CCM itapokwenda kapa 2015

SIDHANI kama kuna atayeshangaa akikiona Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaangushwa katika uchaguzi ujao wa 2015.  Uwezekano wa CCM kwenda kapa 2015 ni mkubwa endapo uchaguzi wa mwaka huo hautokuwa na magube.

Viongozi wa chama wanalijua hilo. Ndio maana baadhi yao wamekwishaanza kuingiwa na wahka na kimuyemuye cha uchaguzi ujao.

Tusisahau kwamba hiki ni chama kilichoshika hatamu za utawala kwa nusu karne sasa tangu Waingereza waondoke Tanganyika na Zanzibar. Lakini kuselelea madarakani kwa muda wote huo kumekidhuru.

Hivi sasa kimefilisika kimaadili na hakina tena ile itikadi ya kisiasa ambayo hapo zamani juu ya taksiri zake ilikuwa ikiwapa wananchi matumaini. Na si wao tu bali hata wengine waliokuwa nje ya mipaka ya Tanzania.

Kuna mambo kadhaa yatayoweza kukichongea chama hicho kianguke 2015. La awali ni ile inayoitwa “ajali ya historia.” Itasadifu kwamba wengi wa wataopiga kura mwaka huo watakuwa vijana waliozaliwa baada ya kuasisiwa CCM.

Hawaijui TANU hawaijui ASP vyama vilivyoungana kuunda CCM. Hawalijui Azimio la Arusha wala hawaijui itikadi yake ya Ujamaa. Na kama wanalijua Azimio hilo kwa kuhadithiwa basi wanaliona hilo Azimio na itikadi yake kuwa ni mizoga mitupu.

Hawaijui Tanzania ilipokuwa ikisifika kwa uadilifu wake wa kisiasa licha ya umaskini wake. Hawayajui maadili yaliyokuwa yakiwaongoza watumishi wa serikali wakiwa pamoja na mawaziri na viongozi wengine.

Mengine yatakayoichongea CCM ni ya kujitakia. Kati ya hayo ni uzembe wake, tuhuma za ufisadi dhidi ya wakuu wake pamoja na utawala mbovu wa serikali yake.

Huo utawala mbovu ndo sababu kubwa iliyoifanya Tanzania iwe hivi ilivyo.

Ingawa takwimu zinaonyesha kwamba uchumi wa taifa unakua lakini umaskini unazidi kuenea. Hali za watu wake wa chini ndizo zile zile za chini kama zilivyo miaka nenda miaka rudi.

Pamoja na dhiki za kimaisha zinazosababishwa na mfumo uliopo wa kiuchumi taifa hilo siku hizilimekumbwa na mivutano ya kijamii. Uliona hatari zaidi ni ule wa kidini unaoibuka mara kwa mara Bara.

Ni viongozi wa serikali ya CCM peke yao wanaokanusha kuwako kwa mvutano huo Bara.

Endapo hapatachukuliwa hatua imara za kuchunguza chanzo cha mvutano huo basi kuna hatari kwamba amani ya nchi itaparaganyika.

Katika hali hii ya sasa inasikitisha kwamba vyama rasmi vya upinzani havina bado ubunifu wa kisiasa na utamaduni wa kuvifanya viwe na muelekeo mbadala wa ule wa CCM ambao ni wa kidemokrasia ya kibepari.

Nachelea kwamba wananchi watapovipa madaraka vyama hivyo vitaziendeleza sera zilizo sawa na za CCM. Hofu kubwa iliyopo ni kwamba viongozi wa vyama hivyo wataendelea na mtindo wa ombaomba kwa kukimbilia kwenda kupiga hodi kwenye milango ya wafadhili. Miongoni mwa wafadhili ni taasisi za unyonyaji kama vile ile ya Mfuko wa Fedha za Mataifa (IMF).

Wataendelea kuwa na mwenendo huo kwa sababu ile niliyokwishaitaja ya kutokuwa na ubunifu wa kisiasa.

Nini kifanywe ili kulinusuru taifa lisizidi kupotoka kwa kukosa dira?

Kinachohitajika kwanza ni kuyajaza mapengo yaliyopo. Pengo kubwa likiwa lile la kutokuwako mavuguvugu ya kijamii yenye nguvu na yenye mizizi ndani ya nchi.

Panahitajika pawepo mavuguvugu aina hiyo ili yaweze kuwajumuisha wakulima, vyama vya wafanyakazi pamoja na wanaharakati walio katika mashirika ya kiraia au asasi za kiraia na waliojitolea kutetea haki za binadamu na nyinginezo.

Hata hivyo, kuwako tu kwa mavuguvugu hayo hakutoshi. Kuwako kwao hakutoweza kubadilisha kitu iwapo hayatokuwa na sera mbadala za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Sera aina hizo ndizo zitazoweza kuleta athari njema katika jamii hasa pale, kwa mfano, zitapoweza kuishurutisha serikali iingilie kati kwa kuchukua hatua zinazostahiki katika sekta za afya, elimu, ajira na mkakati wa kuufyeka au angalau kuupunguza umaskini.

Watanzania wanahitaji wanusuriwe na balaa na majanga ya kiuchumi na kijamii. Lakini labda balaa kubwa linalowakumba ni la viongozi wao.

Sera za viongozi hao ndizo zilizoifanya Tanzania iwe nchi ya ombaomba.  Imekwishazoea kusimama na kikopo chake nje ya milango ya wafadhili. Sera hizo zimelidhuru kabisa taifa.

Kwa hivyo hapana budi ila Watanzania wakingwe wasiendelee kudhuriwa na viongozi wao.

Viongozi wa leo wa CCM ni akhasi pengine kushinda wale wanyonyaji waliokuwa wakipigwa vita na wajamaa wa enzi za Azimio la Arusha.

Vyama vya wafanyakazi vina kazi kubwa.  Vina jukumu la kuwapigania wafanyakazi wawe wanalipwa mishahara ya maana na kuhakikisha kwamba hali zao kazini ni za kiutu na wakati huohuo vina jukumu la kupigania watu wote wenye uwezo wa kufanya kazi wapatiwe ajira. Hiyo si kazi ndogo.

Kadhalika vyama hivyo vinahitajika kuimarisha demokrasia katika jamii na wakati huo huo kuimarisha misingi ya kidemokrasia ndani ya vyama vyenyewe.

Maslahi ya wafanyakazi hayatoweza kutetewa na vyama ambavyo vyenyewe havina utamaduni wa kidemokrasia.

Mageuzi yanaweza yakapatikana.  Uwezekano ni mkubwa. Lakini mageuzi hayo hayatotokea hivihivi tu bila ya kufanyiwa kazi.

Kazi ya kwanza ni kuimarisha ushirikiano baina ya vyama vya wafanyakazi. Kazi ya pili ni kuimarisha ushirikiano baina ya vuguvugu zima la wafanya kazi na vyama vya upinzani.

Hivi sasa vyama vya upinzani nchini Tanzania havivitii maanani vyama vya wafanya kazi. Inaonyesha kama vinavidharau na havitaki pawe na mshikamano wa nguvu hizo mbili katika kuiimarisha demokrasia.

Kuna uwezekano kwamba wale wenye kutaka kuliunganiha vuguvugu la wafanya kazi huenda wasifaulu. Lakini wanaweza pia wakafaulu kwa sababu ni wazi kwamba mageuzi yanaweza kupatikana.

Miaka kama mia moja iliyopita huko Ulaya wanaharakati walikuwa wakichekwa walipokuwa wakiwahimiza wafanya kazi waungane na wawe na vyama vyao vya kupigania maslahi yao. Siku hizo viwanda vilikuwa vimekwisha chipuka Ulaya na vikiwapatia mabepari utajiri usio kifani kwa jasho la wafanya kazi — wenye ujuzi na wasio na ujuzi.

Wafanya kazi hao walikuwa wakifanya kazi katika hali za kinyama.Walikuwa wakinyonywa na wamiliki wa viwanda. Ndipo wanaharakati walipoona kwamba kuna njia moja tu ya kunyanyua maishaya wafanya kazi.

Njia yenyewe ilikuwa kuwaelimisha kuhusu hali zaona haki zao na kuwahimiza waungane waunde vyama vyao.  Wazo hilo lilizitikisa jamii za Ulaya ya miaka hiyo.

Wanaharakati hao wakajitolea kuwaunganisha wafanyakazi.Matunda ya jitihadi zao ni kuzaliwa kwa hili vuguvugu la kisasa la wafanya kazi — vuguvugu ambalo katika nchi nyingi limeongoza harakati za kuleta usawa.

Uchambuzi wa Ahmed Rajab kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 22 Mei 2013

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s