UKAWA waisifu mahakama kiaina

SIKU moja baaada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kushindwa kutoa uamuzi kuhusu aina na ukubwa wa mabadiliko ambayo Bunge Maalumu linaweza kufanya, kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), limesema uamuzi huo ni muhimu kwa mchakato wa Katiba Mpya.

Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutoka kushoto Freeman Mbowe, Ibrahim Lipumba na James Mbatia.

Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutoka kushoto Freeman Mbowe, Ibrahim Lipumba na James Mbatia.

Wakizungumza kwenye ofisi za CHADEMA Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, walisema tangu Februari kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya wajumbe wa UKAWA na wale wa CCM na mawakala wao kuhusu mamlaka ya Bunge Maalum kama yalivyoainishwa kwenye kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

UKAWA walidai kuwa, mamlaka ya Bunge Maalum yana mipaka kisheria na Bunge halina mamlaka ya kubadilisha misingi mikuu ya Rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi, huku CCM na mawakala wake wakidai mamlaka ya Bunge Maalum hayana mipaka, hivyo lina uwezo wa kufanya marekebisho au mabadiliko yoyote kwenye Rasimu ya Katiba.

Kutokana na hukumu iliyotolewa juzi, UKAWA wamesema uamuzi huo wa Mahakama Kuu unathibitisha usahihi wa hoja ya UKAWA kwamba, mamlaka ya Bunge Bunge Maalum yana mipaka kisheria.

Akisoma tamko kwa niaba ya wenyeviti hao, Lissu alisema kuwa, Mahakama kusema Bunge Maalum lina mamlaka ya kufanya maboresho na/au marekebisho kwenye Rasimu ya Katiba, maana yake imekataa dhana ya CCM na mawakala wake kwamba Bunge Maalum lina mamlaka ya kubadilisha Rasimu ya Katiba.

Lissu, alisisitiza kuwa, amri ya Mahakama Kuu haijataja kabisa neno kubadilisha, ambalo liliingizwa kwa nguvu kwenye Kanuni za Bunge Maalum. Kwa hiyo, kanuni ya 3 ya Kanuni za Bunge Maalum inayotafsiri neno ‘hoja’ kuwa ni pamoja na mamlaka ya Bunge Maalum kubadilisha Rasimu ya Rasimu ipo kinyume na matakwa ya kifungu cha 25 cha Sheria na hivyo tafsiri hiyo ni batili.

Akifafanua kauli hiyo, Lissu alisema sio mara ya kwanza Mahakama Kuu kutoa uamuzi ambayo hauonyeshi msimamo kisheria, kwani Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu iliyokuwa inahusu suala la mgombea binafsi, Mahakama Kuu ya Tanzania ilikwepa kutekeleza wajibu wake wa kutenda haki kwa kufuata Katiba na Sheria za nchi kwa kujificha nyuma ya kichaka cha ‘maamuzi ya kisiasa.’

Lissu, aliilaumu Mahakama kwa kushindwa kuweka wazi Mamlaka ya Bunge Maalum ambayo yamewekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na mipaka yake, kwani ilikuwa na wajibu wa kutafsiri Sheria hiyo kama zilivyo Mahakama nyingine zote, kwa kutamka bayana aina na upeo wa mamlaka ya kisheria ya Bunge Maalum kufanya maboresho na/au marekebisho ya Rasimu ya Katiba.

Katiba ya mtutu, kura za Fax na Twiter

Aidha, Lissu alionya kuwa hali ya kisiasa hapa nchini ni tete. Alisema nchi iko chini ya utawala wa kijeshi usio rasmi.

Alisema, kila mahali katika makao makuu ya mikoa, wilaya na majimbo, askari wa Jeshi la Polisi wenye mabomu, risasi za moto, magari ya deraya, farasi na mbwa wametanda ili kujaribu kuzuia maandamano na mikutano ya wananchi wanaopinga mchakato wa Katiba unaoendelea na Jengo linalotumiwa na Bunge Maalum limezingirwa na vikosi vya Polisi.

Kwa hali hiyo, Lissu alisema mchakato wa Katiba umetekwa na Polisi pamoja na Bunge Maalum huku watanzania wakilazimika kuwa mateka wa Jeshi hilo na vyombo vingine vya mabavu.

Alionya kuwa, ni kitu cha ajabu Katiba mpya inatengenezwa kwa mtutu wa bunduki.

“Mchakato wa kimabavu hautakuwa na uhalali wowote wa kisiasa. Sasa baada ya mabadiliko mbalimbali ya Kanuni za Bunge Maalum kuruhusu uchakachuaji… sio tu wa Rasimu ya Katiba, bali pia uchakachuaji wa maamuzi ya wajumbe waliobakia wa Bunge Maalum, ni wazi pia kwamba chochote kitakachotolewa na Bunge Maalum kwa sura ya Katiba inayopendekezwa, kitakuwa batili kisheria vile vile,” alisema na kuongeza.

Kwa sababu hizo, tunawaomba Watanzania wote wenye nia njema na nchi yao, kupinga nchi yetu kugeuzwa kuwa dola ya kipolisi. Tunawaomba wanachama na viongozi wote wa vyama vya UKAWA, kufanya maandalizi ya kupinga vitendo hivi kwa njia mbalimbali za kidemokrasia.

Mbowe: Tunatumia busara kuomba wananchi wasipige Polisi

Akizungumza wakati wa kujibu maswali, Mbowe alisema kuwa, wametumia busara kutoruhusu wananchi wawajibu polisi au kufanya fujo za kuchoma matairi au kurusha mawe ingawa uwezo huo wanao.

Alionya kwa kumnukuu Nelson Mandela, aliyewahi kusema kuwa; ‘Utawala wowote unaotumia jeshi na vyombo vya dola kuzima sauti za raia wake, utawala huo unafundisha raia kutafuta mbinu mbadala za kupinga utawala huo’.

Mbowe, alionya tabia ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano kote nchini, ikiwemo yeye kuzuiliwa kufanya hivyo Jimbo la Hai, Mbunge wa Moshi Mjini kazuiwa na wabunge wa Mwanza huku Katibu Mkuu wa CCM akiendelea na mikutano mikoa ya Pwani na Tanga.

Alimlaumu Rais Kikwete, kwa kushindwa kuwa na msimamo katika mazungumzo waliyozungumza Dodoma na kwamba, ameshindwa kuongoza hata chama na Serikali yake, ndio maana makada mbalimbali hata mawaziri wanampinga na kwenye suala la Katiba, Sitta ameamua kulitumia anavyoona huku akishindwa kuchukua hatua.

Lipumba alia na Sitta

Kwa upande wake, Prof. Lipumba alisema kuwa Sitta anatia aibu, maana anachakachua kila kitu hata kanuni na kwamba, hawana uhaki na akidi ndio maana wameruhusu watu walioko nje ya Bunge kupiga kura.

Lipumba, alisema hii ni aibu kwani hata kwenye Bunge la Uingereza, wabunge wanaoumwa huletwa bungeni ili wapige kura tofauti na anavyofanya Sitta.

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la tarehe 27 Septemba 2014

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s