesema atalifanyia kazi ili kuondokana na sifa hiyo ambayo haiendani na historia na hadhi ya Mkoa huo.

Nae kada wa Chama hicho Dkt. Mwana Omar amewashauri wananchi wa vijijini kutofanya makosa katika uchaguzi mkuu ujao, kwa kuchagua viongozi wenye mwelekeo wa kuikwamua Zanzibar na kuleta ustawi wa wananchi.

Dkt. Mwana ambaye alikuwa daktari wa masuala ya wanawake katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, amesema wananchi wengi wa vijijini hasa akinamama wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa wanapopatwa na matatizo ya afya, na kwamba wakati umefika wa kufanya mabadiliko.

“Wanawake wa vijijini wamekuwa wakipata usumbufu mara dufu ikilinganishwa na wale wanaoishi mjini, kwani wao hasa wale wanaotoka visiwani kama vile Tumbatu hulazimika kusafiri kwa vidau kwenda hospitali za Wilaya ambako inaposhindikana kupatiwa matibabu hutakiwa kuchangia mafuta kwenye gari ya kuhudumia wagonjwa (ambulance) hadi hospitali kuu ya Mnazimmoja”, alisema Dkt. Mwana na kuongeza,
“Na wanapofika huko bado huduma wanazopatiwa hazitoshelezi na baadhi yao hupoteza maisha kwa kukosa huduma zinazostahiki”, alieleza.

Imeandikwa na Hassan Hamad, OMKR.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s