NEC ijipambanue kama mtoa haki wa kweli

Hakuna anayeweza kubisha kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), sasa inakabiliwa na wakati mgumu pengine kuliko wakati mwingine wowote katika kipindi cha miaka 38 ya uhai wake. Tangu izaliwe kwa Katiba ya mwaka 1977 na sheria ya Bunge, NEC imekuwa ikisimamia na kuendesha chaguzi mbalimbali nchini pasipo kukabiliwa na misukosuko mikubwa kama inayojitokeza hivi sasa ambapo mchakato wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu tayari umeanza. NEC isipokuwa makini, ikateleza kwa namna yoyote katika masuala ya msingi, itauweka pabaya mustakabali wa Taifa letu.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Tanzania, Jaji Mstaafu Damian Lubuva.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Tanzania, Jaji Mstaafu Damian Lubuva.

NEC imepitia katika baadhi ya majaribio, ingawa majaribio hayo siyo makubwa kama yale yanayoikabili kwa sasa. Tumeshuhudia jinsi ilivyopata misukosuko katika mchakato wa uandikishaji wa wapigakura katika Daftari la Kudumu siyo tu kutokana na mchakato huo kuanza ukiwa umechelewa, bali pia kutokuwapo fedha, watumishi wala vifaa vya kutosha. Mchakato huo sasa umemalizika, ingawa uliendeshwa katika mazingira yaliyojaa sintofahamu na changamoto kubwa. Wananchi walifurika na kukesha katika vituo vya kupigia kura wakisubiri kujiandikisha. Mashine chache za kielektroniki (BVR) zilizotolewa kwa kazi hiyo zilikuwa zikifanya kazi kwa kusuasua na kusababisha kizaazaa cha aina yake.

NEC inakabiliwa na mtihani mgumu zaidi sasa kutokana na uchaguzi wa mwaka huu kuwa na ushindani wa aina yake ambao haujawahi kutokea tangu vyama vingi vya siasa vianzishwe mwaka 1992. Ni vigumu kutabiri ni upande upi utaibuka mshindi katika uchaguzi ujao. Kampeni za uchaguzi hazijaanza, lakini dalili za awali zinaonyesha kwamba NEC inaweza kusababisha mtafaruku iwapo haitajipanga vizuri na kuhakikisha inatoa haki kwa vyama vyote katika uchaguzi huo pasipo ubaguzi au upendeleo.

Katika mazingira hayo, NEC itafanya makosa makubwa iwapo itapuuzia malalamiko ya vyama vinavyoshiriki katika uchaguzi huo bila kuyafanyia kazi. Huko nyuma NEC ilikuwa ikipuuza au kutupilia mbali bila ya kuyafanyia kazi baadhi ya malalamiko ya vyama vya siasa yaliyokuwa yakielekezwa kwa mamlaka mbalimbali. Matokeo yake ni vyama ambavyo havikuridhika na mchakato wa chaguzi hizo kutotambua matokeo. Sisi tunadhani kwamba huu sasa ni wakati ambapo NEC inalazimika kutega sikio kwa kila tukio linalojitokeza, ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi kauli tata  zinazotolewa na vyama shiriki na asasi mbalimbali.

Mifano ipo mingi kwani kuna viongozi wa vyama ambao wamekuwa wakitoa kauli mbalimbali ambazo kwa namna fulani zinaweza kuwatisha wananchi.

Ni jambo la kawaida kwa kipindi kama hiki kusikia tuhuma mbalimbali zikitolewa na viongozi wa vyama vya upinzani, tena tuhuma nyingi huwa hazijafanyiwa kazi. Hiyo ni hatari kwa sababu zinapowafikia wananchi wanaweza kufanya lolote na kuhatarisha amani ya nchi. Tuhuma nyingine ni kuwapo waraka unaoagiza vyombo vya dola kukusanya vitambulisho vya kupigia kura vya watumishi wake. Pia imedaiwa na mmoja wa viongozi wa juu wa upinzani kwamba chama tawala ni hodari wa kuiba kura.

Tuhuma hizo zinahitaji ushahidi, lakini NEC inapaswa kuwa makini zaidi na kuzifanyia kazi zote.

Tunaishauri NEC iratibu mwenendo wa vyombo vya dola katika uchaguzi huo na kuhakikisha viongozi wa vyama vyote wanazingatia makubaliano waliyosaini kuhusu suala hilo. Ni kwa kufanya hivyo Tume hiyo itajipambanua kama mtoa haki wa kweli na kuepusha mifarakano isiyo ya lazima.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s