CCM yajitapikia, yajipaka, yameza

“Sitapiki nikameza” ni msemo mashuhuri sana katika jamii zetu, ambao mtu huutumia akimaanisha kuwa kamwe hatorudia jambo au kitu ambacho ameshaachana nacho. Kwa bahati mbaya sana, msemo huu ni tofauti na mtazamo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwani wao sio tu hujitapikia, bali pia hujipaka matapishi hayo kabla hawajaanza tena kuyameza. Uchafu ulioje!

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Unguja. Borafya Silima, akimpokea Edward Lowassa mwanzoni mwa mwezi Juni kwenye Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Unguja. Borafya Silima, akimpokea Edward Lowassa mwanzoni mwa mwezi Juni kwenye Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.

Tukumbushane kidogo. Mnamo tarehe 7 Juni 2015, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa aliwasili Zanzibar kwa ajili ya kutafuta watu watakaomdhamini katika harakati zake za kuwania uraisi kwa tiketi ya CCM. Lowassa aliwasili milango ya saa 1:30 usiku katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume na kulakiwa na mwenyeji wake ambaye ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mjini Unguja, Borafya Silima.

Borafya akamtembeza Lowassa na kumtambulisha kwa makada mbalimbali wa CCM ndani ya mkoa huo. Katika kutafuta wadhamini, Borafya alimnadi Lowassa kuwa ni mtu safi asiye na hata chembe ya ubaya. Alimuogesha maji ya utakatifu na kumpaka mafuta ya unabii. Vifijo na nderemo kutoka kwa makada hao vilirindima kila sehemu aliyopita Lowassa kusaka wadhamini. Na hiyo ikawa ni kote Unguja na Pemba alikokwenda kusaka wadhamini, kama ilivyokuwa pia kote Tanzania Bara, chini ya kaulimbiu ya “Safari za Matumaini”.

Mambo yakaenda kama yalivyoenda na hatimaye Lowassa akakatwa ugombea wa CCM na majuzi kuhamia upinzani. Sasa CCM inajikuta ikiwa na wajibu mmoja mbaya sana – kumkana mtu ambaye ilimtangazia usafi wa kinabii na kujinasibisha naye sako kwa bako. Jukumu hili linaonekana kuwa gumu upande wa CCM Taifa, lakini limetupwa moja kwa moja kifuani kwa CCM Zanzibar. Ndio maana jana, tarehe 31 Julai 2015, Borafya akaitisha kikao cha kujipakaza matapishi na kisha kuyameza kwenye ukumbi wa CCM Kisiwandui.

Kwa mara nyengine, akawa ni Borafya aliyethibitisha kuwa Lowassa alikuwa ni mtu safi na aliyeandaliwa kwa muda mrefu na chama chao. Aliongeza kuwa walikuwa wanamuunga mkono mia-fil-mia na zaidi ya yote yeye binafsi alisema kuwa ana mahaba naye. Hapa sijui ni mahaba ya aina gani aliyonayo mzee huyu kwa Lowassa. Jibu analo mwenyewe, lakini waliokuwa wanafuatilia harakati za akina Borafya wakati wa “Safari ya Matumaini” ya Lowassa, wanataja namna safari hiyo ilivyomimina mapesa mifukoni mwao, wengine wakafikia umbali wa kununua magari na viwanja vya kujenga majumba. Yalikuwa maslahi binafsi, kwa hakika.

Sasa Lowassa hafai tena, ni mbaya, fisadi na mlafi wa madaraka. Kwa sasa Lowassa ananuka kama mzoga kwenye pua za makada wa CCM. Kisa! Kahama CCM na kuhamia chadema kuendeleza kile kinachoitwa safari yake ya matumaini. Kumkejeli na kumbeza Lowassa kwa makada hawa ni sawa na kula matapishi yao wenyewe waliyokwisha yatapika. Vyereje leo! Kwani hapo mwanzo hawakumjua Lowassa? Au ni kutokana na hili joto la mabadiliko linalowafukuta ndani kwa ndani?

Kujiunga kwa Lowassa na Chadema sio tu kumewaumiza makada wa CCM visiwani Zanzibar, bali hata upande wa Tanganyika pia. Wamegubikwa na mawazo ambayo yanawala na kuzifyonza siha za miili yao. Sasa wanamvisha Lowassa guo la ubaya badala ya lile la ufalme uliotukuka walilomvisha hapo awali. Wanataka kuuaminisha umma kuwa Lowassa hafai, fisadi, mlafi wa madaraka na ni wa kuogopa kama ukoma! Wanatapatapa kama wafa maji.

Kibaya kwa wote ni kwamba wameshindwa kuzisoma alama za nyakati kama alivyoshindwa Mwenyekiti wao wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kule kwenye vikao vya Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu, Dodoma. Alikosea takribani kwenye kila hatua kwa kushindwa kwake kuusoma wakati. Huu sio tena ule utawala wa Giningi aliousimulia mwandishi mashuhuri Prof. Said Ahmed Mohammed kwenye tamthilia ya Kivuli Kinaishi – ulimwengu wa cheupe kuitwa cheusi na cheusi kuitwa cheupe. Wana-CCM wanaombeza Lowassa na kumwita fisadi wanapaswa wawajibu Watanzania suali hili: Je, baada ya kujiuzulu kwake uwaziri mkuu kwa sakata Richmond, ufisadi ndani ya serikali ya CCM umepungua au umeongezeka? Watanzania wanajuwa jawabu ya suali hilo na Oktoba 25 watalitoa kwenye sanduku la kura.

Hakuna ubishi kuwa Lowassa ni kipenzi cha Watanzania na ana wafuasi wengi. CCM hupoteza muda mwingi kwa kunukuu maneno ya Julius Nyerere kama kwamba ni Msahafu au Biblia ili kuhalalisha maamuzi yao. Lakini cha kushangaza ni kwamba huchagua nukuu ipi waitumie, ipi waipuuzie. Ni Nyerere huyo huyo pia aliyesema: “Sasa ni vizuri mukasikiliza maoni ya wananchi, jee wananchi wanataka nini? Musidhani munaweza mukapata ushindi mukipuuza maoni ya wananchi, mukasema hili ni letu tu! Hamteui katibu wa chama bali munateua mtu atakayekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Hivyo ni vizuri musikilize wananchi wanataka nini juu ya watu wenu, musipuuze maoni ya wananchi hata kidogo. Chama kitakachopuuza maoni ya wananchi, kinaweza kikalia kilio na asipatikane mtu wa kusaidia kupangusa machozi.”

Kikwete aliwaongoza wenzake kupuuzia maneno hayo ya mwasisi wa chama chao ambaye hutaka waonekane kuwa wanamuheshimu sana hata sasa akiwa kaburini aliko. Kikwete alisahau hata njia ambayo ilimfikisha alipo miaka kumi tu iliyopita, akaongoza genge la kupora haki ya wanachama wa CCM walio wengi. Sasa mpira uko upande wa umma. Inafaa ikumbukwe kuwa serikali ni ya wananchi na siyo ya chama cha siasa. Wananchi ndio wenye mamlaka ya kuchagua nani anafaa kuwa kiongozi wao. Unapofanya kinyume chake, huko ni kuwanyang’anya wananchi madaraka na watakuhukumu.

Narudia. Hakuna ubishi hata kidogo kuwa Lowassa anapendwa na Watanzania walio wengi. Kulikata jina lake katika hatua za awali sio tu kulikuwa ni dharau kwa Lowassa mwenyewe, bali hata kwa wananchi wenyewe ambao kimsingi ndiyo wenye mamlaka. Borafya alisema kwenye mkutano wa kujimezesha matapishi kuwa “CCM ilikuwa ina watu wawili tu ambao walilelewa kiuongozi. Kikwete na Lowassa.” Hakukosea kwenye hilo. Sasa mmoja kasimama upande mmoja na mwengine upande mwengine. CCM ingoji gharika itakayowaangamiza Oktoba 25.

Advertisements

One thought on “CCM yajitapikia, yajipaka, yameza

  1. ushasema walipewa pesa na lowasa wengine wakanunua magari, viwanja huoni aliwanunua ndio maana walimsafisha, na jingine alikua mwanachama mwenzao kwa tamaa ya utawala ndio maana kahama CCM kujiunga UKAWA ili apate kutawala, tuache upendo itazamwe haki DK SLaa alistahili hiyo nafasi nimeamini pesa ni adui wa haki tafakari

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s