Ilani ya Chama Cha Wananchi CUF kuelekea kwenye Uongozi mwema na utawala wa haki

UONGOZI MWEMA NA UTAWALA WA HAKI
Tunaamini kuwa uongozi mwema ni uongozi unaowiana, unaoheshimu na unaolinda katiba na sheria za nchi. Watu wanastahiki kuishi kwa amani na haki zao kuheshimiwa. Kutokana na mgogoro wa kisiasa uliokuwepo muda mrefu kabla na hata baada ya kuja Maridhiano, kumejengeka utamaduni miongoni mwa viongozi, watumishi serikalini na hata wananchi wa kawaida kutotekeleza na kutoheshimu katiba na sheria za nchi, na hali hiyo kuathiri mwenendo mzima wa utoaji haki na huduma za serikali kwa wananchi na kupelekea kukosekana kwa utawala wa

3.1. UONGOZI MWEMA
Kumekuwa na matumaini makubwa kwa wananchi baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na jambo lililozaa mashirikiano baina ya wananchi na pia kwa viongozi wa kitaifa ingawa hatua zainapaswa kuchukuliwa ili kuimarisha zaidi Umoja wetu wa Kitaifa na kukabili changamoto zinazoendelea kujitokeza. Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na CUF itachukua hatua zifuatazo:

Itaheshimu ridhaa ya wananchi na itashirikiana na viongozi watakaochaguliwa kihalali katika uchaguzi huru na haki kutoka vyama vyote vya siasa vitakavyopata ridhaa ya kuingia katika Baraza la Wawakilishi katika uendeshaji wa nchi.

Itajenga taifa linaloheshimu haki za wananchi na utawala wa sheria.

Itahakikisha kuwa hakuna mtu yeyote atayekuwa juu ya sheria na kwamba si kiongozi yeyote yule wa ngazi yeyote ile ya kisiasa atakayeachiwa kuwakandamiza wengine kwa kutumia vibaya madaraka aliyokabidhiwa ya uongozi.

Itatunga sheria mpya kuepusha utumiaji mbaya wa madaraka ya umma.

Itahakikisha ina serikali ambayo inaongozwa na utawala wa sheria, na sio kujiegesha katika matakwa na maslahi binafsi ya kiongozi.

Itarekebisha au kufuta sheria zote kandamizi ambazo zinakwamisha misingi ya demokrasia na haki za binadamu. Hatua hii itahakikisha kwamba hakuna atakayeonewa kuanzia siku CUF itakapokabidhiwa madaraka ya kuongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Itawashirikisha wananchi katika kufanya mapitio ya Katiba ya Zanzibar ili iweze kwenda sambamba na misingi ya haki na uwajibikaji chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na Zanzibar mpya tunayokusudia kuijenga kwa pamoja.

3.2. HAKI ZA BINADAMU
Ingawa kumekuwa na hali ya mafanikio kiasi katika uimarishaji wa haki za binadamu tangu Serikali ya Awamu ya Sita na ya Saba yenye muundo wa umoja wa kitaifa kuja madarakani Novemba 2010, kwa ujumla uvunjwaji wa haki za binadamu bado umebakia kuwa ni tatizo kubwa nchini. Ripoti za Hali ya Haki za Binadamu Zanzibar zimekuwa zikionyesha kuwepo na kujikita kwa tabia za kutoheshimiwa na kuvunjwa kwa haki za binadamu kunakofanywa na vyombo vya dola na hata wananchi wenyewe.

Sheria mbaya, mahakama zisizokuwa huru, na vyombo vya dola vinavyofanya kazi kwa kufuata matakwa binafsi ya baadhi ya viongozi wake, badala ya kufuata katiba na sheria, vimesababisha viwango vya haki za binadamu nchini kuendelea kuwa katika hali mbaya.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na CUF itachukua hatua zifuatazo:

Itatekeleza kwa ukamilifu Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu na miongozo yake ili kuhakikisha kila mmoja ana haki ya kuishi na kuamua juu ya mustakbali wake, haki zake za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Tutafanikisha uundwaji wa chombo huru na chenye nguvu cha kusimamia haki za binadamu Zanzibar na kujizatiti na kuzilinda haki hizo kwa kutilia mkazo urudishaji wa heshima na ulinzi wa Haki za Binadamu nchini.

Tutahakikisha kuwa Wazanzibari walionyimwa haki yao ya ukaazi kinyume na Katiba, Haki, na Sheria, wanapatiwa haki zao kwa kupewa kitambulisho cha Mzanzibari Makaazi.

Tutauondoa ubaguzi wa aina yeyote ule katika haki na fursa ya ajira kwa wananchi ndani ya Taasisi za Serikali.

Itahakikisha uhuru wa vyombo vya habari na kuviondoshea udhibiti wa aina yoyote ili kuviwezesha kukua na kuwa jukwaa la kuwatumikia wananchi katika kulinda haki zao na kusaidia kuifanya serikali iwajibike kwa wananchi.

Italinda haki ya uhuru wa kuabudu ili kuhakikisha dini zote zinatendewa haki na wafuasi wao wanapata fursa sawa bila kuingiliwa.

Itaingiza masuala ya Haki za Binadamu kama sehemu ya mitaala maskulini ili kuhakikisha watoto na vijana wanazielewa haki zao.

3.3. VITA DHIDI YA RUSHWA
CUF inaiona rushwa kuwa ni adui wa haki, inayoua uchumi na kuwanyima wananchi haki yao ya msingi ya maisha bora na maendeleo. Rushwa imekithiri na inaonekana kuwa sehemu ya maisha ya kila siku kiasi kwamba unaonekana mtu wa ajabu kama hutoi au hupokei rushwa.

Huduma nyingi za serikali zimekuwa hazipatikani bila ya mwananchi kutoa rushwa. Chanzo kikubwa cha rushwa ni ukiritimba wa madaraka, mishahara midogo ya watendaji Serikalini, maamuzi yasiyofuata taratibu zinazoeleweka na kutowajibishwa kwa wanaoshiriki katika vitendo vya rushwa.

Ingawa Zanzibar tayari imeanzisha sheria na vyombo vya kuzuia rushwa, kuwepo kwa taasisi zaidi ya moja ya kupigana na rushwa kunaleta tatizo jingine la urasimu na kuongeza gharama za uendeshaji lakini pia kuingiliana kwa taasisi hizi kimadaraka na kiufanisi hata kutishia kupotea malengo ya kupambana na rushwa yenyewe. Ufanisi wa taasisi zenyewe upo mashakani kwani pamoja na kuwepo na kero mbali mbali zinazohusu rushwa kuwasilishwa na wananchi katika ngazi tofauti za kijamii na kitaasisi, bado mafanikio ya taasisi hizi kwa Zanzibar haujaonekana.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na CUF itachukua hatua zifuatazo:
Itaanzisha mabadiliko ya muundo na utendaji katika Serikali yatakayolenga kuondosha ukiritimba wa madaraka na kuweka utaratibu wa wazi zaidi katika uendeshaji wa shughuli zake za kila siku.

Itaboresha Sheria na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Zanzibar pamoja kurekebisha muundo wa taasisi zenyewe ili ziweze kufanya kwa ufanisi mkubwa na bila ya kuingiliwa.

Itazifanyia mapitio sheria zilizopo ili kutoa adhabu kali kwa yeyote atakayepatikana na hatia ya rushwa.

Itaboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi kwa kiwango cha kuridhisha ili kufifisha rushwa katika ngazi zote za utumishi Serikalini.

3.4. UHURU WA HABARI NA MAELEZO
Kwa muda mrefu toke kuasisiwa kwake, Chama Cha Wananchi – CUF kimekuwa kikipiga kelele ndani na nje ya nchi kuhusiana na hatari ya ukandamizwaji wa haki ya mwananchi ya kuwa na uhuru wa kupata habari na maelezo bila ya vitisho wala upotoshaji wa dola. Sheria zilizopo za habari, utangazaji, na maelezo zinaendelea kuubana uhuru na haki hiyo ya utoaji na usambazaji habari na zinatoa madaraka makubwa kwa Serikali kuvidhibiti vyombo vya habari.

Isitoshe, Sheria hizo zimepelekea kutokuwepo kwa vyombo vya habari binafsi vilivyo huru na vinavyofanya kazi kwa uwazi na kwa ufanisi.
Pia, vyombo vya habari vya Serikali kwa kiwango kikubwa viko katika hali duni kiutendaji, vifaa na hata maslahi ya wafanyakazi wake na hivyo kushindwa kutekeleza ule wajibu wa vyombo vya habari vya umma (public broadcasting) katika kukuza demokrasia na kuwapa wananchi jukwaa la kutoa maoni na madukuduku yao.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na CUF itachukua hatua zifuatazo:
Itaifuta Sheria iliyopo ya Habari na kutunga sheria mpya itakayohakikisha uhuru wa upatikanaji na utoaji wa habari (Right to Information Act). Sheria hiyo itasimamia haki ya mtu yoyote kutafuta taarifa, kufungua chombo cha habari kilicho huru, kukosoa Serikali, na kujadili muelekeo wa nchi kupitia haki ya raia kupokea, kupata na kutoa habari na maoni yake.

Itaviondoa vikwazo vyote viliopo ambavyo vinazuia uhuru wa waandishi wa habari kujikusanya, waandishi watashajiishwa kuunda jumuiya zao kulinda uhuru wao na maslahi yao.

Itaboresha na kuliendeleza Shirika la Utangazaji Zanzibar (Zanzibar Broadcasting Corporation) ambalo litapewa uhuru kikamilifu usio na mafungamano yeyote yale ya kisiasa na chama au itikadi yeyote ile, na kusimamiwa na Bodi iliyo huru yenye kutambua na kuheshimu ushiriki kamilifu wa wananchi katika mijadala mbali mbali ya kitaifa na kimataifa bila ya udhibiti, upendeleo au ushawishi wa kisiasa.

Itaimarisha na kuboresha maslahi, elimu na mafunzo kwa wafanyakazi wa vyombo vya habari na utangazaji ili kuinua utendaji wao wa kazi na kuongeza ufanisi, na kuwawezesha kufanya kazi zao kitaalamu na kwa kujiamini zaidi.

Itawashajiisha na kuwasaidia wahariri na wandishi wa habari kuunda Baraza la Habari la Zanzibar kwa madhumuni ya kuimarisha ufanisi na usimamiaji wa maadili ya uandishi wa habari.

3.5. UTAWALA WA HAKI NA SHERIA
Kila Dola ulimwenguni lazima iwe na chombo kinachoitwa Mahakama; chombo hiki lazima kiwe huru na kinapaswa kufanya kazi bila kuingiliwa. Mahakama ziko kwa ajili ya kuzitafsiri sheria na kutenda haki. Ili kuwa na sekta huru ya sheria hatuna budi kuwa na Tume ya Ajira ya Sekta ya Sheria iliyo huru, ambayo ina uhuru kamili katika kuajiri Majaji, Mahakimu na wafanyakazi wengine wa Mahkama.

Mara nyingi Mahakama zimetumiwa vibaya na wale wanaoziongoza kutekeleza matakwa binafsi na hivyo kupelekea kunyima haki wananchi, kutisha na kudhalilisha watu, hali iliyopelekea kulalamikiwa na taasisi za ndani na nje ya nchi zinazofuatilia na kuchunguza masuala ya ukiukaji wa haki za binadamu na utoaji wa haki kwa ujumla.

Washitakiwa wamekuwa wanawekwa mahabusu kwa utashi wa Jaji au Hakimu pasina kuzingatia matakwa ya sheria hasa yale yanayohusu haki ya dhamana. Kumekuwa na ulimbikizwaji wa kesi nyingi katika mahakama mbali mbali bila ya hata kusikilizwa madai ya washtakiwa wake, jambo ambalo limezidi kuwatoa imani raia juu ya mahkama na Serikali kwa ujumla.

Licha ya demokrasia ya vyama vingi, bado kuna baadhi ya sheria ambazo zinapingana na kukwaza mfumo huo. Jaji Mkuu hana uajiri madhubuti unaolingana na taratibu za Mahakama duniani. Muundo wa Tume 18 ya Ajira ya Sekta ya Sheria kwa kiasi kikubwa unaifanya ikose uhuru wake kutokana na wajumbe wake wengi kuwa ni wateule wa Rais moja kwa moja.

Majengo na hali ya Mahkama Kuu na Mahkama za ngazi za chini yapo katika hali mbaya inayodhalilisha chombo hicho muhimu cha dola. Hakuna sehemu maalum za kuweka mahabusu watoto na hatuna vituo vya kurekebisha tabia kwa wale waliopatikana na hatia.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na CUF itachukua hatua zifuatazo:
Itaziimarisha Mahakama na kuhakikisha uhuru wake unalindwa kikamilifu, kisheria na kiutendaji.

Itaziboresha Mahakama kwa kuzipa uwezo wa kutosha ili kuhakikisha hakuna ulimbikizwaji wa kesi mahakamani bila ya kusikilizwa lakini pia kutoa dhamana kwa wakati kwa wale washtakiwa wanaopaswa kupata haki hiyo.

Itatoa uhuru kwa Tume ya Ajira ya Sekta ya Sheria na itaweka taratibu bora za uundwaji wake na utendaji wake wa kazi.

Itapanga uajiri wa Jaji Mkuu kwa taratibu za Kimahakama zinazokubalika za ulimwenguni.

Itaweka vituo vya kurekebisha tabia kwa watoto watakaopatikana na hatia za uhalifu wa sheria pamoja na kuwapa fursa ya kuendelea na elimu na mafunzo ya amali wakati wanatumikia katika vituo vya kurekebisha tabia.

Itahakikisha kuwa haki za wafungwa na walio mahabusu zinatekelezwa kwa mujibu wa Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu.

3.6. ULINZI NA USALAMA
Idara Maalum kama vile Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kikosi cha Valantia (KVZ), Chuo cha Mafunzo (Magereza), na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi vinakabiliwa na changamoto kubwa ya kujenga imani ya Wananchi wanowatumikia.

Kutokana na historia yake na utendaji kazi wake huko nyuma, vikosi hivi kwa kiasi kikubwa havijajenga imani ya wananchi wote kuwa ni vikosi vya kutoa huduma maalum na visivyoegemea upande wowote wa kisiasa.

Isitoshe, vikosi hivi na askari wake wamekuwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa vifaa na mahitaji mengine muhimu, mafunzo duni na maslahi yasiyoridhisha. Kwa kiasi kikubwa, ufanisi wa vikosi hivi kama tegemeo la ulinzi, usalama, na uokozi kwa wananchi wote umeshuka na badala yake vijana wa vikosi hivi wamekuwa wakitumiwa mara nyingi katika mambo ya kisiasa. CUF inaamini kuwa wakati umefika kwa vikosi hivi kufanya kazi zao husika kwa mujibu wa taaluma na malengo yao ya kazi (Professional Guards).

Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na CUF itachukua hatua zifuatazo:

Itavipa sura mpya vikosi hivi kwa kuvifanya kuwa vyombo vya kutoa huduma kwa jamii na kuvipatia vifaa na mafunzo muafaka ili viwatumikie wananchi ipasavyo pamoja na kuviwezesha kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.

Itaangalia upya mishahara, maslahi na marupurupu ya askari na watumishi wengine wa Idara hizi Maalum za SMZ kwa lengo la kuwoangezea ari ya utendaji na ushiriki wao katika ujenzi wa Zanzibar mpya.

Itabadilisha jina la KMKM na kuiita Kikosi cha Ulinzi wa Mwambao wa Zanzibar (Zanzibar Coast Guards).

Itahakikisha kuwa vikosi vyote vinapewa mafunzo maalum ili kuweza kutoa huduma ya mwanzo na misaada mingine ya kibinadamu wakati wa maafa.

Itasimamia haki zinazohusiana na maslahi, mazingira ya kufanyia kazi na vitendea kazi kwa kufuata utaratibu uliokuwepo 19 wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Sheikh Abeid Amani Karume ya kushugulikia nyongeza za mishahara na mafao kwa watumishi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Muungano walio Zanzibar.

3.7. UTUMISHI SERIKALINI NA UWAJIBIKAJI
Utumishi Serikalini ndiyo injini ya Serikali imara na yenye ufanisi katika kuwahudumia raia wake. Katika malengo ya kuijenga Zanzibar Mpya yenye vigezo vya ushindani wa kiutendaji na serikali nyengine duniani, jukumu kubwa liliopo mbele yetu ni kuimarisha utumishi Serikalini ili uendane na mahitaji ya wakati huu na wakati ujao ili kufikia viwango vya kimataifa katika utoaji wa huduma.

Tafiti mbali mbali zimeonyesha kuwa Sekta ya Utumishi Serikalini inakabiliwa na changamoto kuu mbali mbali ikiwemo ukosefu wa sifa na ujuzi unaotakiwa, uingizwaji wa watumishi katika migogoro ya kisiasa, ukosefu wa haki za mafao kwa wanaostahiki, ubadhirifu, uwajibikaji na nidhamu.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na CUF itachukua hatua zifuatazo:
Itaunda upya Tume Huru ya Utumishi Serikalini kwa kuzingatia haja ya kuongoza na kusimamia marekebisho makubwa ya Utumishi Serikalini.

Itaanzisha Idara Maalum ya Msimamizi Mkuu wa Huduma za Serikali (Inspector General of Government Services), itakayochunguza na kufuatilia utendaji kazi wa vyombo vya Serikali, ufanisi wao, pamoja na kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu utumishi.

Italinda ajira na maslahi ya watumishi wote wa Serikali na kuwapa fursa za mafunzo wakiwa kazini ili kuongeza elimu, maarifa na ujuzi wao wa kazi kwa lengo la kuinua ufanisi na uwajibikaji.

Itahakikisha kuwa ajira atapewa Mzanzibari yeyote mwenye sifa bila aina yoyote ya ubaguzi.

Itahakikisha kuwa maelezo ya dhamana za kazi yanafuatwa sawa sawa na watendaji wanawajibika ipasavyo katika kazi na dhamana zao.

Itatoa mafao yote muda mfupi tu baada ya mtu kustaafu au kuacha kazi.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s