UKAWA tutashinda uchaguzi – Lowassa

Mkutano Mkuu wa Chadema, kwa kauli moja, umempitisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, papo hapo mwanasiasa huyo akasema Chadema itachukua nchi asubuhi.

Mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA, Edward Lowassa.

Mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA, Edward Lowassa.

Lowassa alipitishwa kuwania urais kwa mwavuli wa Ukawa kwa kuungwa mkono na vyama vyote katika “safari ya uhakika”.

Mbunge huyo wa zamani wa Monduli, aliyejiunga na Chadema Julai 28 akitokea CCM, akiwa na mgombea mwenza, Juma Duni Haji aliyejiunga pia na Chadema akitokea CUF, walipitishwa kwa kupigiwa kura ya ‘ndiyo’ na wajumbe wote wa mkutano mkuu huo uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Kabla ya kujiunga na Chadema, Duni alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF – Zanzibar na Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Kiongozi huyo amelazimika kujiuzulu nyadhifa zote ili kuwa mgombea mwenza wa Lowassa kutokana na sheria za vyama vya siasa na uchaguzi nchini kutaka mgombea urais na mgombea mwenza watoke chama kimoja cha siasa.

Lowassa aliyekuwa amevaa shati jeupe na suruali nyeusi alifika ukumbini hapo saa 5.25 asubuhi akiwa katika msafara wa magari manane na kupokewa na mamia ya wajumbe wa mkutano huo huku wakiimba, ‘rais. rais, rais, rais”.

Katika msafara huo, Lowassa akiwa na familia yake, aliambatana na waliokuwa makada wa CCM ambao pia walijiunga na Chadema akiwamo aliyekuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai.

Wengine ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga, aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, huku Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu akisema kuwa viongozi hao wamepewa kadi za chama hicho kwa niaba ya wenzao watakaojiunga na Chadema siku chache zijazo.

Mkutano huo uliokuwa na shamrashamra za kila aina, ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa; NCCR–Mageuzi, NLD na CUF isipokuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa bado amewekwa kando wakati mchakato huo wa kwenda Ikulu ukiendelea.

Wengine waliohudhuria ni mabalozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali, viongozi wa vyama vya siasa vya nchi jirani, wabunge na viongozi wa dini, akiwamo Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe na Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Gratian Mukoba.

Lowassa: Tutachukua nchi asubuhi

Akihutubia mkutano huo mkuu wa Chadema kwa mara ya kwanza, Lowassa alisema chama hicho kupitia Ukawa kitachukua nchi mapema asubuhi Oktoba 25.

Alisema Watanzania wanajua kuwa Chadema wamepania, wamejipanga na wana uhakika wa kukamata dola mwaka huu.

“Nilianza na safari ya matumaini, lakini sasa nasema hii ni Safari ya Mabadiliko nje ya CCM, tutakamata nchi mapema kabisa asubuhi,” alisema Lowassa.

Hata hivyo, Lowassa alitahadharisha kuwa kuing’oa CCM ni kazi kubwa kama hakutakuwa na mipango na malengo huku akisema hakujiunga na chama hicho akiwaza kushindwa na kwamba hana msamiati wa kushindwa na wala hakwenda kwa bahati mbaya, bali alijiridhisha na kukubaliana na familia yake hadi kufikia uamuzi huo.

“Nimekuja Chadema nikijua kuwa kazi ya chama ni kushika dola na kama si hivyo, hakuna sababu ya kuwa chama, nimejiandaa vizuri kushika dola… watu wanasema Chadema haiwezi, Tanu ilipewa nchi ikiwa na miaka saba, sasa ninyi mna miaka 23,” alisema na kushangiliwa.

Aliongeza,“Najua kazi ni kubwa na mnajitolea, ndiyo maana chama kina nguvu na moyo kama CCM ya zamani si ya sasa, ndiyo maana tumeikimbia,” alisema Lowassa.

Alisema atapita kila jimbo kutengeneza mipango ya ushindi kwa kufanya kampeni za kistaarabu huku akionya… “Mradi wasiibe kura zetu.”

Duni aipiga kijembe CCM

Mgombea mwenza, Duni Haji aliirushia kijembe CCM kuwa inafanya wananchi wawe maskini ili iendelee kuwatawala.

Akizungumza baada ya kuteuliwa na chama hicho kuwa mgombea mwenza, Duni alisema, CCM haiwezi kuwasaidia wananchi kutoka kwenye umaskini kwa sababu sera yao ni umaskini.

“Miaka ya 70 hatukuwa na neno changudoa, jambazi wala panya road. Haya yamekuja kutokana na kushindwa kwa utawala wa CCM. Ukawa tumedhamiria kuchukua madaraka ya nchi hii ili kuleta mabadiliko,” alisema.

Alisema wananchi wamejenga imani na matumaini kwa makubaliano yaliyofanyika jangwani, walipotia saini hati ya makubaliano inayoruhusu vyama kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja kwenye kila nafasi ya uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Akimzungumzia mgombea urais, Duni alisema: “Siyo jambo rahisi kufanya uamuzi mgumu kama aliofanya Lowassa. Wengi bado wapo CCM licha ya kuwa hawapendi mfumo wa chama chao, alichokifanya Lowassa ni ujasiri mkubwa.”

Hata kwake, alisema halikuwa jambo rahisi kuihama CUF na kujiunga na Chadema. Alisema kuwa alikubaliana na viongozi wake, Profesa Lipumba na Maalim Seif Sharif Hamad aende Chadema ili Ukawa ilete ukombozi katika Taifa.

“Profesa Lipumba ananipenda sana na ananikubali haswa… na anajua kuwa hiki ni kifaa. Lakini alikubali nijivue uanachama wa CUF ili niende Chadema kuongeza nguvu ya kuleta mabadiliko, nina imani Ukawa tutashika dola ifikapo Oktoba 25,” alisema.

Alisisitiza kuwa Ukawa ndiyo ufumbuzi wa matatizo ya Watanzania akisema umoja huo unaungwa mkono na wananchi wengi, hivyo hana shaka kwamba utashinda katika uchaguzi ujao.

“Nilikuwa mwanachama wa ASP nilipokuwa kidato cha pili. Nilipoona mambo yanabadilika nami nilibadilika. Lengo kuu la kupigania uhuru lilikuwa ni Mwafrika kumtawala Mwafrika mwenzake ili amlinde, lakini lengo hilo sasa limepotea.

“Ninashangaa kuona askari wa kimaskini aliyepewa bunduki kuwalinda wananchi, anageuka na kuwapiga risasi maskini wenzake, huu ni udhalimu uliotengenezwa na Chama cha Mapinduzi,” alisema.

Ajenda zabadilika

Awali, Mbowe alitangaza kubadili ajenda za mkutano huo ili kuifanya siku ya jana kuwa ya kihistoria, ikiwa ni pamoja na kuwahoji wajumbe wa mkutano kama wanataka kupiga kura ya ‘ndiyo’ au ‘hapana’ au kura ya siri kupitisha mgombea urais na mgombea mwenza na kujibiwa, “Tunataka kura ya ndiyo na hapana.”

“Tunapopigania ndoto ya Taifa lazima tukubaliane kushirikiana na ili ndoto itimie tunamhitaji kila Mtanzania ambaye yupo tayari kushiriki nasi kutafuta ndoto hiyo, waliopo CCM na wasio na vyama vya siasa. Tunahitaji Watanzania wa makabila yote, dini na rangi zote,” alisema Mbowe.

Alisema Mungu yupo na Chadema na katika aina yake ya utendaji wa miujiza kila jambo linalotokea katika chama hicho linatokana na mpango wake.

“Ili tulibadilishe Taifa hili, hatuwezi kujenga uadui wa kudumu. Ili tuyapate mabadiliko ya kweli tunamhitaji kila mmoja ambaye Mungu amempa karata zake, nguvu zake na kupewa kidogo na kikubwa na kwa pamoja tutaunda jeshi la pamoja,” alisema.

Alisema katika safari hiyo wakubaliane kuwa ndoto ya Taifa ni kubwa kuliko mahitaji ya kila mmoja.

“Ushirika wetu una maana pale ambapo tutakubaliana kila mmoja wetu kwa nafasi yake, kuanzia udiwani, ubunge na urais na kazi nyingine yoyote ya kuongoza Watanzania.

“Haya mambo (ya kusimamisha mgombea mmoja) yanahitaji kujitoa, ndoto ya Taifa haiwezi ikatimia kama kila mmoja atatanguliza matakwa yake binafsi. Fursa ni nadra na hiyo fursa inayopatikana kwa u-nadra huo isipotumika historia itatuhukumu,” alisema.

Alisema viongozi wa Chadema ni lazima wajitolee ili kwa pamoja, kupitia Ukawa waweze kufika safari yenye malengo ya kutimiza ndoto ya Taifa.

“Lakini ndoto hii si ya mtu mmojammoja, familia mojamoja au ukoo. Ni ndoto ya Taifa,” alisema.

Alisema Chadema kinapokea wanachama kutoka chama chochote wenye malengo safi na kuwa kwa miaka 25, kimepigana kuingia Ikulu huku viongozi wake wakijitolea.

“Kwenye safari hiyo ya miaka 25 wapo waliokufa, waliopata vilema, waliofukuzwa kazi kwa kusimamia walichokiamini, waliofungwa magerezani na wapo waliohama nchi. Safari hii haikuongozwa na Chadema pekee, iliongozwa na vyama vyote vinavyounda Ukawa.

“Wapo tunaowaita magamba nao wakaamua kimagamba magamba wafunge safari ya matumaini. Wakafunga safari yao wakiitafuta haki na kweli katika nchi hii,” alisema Mbowe.

Alisema walioanza safari ya matumaini waliongozwa na dhamira kwa lengo la kujitoa unyonge na kujifungua minyororo ya chama chao, ili kuitafuta haki na dhamira yao nje ya chama chao.

“Chadema na Ukawa nchi nzima, watu hawa (walioanza safari ya matumaini) hatuna haki na sababu ya kuwahukumu, tuna kila sababu ya kuwatia moyo na kuwaunga mkono na kuwakaribisha miongoni mwetu ili ndoto ya Taifa hili ikatimie,” alisema.

Alisema wanaojiunga Chadema na waliopo ndani ya chama hicho wote ni binadamu na kwamba watakaojiunga na chama hicho na Ukawa wataishi kama wanavyoishi wanachama wa vyama vinavyounda umoja huo.

“Sisemi wanaokuja Chadema hawana dhambi wote, hata sisi wana–Chadema tuna dhambi zetu, uongo?” aliuliza Mbowe na kujibiwa na wanachama, ‘ndiyooo.’

“Sisi ni nani, hiki ni chama cha siasa na siasa ni watu. Chama cha siasa si mahakama.”

Alisema kuna kila sababu ya chama hicho kujenga utamaduni uliozoeleka wa kuwakaribisha Watanzania wengine katika chama hicho ambao wanaamini kupitia Chadema na Ukawa kuwa ndoto ya Taifa inakwenda kutimia.

Alisema Chadema imejengwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia na kifamilia na ndani ya chama hicho, hakuna aliye mkubwa kuliko mwingine.

“Tukikubaliana kusonga mbele tunasonga mbele. Mnaokuja Chadema tusaidieni kulinda umoja wetu na yale mabaya mliyokuwa nayo katika chama chetu cha zamani tumewasamehe na huku mtuletee mazuri yote mliyopata katika chama chenu cha zamani…”

“Vyama vya siasa ni vyombo vya uchaguzi ni magari na madaraja ya kutuvusha kwenda katika ndoto ya Taifa.

“Watu wanashangaa leo kuambiwa kuwa Duni ndiyo mgombea mwenza wa Ukawa. Huyu (Duni) mpaka jana (juzi), alikuwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ila kwa sababu ya uzito wa ndoto ya Taifa, ameona ajiuzulu uwaziri ili kusaidia kufanikisha ndoto,” alisema.

Akizungumzia katiba ya chama hicho kuhusu kupitisha mgombea urais alisema, “Katiba ya Chadema imetoa maelekeo jinsi ya kumpata mgombea urais na mgombea mwenza. Kifungu cha 7.16, kinazungumzia kazi za Kamati Kuu, ikiwamo ya kufanya utafiti wa wagombea wa urais na mwenza na kuwasilisha ripoti kwa Baraza Kuu kwa ajili ya mapendekezo kwa Mkutano Mkuu. Kamati Kuu ilifanya utafiti.”

Alisema katika utafiti huo, Kamati Kuu kwa kauli moja, ilipendekeza kwa Baraza Kuu la chama hicho Lowassa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na ikapendekeza vyama vinavyounda Ukawa kutoa mapendekezo yao kuhusu uamuzi huo.

“Halikuwa jambo jepesi na tulipishana kauli hadi usiku wa manane. Utafiti wetu mbalimbali ulituambia kwamba Lowassa akipeperusha bendera kupitia Ukawa na kundi lake kubwa ndani ya CCM ndoto za Taifa hili zinakwenda kutimia.”

“Wote, akiwamo Dk Slaa walikubali. Tulimwalika Lowassa katika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema na kumhoji, pengine watu wa pembeni walishauri tofauti lakini vikao vya chama viliamua kuwa Lowassa ndiyo mgombea,” alisema.

Akizungumza wakati akifunga mkutano huo alisema, “Tumekubaliana kuunganisha nguvu kwa utaratibu huu, wapo wabunge ambao watakosa nafasi, watakaokosa nafasi naomba tuvumiliane na hii ni kwa wanaogombea udiwani, ubunge na urais. Watu ni wengi na utaratibu huu lazima utawaacha wengine kando. Watakaoachwa waendeleze moto wa kukiimarisha chama.”

Mkutano wenyewe

Mkutano huo ulianza kwa wajumbe wengi kutiririka katika eneo la ukumbi huo kuanzia saa tatu asubuhi wakisubiri kugawiwa sare za mkutano huku asilimia kubwa wakiwa wamevaa vitambulisho vyenye picha na maandishi… ‘Lowassa 2015.’

Viongozi wakuu na wageni maalumu walianza kuwasili saa 4:10 asubuhi wakiongozana na Kaimu Katibu Mkuu, Salum Mwalimu na kufuatiwa na wenyeviti wenza wa Ukawa, Maalim Seif na Mbowe.

Wafanyabiashara nao hawakusita kutafuta riziki pale walipojitokeza kuuza nguo na mapambo mbalimbali kama skafu, kofia, beji na mabango yenye picha ya Lowassa.

Tofauti na ilivyozoeleka, idadi ya wafuasi nje ya ukumbi haikuwa kubwa kumsindikiza Lowassa na hata alipoingia saa 5.25 asubuhi hawakuwa wameugundua msafara na baada ya kung’amua walianza kuimba “rais, rais, rais.”

Asilimia kubwa ya wafuasi waliojitokeza, walivalia fulana za chama hicho zenye mistari ya rangi nyekundu, nyeupe, bluu na nyeusi huku wengine wakiwa wamevalia fulana zenye maandishi ya 4u Movement na “Zuia goli la mkono 2015”.

Barabara ya Sam Nujoma, hadi eneo lote la Mlimani City ulipokuwa ukifanyika mkutano huo lilipambwa kwa bendera za Chadema na kuchagizwa na sare na wajumbe hao kiasi cha kufanya rangi zinazotumiwa na chama hicho kutawala.

Ulinzi uliimarishwa kila kona ukihusisha askari polisi na walinzi wa chama hicho, “Red Brigade” ambao walikuwa na kazi ya kuwarudisha nyuma wafuasi waliokuwa wakiwakimbilia viongozi mbalimbali kwenda kuwasalimia.

Eneo lote la Mlimani City lilijaa magari kiasi cha baadhi ya wajumbe wa mkutano huo kukosa maegesho na kulazimika kuegesha nje.

Kabla ya kumkaribisha Mbowe, Mwalimu alielezea shughuli na mikakati mbalimbali iliyofanywa na chama hicho katika kujiimarisha na kuongeza uimara na Ukawa.

Alisema Ofisi ya Katibu Mkuu ilifanya mambo makuu matatu ambayo ni kutoa hamasa kwa makada wote, kufanya oganaizesheni mbalimbali za chama na kutekeleza agizo la kufanya usajili wa makada wapya kutoka vyama vingine, hususan CCM.

Katika oganaizesheni, alisema walifanya mafunzo kwa viongozi wote wa chama na watiania na kuimarisha kanda 10 za chama hicho.

Huku akifananisha usajili wa wafuasi kutoka vyama vingine kuingia Chadema na usajili wa mpira wa miguu barani Ulaya, Mwalimu alisema:

“Mheshimiwa mwenyekiti usajili uliotufanyia katika dakika za majeruhi siyo ushindi wa ligi kuu pekee, bali wa ligi ya mabingwa Ulaya.”

Imeandikwa na Fidelis Butahe, Ibrahim Bakari, Nuzulak Dausen na Peter Elias

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s