Maalim Seif achukua fomu ya Kugombea urais, aeleza mazito

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, jana alichukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar ikiwa ni mara ya tano safari hii chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Kiongozi huyo ambaye ni katibu Mkuu wa CUF, aliwasili Ofisi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC eneo la Bwawani akisindikizwa na viongozi wa ngazi za juu wa vyama vinavyounda Ukawa.

Waliomsindikiza Maalim Seif katika safari mbali na mamia ya wafuasi wake, ni pamoja na mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa na mgombea mwenza, Juma Duni Haji.

Katika hafla hiyo, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe aliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu, huku chama cha APPT-Maendeleo kikituma ujumbe wake katika hafla hiyo.

Mbali na kuungwa mkono na Ukawa, safari hii Maalim Seif yuko bega kwa began a waliokuwa vigogo wa CCM wakiwa mashuhuri na wasindikizaji wake.

Miongoni mwa kigogo aliyeshuhudia akipokea fomu kutoka kwa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, ni mmoja wa waasisi wa CCM na Maridhiano ya Zanzibar, Mzee Hassan Nassor Moyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Maalim Seif alisema mambo atakayoyashughulikia pindi atakapochaguliwa kuwa rais wa Zanzibar ni yale yote yanayomgusa Mwananchi moja kwa moja.

“Kwa kweli, kwa hali ilivyo katika nchi, mambo mengi yanahitaji kushughulikiwa, karibu yote kabisa. Lakini vipao mbele ni yale mambo yanayomgusa mwananchi moja kwa moja. Umasikini ambao Wazanzibari walio wengi wamo katika hali hiyo, afya bora ya uhakika, elimu bora ambayo itamfanya kijana yoyote yule atakapomaliza awe na sehemu ya uhakika ya kujiajiri au kuajiriwa na kujenga na kuimarisha uchumi wa Zanzibar”

Pia Maalim Seif aliilaumu tume hiyo kwa kusema kuwa bado haijabadilika na haina umakini hasa kwa kushindwa kuweka bayana mipaka ya majimbo mapya ya uchaguzi yaliyotangazwa hivi karibuni.
Alisema hali hiyo inawachanganya na kuwanyima fursa ya msingi wapiga kura na kuwapa shaka wananchi wa Zanzibar katika kutekeleza haki yao ya kidemkrasia.

Maalim seif alisema kuwa hata Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, ameshindwa kutekeleza ahadi aliyoitoa mara tu alipotangazwa kushinda nafasi hiyo, Oktoba 31, 2010 ya kufanyia marekebisho sekretarieti ya Tume hiyo.

“Wakati wa kutangazwa matokeo ya uchaguzi mwaka 2010. Niliwahi kumwambia Rais Shein ambaye kwa wakati huo alikuwa rais mteule kuwa kuna mambo ayafanyie marekebisho, na moja ilikuwa ni Tume ya Uchaguzi. Na yeye alipojibu akaahidi umma pale kuwa atayashughulikia yote niliyosema. Nasikitika sana kusema, Sana! Sana! Sana! Kuwa mpaka sasa hakuna hata jambo moja ambalo mwezangu Yule kayafanya. Pamoja na mimi kumuandikia barua mara tatu kumkumbusha, kwamba ulitoa kauli hii, lakini hakuna lolote lililofanywa”

Hata hivyo Maalim Seif alitoa changamoto kwa wagombea wengine wa urais wa Zanzibar akiwemo Dk Shein, watamke na kukiri kwamba watakubali matokeo ya kushindwa iwapo uchaguzi huo utakuwa wa huru na wa haki.

Tumejiandaa
Maalim Seif alisema safari hii chama chake na safu yote ya upinzani wamejiandaa vya kutosha kwa ajili ya ushindi, licha ya kile alichokitaja kama hujuma, vitisho na mizengwe kutoka chama tawala.

Aliyataja mafanikio aliyoyapata hivi karibuni katika ziara yake ya Mafya na Mkoa wa Lindi kuwa ni pamoja na kuvuna wanachama 1,200 hatua aliyosema ni ukomavu mkubwa wa chama hicho.

Kiongozi huyo alirejea kauli yake kuwa mara hii CUF haitokubali kupokwa ushindi endapo itashinda kihalali.

Aliahidi kwa niaba ya Ukawa kuwa, upinzani utafanya kampeni kuanzia uzinduzi Agost 29 Jijini Dar es Salaam na Septemba 7, kwa upande wa Zanzibar kwa kunadi sera na maendeleo, si fujo, matusi wala vyenginevyo, ili kushawishi na kuhakikisha umma wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, unaelekeza kura zao upande huo na kuleta ushindi wa kihistoria.

Leave a comment