CUF yamshauri Rais Shein kumdhibiti Haji Omar Kheir

“CUF iinaendelea kumshauri Rais Ali Mohamed Shein, akiwa kiongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kufuatilia nyendo za watendaji wa serikali yake ili kuwadhibiti viongozi wa aina ya Haji Omar Kheir waliotayari kuhatarisha amani ya nchi kwa maslahi yao binafsi ili kulinda amani hiyo na kufikia lengo la kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.”

Waziri Haji Omar Kheri

Waziri Haji Omar Kheri

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tarehe 08/03/2015, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kanda Maalum na Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu, Mheshimiwa Haji Omar Kheir alifanya Mkutano wa hadhara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Tawi la Chama hicho katika eneo la Tumbatu Gomani katika Jimbo la Tumbatu.

Mkutano huo, ulikuwa ni mfuliulizo wa Mikutano ya Kiongozi huyo baada ya ule wa tarehe 21/12/2014 ambao alisikika akitoa viapo na kusema kuwa ana taarifa za kutosha kuwa kuna vijana wameandaliwa kufanya vurugu katika eneo hilo na kuwa yeye binafsi yupo tayari kupambana na vijana hao.

Ifahamike kuwa vijana anaowakusudia Haji Omar Kheir ni wale wote wanaoonekana kwenda kinyume na matakwa ya CCM na wanaoonekana kukiunga mkono CUF-Chama Cha Wananchi. Zaidi, Kiongozi huyo alisikika akisema kuwa, atahakikisha kuwa vijana hao wanafanyiwa kama walivyofanyiwa wafuasi na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu.

Ni vizuri ikakumbukwa kwamba, utaratibu uliotumika kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wafuasi wa UAMSHO wanaoshikiliwa na jeshi la Polisi ulikuwa ni wa kuingiliwa majumbani mwao saa nane za usiku, kuwekwa kusikojulikana kwa siku kadhaa, kufunguliwa mashitaka katika Mahkama za Tanganyika na kuwekwa Magerezani mjini Dare es Salaam. Pia, washitakiwa hao waliwahi kulalamika Mahkamani juu ya ukiukwaji mkubwa wa Sheria za nchi unaofanywa dhidi yao na unyama wanaofanyiwa ikiwemo kuingiliwa kinyume na maumbile.

Katika Mkutano wake wa tarehe 08/03/2015, Kiongozi huyo alitumia muda mwingi kuwagawa wananchi wa Tumbatu kwa mujibu wa maeneo yao, itikadi zao, na historia za vyama vya siasa vya zamani vya Zanzibar na kuwachonganisha baina yao kwa kuwatumia wazee wa CCM wa eneo la Tumbatu Gomani kuwadhalilisha, kutumia lugha mbaya na chafu na kukata uhusiano wa kidugu baina yao na wananchi wa Tumbatu Chwaka.

Mbali na bendera za CUF za matawi mawili kushushwa na kuchanwa, kuchomwa moto nyumba moja na kuvunjwa kwa nyumba nyingine za wafuasi wa CUF-Chama Cha Wananchi ni miongoni mwa athari kadhaa zilizotokana na chuki na hasama zilizopandwa na Haji Omar Kheir kwa wakaazi wa Tumbatu. Bendera ya kwanza ilishushwa katika Barza ya CUF Mkwakwani katika kijiji cha Chwaka Tumbatu na ya pili ilishushwa na kuchanwa katika Tawi la Kichangani D. Pia, Maskani ya CCM imetiwa moto na hivyo kupelekea Mkutano wa hadhara wa CUF-Chama Cha Wananchi wa tarehe 14/03/2015 kuzuiliwa

Kimsingi, mambo haya yanayotokea na kuendelea katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Tumbatu na Wilaya ya Kaskazini Unguja ni mpango maalum uliopangwa, kuratibiwa na kufadhiliwa na CCM na Viongozi wao muflis kwa lengo la kuwatisha wananchi na kuwabambikizia kesi ili kutimiza malengo ya Viongozi hao kama yalivyoelezwa na Haji Omar Kheir katika Mikutano yake ya hadhara tuliyoitaja.

Ili kuinusuru nchi na malumbano, malalamiko na migogoro itakayopelekea kuvurugika kwa amani ya nchi, CUF-Chama Cha Wananchi:

• Kinaendelea kumtaka Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa Kiongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kufuatilia nyendo za watendaji wa Serikali yake ili kuwadhibiti Viongozi wa aina ya Haji Omar Kheir waliotayari kuhatarisha amani ya nchi kwa maslahi yao binafsi ili kulinda amani hiyo na kufikia lengo la kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

• Kinavishauri vyombo vya Habari vya Serikali kuacha ushabiki wa kisiasa na kutoa taarifa za matukio yote kwa mujibu wa taaluma ya uandishi wa habari. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari vya serikali hasa gazeti la Zanzibar Leo la siku ya Jumapili March 15, 2015 kuhusu matukio ya Tumbatu imethibitika kwamba taarifa hizo zimepotoshwa na kuripotiwa kwa kuzingatia athari zilizotokea kwa Chama cha CCM na kupuuza athari za upande wa CUF.
• Kinawaomba wananchi wa Tumbatu kutokubali kuchokozeka kutokana na vitimbi vya CCM na viongozi wao waliochuja na kufilisika kisiasa.

• Kinalitaka jeshi la Polisi kutokubali kutumiwa kisiasa na baadhi ya Viongozi wa Serikali. Utaratibu mpya ulioibuka ndani ya jeshi hilo wa kuzuia Mikutano ya CUF kwa vigezo na maelezo ya sababu za kiintelijensia zinazotolewa na Jeshi la Polisi hazikubaliki na zinaweza kupelekea kuvunjika kwa amani ya nchi kwa sababu zinaonekana kuwa na viashiria vya mashinikizo kwa lengo la kuibeba CCM.

• Kinawataka wananchi wa Zanzibar kutokuvunjika moyo na kutishika kwa vitimbi vya CCM na kutokubali kutolewa katika mstari wa mapambano kwani nguvu ya Umma ya CUF ya kudai Mamlaka Kamili ya Zanzibar Kitaifa na Kimataifa haizuiliki tena kwa njia yoyote.

Imetayarishwa na Kurugenzi ya Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma.

…………………………..……….
SALIM A. BIMANI
MKURUGENZI WA H/U/M/UMMA

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s