Usilolijuwa usiku wa kiza

Wahenga wa Kiswahili husema “usilolijua usiku wa kiza”. Ni kawaida ya mwanaadamu ya kutojua jambo analolifanya kuwa mwisho wake litaleta athari gani, kwake au kwa jamii iliyomzunguka. Binadamu hufanya matendo mbali mbali duniani lakini baadhi yao hujikuta wakijutia yale waliyoyafanya baada ya kuona athari zake.

Muhammed Seif Khatib

Muhammed Seif Khatib

Hali hiyo ndiyo iliyomkumba msomi na mwandishi mashuhuri wa fasihi ya Kiswahili nchini, Muhammed Seif Khatib, miongoni mwao mkusanyiko wa makala zake za safu ya “Kipanga” kwenye gazeti la Mzalendo linalomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho mwandishi huyo ni katika makada wake waliobwagwa hivi majuzi kwenye mbio za ubunge.

Kwenye mkusanyiko na mtiririko huo wa Kipanga kuna makala kadhaa kama vile “Historia haitafutika”, “Wazimu ni ncha saba”, “Mwenye njaa hana chaguo” na “Juzi na jana si kama ya leo” na hii ya mwisho imenivutia zaidi na nitaitumia leo kuonesha kuwa naye Muhammed Seif kuna mambo yaliyokuwa usiku wa giza kwa kutokuyatambua kwake.

Katika hadithi hiyo, mwandishi anakusudia kutueleza kuwa wakati wa mabadiliko unapofika basi hauna alele mama wala sumile. “Kila nyakati na watu wake. Fikira hubadilika. Mawazo hugeuka. Utashi nao husahaulika. Mawazo ya wananchi hayajaganda kama barafu! Fikira nazo siyo yabisi! Akili na mawazo haya ni ya watu sio wanyama. Wanaweza kudanganywa mara moja mbili lakini sio daima dawamu. Ghiliba kwao haidumu. Leo haiwi leo kila siku! Leo ni siku tuliyonayo. Mambo yake na watu wake wanakuwa na tabia ya kileo,” anasema Muhammed Seif.

Ukiyaangalia hayo maneno aliyoyaandika gwiji huyu ni wazi yanamfukuta na kumuunguza ndani kwa ndani, kwani hali hiyo ndiyo iliyopo hivi sasa katika siasa zetu nchini Tanzania. Naam, sadakta mawazo na fikra za wananchi havijaganda, na hivi sasa wanayatafuta mabadiliko kwa udi na uvumba. Ni vigumu kwa sasa kuwadanganya wananchi, wamedanganywa walipodanganywa na sasa wanaonekana wansema basi.

Katika kuonesha kuwa mawazo ya wananchi hayajaganda, na hawadanganyiki tena, imejidhihirisha wazi wazi katika kura za maoni za chama cha mapinduzi ambazo zililenga kuchagua viongozi wa udiwani, ubunge na uwakilishi ambao watapeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao hapo oktoba 25. Muhammed Seif Khatibu na Vigogo wengine wa chama hicho walitupiliwa mbali na wananchi. Wamechezeshwa kwata na kunin`ginizwa kichwa chini miguu juu.Ni hakika wamechokwa. Walikuwa hawawatumikii wananchi na badala yake walikuwa wakitumikia matumbo yao na familia zao. Usaliti ulioje.

Ingawaje tunajua kuwa watapitishwa kupitia kamati yao ya siasa lakini hiyo itakuwa khatari kubwa kwa chama cha mapinduzi, kuwalazimisha wananchi kula chakula wasichokitaka. Ni hakika watakisusia.

Katika utawala wote wa chama cha mapinduzi hadi sasa wananchi wamekuwa wakinyanyanyaswa na kupigwa hususan pale wanapodai haki zao za msingi. Kwa mfano mwaka 2001 jeshi la Polisi likiongozwa na aliyekuwa jenerali wao Mahita, walikwenda kuwauwa kwa kuwamiminia risasi wananchi wa kisiwa cha Pemba wakati walipokuwa wakitekeleza haki yao ya kikatiba kwa kufanya maandamano ya amani. Damu za watu zilimwagika mithili ya maji yanavyotoka mferejini. Mamia ya watu walipoteza maisha. Ni kipidi ambacho Zanzibar ilikuwa inanuka damu.

Zaidi ya hayo, ni hivi juzi tu ambapo wabunge wa CCM walikwenda kuwauzia wazanzibari nchi yao hivi hivi bila ya hata chembe ya uzalendo. Cha kushangaza hata huyu msomi na gwiji wa fasihi ambaye alikuwa akihubiri uzaleno katika vitabu vyake kadhaa alishiriki kikamilifu kuiangamiza nchi ya Zanzibar. Huu ni unafiki wa hali ya juu. Wamekwenda kuwawakilisha wananchi kinyume na maagizo yao na kudiriki kupiga ngoma na kukata viuno baada ya kuwafanyia wazanzibari udhalimu mkubwa kwa nchi yao. Munadhani wananchi hawakumbuki? Hapana wanakumbuka sana na watawahukumu.

Pia, Muhammed Seif Khatib anaendelea kukisifu chama chake cha CCM ambacho kwenye kitabu cha “Kipanga”amekibatiza na kukipa jina la “chama dume” kuwa ni chama chenye uadilifu na chenye sera imara. Hapa muandishi anasema
“Chama dume ni chama chenye “kunyanyasa” wapinzani kwa sera zake nzuri. Chama hiki chenye viongozi wake waadilifu na mahiri kimejidhihirisha umahiri wake katika miaka mine iliyopita”

Sasa hapa inabidi tujiulize jee ni sera gani nzuri walizonazo chama cha mapinduzi? Jee ni uadilifu upi uliomo kwenye chama cha mapinduzi?. Tuaweza kusema kuwa chama kina uadilifu endapo kitatii na kufuata misingi mikuu ya kidemkrasia na utawala wa sheria. Lakini kwa bahati mbaya sana chama cha CCM kinajifanya hamnazo kwa kuipa kisogo misingi hiyo na kujifanya wao kuwa wako juu ya sheria. Huu ni udikteta uliokubuhu.

Ni hivi majuzi tu ambapo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alipoeleza bayana mbinu chafu ambazo watazitumia ili kushinda uchaguzi ujao hapo tarehe 25 Oktoba mwaka huu. Amesema watashinda jaapo kwa bao la mkono. Kwa wasioelewa bao la mkono alilomaanisha kada huyu ni wizi wa kura ambao ndiyo imekuwa ni ngazi katika maisha yao yote ya kupandia kuelekea Ikulu.

Rushwa, ubinafsi, ubabe na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu vimekuwa ni mazoea ya chama cha mapinduzi. Hakuna usawa miongoni mwa wananchi. Vijana wengi hawana ajira kutokana na mfumo mbovu unaoongozwa na chama hicho. Wakati umefika sasa wa kusema basin a wananchi wameonesha kuchoshwa na hayo. Naam ni hakika “Juzi na jana si kama ya leo” Waachwe tu waselemee arijojo.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s