Lipumba ajitosa urais

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, jana amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Prof. Ibrahim Lipumba akizungumza katika Kongamano la Diamond Jubilee, Agosti 28, 2008

Prof. Ibrahim Lipumba akizungumza katika Kongamano la Diamond Jubilee, Agosti 28, 2008

Prof. Lipumba ni mgombea wa kwanza kuchukua fomu katika vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), akitaja vipaumbele vinne ambavyo atavishughulikia kama atapitishwa na chama chake na kuongoza nchi.

Vyama vingine vinavyounda umoja huo ni Chama Cha National League for Democracy (NLD), Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha NCCR-Mageuzi.

Mbali ya kuahidi kuwashughulikia mafisadi katika utawala wake, Prof. Lipumba alivitaja vipaumbele vyake kuwa ni kutoa ajira, kuboresha huduma za afya, miundombinu, kupambana na vitendo vya ufisadi ambavyo vinakwamisha maendeleo.

Prof. Lipumba alichukua fomu hiyo katika Hoteli ya Blue Pearl, iliyopo katika jengo la Ubungo Plaza na kusisitiza kuwa, Taifa linakabiliwa na changamoto ya tatizo la ajira kwa vijana.

Alisema changamoto hiyo inachochea kuibuka kwa vikundi vya uhalifu kama ‘Panya Road’ ambacho ni matokeo ya vijana wengi kukosa ajira wakati jiografia ya nchi ni nzuri ili kuwawezesha vijana wawe na ajira hususan kupitia bandari.

“Mtwara kuna bandari yenye kina kirefu inayoweza kuwa kituo cha viwanda, biashara…gesi asilia imegundulika huko hivyo kama kama bandari hii itaboreshwa na nyingine hususan iliyopo mkoani Tanga ambako wana ardhi nzuri na mazao mengi hustawi.

“Tukianzisha viwanda vya kutosha, tatizo la ajira litakwisha…katika eneo la afya, nitahakikisha kunakuwa na Hifadhi ya Jamii hasa kwa wazee ambao Serikali ya CCM imeshindwa kuwasitiri,” alisema.

Aliongeza kuwa, upo umuhimu wa kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya afya ambapo hivi sasa, ufisadi umekuwa kikwazo cha kuifanya sekta hiyo ishindwe kupiga hatua.

Alisisitiza umuhimu wa kuwajengea watoto utaratibu wa kupatiwa lishe bora ili waweze kuwa na uwezo mzuri wa kufikiri ambapo katika eneo la miundombinu, atajenga barabara za lami ili kuiunganisha Tanzania na nchi jirani ziweze kutumia bandari zetu.

Prof. Lipumba miundombinu ikiboreshwa, itasaidia kutoa ajira pamoja na kuongeza ulinzi wa nchi akitolea mfano wa nchi jirani ya Rwanda kuwa nchi hiyo inategemea bandari za Tanzania kuingiza mizigo yake hivyo kuna umuhimu wa kuendeleza uhusiano ili kuchochea maendeleo ya nchi.

“Nikifanikiwa kuwa rais wa Tanzania, sitakuwa na huruma na mafisadi katika utawala wangu…kuhusu suala la Katiba Mpya,  kuna mambo ya msingi ambayo yalikuwepo kwenye rasimu ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba lakini katika Katiba
Inayopendekezwa hayapo,” alisema Prof. Lipumba.

Aliyataja mambo yaliyowekwa kando kuwa ni mfumo wa Muungano, uadilifu, uwajibikaji ambapo rasimu ilisema tatizo kubwa la ufisadi linachangiwa na viongozi kupewa zawadi.

“Katika rasimu kuna kifungu kilieleza viongozi wa Tanzania wasiwe na akaunti nje ya nchi lakini nacho hakipo, nikiingia Ikulu nitahakikisha maoni ya wananchi yaliyonyofolewa katika Rasimu ya Katiba yote yanarejeshwa kwa maslahi ya Taifa,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa chama hicho ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, alisema Watanzania wapo tayari kwa mapinduzi kwani wamechoka kuwa chini ya utawala wa Serikali ya CCM.

Alisema Watanzania wanataka kuingia katika mwaka mpya wa maamuzi na kuishi kama binadamu wengine kwa kupata haki sawa ambapo tofauti ya walionacho na wasionacho wataiondoa na kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na rasilimali za nchi.

Aliongeza kuwa, umefika wakati Watanzania kufanya maamuzi magumu ya kuchagua kiongozi ambaye si mbinafsi, anayejua matatizo ya wananchi.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s