Ilani ya Chama Cha Wananchi CUF, Katika kukuza Biashara Kwa Kuondosha Urasimu na Kupunguza Viwango vya Ushuru na Kodi

Zanzibar ni nchi ya Visiwa vidogo na hivyo ina changamoto nyingi za kiuchumi na kimaendeleo. Udogo wa ardhi yake, kuzungukwa kwake na bahari, matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi na kuongezeka kwa kina cha bahari, pamoja na changamoto na athari za kimazingira kwa uchumi na jamii yake kunaleta haja kubwa na ya haraka ya mapinduzi ya kiuchumi na kimaendeleo kwa jamii yake nzima katika kupambana na unyonge na umaskini unaowakabili na kuelekea katika taifa lenye hadhi ya uchumi wa kati. CUF inaamini kuwa njia pekee ya kuitoa Zanzibar katika janga la unyonge na umaskini na kubadilisha hali ya maisha ya watu ni kuitumia neema tuliyopewa ya kijiografia, maliasili na kihistoria kuigeuza Zanzibar kuwa kituo kikuu cha kibiashara cha Afrika ya Mashariki na Magharibi ya Bahari ya Hindi.

Neema hii ipo katika sekta ya uagizishaji, uwekezaji katika maliasili za pwani na baharini kama utalii na uvuvi, miundombinu ya sekta mpya ya mafuta na gesi, bandari huru, na mabenki. Yote haya yatafanikiwa pale tutakapoweza kwa kauli moja kuitoa Zanzibar ndani ya sera zilizofeli za “kusawazisha uchumi” kwa jina la Muungano na kuifanya ipumue na sera zake wenyewe ndani ya Muungano wa Haki, Heshima na Usawa. Dira ya mabadiliko ya CUF ni kuhakikisha kuwa Zanzibar inarejesha haki yake ya maamuzi katika ushuru, kodi na mapato.

Usawazishaji wa kodi uliofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mwaka 1999, pamoja na kuipunguzia sana mapato SMZ umeathiri vibaya sana ajira na mapato ya watu wengi wanaotegemea bandari na biashara kwa mapato yao. Hatuonekani kuwajali maelfu ya watu hao wanaojiajiri na kuipatia mapato makubwa serikali. Hata baada ya Usawazishaji huo wa kodi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano inabagua bidhaa zinazopitia Zanzibar kwenda Tanzania Bara kwa kuziwekea vikwazo kwa kuzitoza kodi na ushuru mara mbili na kuacha huru zile zinazotoka Tanzania Bara kuja Zanzibar. Pia kunaonekana wazi kuwa kuna nia ya kuiua bandari ya Zanzibar na kuangusha uchumi wake ili Zanzibar ishindwe kujitegemea.

Halikadhalika, utitiri wa kodi unazifanya bidhaa zipitazo Zanzibar kuwa na bei kubwa na zisiuzike katika soko la nje.
Kwa kufuata mfumo wa uchumi wa soko huria, Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF itachukua hatua zifuatazo:

Itairudisha Zanzibar katika hadhi yake ya kuwa kituo kikuu cha biashara na huduma katika eneo lote la Afrika Mashariki kwa kutekeleza sera zitakazoweka mazingira mazuri na yanayovutia ya kufanyia biashara na kuleta uwekezaji mkubwa.

Itaimarisha zaidi miundombinu na huduma za bandari zetu na viwanja vya ndege ili viwe na uwezo wa ushindani na ufanisi zaidi katika eneo la Afrika Mashariki na Magharibi ya Bahari ya Hindi.

Itafungua milango ya biashara kwa kuitangaza Zanzibar kuwa Bandari Huru (Free Port) ili kuwavutia wafanyabiashara wenye kulenga soko la Afrika ya Mashariki na Kati. Lengo la sera hizi ni kufikia ile ndoto ya muda mrefu ya kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki.

Itahakikisha shughuli za uingizaji bidhaa nchini zinafanyika kwa uwazi, bila ya usumbufu kwa wateja, na kwa uharaka na ufanisi mkubwa lakini pia katika viwango vidogo kabisa vya ushuru na kodi kulingana na uchumi wa nchi yenyewe ya Kisiwa.

Itatoa kipaumbele katika kutengeneza mikakati na mipango kazi ya uingizaji wa vifaa vya miundombinu ya sekta ya mafuta na gesi katika kuharakisha na kurahisisha maendeleo ya sekta hii ya mafuta na gesi.

Itashirikiana na washiriki wa kibiashara wa kikanda katika utekelezaji wa misingi ya “Transit Trade” kwa ajili ya nchi zisizo na bahari (Landlocked States) za Afrika.

5. TUTAKUZA BIASHARA KWA KUONDOSHA URASIMU NA KUPUNGUZA VIWANGO VYA USHURU NA KODI
Zanzibar ni nchi ya Visiwa vidogo na hivyo ina changamoto nyingi za kiuchumi na kimaendeleo. Udogo wa ardhi yake, kuzungukwa kwake na bahari, matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi na kuongezeka kwa kina cha bahari, pamoja na changamoto na athari za kimazingira kwa uchumi na jamii yake kunaleta haja kubwa na ya haraka ya mapinduzi ya kiuchumi na kimaendeleo kwa jamii yake nzima katika kupambana na unyonge na umaskini unaowakabili na kuelekea katika taifa lenye hadhi ya uchumi wa kati. CUF inaamini kuwa njia pekee ya kuitoa Zanzibar katika janga la unyonge na umaskini na kubadilisha hali ya maisha ya watu ni kuitumia neema tuliyopewa ya kijiografia, maliasili na kihistoria kuigeuza Zanzibar kuwa kituo kikuu cha kibiashara cha Afrika ya Mashariki na Magharibi ya Bahari ya Hindi.

Neema hii ipo katika sekta ya uagizishaji, uwekezaji katika maliasili za pwani na baharini kama utalii na uvuvi, miundombinu ya sekta mpya ya mafuta na gesi, bandari huru, na mabenki. Yote haya yatafanikiwa pale tutakapoweza kwa kauli moja kuitoa Zanzibar ndani ya sera zilizofeli za “kusawazisha uchumi” kwa jina la Muungano na kuifanya ipumue na sera zake wenyewe ndani ya Muungano wa Haki, Heshima na Usawa. Dira ya mabadiliko ya CUF ni kuhakikisha kuwa Zanzibar inarejesha haki yake ya maamuzi katika ushuru, kodi na mapato.

5.2.UAGIZISHAJI WA BIDHAA YA MAFUTA
Serikali inayoongozwa na CCM imeshindwa kuwa wazi katika ukiritimba na uhodhi wa biashara wa baadhi ya wafanyabiashara wachache wanaonekana kuwa na ushawishi wa kisiasa. Kuna upotevu mkubwa wa fedha za umma katika biashara hii. Bei ya mafuta imekuwa ikipandishwa mara kwa mara kufidia upotevu wa mapato. Kupanda huko kwa bei ya mafuta kunapelekea kuongezeka kwa bei ya huduma zote na bidhaa nyingi na matokeo yake ni kumtwika mzigo mkubwa sana mwananchi wa kawaida.

Vile vile tunaona ongezeko la matumizi ya gesi ya kupikia (LPG), ambalo ni jambo la faraja kwa vile litasaidia sana kupunguza matumizi ya makaa na hatimae kupunguza ukataji wa miti. Hata hivo bidhaa hii inaonesha kutokudhibitiwa na kuonekana kuuzwa kiholela, jambo ambalo linaweza kuleta madhara makubwa pindipo pakitokea hitilafu katika mitungi hiyo ya gesi.

Baada ya kilio cha muda mrefu, Zanzibar imeanzisha Taasisi mpya ya Udhibiti ya Huduma ya Zanzibar (ZURA). Hata hivyo Taasisi hii inahitaji kuwezeshwa vyema ili kuweza kufanya majukumu yake kwa ufanisi kwa kuipatia nyenzo kama vile ofisi, rasilimali watu na vitendea kazi ili kuweza kuidhibiti biashara ya huduma za mafuta, umeme, maji na gesi za matumizi ya nyumbani ili kuleta ufanisi, usalama na kuondoa usumbufu wa upatikanaji na upandaji holela wa bei za bidhaa hizi.

Serikali imeshindwa kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa mafuta na kusababisha upungufu wa mara kwa mara unaozorotesha utendaji katika sekta zote. Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF itafanya yafuatayo:

Itahakikisha kuwa kila Mzanzibari mwenye uwezo wa kufanya biashara ya uagizaji mafuta kutoka nje basi anapata fursa hiyo kwa mujibu wa sheria na viwango.

Bila ya kuathiri mpango wa bajeti wa taifa, Serikali itashirikiana na waagizaji na wawekezaji wa mafuta katika kudhibiti mfumuko wa bei ya mafuta kwa wananchi na kwa kuzingatia soko la bidhaa za mafuta la dunia.

Itaongoza kwa njia ya uwazi fursa sawa kwa wakala wote wa biashara ya mafuta kuendesha biashara hiyo kwa kufuata kanuni na taratibu halisi zilizowekwa.

Itamlinda mwananchi dhidi ya ukitirimba wowote wa biashara ya mafuta unaofanywa kinyume na sheria.

Itaunda sera na sheria mpya inayohusu usimamizi wa uagizaji, usambazaji, uhifadhi na uuzaji wa gesi ya kupikia (Cooking Gas) ili kudhibiti biashara holela ya bidhaa hii kwa usalama na viwango vya bidhaa yenyewe.

Itaweka kipaumbele kwa mamlaka ya ZURA ili kuhakikisha inasimama wenyewe kwa muda mfupi na kuondoa kero kwa wananchi wetu.

5.3. USAFIRISHAJI WA MAZAO YA KILIMO NA BAHARI
Ubinafsishaji wa zao la karafuu umekuwa ni mada nyeti sana katika maisha yetu. Serikali siku zote imekuwa ni msimamizi mkuu wa zao hili katika uzalishaji, usafirishaji, utafiti, na uendelezaji wake. Malalamiko mara nyingi yamekuwapo katika kumpatia faida ya kweli mkulima wa zao hili na hapo ndipo pamekuwa pakitokea suitafahamu baina ya Serikali na wakulima na kupelekea kudorora kwa zao hili.
Hata hivyo, marekebisho makubwa yaliweza kufanyika mara tu baada ya maridhiano na hali ya mkulima kwa kiasi imekuwa ikiendelea kunyanyuka japokuwa na changamoto mbali mbali. Lakini mafanikio haya yanatakiwa kusimamiwa zaidi yaendelee kulinyanyua tena zao hili.

Lakini hakuna njia thabiti kama zile za ufufuaji wa zao la karafuu ambazo zimechukuliwa kuwasaidia wananchi kuendeleza uzalishaji na uuzaji wa mwani. Yote haya yanafanyika katika hali ambayo mazao ya matunda na viungo pamoja na mazao mengine ya bahari Zanzibar yamekosa kabisa sera bunifu za uwekezaji na usafirishaji.

Serikali ya CCM imeshindwa kabisa kuendeleza Maeneo Huru ya Fumba na Micheweni kutengeneza na kusafirisha bidhaa kama hizi nchi za nje (EPZ).Pia, Serikali inayoongozwa na CCM inaonekana imeridhika na kusafirisha bidhaa ghafi na kupelekea bidhaa hizo nje zikiwa na thamani ndogo katika soko la kimataifa bila ya kujali maslahi ya wakulima wa mazao haya.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF itatekeleza hatua zifuatazo katika kurekebisha hali hii:
Itaendelea kubuni mbinu mbali mbali mbadala za kumwezesha mkulima wa biashara ya karafuu kuweza kupata maslahi zaidi ya jitihada zake chini ya usimamizi wa Serikali.

Itaipa msukumo sekta binafsi kuimarisha kilimo, uchambuaji na uuzaji nje wa viungo na kushindana katika soko la nje.

Itaunda sera bunifu za uwekezaji, uzalishaji na usafirishaji wa mazao ya bahari kama vile mwani, kaa, chaza, majongoo ya pwani, samaki wa kufuga, n.k. pamoja na kuongeza mpango kazi wa kuwasaidia wananchi wanaojishughulisha na sekta hii.

Itaviondoa vipingamizi vyote vinavyozuia maendeleo ya Maeneo Huru na Bandari Huru kwa kuimarisha huduma muhimu za kiuchumi na kijamii, kuimarisha mfumo wa sheria, kutangaza Zanzibar mpya iliyotokana na Maridhiano, pamoja na kuwashajiisha Wazanzibari wa ndani na nje washiriki katika maeneo haya ya kiuchumi.

Itajitahidi kuingiza teknolojia mpya ya kuziongezea thamani bidhaa zinazokusudiwa kusafirishwa kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo humu humu nchini.

5.4. VIWANDA NA UZALISHAJI
Sekta ya uzalishaji viwandani inachangia chini ya asilimia 3 ya Pato la Taifa. Hali hii mbaya inatokana na dhamira ya makusudi ya kuhakikisha Zanzibar haiendelei kiviwanda. Inasikitisha sana kuona kuwa karibuni viwanda vyote vilivyokuwepo kabla na baada ya Mapinduzi vimekufa.

Viwanda binafsi vilivyoanzishwa katika miaka ya karibuni vimeshindwa kuhimili ushindani na Tanzania Bara na soko zima la Afrika Mashariki kwa sababu ya kodi na tozo kubwa za Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Viwanda vichache sana ndivyo vilivyopo na hivi peke yake haviwezi kuleta tija yeyote ya kitaifa kwa ujumla.

Serikali inayoongozwa na CCM imeshindwa kuweka huduma muhimu za kiuchumi na kijamii zinazolenga katika utekelezaji na uendelezaji wa shughuli za viwanda hapa Zanzibar. Bado hakuna sera wala mipango kazi madhubuti nchini ya kukaribisha fursa mbali mbali za uwekezaji katika viwanda. Sera ya viwanda hakuna. Miundombinu ya kuwa na sekta bora ya viwanda bado haipo. Vivutio (incentives) vya kuwezesha uimarishaji wa sekta ya viwanda hakuna. Na pia hakuna maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya kujenga viwanda vya kudumu.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF itatekeleza hatua zifuatazo katika kurekebisha hali hii:
Itaunda Baraza la Taifa la Viwanda ili kuimarisha ushirikiano wa dola na jamii kwa masuala yanayohusu uendelezaji wa sekta binafsi.

Itahakikisha kwamba mambo yatakayopewa kipaumbele katika kukuza sekta ya viwanda ni yale yanayohusika 32 kwa karibu na maliasili zetu zilizopo nchini.

Itahakikisha kwamba inaelekeza sehemu ya kutosha ya matumizi ya umma katika kukuza mfumo muafaka na unaovutia wa kifedha, kisheria, kijamii na kiteknolojia ambamo wenye viwanda wanaweza kuendeleza shughuli zao kwa ufanisi.

Itaunda sera ya viwanda inayokwenda sambamba na mabadiliko ulimwenguni.

Itahakikisha kuna mahusiano mazuri viwandani na uongozi bora wa mashirika ya serikali.

Itatenga maeneo maalum ya kujenga viwanda vya kudumu.

Itashajiisha wawekezaji wa kibenki kufungua mabenki ya viwanda.

Itahakikisha kuwa Mamlaka ya Viwango Zanzibar (Zanzibar Bureau of Standards) inafikia hadhi ya ushindani wa kimataifa kupitia mashirikiano zaidi na Taasisi ya Viwango Ulimwenguni (International Standardization Organization).

5.5. SEKTA ISIYO RASMI (JUA KALI)
Wafanyabishara ndogo ndogo wanaojishughulisha na sekta hii (Jua Kali) wamekuwa wakipewa usumbufu, vitisho visivyokwisha na unyang’anyi wa kimacho macho wa mali zao. Hakuna mazingira muafaka ya kiutendaji kwa sekta isiyo rasmi. Hakuna usalama wa mali ya wafanyabiashara katika sekta isiyo rasmi. Sekta isiyo rasmi inaumizwa na mzigo mzito wa kodi isiyolipika. Serikali haijaonyesha kutambua na kuthamini kabisa sekta hii hadi kuonekana kama inaipiga vita.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF itatekeleza hatua zifuatazo:
Itaheshimu na kuthamini sekta isiyo rasmi na kuwapa nguvu wale walioamua kujiendeleza kwa kujiajiri na kuzalisha mapato.

Itawawekea wajasirimali wa Jua Kali mazingira mazuri na endelevu sekta hiyo isiyo rasmi iweze kustawi.

Itaweka na itasimamia taratibu za kisheria zinazosaidia kuongoza shughuli hizo na mali zao.

Itaondoa urasimu na kupunguza mzigo wa kodi kwa sekta isiyo rasmi.

Itasaidia katika utoaji wa elimu ya uwezeshaji wa kitaaluma (Capacity building) pamoja na kutafuta miundombinu endelevu na ya kibinadamu kwa wafanyabiashara wake.

5.6. UKUZAJI WA UTALII
Sekta ya Utalii imekuwa katika kasi ya kuridhisha na hata kufikia mahala Serikali imetangaza kwamba imelipiku zao la karafuu kama chanzo kikuu cha mapato ya fedha za kigeni kwa Zanzibar. Serikali imetangaza kwamba idadi ya watalii wanaoingia Zanzibar imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Hili ni jambo la kutia moyo hata kukitiliwa maana kuwa Zanzibar ni nchi ya uwekezaji.

La ajabu ni kuwa ukusanyaji wa mapato umekuwa ukishuka kila mwaka. CUF inaamini kuwa Serikali inayoongozwa na CCM haina Sera ya Utalii iliyo muafaka na iliyopangika kulingana na umuhimu ambao sekta hii imekuwa nayo katika uchumi wa Zanzibar. Kwa nini basi pamoja na mafanikio yote hayo tunayoelezwa, Zanzibar ibaki kuwa nchi yenye umaskini mkubwa takriban miaka 30 sasa tangu uwekezaji katika utalii ulipoanza?

Suala la vivutio limekuwa ni mtihani mwengine kwa sekta hii. Pamoja na kuwepo vivutio vya maliasili za ufukweni na baharini, bado sekta ya utalii Zanzibar haijaweza kuunganishwa na sekta nyingine za kibiashara na uwekezaji katika utoaji wa huduma kwa watalii.
Bado Wazanzibari hawajapata fursa inayostahiki ya kupata ajira katika sehemu za utawala (Managerial Position) za uendeshaji wa hoteli. Hakuna fursa 33 za kuwawezesha Wazanzibari kuhitimu katika sekta ya utalii kwa viwango vya kimataifa.

Halikadhalika, Serikali inayongozwa na CCM imeshindwa kuwavutia wawekezaji wa mahoteli ya kitalii ya daraja la kwanza. Imeshindwa kuitangaza Zanzibar kwa watalii wa hadhi ya juu. Imeshindwa kuweka utaratibu mzuri kiutawala na kiuchumi na kukusanya mapato ya utalii hasa mahotelini na katika makazi yasiyo rasmi. Lakini pia, ukuzaji wa utalii kwa wakati huu ni wa kushtukia na kubahatisha tu wakati huduma kwa ajili ya utalii wa ndani ni finyu.

Hakuna kinga dhidi ya tabia za kuchafua mazingira katika maeneo muhimu yanayowavutia watalii. Na mfumo huu uliopo unaolelewa na Serikali ya CCM umeshindwa kuiepusha jamii na taathira mbaya zinazotokana na utalii, hasa kiutamaduni na kijamii au kutoa taaluma ya kutosha kwa wafanyakazi wa sekta hii na kusababisha wawekezaji kuagiza wafanyakazi kutoka nje, hivyo kupelekea Wazanzibari kukosa ajira.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF itachukua hatua zifuatazo:
Itaanzisha sera muafaka ya utalii endelevu (Sustainable Tourism) inayojali usawa wa kijamii (social equity) katika maslahi yao mbali mbali kama vile maji safi, nishati, barabara, matumizi ya haki ya umiliki wa ardhi, malisho ya mifugo, kilimo, madiko yao ya uvuvi pamoja na maeneo yao ya kuvulia ya mwambao.

Itatekeleza mkakati maalum wa kuwavutia wawekezaji wa mahoteli ya kitalii ya daraja la kwanza kwa kuwekeza zaidi katika miundombinu ya mahoteli, barabara, mawasiliano, maji, nishati na ardhi.

Itatekeleza mpango madhubuti wa kuitangaza Zanzibar kwa watalii wa hadhi ya juu.

Itaimarisha maeneo yote ya vivutio vya watalii kwa kuhakikisha vinatunzwa na kuenziwa na kuwekwa katika mazingira ya usafi yanayoendana na viwango vya kimataifa ili kuikuza Zanzibar kama kituo cha watalii wa daraja la juu.

Itahakikisha uhifadhi wa visiwa vidogo vidogo vilivyo kando ya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya asili ya viumbe vya baharini.

Itaimarisha na kukuza uwezo uliopo wa kukusanya mapato ya serikali katika sekta ya utalii ili kukuza na kupanua ukusanyaji.

Itachukua hatua muafaka za kuzuia utalii usiathiri na kubadili hazina ya utamaduni mzuri wa Zanzibar pamoja na kuhifadhi mazingira yake.

Itaongeza zaidi ubunifu wa vivutio kwa watalii ili waongeze siku za kukaa nchini na hivyo kukuza pato la Taifa linalotokana na utalii.

Itasomesha vijana wa kutosha wa masomo ya utalii kwa ngazi zote ili waweze kuajiriwa katika soko la utalii hasa katika maeneo ya ngazi za juu.

Utalii wa kibiashara, utalii wa tiba na vivutio vinginevyo vitawekewa vipaumbele maalum vya mipango ya taifa.

Itahakikisha Sheria ya kamisheni ya utalii inaweka kipaumbele kwa Wazanzibari.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s