UKAWA wakuna vichwa kwa masaa 48

Saa 48 zilizotumika kikaoni kutafuta muafaka wa majimbo yenye utata ndani ya umoja wa vyama vya upinzani vilivyo chini ya Ukawa, zimekatika bila mafanikio na  mvutano unaonekana kubakia kwenye majimbo 12 kati ya 239 waliyopanga kugawana.

Mwenyekiti  mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe akizungumza wakati wa mkutano na waandishi  wa habari, Dar es Salaam jana. Wengine ni wenyeviti wenza,James Mbati,  Profesa Ibrahim Lipumba na  Dk Emmanuel Makaidi.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana. Wengine ni wenyeviti wenza,James Mbati, Profesa Ibrahim Lipumba na Dk Emmanuel Makaidi.

Vyama hivyo vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia kiti cha urais hadi udiwani, lakini kazi ya kugawana majimbo imekuwa ikivisumbua na ilitarajiwa kuwa ingemalizika juzi baada ya viongozi kukutana kwa siku mbili kuanzia Jumanne.

Lakini habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa wajumbe walishindwa kufikia muafaka kwenye majimbo 12.

Hata hivyo, viongozi hao wa vyama hivyo walikataa kutaja majimbo hayo yaliyosalia.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya CUF, viongozi wa vyama vinne vinavyounda Ukawa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Emmanuel Makaidi (NLD) walisema tayari wamefikia muafaka katika majimbo 227 kati ya majimbo 239 yaliyopo nchini.

“Tangu juzi tupo hapa tukijadili namna ya kuwapata wagombea wa Ukawa wa ngazi zote za udiwani, ubunge na urais. Kwa kiasi kikubwa tumekamilisha kazi ya kupata wagombea ubunge kwa zaidi ya asilimia 95 ya majimbo yote ya uchaguzi, majimbo 12 yaliyobaki tunaendelea kuyashughulikia na tutayapatia ufumbuzi muda si mrefu,” alisema Mbatia aliyezungumza kwa niaba ya wenyeviti wenzake.

Viongozi hao, kila mmoja kwa nyakati tofauti, walijigamba kuwa umoja wao huo upo imara na kwamba wale wanaopiga ramli kuwa utavunjika, wataendelea kusubiri lakini kamwe jambo hilo halitatokea.

Mbowe

Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, Mbowe alisema hatua iliyofikiwa kwa sasa inatia matumaini ya kufanikiwa kwa mpango wa kusimamisha mgombea mmoja wa ubunge, udiwani na urais.

“Kwa wale wanaopiga ramli ya kuvunjika kwa Ukawa hawatafanikiwa. Tutasimamisha mwakilishi mmoja kuanzia udiwani, ubunge mpaka urais. Tunajua hitaji la Watanzania kwa sasa ni kuwaondoa kwenye kifungo cha CCM,” alisema Mbowe.

Alipoulizwa kuhusu mvutano wa majimbo hayo 12, Mbowe alisema siyo jambo la kushangaza kwa vyama vinne kutovutana katika mgawanyo wa majimbo hayo kwani kila chama kinajiamini na kinahitaji kupata mwakilishi.

“Tuko vyama vinne,  itakuwa ajabu kama mvutano utakosekana, lakini tumepata asilimia 95. CCM wenye chama kimoja hawajatangaza mgombea hata mmoja.”

Mbowe alisema madai ya kuchelewa kutangaza wagombea wa Ukawa katika ngazi za ubunge, udiwani na hata ile kubwa ya urais  ni mkakati wa kisiasa na kwamba watayataja muda muafaka utakapowadiwa.

“Sisi hatutegeani na CCM, muda utakapofika tutawaambia Watanzania,” alisema Mbowe.

Mbowe pia alisema maandalizi hafifu yanayofanywa katika uboreshaji Daftari la Wapigakura ni mipango wa makusudi unaofanywa na Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kumwongezea Rais Jakaya Kikwete na serikali ya CCM muda wa  kukaa Ikulu.

“Miezi mitatu tu imebakia kabla ya kampeni za uchaguzi, lakini mpaka sasa hatujui ratiba, majimbo yaliyogawanywa, watumishi watakaotumika, vituo vitakuwaje vya uchaguzi na hata daftari la kupigia kura ndiyo bado halijamaliza hata mikoa miwili, hiyo ni hatari sana kwa Taifa. Tunaionya NEC isijaribu kufanya mbinu zitakazosababisha kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu,” alisema Mbowe.

Mbatia

Kwa upande wake, Mbatia, ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema ahadi na kauli za NEC zimekuwa na utata hali inayowafanya waondoe uaminifu kwa Tume hiyo.

Mbatia alisema mpaka sasa kuna mashine 1,100 tu za BVR kati ya mashine 8,000 zinazotakiwa kuingia nchini kwa ajili ya kufanyia kazi.

Alisema tathmini waliyofanya inaonyesha kwamba, endapo kila kituo kitatumia siku 14 za uandikishaji wa wapigakura, yaani vituo 40,000, zoezi hilo litatumia siku 353, sawa na mwaka mmoja.

“Kwa sasa kati ya Watanzania milioni 24 wanaotakiwa kuandikishwa kwenye daftari hilo, ni Watanzania chini ya 200,000 tu ndiyo walishaandikishwa huku miezi iliyobakia ikiwa ni mitatu tu,” alisema Mbatia.

Kuhusu mpango wa kufanyika Uchaguzi Mkuu na Kura ya Maoni kwa wakati mmoja, Mbatia alisema jambo hilo haliwezekani kwa mujibu wa Katiba, na kuwa kura ya maoni inayo sheria yake na mpaka sasa sheria hiyo tayari imevunjwa na NEC.

“Kwa hivyo tunaitaka NEC itamke kusitisha mpango wake wa kuunganisha matukio hayo mawili, lakini pia itoe tamko la kufanyika Uchaguzi Mkuu kama ilivyo kawaida kikatiba,” alisema.

Hata hivyo, tayari NEC imeshaeleza kuwa itakuwa vigumu sana kufanya mambo hayo mawili kwa wakati mmoja kwa kuwa kila tukio lina mahitaji yake tofauti.

Profesa Lipumba

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema NEC, haijaanza maandalizi yoyote licha ya kubakia miezi sita tu kabla ya Uchaguzi Mkuu na kuongeza kuwa wamebaini  zipo njama za kuuahirisha ili kumuongezea muda Rais Kikwete na CCM.

Profesa Lipumba alisema kwa Sheria ya Kura ya Maoni, hakuna uwezekano wa jambo hilo kufanyika tena bila kwanza kufanya marekebisho ya sheria hiyo.

Alisema Kura ya Maoni ilitakiwa ifanyike ndani ya siku 124 kutoka tarehe Rais Kikwete alipotoa tangazo la kura ya maoni pale alipotamka kuwa kura hiyo itafanyika 30 Aprili  2015.

“Kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa chini ya sheria hiyo imewekewa muda wake na muda huo hautakiwi kubadilika… tangazo la Kura ya Maoni likishatolewa na tarehe kutangazwa, haibadilishwi kwa sababu yoyote ile. Hivyo hakuna namna yoyote ya kuahirisha Kra ya Maoni na kuifanya tarehe nyingine yoyote” alisema Lipumba.

Dk Makaidi

Mwenyekiti wa NLD, Dk Makaidi alisema zipo dalili na ushahidi kuwa uchaguzi ukifanyika mwaka huu CCM itang’olewa madarakani na kwa kulijua hilo, Serikali inafanya kila njia ili kuahirisha uchaguzi usifanyike mwaka huu.

“Kubadili Katiba ya sasa kwa lengo la kuahirisha uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu sio tu kutaathiri misingi muhimu ya Katiba ya sasa, bali pia kutaathiri amani ya nchi yetu. Tumeona kinachoendelea Burundi baada ya Rais Pierre Nkurunzinza na chama chake kuamua kujiongezea muda wa kutawala nchi hiyo,” alisema.

“Tumeona yanayoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Conga (DRC) baada ya Joseph Kabila kutaka kufanya hivyo, Kikwete na wana-CCM wenzake wasitake kuiingiza nchi yetu katika majanga yasiyokuwa na sababu,” alisema.

Chanzo: Mwananchi la tarehe 1 Mei 2015

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s