Ukawa asilimia 95

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na baadhi ya vyama vya siasa za upinzani nchini, umesema hadi sasa wamekubaliana kuachiana majimbo  227 kati ya 239 yaliyoko Tanzania Bara na Zanzibar.

Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba, akiwa na viongozi wenzake wa UKAWA, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Freeman Mbowe wa CHADEMA.

Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba, akiwa na viongozi wenzake wa UKAWA, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Freeman Mbowe wa CHADEMA.

Umoja huo ambao unaundwa na vyama vya Chadema,  CUF, NCCR-Mageuzi na NLD umesema kuwa kumekuwa na mvutano mkubwa baina yao unaotokana na kila chama kuvutia upande wake.

JAMES MBATIA
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alisema hata hivyo, hadi sasa kikao chao cha siku mbili kimezaa matunda, baada ya kukubaliana kuachiana majimbo 227, ambayo ni sawa na asilimia 95 huku wakiendelea kujadiliana kuhusu majimbo 12 yaliyosalia.
Mbatia, ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, alisema hayo katika mkutano na waandishi wa habari, ulioitishwa na Ukawa, jana jijini Dar es Salaam kuzungumzia msimamo uliopo ndani ya Umoja huo.
Alisema hali hiyo haimaanishi kuwa Umoja huo unakabiliwa na mgogoro wala mpasuko, bali inatokana na mazungumzo, ambayo alisema yanaendelea vizuri na kwamba, viongozi wa vyama hivyo bado wana msimamo wa pamoja.
FREEMAN MBOWE
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka Umoja huo kutaja majimbo 12 yanayovutaniwa na vyama hivyo, ambayo kila chama kimegawiwa kati ya yale 227, alisema hawawezi kuyataja kwa kuwa muda wa kufanya hivyo bado haujawadia.
 Hata hivyo, Mbowe, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Hai, alisisitiza msimamo wa Ukawa kwamba, yeyote atakayesimama kugombea urais iwe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, ubunge au udiwani kupitia vyama hivyo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, atakuwa ni mmoja kutoka katika Umoja huo.
“Sasa wale wanaopiga ramli kwamba Ukawa itavunjika, tunawaambia Ukawa haitavunjika,” alisema Mbowe.
Alisema pia wakati ukifika watamtaja mgombea urais na udiwani atakayepitishwa kupitia Ukawa na kwamba, hadi sasa mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) naye pia bado hajatangazwa.
DK. EMMANUEL MAKAIDI
Mjumbe wa Ukawa, ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha NLD, Dk. Emmanuel Makaidi, alisema hawashindwi kumtangaza mgombea urais kupitia Umoja huo.
“Lakini (mgombea urais) yupo. Hatungojei CCM. Kwanza (CCM) hawana mgombea, wote ni majanga, kuna wa Epa, kuna Escrow. Ndiyo maana ninasema wote ni majanga. Siku ikifika tutamtangaza,” alisema Dk. Makaidi.
Awali, Mbatia alisema licha ya uandikishaji wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura kusuasua, lazima daftari hilo liwepo, linaloheshimika, kukubalika na kutekelezeka.
Alisema taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) inaonyesha kuwa hadi kufikia jana, mashine za kuandikisha wapigakura kwa kutumia mfumo wa elektroniki wa BVR (kits BVR) zilizopo ni 298 wakati taarifa kutoka kwenye kamati ya Bunge zinaonyesha kuwa ni 1,100.
Mbatia alisema hali hiyo inaacha swali gumu kujua nani mwenye kauli ya kweli.
Hata hivyo, alisema hawaiamini Nec kwa kuwa wamekuwa wakitoa kauli zisizo na uhakika, ukweli na za kuaminika na kwamba, utata uliopo kuhusu siku za kuandikisha wapigakura unaweza kuifikisha nchi pabaya kama hatua za haraka hazitachukuliwa.
Alisema hali hiyo inaanza kuonyesha dalili zote kuwa uchaguzi mkuu hauwezi kufanyika Oktoba, mwaka huu, kama inavyotarajiwa.
Naye Mbowe alisisitiza Ukawa kutokuwa na imani na Nec akisema hadi sasa haijafanya lolote linaloweza kuwashawishi kuhusu maandalizi ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Alisema badala yake Nec imekuwa ikifanya mambo yake kwa siri, huku yale ya wazi ikionyesha dhahiri kuipendelea CCM.
“Tume ni majanga kama vile serikali ya CCM. Ukichanganya majanga mawili inakuwa matatizo,” alisema Mbowe.
Alisema kutokana na hali hiyo, katika mazingira ya kawaida, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, hadi hivi sasa asingekuwapo ofisini.
“Kikundi cha watu 20 (wa Nec) kinaweza kuwaingiza kwenye machafuko watu milioni  45. Leo (jana) ni tarehe 30. Hakuna maandalizi yoyote ya uchaguzi mkuu halafu mwenyekiti anasema uchaguzi mkuu uko palepale?” alihoji Mbowe.
Alisema hali hiyo inaonyesha kuwapo mkakati wa makusudi unaofanywa na serikali kutaka kuuongezea muda zaidi utawala wa Rais Kikwete kuendelea kukaa madarakani.
PROFESA LIPUMBA
Katika tamko la Ukawa, Mwenyekiti Mwenza wa Umoja huo, Prof. Ibrahim Lipumba, aliungana na Mbowe akisema kuna dalili zinazoonyesha kuwapo njama za kuahirisha uchaguzi mkuu na kumuongezea Rais Kikwete na CCM muda wa kutawala.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi haijaanza maandalizi yoyote kwa ajili ya uchaguzi mkuu licha ya kwamba imebaki miezi sita tu uchaguzi huo ufanyike kwa mujibu wa katiba,” alisema Prof. Lipumba.
Aliongeza: “Shughuli zinazohusiana na maandalizi ya uchaguzi mkuu na vifaa vinavyotumika kwa ajili yake, ambavyo kwa taratibu za miaka yote huanza kufanyika angalau mwaka mmoja na nusu kabla ya siku ya uchaguzi hazijaanza kufanyika, vifaa vinavyohitajika havijanunuliwa na fedha kwa ajili hiyo hazijatengwa hadi sasa.”
Alisema Ukawa haitakuwa tayari kuunga mkono jitihada zozote za kumuongezea rais Kikwete na CCM muda wa kutawala kwa kuahirisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kuhusu upigaji kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa kufanyika siku moja na uchaguzi mkuu, Mbatia alisema kila mchakato una sheria yake, hivyo utekelezaji wake hauwezi kuchanganywa pamoja.
Hivyo, akashauri upigaji wa kura ya maoni kuwekwa pembeni usubiri mpaka baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu kufanyika.
Alisema hiyo inatokana na kura ya maoni kutokuwa hitajio la kikatiba na kwamba, haoni mchakato wake utafanyika kwa kutumia sheria ipi kama si kutaka kulisababishia taifa migogoro.
“Hitaji kuu la kimsingi ni uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais,” alisema Mbatia na kuwataka wananchi kuhakikisha wanajitokeza kujiandikisha katika daftari hilo kwa ajili ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu.
Dk. Makaidi alisema CCM ina wasiwasi wa kuangushwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu na ndiyo maana wanapanga njama za kutaka kusogeza mbele muda wa kufanyika kwake.
Alisema pia hali ya uchumi ni mbaya, hivyo serikali inaona kuitisha uchaguzi mkuu, hauwezi kufanyika kwa sababu wananchi wana njaa. Hata hivyo, alisema lazima uchaguzi mkuu ufanyike, vinginevyo wataandaa maandamano ya wananchi.

“Kwa maana hiyo, serikali itangaze uchaguzi upo,” alisema Dk. Makaidi.

Chanzo: Nipashe la tarehe 1 Mei 2015

Advertisements

One thought on “Ukawa asilimia 95

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s