“Safari ya Mabadiliko” yaanza upya na haizuliki

Hakuna anayeweza kukanusha kuwa sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaingia kwenye kipindi cha kisiasa ambacho haijawahi kuingiapo tangu kuasisiwa kwake mwaka 1964. Ni hapo jana tu ambapo vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa limechukua sura mpya katika nchi yetu ya Tanzania kwa kushuhudia aliyekuwa waziri mkuu na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, akiteuliwa rasmi kupeperusha bendera ya urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Viongozi wa CHADEMA na UKAWA kwenye picha ya pamoja baada ya mkutano mkuu wa CHADEMA kumpitisha rasmi Lowassa na Duni kwenye ugombea urais wa Muungano.

Viongozi wa CHADEMA na UKAWA kwenye picha ya pamoja baada ya mkutano mkuu wa CHADEMA kumpitisha rasmi Lowassa na Duni kwenye ugombea urais wa Muungano.

Lowassa ameanza upya safari yake nyengine aliyoipa jina la “safari ya mabadiliko” badala ya ile ya matumaini kukwama wakati akiwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Kwa kauli yake, Lowassa alisema: “Nilianza safari ya matumaini, lakini sasa nasema hii ni safari ya mabadiliko nje ya CCM. Tutakamata nchi mapema kabisa asubuhi”

Na Khelef Nassor

Na Khelef Nassor

Ni ukweli usiopingika kuwa hatua hiyo imekuwa ni pigo kubwa kwa wana-CCM kutokana na kuwa wingi wa wafuasi wa chama hicho wakiwemo vijana wa jinsia zote kuungana naye ili kuendeleza harakati za mabadiliko nchini.

Kwa upande mwengine, historia pia imejitokeza kwa upande wa Chama cha Wanachi (CUF) ambapo mmoja wa viongozi wake, Juma Duni Haji, ambaye hadi juzi usiku alikuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho, kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Lowassa. Duni, ambaye alikuwa pia waziri wa miundimbinu na mawasiliano katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alilazimika kuachia wadhifa yake hiyo ili kutoa fursa kwake yeye kujiunga na Chadema kuendeleza “Safari ya Mabadiliko”.

Haukuwa uamuzi rahisi hata kidogo, lakini alifanya hivyo baada ya chama chake kuridhia. Kujiunga kwa Duni ndani ya Chadema ni miongoni mwa mikakati madhubuti juu ya kile kilichoitwa “Kampeni ya Delete-CCM” iliyoasisiwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Viko baadhi ya vyama siasa na baadhi ya vyombo vya habari vinajaribu kuupotosha umma kwa kuwaeleza wananchi mambo ya uongo. Kwa mfano ni hapo jana tu, ambapo gazeti la UHURU linalomilikiwa na CCM lilipochapisha taarifa inayoashiria kuwa kuna mvurugano na mfarakano mkubwa ndani ya CUF, taarifa ambayo ilikanushwa vikali na viongozi wa chama hicho akiwemo Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad na Mkurugenzi wa Nje, Ismail Jussa Ladhu.

Gezeti la UHURU lilichapisha taarifa katika ukurasa wake wa mbele ikiwa na kichwa cha habari kinachosomeka “Lipumba aachia ngazi” na kuacha maswali mingi kwa baadhi ya wananchi. Lengo lilikuwa ni kuwadanganya wana-CUF kuwa chama chao hakiko salama baada ya ujio wa Lowassa. Hatua hiyo inaonesha ni jinsi gani CCM ilivyovurugika baada ya kada wake huyo wa zamani kujiunga na CHADEM na UKAWA.

Hapana shaka, UKAWA ni tishio kubwa kwa uhai wa CCM madarakani na ndiyo maana wanakwenda mbio usiku na machana ili kuhakikisha umoja huo unapotea. Wanatumia kila wakala wanayeweza kumnunua ndani ya vyombo vya habari na hata kwenye vyama vinavyounda UKAWA, kuhubiri na kuitangaza mipasuko ndani ya vyama hivyo ili kupandikiza khofu na chuki kwa baadhi ya wafuasi. Wanatamani umoja huo utengane na usifungamane. Ama kweli mwisho wa maji daima huwa ni tope.

Lakini kama alivyosema mgombea urais wa Zanzibar kupitia UKAWA, Maalim Seif, wimbi hili la mageuzi safari hii ni kubwa mno na ni vigumu sana kulizuia kwani wakati umewadia. Mabadiliko hutokezea katika nchi yoyote ile pindi serikali yake inaposhindwa kukidhi matakwa ya wananchi wake. CCM isijidanganye kwa kuwa eti inamiliki dola. Kukimbilia dola ni kuonesha dhahiri kuwa imeshindwa kuwaongoza wananchi na kusalia kwake madarakani kunagubikwa na kila aina ya hila na mizengwe.

Ziko vyama kadhaa vikongwe hapa Afrika ambavyo vilijidaganya kuwa serikali zao zingedumu dawamu, lakini wapi! Wananchi walichukua madaraka yao na kuwapa watu wengine. Hebu tujiulize kiko wapi chama cha CDP cha Blaise Compaore wa Bukina Faso? Iko wapi KANU ya Kenya? Kiko wapi chama cha PDP cha Goodluck Jonathan wa Nigeria?

Vyote hivi vilikuwa vyama vilivyoongoza nchi hizo, lakini hatimaye wenye nchi zao, ambao ni wananchi, wakaviondoa. Inafaa nao CCM wakajifunza kupitia kwa wenzao, kwani ni vigumu kulizuia wimbi la mabadiliko na nguvu ya wananchi.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s