Kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi

Hali ya kisiasa nchini Tanzania inaendelea kuchukua sura mpya kadiri siku zinavyosonga mbele kuelekea uchaguzi mkuu hapo Oktoba 25 mwaka huu. Wanasiasa wamekuwa wakihama vyama vyao na kuhamia vyengine wanakoona kuna tija kubwa kwao. Viko vyama vilivyopata athari kubwa baada ya makada wao kuvuhama vyama hivyo na kuhamia vyama vyengine ili kuendeleza harakati zao za kisiasa.

Mwenyekiti chama cha wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akilakiwa na wanachama wa chama hicho alipokuwa akiwasili katika ukumbi wa mkutano kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea urais  kupitia CUF Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, akilakiwa na wanachama wa chama hicho alipokuwa akiwasili katika ukumbi wa mkutano kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia CUF.

Miongoni mwa makada waliovihama vyama vyao na kujiunga na vyama vyengine ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kasulu Mjini, Moses Machali aliyetoka NCCR MAGEUZI na kujiunga na chama cha ACT Wazalendo kuungana na kada wa zamani wa CHADEMA, Zitto Zuberi Kabwe. Wengine walivihama vyama vyao ni mbunge wa Kahama, James Lembeli na mbunge wa viti maalum Ester Bulaya, ambao wote wanatoka katika chama cha mapinduzi (CCM).

Haikuishia hapo tu, chama cha CCM kilikumbwa na dhoruba ya kupoteza wanachama wake nguli ambapo aliyekuwa wazairi mkuu wa zamani Mheshimiwa Edward Lowasa alikihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinachounda UKAWA baada ya kile alichosema hakutendewa haki na chama hicho. Kujiunga kwa Lowasa na CHADEMA, kulifungua milango kwa utitiri wa wafuasi wa kada huyo kujiunga na upinzani. Madiwani wengi na wenyeviti waliokuwa wakimuunga mkono kada huyo walihamia Chadema.

Licha ya kuhama kwa Lowassa ndani ya CCM bado chama hicho kilijitapa kwa msemo unaosema “kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi” na kuahidi kuingia ikulu kwa kishindo kikubwa.

Ukiachia makada wa CCM kujiuga na Chadema, lakini pia wapo wengine waliojiunga na vyama vyengine vya siasa kama vile ADC, NCCR, CUF na vyama vyengine. Hiyo ndiyo hali tuliyonayo hivi sasa katika siasa zetu za Tanzania. Sijui kama ndiyo ni kukua kwa demokrasia ama vyenginevyo, wataalamu watatuambia.

Katika hali ya kustaajabisha sana, CUF nayo imekumbwa na kadhia kubwa ambapo miongoni mwa makada wake, Mwenyekiti Profesa Ibraahim Lipumba, aliachia ngazi za chama hicho kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo mzima ndani ya UKAWA unajumuisha vyama vya CHADEMA, NCCR, CUF na NLD.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari hapo jana, Profesa Lipumba alisema: “Nimeshiriki katika vikao vingi vya ukawa vilivyotufikisha hapa. Hata hivyo dhamira na nafsi yangu inanisuta kuwa katika maamuzi yetu ua Ukawa tumeshindwa kuenzi na kuzingatia Tunu za Taifa za utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, na uwajibikaji. Rasimu ya katiba na maudhui yake tumeyaweka kando. Waliyoipinga Rasimu ya Katiba ya Wananchi ndani ya Bunge Maalum la Katiba ndiyo tunaamini wataturahisishia kushinda uchaguzi. Tumeshindwa kuongoza maadili.”

Wengi wameshangazwa sana na hoja zilizotolewa na mwanasiasa huyu, wakimtuhumu kuwa kigeugeu. Wako wanaosema kuwa profesa huyu wa uchumi na mwanasiasa mashuhuri ameshindwa kuwa na msimamo thabiti juu ya kile anachokiamini. Ni hivi karibuni tu ambapo Lipumba aliungana na viongozi wenzake wanaounda UKAWA kumpokea Lowassa na kumkaribisha katika umoja huo. Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 27 Julai mwaka huu, ni Lipumba aliyeonekana kumuunga mkono Lowassa jambo ambalo sasa anaonekana kulipa kisogo.

Miongoni mwa aliyonukuliwa akisema siku hiyo ni kuwa: “Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, tujiulize tangu amejiuzulu je, ufisadi umepungua au umeongezeka ndani ya Serikali ya CCM? Kimsingi hili suala la kimfumo tu ndilo linalosababisha ufisadi ndani ya CCM” alisema. Kauli yake hii inaonesha wazi kwamba Lipumba aliunga mkono mia kwa mia ujio wa Lowassa ndani ya UKAWA, lakini kujiondoa kwake uwenyekiti wa CUF kwa ujio huo huo, kunatilika mashaka.

Wasiwasi juu ya kung’atuka kwa Lipumba unasafiri hadi nje kabisa ya ujio wa Lowassa. Mtu anaweza kabisa kudhania kuwa huenda alitakiwa kufanya hivyo na baadhi ya vyama visivyopenda mabadiliko na muenendo mzima wa UKAWA. Angalia, kwa mfano, kuwa ni  hapo juzi tu gazeti la UHURU la Agost 4, 2015 linalomilikiwa na CCM lilipochapisha taarifa katika ukurasa wake wa mbele yanye kichwa cha habari kinachosomeka “Lipumba aachia ngazi.”

Taarifa hii inaonesha wazi kuwa CCM ilijua kila kitu juu ya mustakbali mzima wa Profesa Lipumba na hivyo huenda uamuzi wake wa kung’atuka kwenye nafasi yake uwenyekiti haukuwa bure. Kwa mini CCM iipate taarifa hizi kiasi cha kujiamini na kwenda kuzichapisha kwenye gazeti lao? Haiwezi kumuingia akilini kwa yoyote yule anayefikiri na kuyachambua mambo kwa kina.

Kumekuwa na mazungumzo ya hapa na pale wanaotabiri kuwa CUF kitapoteza dira mara baada ya kuondoka kwa Profesa Lipumba. Hata hivyo, vipo vyama vingi ambavyo vimepoteza wanachama wake ambao walikuwa viungo wakubwa.Kwa mfano, CCM ilimpoteza Agustino Liyatonga Mrema ambaye alikuwa muhimili mkubwa lakini chama hicho kimeendelea kuwepo, Chadema pia waliwafukuza wanachama wao mashuhuri akiwemo Samson Mwigamba, Profesa Kitila Mkumbo pamoja na Zitto Kabwe lakini chama hicho kimekuwa ni mwiba mkali kwa CCM na vyama vyengine vya upinzani. Kwa upande wa CUF, nao wamepoteza makada wake kadhaa akiwemo Fatma Magimbi, Khatib Hassan, Juma Othman ambao walijiunga na CCM, na pia Hamad Rashid ambaye ameungana na chama cha ADC.

Ni hali ya kawaida kwa mwanachama wa chama chochote cha siasa kuhama kutoka kwenye chama kimoja na kujiunga na chama chengine. Kwa sasa ni wajibu wa CUF kulipa kisogo suala la kujiuzulu kwa mwenyekiti wake na kujikita zaidi katika maandalizi ya uchaguzi mkuu hapo Oktoba 25 kwani Waswahili wanasema: “Kuvunjika kwa koleo, sio mwisho wa uhunzi”.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s