Hamad Rashid, Wananchi hawahadaliki kwa siasa nyepesi

Kwanza napenda kuanza makala hii kwa kumnukuu nguli wa fasihi ya Kiswahili na kada maarufu wa chama cha mapinduzi Muhammed Seif Khatib. Katika moja ya hadithi yake fupi ijulikanayo kama “Juzi na jana si kama leo” iliyomo katika kitabu chake maarufu cha “Kipanga”, Muandishi huyu anasema

“Kila nyakati na watu wake. Fikira hubadilika. Mawazo hugeuka. Utashi nao husahaulika. Mawazo ya mwananchi hayajaganda kama barafu! Fikira sio yabisi! Akili na mawazo haya ni ya watu sio wanyama. Wanaweza kudananywa mara moja mbili lakini sio daima dawamu. Ghiliba kwao haidumu. Leo haiwi leo kila siku! Leo ni siku tuliyonayo. Mambo yake na watu wake wanakuwa na tabia za kileo”

Haya ni maneno kuntu ya nguli wa fasihi mzaliwa wa Umbuji kisiwani Unguja Muhammed Khatib . Ukiutazama mwenendo mzima wa hali ya kisiasa nchini mwetu utagunduwa kuwa maneno aliyoyasema (Rejea nukuu ya hapo juu) yanasadifu moja kwa moja na hali ya kisiasa tuliyonayo. Wananchi sasa wameshashtuka kutoka katika usingizi mzito ulioambatana na kiza totoro.

Kwa bahati mbaya sana wapo baadhi ya wanasiasa wanaowaona wananchi kama wagonjwa wa akili wasiojua kusi wala kaskazi, mchana wala usiku na mbivu wala mbichi. Miongoni mwao ni kada wa Zamani wa Chama Cha Wananchi CUF na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Muhammed ambaye kwa sasa ni mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC).

Ni hapo juzi tu ambapo kada huyu alifika katika Ukumbi wa Salama Hall wa hoteli ya Bwawani kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea kiti cha uraisi wa Zanzibar. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha alimkabidhi Hamad Rashid fomu zake na akamsomea taratibu za ujazaji wa fomu hizo sambamba na sheria ambazo zinapaswa kufuatwa.

Mara baada ya kupokea fomu zake, kada huyu alizungumza na waandishi wa habari. Alitumia muda mwingi kujisifu na kujitapa kuwa yeye ndiyo suluhisho pekee la kuwatoa Wazanzibari kutoka kwenye minyororo ya dhiki na tabu, na kuwapeleka kwenye Zanzibar mpya yenye kila aina ya raha na maendeleo makubwa. Unafiki ulioje.

Alipoulizwa baadhi ya maswali yenye kujenga hoja ndani yake, alionekana kusuasua na kujaribu kuupindisha ukweli.

Katika moja ya maelezo yake, Hamad Rashid alisema atakapochaguliwa na wananchi wa Zanzibar kuwa rais, basi atahakikisa kuwa ataheshimu mawazo ya wananchi pindi watakapoamua wenyewe kufanya maamuzi juu ya nchi yao likiwemo suala zima la katiba.

Nilipatwa na mshangao kidogo. Nilijiuliza ni mawazo ya gani na katiba ya sayari ipi anayoizungumzia mkereketwa huyu? Kwa bahati nzuri si kuwa peke yangu tu ambaye nilikuwa na mshangao huo. Wapo baadhi ya wengine waliokuwa wakinon`gona chini kwa chini ishara ya kutokielewa kile alichokuwa akikizungumza.

Mshangao wangu ulikuja baada ya kuona kuwa Hamad Rashid ndiye aliyeshirikiana na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi katika kuiuza Zanzibar kwa Tanganyika kwenye Bunge Maalum la Katiba. Wabunge wa CCM kutoka bara na Zanzibar walishirikiana kikamilifu katika kuyachakachua maoni ya Wananchi na kuingiza ajenda zao ambazo zitaleta tija kwao na chama chao.

Vyama vya upinzani vikiongozwa na CHADEMA, CUF na NCCR Mageuzi vilidiriki kutoka katika Bunge hilo baada ya kuona Chama Cha Mapinduzi kinajaribu kuchakachua maoni ya wananchi lakini kwa upande wake Hamad Rashid, aliungana na wahafidhina weningine wa CCM kuiangamiza Zanzibar kwa kuweka vipengele ambavyo vinaiangamiza moja kwa moja.

Leo hii anakuja kujitapa kuwa yeye ni Mzanzibari mzalendo na kwamba ataheshimu maoni ya wananchi wake. Sasa hapa wengi wetu tunajiuliza kama lengo lake ni kuheshimu mawazo ya wananchi na kuitetea Zanzibar, mbona hakuonesha mfano huo kwenye Bunge Maalum la Katiba?. Huo ni unafiki na uzandiki ambao haupaswi kufumbiwa macho hata kidogo.

Kiongozi anayepaswa kuchaguliwa na wananchi kuiongoza Zanzibar, ni Yule ambaye atajitolea kwa hali na mali katika kutetea maslahi mapana ya Zanzibar. Kwani Zanzibar ndiyo mama yetu. Sisi sote Wazanzibari tunatoka katika tumbo la mama yetu huyu mpendwa. Tumezaliwa, tumekuwa, na tutakufa tukiwa na utambulisho wetu wa uzanzibari. Yoyote Yule anayehatarisha uhai wa mama yetu huyu (Zanzibar) ni wa kumpisha mbali, na ni wa kuogopa kama ukoma.

Wakati mahojiano yakiendelea baina ya Hamad Rashid na waandishi wa abari nilibahatika kumuuliza swali, swali lenyewe lilikuwa hivi: “Mheshimiwa Wazanzibari wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu juu ya swala zima la Muungano, wengi wanasema muungano uliopo hauna tija kwao kwani unaikandamiza zaidi Zanzibar. Rasimu ya katiba ya Jaji Warioba ilifufua matumaini yao na waliiyona kama muarubaini tosha wa kutatua kero hizo, lakini kwa bahati mbaya sana wajumbe wa Bunge maalum la Katiba waliobakia kwenye Bunge hilo kwa kiasi kikubwa walitengua maoni yao na kubwa zaidi wewe ulikuwa ni sehemu ya wajumbe hao. Sasa una lipi la kuzungumza ili wananchi wa Zanzibar wajenge imani na wewe?”

Swali hilo lilionekana kumchoma na kumfukuta ndani kwa ndani, alianza kupepesa macho, akili ilimruka na damu ikampauka na hakujua ajibu nini, ghafla akaanza kutoa maelezo yasiyo na mashiko badala ya kujibu swali. Majibu aliyoyatoa yalikuwa haya: “Unajua napenda kusema kitu kimoja, Wazanzibari wanataka maendeleo ili waweze kuondokana na maisha magumu. Kwa hivyo hatuwezi kuvunja muungano kwani kufanya hivyo ni kuwanyima fursa Wazanzibari walio wengi kufaidika na rasilimali zilizoko Tanzania bara”

Majibu ya kustaajabisha sana. Hivi tujiulize yale maadini yaliyoko Geita na Mwadui Mkoani Shinyanga, yamemnufaisha vipi mzanzibari? Au ndiyo kuwaona Wazanzibari kuwa si watu wenye upeo wa kuyafikiri mambo kwa kina? Au ndiyo kufilisika kisiasa huko? Ni vyema kada huyu angetoa maelezo ya kutosha juu ya vipi Zanazibar na Mzanzibari ananufaika na rasilimali zilizoko Tanganyika na sio kutoa maelezo yasiyokuwa na mshikamano wa hoja (Premises) ndani yake.

Ni muda mrefu sasa, kiongozi huyu amekuwa akienda kaskazini na kusini, Mashariki na Magharibi mwa viunga vya Zanzibar na kunadi kuwa Wabunge pamoja na Wawakilishi wa Zanzibar waliotoka katika Bunge Maalum la Katiba wameisaliti Zanzibar na kumuacha yeye peke yake kuitetea.

Kwa hakika muda tulionao sasa ni vigumu kuwadananya wananchi kwa siasa nyepesi namna hiyo.Sasa mbona yeye hakuonesha mfano wa utetezi wake huko bungeni? Alichokifanya ni kutumia mwanya ule kuiangamiza zaidi Zanzibar. Alieka uzalendo nyuma na kuangalia maslahi yake binafsi.

Zanzibar inahitaji kiongozi mchapakazi, mzalendo na mwenye uchu wa kuwaletea maendeleo Wazanzibari. Ili upewe mamlaka ya kuiongoza dola ya Zanzibar ni lazima uwajaze imani wananchi na wakuone kuwa wewe ni mtu sahihi wa kuweza kulisimamia hilo. Vyenginevyo watakususia. Mheshimiwa Hamad Rashid ameshindwa kuonesha mfano wake tu! kwenye Bunge Maalum la Katiba, jee wananchi watamuaminije kwenye kwenye nafasi ya uraisi? Zama za kuwadanganya wananchi zimeshapitwa na wakati. Ni vyema ukajipanga upya!.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s