Maalim Seif Kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema endapo wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kuwaongoza, atalishughulikia suala zima la muungano ikiwa ni pamoja na kuipatia Zanzibar mamlaka yake kamili.

Maalim Seif ameyasema hayo wakati alipokuwa akiwautubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho katika uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti mjini Unguja ambapo viongozi mbali mbali wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi Ukawa akiwemo Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa na Mgombea mwenza wake Juma Duni Haji waliudhuria katika uzinduzi huo.

Aidha Maalim Seif aliwalaumu viongozi wa CCM kwa kudai wamekwenda kuiyuza Zanzibar kwenye Bunge maalum la katiba kwa kuruhusu kupitisha vipengele kandamizi vinavyoinyima Zanzibar mamlaka yake na hivyo ameahidi kushirikiana na Edward Lowassa kulishughulikia suala hilo wakati watakapoingia madarakani.

“Hatuwezi kukubali kabisa kabisa. Tutairejesha rasimu ya Jaji Warioba, na kuomba Bunge la katiba lifanye kazi chini ya muongozo wa rais Lowassa na rais Seif Sharif Hamad” Alisema Maalim Seif .

Hata hivyo Maalim Seif aliwaahidi wananchi wa Zanzibar kuwa katika uongozi wake atazingatia misingi ya demokrasia na utawala bora ili wananchi wake waweze kuishi katika nchi yao kwa amani na utulivu.

“Nataka nikiwa rais wenu nianzishe misingi ya utawala bora ili nyinyi wananchi muishi katika nchi yenu bila ya woga, bila ya hofu na mwende kifua mbele kwa kujifakharisha na nchi yenu. Siwezi kukubali kumuona Mzanzibari yoyote anadhalilishwa” Aliongeza Maalim Seif.

Pia aliongeza kwa kusema atahakikisha mashekhe wa Kizanzibari waliopelekwa katika mahakama za Tanzania bara wanarudishwa mara moja katika mahakama ya Zanzibar ili waweze kuhukumiwa Zanzibar.

“Nashangaa tunaambiwa nchi hii ina rais, nchi hii ina Baraza la Wawakilishi na pia ina mahakama. Mahakama kuu ya Zanzibar ina uwezo sawa na mahakama kuu ya Tanzania bara. Leo viongozi wajuu wenye mamlaka katika nchi hii bila ya kutushauri sisi wenzao katika Serikali wameamua mashekhe wetu kuwapeleka bara. Mimi nasema nikiwa rais watarudi hapa hapa Zanzibar na kama wana makosa watahukumiwa na mahakama za hapa Zanzibar” Alifafanua.

Akizungumzia Uchumi wa Zanzibar, Maalim Seif alisema wakati atakapokuwa madarakani ataujenga na kuimarisha Uchumi wa Zanzibar ambapo alikumbusha kuwa ahadi yake ya kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika ya Mashariki bado iko pale pale.

“Tutaibadilisha Zanzibar iwe Singapore ya Afrika ya Mashariki.Tutaweza kuakikisha tunajenga Bandari ya kisasa sio kwa maneno lakini kwa vitendo” Alifafanua.

Hata hivyo alisema atafungua benki ya uwekezaji ya Wazanzibari ambayo itatoa mitaji na mikopo kwa wanachi wa Zanzibar ili waweze kujiajiri wenyewe.

“Wale vijana watakaojishughulisha na uvuvi au kilimo, hiari yao! Benki itakuwepo, itatoa mikopo tena mikopo nafuu, masharti nafuu na kila mmoja ataweza kumudu na kujiendeleza maisha yake” Aliongezea.

Pamoja na hayo mgombea huyo ambaye alionekana kuzikonga nyoyo za wananchi waliohudhuria katika mkutano huo na kushagiliwa kila wakati aliwaeleza wananchi hao kuwa atalisimamia kikamilifu suala la mafuta na gesi kwa kuunda wizara mpya ya mafuta na gesi ambayo itashughulikia suala zima la mafuta na gesi pamoja na kuandaa sera na sheria zake zitakazosimamia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya maridiano ya Zanzibar, Mzee Hassan Nassor Moyo amewataka wananchi wa Zanzibar kumchagua Maalim Seif kwani ni kiongozi anayejali maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari.

Aidha Moyo amewataka wananchi hao kutowachagua Wabunge na Wawakilishi wa CCM ambao kazi yao ni kuhubiri chuki na ubaguzi kwani kufanya hivyo kutapelekea kuwagawa Wazanzibari ambao wako kitu kimoja.

Naye Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa amesema Chama Cha Mapinduzi kimeshindwa kuendesha kampeni za kistaarabu kutokana na kitendo chao cha kuyapachua na kuyachana mabango ya wagombea wa Ukawa jambo ambalo amelitaja kuwa ni kinyume na taratibu.

Pamoja na hayo Lowassa aliongeza kuwa CCM hawatoweza kuiba kura kwani wamejipanga vizuri kwa ajili ya kuzilinda kura zao na hivyo amewataka wananchi wa Zanzibar kuwaunga mkono yeye na Maalim Seif kwa kuwapigia kura kwa wingi kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Kwa upande wake Msaidizi Meneja Kampeni, Mansour Yussuf Himid amelikosoa vikali jeshi la Polisi kwa kudai jeshi hilo limekuwa likiwadhibu kwa kuwapiga na kuwalawiti wananchi badala ya kuwalinda.

Aidha amesema mfumo wa Muungano uliopo sasa hauna maslahi kwa Zanzibar kwani umekiuka malengo yote ya Muungano ambayo yamewekwa na muasisi wake ambaye ni Mzee Abeid Aman Karume.

“Mzee wetu Karume alipindua ili tujitawale, tusimamie haki kwa Wazanzibari wote, lakini CCM wamekosa radhi na muda wao wa kuondoka madarakani umefika” Alisema.

Alisema wanaitaji kiongozi atakayesimamia utu,umoja na misingi ya muungano kwa Wazanzibari ambaye kwake yeye anamuona Maalim Seif Kama mtu sahihi wa kushika nafasi hiyo kutokana na kujitolea kwake katika kutetea maslahi ya wazanzibari.

Chama Cha Wananchi CUF hapo jana kimezindua rasmi kampeni zake za uchaguzi mkuu kwa upande wa Zanzibar ambapo leo watakuwepo Kwenye uwanja wa Tibirinzi kisiwani Pemba kuendeleza kampeni zao.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s