Tanzania inaelekea kwenye mzozo wa madeni – BUK

Baraza Kuu linasikitishwa na kustushwa na kasi ya kuongezeka kwa deni la taifa. Deni la nje limeongezeka zaidi ya mara 3 toka dola za Marekani bilioni 4.1 mwaka 2006 na kufikia dola bilioni 14.5 Januari 2015. Deni la ndani limeongezeka toka shilingi bilioni 1729 mwaka 2006 na kufikia shilingi billion 7,481. Deni la Taifa la ndani na nje mpaka sasa deni hilo limefikia Tshs Trilion 32.9 ambazo deni la nje ni 25.4 na zilizobaki ni deni la ndani. Serikali bado inajipongeza kuwa Tanzania inakopesheka. Na sasa serikali inakopa madeni makubwa yenye masharti ya kibiashara. Kasi ya kuongezeka kwa Deni la Taifa kunatishia kuliingiza taifa katika mgogoro wa madeni. Ikumbukwe Rais Mkapa alitumia muda mrefu wa uongozi wake kutimiza masharti yaliyowekwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia ikiwa ni pamoja na kubinafsisha mashirika ya umma ili Tanzania isamehewe madeni. Baraza Kuu limewaagiza Wabunge wa CUF washirikiane na Wabunge wenzao wa vyama vya UKAWA katika Bunge lijalo la Bajeti kuidhibiti serikali iache kuendelea kuongeza Deni la Taifa kwa kasi hii ya kutisha.

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Haruna Lipuma

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI                                                                                                               17 Aprili 2015

MAAZIMIO YA KIKAO CHA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA KILICHOFANYIKA OFISI KUU YA CHAMA ,UKUMBI WA SHABAN KHAMIS MLOO, JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 14-15 APRILI, 2015
Baraza Kuu la Uongozi Taifa la The Civic United Front (CUF- Chama Cha Wananchi) limekutana katika kikao chake cha kawaida kwa mujibu wa Katiba ya Chama. Kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa Chama- Taifa, Mhe. Prof Ibrahim Lipumba na kufanyika katika Ukumbi wa Shaban Khamis Mloo , jijini Dar es salaam, Tarehe 14-15 Aprili, 2015. Katika kikao hicho, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limepokea, limejadili na kuzifanyia maamuzi agenda 11 zilizowasilishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa.

Baada ya mjadala wa kina kuhusiana na agenda hizo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo:

1. UTEKELEZAJI WA KAZI ZA CHAMA KIPINDI CHA NOV. 2014 HADI MACHI 2015

Baraza Kuu limepokea Taarifa ya Kazi za Chama kwa kipindi cha Novemba 2014 hadi Machi 2015, na limeipongeza Kamati ya Utendaji kwa Kazi ilizofanya ya kusimamia programu ya ujenzi na uimarishaji wa Chama katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi kilichopangwa pamoja na changamoto za kiutendaji zinazowakabili. Baraza Kuu limetoa msisitizo kwa Kamati Tendaji kuendelea kujipanga zaidi na kuendeleza Mapambano ya kuing’oa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

2. MIGOMO NA MIGOGORO KATI YA SERIKALI NA MAKUNDI YA WANANCHI

Baraza Kuu la Uongozi limesikitishwa na udhaifu wa Serikali katika kushughulikia masuala kadhaa ambayo ni kiunganishi cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii. Udhaifu huo umesababisha migomo na migogoro mbalimbali kama vile ya wafanyabiashara kutumia mashine za EFD, vijana waliomaliza mafunzo ya JKT kutotimiziwa ahadi za ajira na mgomo wa madereva wa mabasi. Badala ya serikali kutekeleza wajibu wake na kufanya mazungumzo na makundi haya ya wananchi, imewageuzia kibao na kutumia nguvu kubwa ya kuwadhibiti na askari kuwapiga na kwarushia mabomu. Migogoro hii imesababisha hasara kubwa kwa wananchi na pia kupunguza mapato ya serikali. Baraza Kuu linalaani vitendo vya kuwapiga, kuwakamata na kuwabambikizia kesi viongozi wa wafanyabiashara, madereva na vijana waliomaliza JKT.

3. UPORAJI WA ARDHI ZA WANANCHI

Baraza Kuu limestushwa na kuendelea kwa uporaji wa ardhi za wananchi unaofanywa na wawekezaji matapeli kwa kushirikiana na watendaji ndani ya serikali. Pamoja na Tanzania kuwa na ardhi ya kutosha kwa raia wake, ugawaji wa mapande makubwa ya ardhi kwa wawekezaji yataleta mtafaruku na uvunjifu wa amani na kuwafanya raia wazawa kuwa masikini wa kudumu. Baraza Kuu limetoa wito kwa wabunge wake kuiwajibisha serikali katika vikao vya Bunge kuhusu ugawaji hovyo wa ardhi ya wananchi kwa wawekezaji matapeli.

4. HALI YA UCHUMI

a) Ajira
Baraza Kuu limesikitishwa na hali mbaya ya ukosefu wa ajira. Vijana wasiokuwa na ajira wanakata tamaa ya maisha na wanaweza kujiingiza katika shughuli za uhalifu na za kuvuruga amani kama vile “Panya Road.” Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa mwaka 2012 sekta rasmi iliajiri wafanyakazi wa kudumu 1,323,773 tu sawa na asilimia 5.8 ya nguvukazi yote. Nguvukazi ya Watanzania milioni 16 ilijiajiri katika sekta ya mkulima mdogomdogo kupata mahitaji yao ya maisha. Sekta isiyo rasmi ambayo inategemewa na watu wengi mijini iliajiri watu milioni 2.5. Vijana laki nane wanaingia katika soko la ajira kila mwaka lakini sekta rasmi ina nafasi za ajira 20000 – 30000 tu. Baraza Kuu limeagiza waandaaji wa Manifesto ya Uchaguzi ya CUF na UKAWA kujikita katika suala la kukuza uchumi unaoongeza ajira nzuri (decent employment) kwa Watanzania.

b) Deni la Taifa
Baraza Kuu linasikitishwa na kustushwa na kasi ya kuongezeka kwa deni la taifa. Deni la nje limeongezeka zaidi ya mara 3 toka dola za Marekani bilioni 4.1 mwaka 2006 na kufikia dola bilioni 14.5 Januari 2015. Deni la ndani limeongezeka toka shilingi bilioni 1729 mwaka 2006 na kufikia shilingi billion 7,481. Deni la Taifa la ndani na nje mpaka sasa deni hilo limefikia Tshs Trilion 32.9 ambazo deni la nje ni 25.4 na zilizobaki ni deni la ndani. Serikali bado inajipongeza kuwa Tanzania inakopesheka. Na sasa serikali inakopa madeni makubwa yenye masharti ya kibiashara. Kasi ya kuongezeka kwa Deni la Taifa kunatishia kuliingiza taifa katika mgogoro wa madeni. Ikumbukwe Rais Mkapa alitumia muda mrefu wa uongozi wake kutimiza masharti yaliyowekwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia ikiwa ni pamoja na kubinafsisha mashirika ya umma ili Tanzania isamehewe madeni. Baraza Kuu limewaagiza Wabunge wa CUF washirikiane na Wabunge wenzao wa vyama vya UKAWA katika Bunge lijalo la Bajeti kuidhibiti serikali iache kuendelea kuongeza Deni la Taifa kwa kasi hii ya kutisha

c) Kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania
Thamani ya shilingi ya Tanzania ukilinganisha na dola ya Marekani imeporomoka kwa kasi kubwa. Wakati Rais Kikwete anaanza awamu ya kwanza mwaka 2005 dola 1 ilikuwa na sawa na shilingi 1165.5. Hivi sasa dola ni zaidi ya shilingi 1805. Toka mwaka 2014 kasi ya kuporomoka kwa shilingi kumeongezeka sana. Kuporomoka kwa shilingi kunaongeza gharama za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kama vile mafuta ya petroli, dawa, mbolea na pembejeo za kilimo, mashine, vyakula n.k. na kwa hiyo gharama za maisha ya wananchi zinaongezeka. Sababu za ndani za kuanguka kwa thamani ya shilingi ni ufisadi na utoroshaji wa fedha za kigeni nje ya nchi, kupunguzwa kwa misaada ya bajeti kwa sababu ya ufisadi wa IPTL/Tegeta Escrow Account na ongezeko la mikopo ya ndani ya serikali ambayo haitumiwi vizuri kuongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa na huduma. Tanzania inahitaji mabadiliko ipate serikali adilifu itakayo kuwa na matumizi mazuri wa fedha za umma kuongeza tija na uzalishaji, na kudhibiti utoroshaji wa fedha za kugeni nje ya nchi.

d) Kufungwa kwa baadhi ya shule za sekondari kwa ukosefu wa chakula 
Hali ya fedha ndani ya serikali ni mbaya. Wizara, idara na taasisi nyingi za serikali zinapewa fedha za kukidhi mishahara tu. Matumizi mengine yanatengewa fedha kidogo. Baraza Kuu lina laani usimamizi mbovu wa Wizara ya Elimu uliopelekea shule kadha za Sekondari hapa Nchini kufungwa kutokana na kukosekana kwa Chakula. Hali hii inaonyesha uwezo mdogo wa Viongozi wa Serikali katika kusimamia upatikanaji wa elimu bora ambayo ni haki ya msingi ya vijana wetu. Walimu wengi hawajalipwa stahiki zao. Askari polisi hawalipwi posho wanazostahiki. Hospitali na zahanati hazina dawa. Wakati shule zinafungwa kwa kukosa chakula na zahanati hazina dawa ziara za Rais nje ya nchi zinazotumia mabilioni ya shilingi zinaendelea kwa kasi na ari ya juu. Baraza Kuu limeitaka Serikali kupeleka fedha za chakula na kufungua shule zote za sekondari zilizofungwa kwa ukosefu wa chakula. Bunge la bajeti bila kujali itikadi ya vyama liwajibishe serikali kwa kutoheshimu bajeti inayopitishwa na Bunge.

5. AJALI NA MAAFA

a)Ajali za Barabarani 
Baraza Kuu linasikitishwa na ongezeko la ajali za Barabarani hapa nchini. Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani ameeleza kuwa kati ya Januari na Machi, mwaka huu, watu 866 walipoteza maisha yao na wengine 2,370 kujeruhiwa kutokana na ajali mbalimbali za barabani. Ajali hizi zinazotokea kila siku na kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu, majeruhi wengi na kuteketea kwa mali za Watanzania. Kwa kipindi chote serikali haijawa na suluhisho la kudumu au kuchukua hatua stahiki kupunguza ajali hizo. Siku za nyuma mabasi ya abiria yalitakiwa kufunga vidhibiti mwendo “speed governor” lakini utaratibu huu haujulikani ulifanikiwa kwa kiasi gani na sababu gani uliondolewa. Siku zote serikali imekuwa na kauli zisizo za uhakika kwa mfano imewataka madereva kupata vyeti vipya vya mafunzo huku ikijua kuwa vyeti hivyo vinauzwa mitaani.

Sababu za ajali nyingi ni miundombinu mibovu, magari mabovu, madereva kwenda mwendo wa kasi, mafunzo hafifu ya usalama barabarani kwa madereva wa malori na mabasi ya abiria, vitendo vya rushwa katika utoaji wa leseni na usimamizi wa usalama barabarani. Baraza kuu la uongozi linaitaka serikali kufanya utafiti wa kina juu ya sababu za ongezeko la ajali za barabarani kila uchao na kuweka utaratibu madhubuti wa kusimamia usalama barabarani ili kunusuru maisha ya Watanzania na mali zao.

b) Maafa 
Baraza Kuu limesikitishwa na kuhuzunishwa na maafa yaliyotokea sehemu mbali mbali za nchi na kusababisha vifo na kuharibiwa kwa mali za wananchi. Baraza Kuu linatoa pole kwa wananchi wa mikoa ya Shinyanga kutokana na madhara yalitokana na mvua ya mawe na radi na kusababisha kupoteza maisha ya watu kadhaa na uharibifu mkubwa wa mali. Aidha Baraza Kuu linatoa pole kwa wakaazi wa mkoa wa Dar es Salaam, mtaa wa Mnyamani kwa maafa yaliyowafika kutokana na mvua kubwa na kutotengenezwa miundombinu ya mitaro ya kupitisha maji. Serikali inawajibika kukarabati miundombinu ya kupitisha maji kabla ya msimu wa masika. Pia Baraza Kuu linatoa pole kwa wakaazi wa mkoa wa Kigoma kwa maafa waliyopata kutokana na radi.

c) Mauaji ya Albino
Baraza Kuu bado linasikitishwa na uvunjaji wa haki za binaadamu unaofanywa na watu wenye imani za kishirikina na tamaa ya utajiri wa haraka kwa mauaji ya Albino hapa nchini. Pamoja na ahadi za Jeshi la Polisi na Serikali kuwalinda Albino, ni wazi serikali inaonekana kushindwa kutekeleza wajibu wake kuwalinda raia wake. La kusikitisha zaidi hata zile kesi ambazo mahakama ilikwisha amua kuzitolea hukumu Rais ameshindwa kuzichukulia hatua za utekelezaji. Baraza Kuu la uongozi lina laani mauaji na kukatwa viungo vya albino yanayoendelea kutokea nchini. Vinaitaka serikali kutimiza hukumu za wale waliopatikana na hatia na kuweka mkakati madhubuti wa kuwalinda raia wenye ulemavu wa ngozi.

6. KUHUSU SUALA LA KUANDIKISHA WAPIGA KURA 

Baraza Kuu limesikitishwa na ukosefu wa uwazi na ukweli katika zoezi la uandikishaji wapiga kura. Tarehe 7 Februari 2013 Rais Kikwete alizindua vitambulisho vya taifa vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na akaeleza bayana kuwa kwa kuwa shughuli ya kutoa vitambulisho ina gharama kubwa vitambulisho vya taifa ndivyo vitakavyotumika kupigia kura. Hoja yaRais ilikuwa na mantiki. Gharama ya kuandikisha na kuchapisha vitambulisho vyenye alama ya muili za kibaolojia (biometric ID) ni kubwa. Hakuna sababu ya raia wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kuwa na vitambulisho viwili kimoja cha utambulisho wa taifa na kingine cha kupigia kura. Rais alieleza kuwa “Lazima kabla ya uchaguzi wa 2015 Watanzania wote wanaostahili wana Vitambulisho. Kwa sababu hiyo tutaiwezesha NIDA kwa hali na mali itekeleze kazi yake. Nimeishazungumza na Waziri wa Fedha wakiwa pamoja na Katibu Mkuu wake kuhakikisha kuwa zoezi hili linatengewa fedha za kutosha.” Hata hivyo Serikali haikufanya uratibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Tume ya Uchaguzi ili taasisi mbili zishirikiane na kukamilisha zoezi hili. NIDA haikupewa fedha za kutosha kukamilisha zoezi la kuandikisha na kutoa vitambulisho vya taifa.

Sheria inahitaji Tume kuboreshaDaftari la Kudumu la Wapiga kura alau mara mbili kati ya uchaguzi mkuu na unaofuata. Kwa makusudi Serikali ya Rais Kikwete imevunja sheria ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura. Tarehe 29 Januari 2014 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) Jaji Damian Lubuva alisema daftari la kudumu la wapigakura litaboreshwa kabla ya kuanza kwa upigaji wa kura ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya. Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari na kueleza kuwa tume hiyo imeshapata fedha kutoka serikalini kwa ajili ya kuendesha mchakato wa kufanya maboresho hayo. “NEC inawataka wananchi kutokuwa na wasiwasi juu ya suala hili. Jukumu la kusimamia na kuendesha mchakato huu ni la tume hii hivyo vyombo vingine visijiingize katika shughuli zisizowahusu.”

Mwezi Julai 2014 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi alieleza kuwa zoezi la kuandukisha wapiga kura litaanza Septemba 2014 katika vituo 40,015 nchi nzima na kila kituo kitandikisha wapiga kura kwa siku 14. Hata hivyo zoezi hili halikuanza mwezi wa Septemba. Badala yake, mwezi Desemba Tume iliandikisha katika kata chache katika majimbo matatu kama majaribio.

Tume ya Uchaguzi imeanzisha mchakato wa kuandikisha wapiga kura bila kutengewa fedha za kutosha za kununulia vifaa, kuajiri na kuwapa mafunzo wafanyakazi husika, na kutoa elimu kuhusu kujiandikisha kwa wananchi. Tume ilikadiria kuhitaji vifaa (Registration Kits) 15,000 ili kukamilisha zoezi la kuandikisha wapiga kura milioni 24. Serikali ilipunguza idadi ya vifaa na kuidhinisha Tume iagize vifaa 8000. Vifaa 250 tu ndivyo vilivyoingia nchini mwaka 2014. Hivi karibuni Tume imeeleza kuwa imepokea vifaa vingine 248. Jumla ya vifaa vyote 498. Waziri Mkuu alieleza kuwa serikali imeishatoa asilimia 78 ya fedha inayohitajika katika uandikishaji wa wapiga kura. Hata hivyo hakutaja kiasi halisi. Kutokuwepo uwazi katika suala hili kunaashiria ufisadi na wizi wa fedha zilizotengwa kununulia BVR Kits
Baraza Kuu linasikitishwa na kasi ndogo ya uandikishaji kwenye Daftari la Kudumu. Mpaka sasa Tume haijamaliza uandikishaji wa Mkoa mmoja wa Njombe na woe walioandikishwa katika Mkoa huo hawazidi wapiga kura 200,000.

Baraza Kuu linaitaka Serikali kukaa na wadau wote wa uchaguzi na hususan vyama vya siasa kutathmini kwa pamoja hali halisi ya uandikishaji wapiga kura na kuweka mkakati utakaohakikisha wananchi wote wanaostahiki wanandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Mwezi October 2015.

7. KURA YA MAONI

Baraza Kuu linasikitishwa na hatua ya Rais kuingilia mamlaka ya Tume na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni kuwa tarehe 30 Aprili. Rais alitangaza siku ya kupiga kura akiwa katika ziara Jamhuri ya Watu wa China. Tume ya Uchaguzi ilielekea kuikubali siku hiyo wakati Tume ndiyo imepewa jukumu la kisheria la kutoa taarifa ya siku na muda wa kupiga kura. Tume huru ilipaswa kutoa kauli ya wazi kuwa jukumu la kutangaza siku ya kura ya maoni ni la Tume na siyo taasisi au kiongozi mwingine.

Baraza Kuu limekubaliana na kauli ya Viongozi wa UKAWA kutoshiriki kwenye Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa mchakato wa kuipitisha Katiba Inayopendekezwa katika Bunge Maalum haukuwa halali. Maoni ya wananchi yalichakachuliwa. Pamoja na mapungufu mengi, kuondolewa kwa Uwajibikaji, Uwazi na Uadilifu kuwa Tunu za Taifa kwenye Katiba Inayopendekezwa kunasaliti maoni yaliyotolewa na wananchi. Kuondoa vifungu vinavyozuia viongozi wa umma kumiliki akaunti za benki nje ya nchi na kutangaza zawadi wanazopewa na kuzikabidhi Serikalini zinaonesha wazi kuwa Katiba inayopendekezwa ina lengo la kuwalinda mafisadi.

Baraza Kuu la Uongozi linamtaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva kuwa muadilifu, kutoyumbishwa na kutekeleza wajibu wa kazi zake ili kujenga taasisi bora na kujijengea heshima katika jamii yetu. Tume itamke wazi kuwa kura ya maoni haiwezi kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu kwani Tume haina muda wa kutosha kusimamia uandikishaji wapiga kura, kukamilisha maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 na kuandaa kura ya maoni.

Baraza Kuu linaitaka tume ya uchaguzi kuhakikisha uandikishaji wa daftari la wapiga kura unakamilika na uchaguzi unafanyika kwa wakati.

8. KUHUSU UCHAGUZI MKUU UNAOTARAJIWA KUFANYIKA MWEZI OKTOBA 2015

Baraza Kuu linaitaka Serikali kurejea makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha Rais na viongozi wa TCD kufanya marekebisho machache ya Katiba ya 1977 kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015. Marekebisho hayo ni kuruhusu uwepo wa a) Tume Huru ya Uchaguzi, b)Mgombea huru, c) Mshindi wa nafasi ya Urais apate kura zaidi ya 50% d) Matokeo ya Urais yaweze kuhojiwa Mahakamani.

9. KUHUSU UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU UNAOFANYWA NA JESHI LA POLISI

(a) Baraza Kuu lina laani na kusikitishwa na matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na udhalilishaji unaofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya raia wasiokua na hatia, kuwatesa kwa vipigo na matendo mengine na hatimae kubambikiziwa kesi zisizo na ushahidi.

(b) Baraza Kuu lina laani na kupinga vitendo vya udhalilishaji na uvunjwaji wa haki za binaadamu uliofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya anachama wetu akiwemo Mwenyekiti taifa tarehe 27 Januari 2015 kwa kuwapiga na kuwajeruhi kisha kuwabambikia kesi ya kula njama kutenda uhalifu. Mwenyekiti alienda kutoa taarifa kuwa maandamano na mkutano wa hadhara umeziwiwa na Polisi walipeleka taarifa ya kuzuia mkutano tarehe 26 Januari saa 12.30 jioni wakati watendaji wa Ofisi Kuu hawapo. Baraza Kuu linawapongeza Wabunge wa UKAWA kwa kulijadili suala hili Bungeni.

(c) Baraza Kuu linalaani vikali vitendo vya kiharamia vya kushambuliwa kwa msafara wa wanachama wa CUF waliokuwa wakitoka mkutanoni Makunduchi. Wanachma wengi waliumizwa kwa kupigwa mawe, chupa na kukatwa na visu. Baraza Kuu limelitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika na uharamia huu. Pia Baraza Kuu linalaani kuchomwa moto kwa ofisi za chama cha CUF Dimani na Tumbatu. Linawataka Polisi kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.

(d) Baraza Kuu lina laani kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani kuhusu wafuasi wa vyama vya siasa kutoruhusiwa kushiriki kwenye mikutano ya hadhara kwa wingi nje ya wilaya zao. Baraza Kuu linaiona kauli hii inakiuka katiba ya nchi inayompa uhuru kwenda popote anapotaka alimuradi asivunje sheria. Pia kauli hii inaipinga Sheria ya Vyama vya Siasa inayowapa uhuru wananchi kwenda eneo lolote ndani ya nchi yetu na kuhudhuria na kusikiliza mikutano ya vyama vya siasa.

(e) Baraza Kuu linalaani kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya kuzitishia kuzifunga taasisi za kidini zinazopinga Katiba Inayopendekezwa. Serikali haina mamlaka ya kuwaziba midomo viongozo wa dini wasijadili masuala ya jamii, wasikemee ufisadi na kudharauliwa maoni ya wananchi. Baraza Kuu linamtaka Waziri Chikawe awaombe radhi viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla kwa kauli yake ya kuwanyanyasa na kuwatisha viongozi wa dini

(f) Baraza Kuu lina itaka Serikali kuiweka wazi Ripoti ya Jaji Msumi ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza. Kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanyika wakati wa kutekeleza Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo iligeuka kuwa Operesheni Tokomeza Mali na Maisha ya Watanzania waliokua wanaishi mipakani au karibu na mipaka ya mbuga za wanyama na hifadhi za taifa. Usambazaji wa ripoti hiyo utasaidia kuwabaini waliotenda makosa hayo na hivyo kuziwezesha Taasisi mbali mbali kusimamia mapendekezo yalioanishwa ndani ya Ripoti hiyo.

10. KUHUSU MASHIRIKIANO YA VYAMA VINAVYOUNDA UKAWA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

(a) Baraza Kuu lipomekea Taarifa ya Mashirikiano ya Vyama vya NCCR,NLD,CUF na CHADEMA (UKAWA) na kubariki hatua zote zilizofikiwa na umoja huo.

(b) Baraza Kuu linawapongeza viongozi wa UKAWA kwa hatua za ushirikiano zilizofikiwa na kwahimiza waendelee na juhudi hizo kwa lengo la kuing’oa CCM madarakani na kujenga taifa linaloongozwa na misingi ya uadilifu, uwajibikaji na uwazi na lenye haki sawa kwa wote. Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu.

HITIMISHO
Baraza Kuu linatoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi za vyama vya UKAWA kushirikiana katika azma la kukin’goa CCM, chama cha mafisadi, toka madarakani. UKAWA unaendeleza maengo ya CUF:

• Kuwaunganisha Watanzania ili wakatae uonevu, kudhalilishwa, kunyanyaswa, kubaguliwa au maovu mengine yanayoweza kufanywa dhidi ya heshima ya utu wa binadaamu, yawe yanayotendwa na Serikali, kikundi cha watu walio na uwezo kwa ajili ya mabavu yao au kwa ajili ya kujinufaisha kwao kiuchumi au kisiasa na kiitikadi au kwa kujali dini, kabila, jinsia au rangi zao.
• Kulinda na kuendeleza haki za binadamu kama zilivyotamkwa katika matangazo makuu ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi huru za Afrika, na kulinda taasisi zitakazohakikisha kwamba haki hizo zinaheshimiwa na zinatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
• Kudumisha, kulinda na kustawisha demokrasia kwa kuhakikisha kwamba wananchi wote wana haki na fursa sawa ya kuchagua viongozi wa siasa wa kuendesha serikali yao wakiwemo Rais, Wabunge,Wawakilishi, Madiwani viongozi wa serikali za vitongoji, vijiji na mitaa, na wajumbe wa vyombo vyote vitakavyowekwa na wananchi wenyewe moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi wao.
• Kuhakikisha kwamba wananchi wana madaraka ya kujiamulia wenyewe masuala yote ya maendeleo yao kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na hivyo kuondoa mtindo wa kupangiwa na wajanja wachache wenye ukiritimba wa wazi na uroho wa madaraka au mali wanazotaka kuzipata kwa njia zisizokuwa za halali Kuondoa mambo yote yanayoruhusu rushwa,ufisadi, ubadhirifu, uonevu, ukandamizaji na ubaguzi wa aina yeyote.

Tutashirikiana na vyama vyote vya UKAWA katika mapambano ya kupata serikali itakayoheshimu maoni ya wananchi na kuwapatia Katiba inayolinda maslahi yao na kuhakikisha kuwa maliasili na rasilimali za nchi zinatumiwa kwa manufaa na maslahi ya wananchi wote.

HAKI SAWA KWA WOTE
Imetolewa na:
Baraza Kuu La Uongozi la Taifa
Tarehe 17 Oktoba 2015

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s