Maalim Seif: Tutapambana nao, watakaoyachezea maridhiano yetu

Mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amesema endapo wananchi watamchagua kuwa rais wa Zanzibar, ataimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kupanua wigo wa mgawanyo wa madaraka kuanzia ngazi ya juu hadi kwenye ngazi za Masheha.

Maalim Seif ameyasema hayo hapo jana wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi wa majimbo ya Mpendae na Jan`gombe katika mkutano uliofanyika katika uwanja wa Kwabinti Amrani ikiwa ni muendelezo wa mikutano ya kampeni inayofanywa na chama hicho.

Aidha Maalim Seif amewambia wananchi kuwa katika uongozi wake atahakikisha anaimarisha maridhiano na kuahidi kutowafumbia macho wale wote watakao hatarisha ustawi wa maridhiano hayo.

“Ukitaka kuchezea maridhiano tutakufa na wewe. Kusema kweli hadi sasa maridhiano yetu hayajafanikiwa sawa sawa kama vile ambavyo tumetarajia” Alisema Maalim Seif na kushangiliwa na umati mkubwa uliohudhuria mkutano huo.

Pia aliwahakikishia wazanzibari kuwa atahakikisha anasimamia suala zima la Umoja na Mshikamano miongoni mwa Wazanzibari na kueleza kuwa huo ndiyo msingi wa amani.

“Amani bila ya umoja na mshikamano itakuwa haina maana yoyote katika nchi kwani wananchi watakosa kukaa pamoja na kupanga mustakbali wa nchi yao” Aliongeza Maalim Seif.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, amelaumu vikali watumishi wa serikali kujishirikisha na mambo ya siasa, hivyo amesema Serikali itakayoongozwa na Chama cha CUF haitoruhusu watumishi wa umma kushiriki kwenye siasa na badala yake watabakia kuwa ni watumishi wa wananchi.

“Katika uongozi wangu watumishi wa Serikali hawatoruhusiwa kushiriki kwenye siasa na badala yake watakuwa watumishi wa Serikali” Alisema.

Pia aliutumia mkutano huo kuwatambulisha wagombea wa Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kwa Majimbo ya Jan`gombe na Mpendae.

Wagombea walitambulishwa ni pamoja na Muhammed Yussuf mgombea Ubunge jimbo la Jan`gombe, na Ali Haji Mwadini ambaye anagombea nafasi ya Uwakilishi. Kwa upande wa jimbo la Mpendae mgombea wa ubunge ni Omar Moh`d Omar na Uwakilishi ni Ali Hamad Ali. Madiwani ni Hassan Rashid Khamis ambaye anagombea wodi ya Mpendae na Mbarouk Abdalla Suleiman kwa upande wa wodi ya Migombani.

Hata hivyo Maalim Seif alilazimika kusitisha hotuba yake kufuatia hali ya Sintofahamu iliyoibuka kufuatia kupita kwa gari ya matangazo iliyokuwa ikitangaza mkutano wa CCM kwenye barabara karibu na eneo lililokuwa likifanyika mkutano huo na kuzua tafrani kwa wananchi waliohudhuria uwanjani hapo.

Mkutano huo wa Chama Cha Wananchi CUF mjini ni wa tatu kufanywa na chama hicho baada ya ule wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika Kiwanja cha Demokrasia Kibandamaiti na ule wa Tibirizi Kisiwani Pemba, ikiwa ni muendelezo wa mikutano ya kampeni inayofanywa na chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s