Lowassa awa waziri mkuu wa kwanza kuhamia upinzani

Hayawi hayawi sasa yamekuwa. Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameweka rekodi ya kuwa kada wa kwanza aliyewahi kushika nafasi ya waziri mkuu kukihama chama tawala, CCM na kujiunga na upinzani.

Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Lowassa, akizungumza mara baada ya kujiunga rasmi na CHADEMA.

Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Lowassa, akizungumza mara baada ya kujiunga rasmi na CHADEMA.

Katika orodha ya mawaziri wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu uhuru, Lowassa ni waziri mkuu wa tisa kushika madaraka hayo. Alishika wadhifa huo kuanzia Desemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008.

Makada wengine wa CCM waliowahi kushika wadhifa wa waziri mkuu ni, Julius Nyerere, Rashidi Kawawa, Edward Sokoine, Cleopa  Msuya, Dk Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, John Malecela, Frederick Sumaye na Mizengo Pinda.

Lowassa atengeneza historia

Lowassa ni kati ya mawaziri watatu waliowahi kuwania urais mara mbili na kushindwa. Wengine ni Malecela (1995 na 2005), Sumaye (2005 na 2015). Mbunge huyo wa Monduli aliyejitokeza 1995 na 2015 na ambaye amekuwa akisononeka namna mchakato wa kupata mgombea ulivyoendeshwa, ameamua kuhamia upinzani ili kuweka haki ndoto ya safari yake ya matumaini.

Katika kipindi cha wiki tatu sasa, kumekuwapo minong’ono ndani na nje ya CCM na kwenye mitandao ya kijamii, kwamba nchi itatikisika kutokana na fununu za Lowassa kuhamia upinzani.

Kulikuwapo kila aina ya propaganda za kubeza hatua hiyo na nyingine zikipongeza na kutahadharisha kuwa, kama angehamia upinzani, ungekuwa mwisho wa CCM.

Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, mawaziri wakuu sita wamewahi kuomba kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera ya urais na kushindwa, lakini hakuna aliyethubutu kuhama chama hicho tawala.

Kiini cha Lowassa kuhama

Mwaka huu, Lowassa alijitosa kwa mara ya pili kuwania urais, akiungana na makada wengine 37 wa CCM waliorudisha fomu wakiwamo Sumaye na Pinda.

Majina ya Lowassa na mawaziri wakuu wenzake hayakupenya hata Tano Bora, yaliishia katika Kamati ya Maadili. Wajumbe watatu wa Kamati Kuu walifichua kile walichodai ukiukwaji mkubwa wa kanuni kwani kamati iliyopaswa kuchuja majina ni Kamati Kuu na siyo Kamati ya Maadili.

Dk Emanuel Nchimbi ambaye amekuwa mjumbe wa CC kwa miaka 17, Sophia Simba na Adam Kimbisa, walitangaza rasmi kujiweka kando na maamuzi hayo ya Kamati Kuu.

Akizungumza na wanahabari usiku wa Julai 10 mjini Dodoma, Dk Nchimbi alisema kanuni zilitaka majina yote 38 kupelekwa Kamati Kuu yenye jukumu la kuchuja. Badala yake Dk Nchimbi alisema Kamati ya Maadili ilipoka majukumu ya Kamati Kuu na kukata majina ya wagombea likiwamo la Lowassa kwa manufaa ya wagombea wachache wasiokubalika.

“Katiba yetu inataka mtu anayekubalika apewe nafasi ya kwanza lakini kikao cha leo (cha CC), kilionekana kuminya wanaokubalika kwa faida ya wasiokubalika,” alisema Dk Nchimbi. “Sisi watatu tunatangaza kujitenga na maamuzi hayo na tunatangaza kutoyaunga mkono maamuzi hayo,” alisisitiza Nchimbi, kauli iliyoashiria dhahiri kuwapo kwa mpasuko ndani ya CCM.

Waliopenya hadi Tano Bora ni Benard Membe, Dk Asha Rose Migiro, Dk John Magufuli, Balozi Amina Salum Ally na Januari Makamba.

Mpasuko huu uliendelea hadi kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) ambako hata mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete alipoingia ukumbini, wajumbe walimwimbia “Tuna imani na Lowassa”.

Baada ya vuta nikuvute, hatimaye wajumbe walikubali kupiga kura na yakapatikana majina matatu ya Dk Magufuli, Balozi Amina na Dk Migiro.

Mkutano mkuu ulimchagua Dk Magufuli kuwa mgombea urais lakini wakati anatangazwa Lowassa hakuwapo ukumbini.

Siku chache baadaye, mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru alijitokeza na kueleza kuwa Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM iliteka majukumu ya CC ya CCM na kuamua kuchuja majina ya makada waliojitokeza kuwania urais kinyume cha kanuni ili tu kumuengua Lowassa.

Chanzo: Mwananchi la tarehe 29 Julai 2015

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s