Maalim Seif wa Z’bar kama Pepe Mujica wa Uruguay

Ni jambo la kawaida kukuta watu ambao hawatoki familia au nasaba moja kufanana hadi kunasibishwa  kwamba ni ndugu wa damu. Yawezeka wakawa watu kutoka nchi moja ama tofauti, pia yawezekana hata rangi kutofautiana lakini sura zikafanana. Muda mwengine pia hutokea hata watu wasifane kwa rangi, sura au kabila, lakini watu wanaweza kufanana kupitia mambo mengine tofauti mfano, sauti, mwendo, mavazi, matendo na mambo kadhaa wa kadhaa yahusianayo.

Rais mstaafu wa Uruguay, Jose Mujica

Rais mstaafu wa Uruguay, Jose Mujica

Nimewahi kusikia mara kadhaa wa kadhaa baadhi ya watu wasiomjua Maalim Seif Shariff Hamad ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar wakisema anapenda madaraka, mara anapenda ukubwa, au mengine kama hayo, ambayo huyasema kwa sababu ya ujinga wao kwa tabia na hulka za Maalim Seif. Hata hivyo, hata kwa hao wanaomsema hivyo kwa kutokumjuwa kwao, bado nao hutawasikia wakisema kiongozi huyu ni mlafi wa mali za umma, amejikusanyia mali kwa njia zisizo halali na mengineyo ya kashfa kama hizo. Ndio maana nikapata wazo la kuwaelimisha wenzangu wasiomjua kwa kumfananisha Maalim Seif wetu wa Zanzibar na Rais msaafu wa Uruguay, José Alberto “Pepe” Mujica Cordano, ambaye anasemekana kuwa ndiye rais masikini kabisa duniani.

Maalim Seif alizaliwa  mwaka 1943 katika kijiji cha Nyali, Mtambwe kisiwani Pemba, akiwa ametanguliwa kwa miaka minane tu raisi huyo wa Uruguay, ambaye alizaliwa mwaka 1935. Rais huyo mstaafu wa Uruguay hana nyumba anayoimiliki yeye mwenyewe, kitu ambacho Maalim Seif Sharif Hamad kinamfanya afanane na rais huyo kwa kuwa tangu nipate kumjuwa na kumsikia, sijawahi kumsikia Maalim Seif kumiliki nyumba.

Katika maisha ya kumfahamu kwangu alikuwa akiishi kwa muda mrefu katika mtaa wa Mtoni Kidatu, eneo lililopachikwa jina la “Kwa Sefu” na wapitanjia. Nilipofuatilia kutaka kujuwa ikiwa ile nyumba ni yake, jawabu likaja kwamba ni nyumba ya serikali kupitia Shirika la Umeme, ambapo  yeye anaishi pale kwa heshima ya kuwa Waziri Kiongozi Mstaafu wa Serikali ya Zanzibar.

Rais mstaafu wa Uruguay aliingia madarakani mwaka 2010, halikadhalika Maalim Seif alianza kuwa makamu wa kwanza wa rais mwaka 2010, tafauti ikiwa Pepe Mujica aliingia Machi na Maalim Seif mwenzi Novemba. Rais wa Uruguay aliposhinda uchaguzi wa Urais alikataa kuishi katika nyumba ya kifakhari, ambayo imetengenezwa maalum kwa matumizi ya rais na kuendelea kuishi katika nyumba ya mke wake. Maalim Seif naye alipenda kuendelea kuishi katika nyumba ile ya Mtoni Kidatu baada ya kuchaguliwa kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, lakini maafisa wa usalama walimkatalia na serikali kuja na hoja ya kwamba imeamua kumbadilishia nyumba kwa kuwa nyumba hiyo aliyokuwa akiishi ni ya Serikali pia, hivyo tayari imepangiwa matumizi mengine hivyo hakuwa na budi akubali kuhamishwa.

Rais Mstaafu wa Uruguay, anamiliki gari ya kizamani sana aina ya Volkswagen Beetle ambayo ni ya mwaka 1987, ambapo kwa sasa hata kama akiamuwa kuiuza basi haiwezi kununuliwa. Maalim Seif hajawahi katika maisha yake kumiliki hata baiskeli yake mwenyewe wachilia mbali gari.

Rais mstafu wa Uruguay aliwahi kupigwa risasi mara sita na alitumikia kifungo miaka 14 jela ambapo muda wake mwingi kizuizini hapo alikua katika mazingira magumu na kutengwa, mpaka alipoachiliwa huru mwaka 1985 wakati Uruguay ilivyorudi kwenye demokrasia. Ingawa Maalim Seif sina kumbukumbu ya kwamba aliwahi kufyatuliwa risasi, lakini naye alifungwa jela kwa kipindi cha miezi 30 kuanzia mwezi wa Mei 1989 hadi Novemba 1991. Jitihada mbalimbali zikachukuliwa za kidiplomasia, shirika la Amnesty International na wasomi kudai atolewe jela. Baada ya hapo akatolewa pamoja na masharti na vikwazo vingi. Pia kwa muda huo wa miezi 30 jela anaungana na na rais mstaafu Uruguay kwa kuwa alikuwa na mazingira magumu kule jela alikokuwepo.

Jela ndiyo iliyomfanya Maalim Seif kufuga ndevu. Kabla ya kuingia jela alikuwa akionekana mara nyingi na sharubu ndogo tu. Rais mstaafu wa Uruguay alisema hali ile iliyokabiliana nayo jela ndiyo iliyombadilisha mtazamo wake juu ya maisha na anakwambia ‘mimi naitwa rais maskini lakini mimi wala sihisi umaskini wowote, watu masikini ni wale ambao kazi yao ni kuishi maisha ya gharama ambayo inawasababisha kufanya kazi sana ili waendelee na maisha ya gahrama na kupata zaidi”.

Sijawahi kumsikia Maalim Seif akisema kwamba ameamuwa kuishi maisha ya kawaida, maisha ya kutopenda fakhari za kiuongozi kwa athari alizozipata jela, lakini nadhani hiyo ni ahadi yake ndani ya nafsi yake kwamba hapendi kuona kuona mali za umma zinatumika ovyo kwa kujinufaisha yeye na familia yake kama tunavyoona kwa viongozi wengi wa Serikali ya Zanzibar na hata ile ya Muungano ambapo Zanzibar ni mshirika. Kutokana na azma yake hiyo ya kutofanya ufujaji wa mali za umma, kutokuwa na matumizi mabovu ya madaraka ni vitu vilivyomfanya awe kiongozi maskini, lakini napenda nimkatalie kama alivyokataa mwenyewe rais mstaafui wa Uruguay kwamba yeye si masikini na Maalim Seif si masikini bali ni tajiri mkubwa kwa kuwa watu wengi wanampenda kwa tabia na jinsi anavyoishi maisha rahisi na maisha ya kiungwana sambamba na kinaya ya roho. Huo ndio utajiri wake.

Kabla ya kukamata hatamu za urais, rais mstaafu wa Uruguay aliwahi kupitia kuwa waziri wa mifugo, kilimo na uvuvi wa nchi hiyo, aliiyongoza Uruguay vizuri sana kupitia wizara hiyo, aliondowa uzembe kazini, uchelewaji uliondoka, utendaji usioridhisha ulishughulikiwa, na kwa muda ambao alikuwa waziri katika wizara hiyo hakuna mfanyakazi aliyewahi kufika mapema kazini kabla yake, nikimaanisha yeye ndiye aliyekuwa akifika kazini mwanzo kushinda watendaji wengine wote isipokuwa walinzi ambao mara nyingi wao hupishana zamu. Halikadhalika, awali Maalim Seif aliwahi kuwa waziri wa elimu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali hiyo, katika wakati wake alipokuwa na nyadhifa hizo, waliokuwa waajiriwa wa wizara hizi zama hizo yeye alipokuwa Waziri wana mengi ya kusimulia kwani alikuwa akifanya ziara za kushtukiza mashuleni wakati alipokuwa waziri wa elimu ili kuangalia maendelo yakinifu ya mashuleni na hadi alifikia kuanzisha mabuku ya mahudhurio makazini na kupiga mstari mwekundu mara aingiapo yeye ofisini ili kuwagumduwa wachelewaji na waondokaji mapema makazini. Aliyafanya hayo yote kwa ajili ya maendeleo ya taifa la Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Rais mstaafu wa Uruguay katika nyakati zake zote za uongozi, tangu akiwa waziri hadi kufikia kuwa rais wa nchi hiyo hakuwa akipenda kuitwa majina ya utukufu kama vile mheshimiwa na mengineyo yanayoashiria utukufu, yeye alipenda kuitwa bwana akimaanisha kuwa ni mwanamme na vile vile mwanamme aliye na mke na pia, ni mtunzaji wa mbwa wake aliyekuwa na miguu mitatu. Hata hivyo, jina lake analolipenda zaidi ni “Pepe” ambalo kwa Kihispania ni alama ya jina la Jose au Joseph. Hali kadhalika kwa Maalim Seif yeye hupenda aitwe kwa jina lake la lililotokana na kazi yake ya ualimu ambayo aliifanya katika miaka yake awali kabla ya kuwa kiongozi wa chama na serikali, “Maalim”.

Makala ya Ali Mohamed Ali

Advertisements

One thought on “Maalim Seif wa Z’bar kama Pepe Mujica wa Uruguay

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s