Vuai Ali Vuai athibitisha ubora wa CUF

Kwamba CUF – Chama cha Wananchi ni taasisi inayowajenga wanaoiamini kuwa raia wa kupigiwa mfano, sasa sio tena jambo la kulisema kwa manufaa ya kusaka kete za kisiasa tu, bali ni ukweli ulio wazi kwa kila mwenye kutaka kuuona – hata kwa maadui wa chama hiki, sikwambii kwa marafiki zake. Sifa za wanachama, wafuasi na wapenzi wa CUF zimejengeka katika misingi ya aina yake kama ilivyo desturi ya kila kitu katika dunia kilivyojengeka katika misingi maalum. Hadi mtu kufikia kupewa sifa yake stahiki ni lazima awe ametimiza misingi ama vigezo vyote vya sifa hizo.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, akihutubia mkutano wa Alhamisi tarehe 14 Mei 2015, Magogoni kwa Mabata.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, akihutubia mkutano wa Alhamisi tarehe 14 Mei 2015, Magogoni kwa Mabata.

Kabla ya kuzionesha sifa njema za wana-CUF, kwanza ningeomba tuone misingi ya sifa ilivyojengeka ndipo tuone jee ni kweli angalau wana-CUF wanao japo msingi mmoja katika misingi ya sifa? Baadhi ya misingi iliyojenga neno sifa ambayo ameielewa na Bwana Jere Brophy wa Michigan University, 1981, katika kiwango cha taasisi, ni kama ifuatavyo:

• Sifa itolewe kutokana na tabia maalum au ya kipekee kwa taasisi husika
• Sifa itolewe kutokana na uhodari wa anaesifiwa kwa taasisi husika
• Sifa ionyeshe kuwa ni zawadi kutokana na utendaji wa hali ya juu kwa mtu au katika taasisi husika
• Sifa hutolewa baada ya anayesifiwa kutoa mchango wa hali ya juu kwa muda uliopo na baadae kwa taasisi husika.

Basi kwa misingi hiyo minne niliyoitaja hapo, iwapo mtu atakuwa na msingi mmoja katika hayo, hana budi kupatiwa sifa yake. Napenda nithibitishe kwamba ni kweli CUF na wanachama wake wametimiza sifa na vigezo ambavyo mtu anastahiki kupewa sifa ama kusifiwa kwa asilimia zote.

Labda kwa kuwa mimi mwenyewe ni mwana-CUF nitaonekana kuwa ni mwamba ngoma ninayevutia upande wangu tu. Lakini kwa kumsikia mtu kama Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, katika viwanja vya Magogoni siku ya tarehe 14 Mei 2015 akiwasifu CUF na wanachama wake, utajuwa wazi kuwa kizuri hujiuza, kibaya kikajitembeza. Sifa za CUF hazisemwi na marafiki tu wa CUF, bali pia maadui zake.

Katika mkutano huo, ambao awali uliksudiwa uwe wa mkoa mzima Mjini Magharibi ambao sasa una wilaya ya tatu na kupangiwa kuhutubiwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, Mheshimiwa Vuai alitambuwa kuwepo kwa wana-CUF wengi kwenye mkutano huo, na akasema kwamba wana-CUF ni watu walioilewa hasa maana ya demokrasia ya vyama vingi pale: ”Kwa CUF kuja kwenye mikutano ya CCM si kosa, hiyo ndiyo demokrasia.”

Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar akaendelea kuwashajiisha wanachama wa CCM, ambao wote wakijumlishwa walikuwa hawafiki 70 kwenye mkutano huo wa mkoa mzima, kwamba nao wahudhurie mikutano ya CUF. “Kama nyinyi CCM mnavyokwenda katika mikutano yao” lakini cha ajabu wana-CCM hao wakapinga kwamba wao hawaendi katika mikutano ya CUF na huku wakiwa na jazba kumwambia kiongozi wao kwamba na wao CUF wasije kwenye mikutano yao.

“Tumeleta vyama vingi ili tuelimishane wana CCM. Hivyo CUF kuja katika mikutano ya CCM sio kosa. Tusiwabugudhi wanapokuja katika mikutano yetu, kwa sababu wanafanya jambo jema na sisi tuwaunge mkono na naomba nichukue fursa hii niwasifu na niwapongeze sana wana-CUF”. Ndivyo alivyosema Naibu Katibu Mkuu Vuai Ali Vuai.

Hivyo kwa mnasaba wa maneno ya Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM na kwa vigezo alivyovitoa Brophy wa Chuo Kikuu cha Michigan mwaka 1981, ni wazi kuwa  wanachama na wapenzi wa CUF wamebeba vigezo hivyo. Hongera zangu kwa wana-CUF wote.

Lakini lazima tukubali kwamba vigezo vyenu na sifa havikuja bure bure. Juhudi zenu pamoja na viongozi wenu kuanzia ngazi za juu hadi shinani, kwa kuwa ndani ya CUF watu wanaaminiana katika mambo yote yenye umuhimu katika nchi, hakuna usaliti, hakuna udanganyifu, hakuna ujunjifu wa amani, hakuna ubaguzi wa aina yeyote. Viongozi wanaojua wajibu kwa nafsi zao na kwa wanaowangoza wamekuwa wakiwasomesha maana ya demokrasia tangu chama kikiwa na mzizi mmoja mwaka 1992 hadi sasa kimekuwa chama dume kilichoeneza mbegu zake kila kona, hadi kimeenea Tanzania na Zanzibar hadi maeneo yaliyokuwa hayakufkiriwa kwamba kuna siku atapatikana angalau mwanachama mmoja.

Si ajabu, kwa hivyo, kwamba mtu kama Vuai Ali Vuai, ambaye kwa hakika ni adui mkubwa wa CUF, anajikuta hana budi ila kuwamwagieni sifa munazostahiki, si kwa kuwa yeye ni muungwana sana kusifia kila kitu, lakini kwa kuwa nyinyi ni wema sana kiasi cha kwamba hakuna hata mbaya ambaye anaweza kuzidiwa kila siku na ubaya wake kwenu. Lazima khulka yenu itambadilisha tu.

Sifa na alizokumwagieni Vuai Ali Vuai ni ishara njema. Pamoja na hisia zozote mbaya anazoweza kuwa nazo, kauli yake haikuwa ya kijinga wala jazba bali ilitoka ndani ya upeo wa elimu na maarifa yake. Wana-CUF munaweza kuvimbisha vichwa vyenu kwa fakhari hii, lakini nasaha zangu kwenu ni kwamba musije mukalewa kwa sifa hizo mukajiacha katika upiganaji wa kuitetea nchi yenu. Ongezeni juhudi katika kuelimisha jamii iliyowazunguka. Hakikisheni munatoa taarifa muhimu kwa viongozi unapobaini uharamia wowote unaofanywa na wapinzani wenu. Jiandikisheni na waliowazunguka na waelimishe umuhimu wa kuchagua kuipigia kura CUF na wagombea wake wote.

Hiyo ndio maana ya pongezi kutoka CCM kupitia Naibu Katibu Mkuu wake Zanzibar kwenu nyinyi wapenzi na wanachama wa CUF.

Makala ya Ali Mohammed Ali.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s