Katiba Mpya: Ufafanuzi wa Maoni ya CUF

Kwamba shughuli zote za uendeshaji wa mamlaka za dola zitafuata misingi ya uwazi, ukweli na uwajibikaji na kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litakagua na kudhibiti utendaji wa vyombo vya dola pamoja na kuridhia mikataba muhimu ya umma. Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na la Zanzibar yatafanya hivyo kwa mamlaka za Tanganyika na Zanzibar kila moja kwa eneo lake na kwa mambo yahusuyo serikali husika na si vinginevyo.

 

UCHAMBUZI NA UFAFANUZI WA MAONI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-CHAMA CHA WANANCHI) KWA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA:

1. DIRA YA TAIFA:

a) Lengo kuu la Taifa letu ni kujenga Tanzania yenye haki sawa kwa wananchi wote na inayoheshimu haki za binadamu kwa vitendo.
b) Amani na utulivu ni msingi muhimu wa maendeleo. Haki sawa kwa wananchi wote ndiyo msingi wa kuendeleza amani na utulivu wa kweli. Kila Mtanzania ana wajibu wa kujenga jamii inayoheshimu haki za kila mwananchi ili kudumisha amani na utulivu.
c) Wananchi wote wawe na fursa ya kujiendeleza kwa juhudi zao wenyewe na kwa mchango wa kila Mtanzania tujenge Taifa linalojitegemea lenye neema kwa wote, uzalendo na mshikamano wa kitaifa linaloweza kuhimili ushindani wa kiuchumi katika ulimwengu wa utandawazi.
d) Kujenga utamaduni wa kuchapa kazi kwa bidii, nidhamu, uadilifu na tija ya hali ya juu na kila Mtanzania awe na ari ya kujifunza na kujiendeleza katika maisha yake yote.
e) Kujenga utamaduni wa kuheshimiana, kuvumiliana na kupendana bila kujali tofauti zetu za ukanda, kabila, rangi, dini na jinsia.
f) Kutumia maliasili na raslimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wote huku tukizingatia ulinzi wa mazingira.

2. MAADILI NA MISINGI MIKUU YA TAIFA:

2.1 MAADILI
CUF inapendekeza katiba iainishe Maadili ya Taifa. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayoongozwa na maadili yafuatayo:-
a) Binadamu wote wanastahili heshima na ulinzi wa utu wao.
b) Haki sawa kwa Watanzania wote. Haki hizo ni za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
c) Ni wajibu wa kila Mtanzania kuchapa kazi kwa bidii na kujiendeleza katika maisha yake yote.
d) Umoja na mshikamano wa Watanzania wote.
e) Ubaguzi wa rangi, dini, kabila, kikanda, jinsia haukubaliki kabisa katika kuendesha shughuli za umma.
f) Maliasili na raslimali za Tanzania zitatumiwa kwa manufaa ya Watanzania wote na kuzingatia ulinzi na uhifadhi wa mazingira.

Kwa kuzingatia maadili ya Taifa viongozi wataheshimu na kufuata maadili yafuatayo:-
a) Kuwa uongozi ni dhamana na utatumiwa kwa ajili ya maslahi ya Taifa na ya wananchi wote kwa ujumla na kamwe hautatumiwa kwa maslahi binafsi, ubaguzi, upendeleo au kwa ajili ya kujilimbikizia mali;
b) Kuwa mali na rasilimali za umma zitatumiwa na kulindwa kwa maslahi ya Taifa na kamwe viongozi wa umma hawatatumia nafasi na mamlaka waliyokabidhiwa kutwaa, kuiba, kufuja au kujibinafsishia mali na rasilimali za umma;
c) Kuwa rushwa, ufisadi na uhujumu wa uchumi wa Taifa ni maangamizi ya Taifa, hivyo viongozi hawatashiriki kwa namna yeyote ile katika vitendo vya rushwa, ufisadi na uhujumu wa uchumi wa Taifa;
d) Kiongozi hatafanya maamuzi katika mambo yenye mgongano kati ya maslahi yake binafsi na maslahi ya umma;
e) Viongozi wa umma hawatafanya biashara, kuajiriwa au kuifanyia kazi taasisi yoyote binafsi kwa ajili ya kujinufaisha binafsi.
2.2 MISINGI
CUF inapendekeza katiba iainishe masuala ya Msingi ya demokrasia, haki na usawa. Taifa litaongozwa na kuishi kulingana na misingi mikuu ifuatayo:-
a) Kwamba chanzo cha mamlaka ya dola ni wananchi kwa hivyo mamlaka za dola zitapata uhalali wake kutokana na ridhaa ya wananchi na serikali zote tatu na mabunge yote matatu yatawajibika kwa wananchi;
b) Kwamba, ufisadi, ujinga, maradhi na umaskini ni maadui wa Taifa kwa hivyo lengo kuu la sera, sheria na serikali zote tatu na juhudi za wananchi wote ni kuwaangamiza maadui hawa;
c) Kwamba wananchi wanayo haki ya kushiriki katika shughuli za mamlaka za dola kwa mujibu wa Katiba.
d) Kwamba haki, usawa na ustawi wa kila mwananchi ndio ngao ya umoja, undugu, mshikamano na amani ya Taifa;
e) Kwamba kuheshimu na kulinda utu na haki zote za binadamu na pia kutii Katiba na sheria ndio msingi mkuu wa utamaduni wa Taifa;
f) Kuhakikisha kuwa hakuna unyonyaji wa mtu na mtu mwingine;
g) Kwamba maliasili, mazingira na utajiri wa Taifa ni rasilimali za Taifa kwa ajili ya wananchi wote wa Tanzania kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo na kamwe hazitafujwa, kupokonywa au kuvunwa kinyume cha maslahi ya Taifa;
h) Kuhakikisha kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa kwa ulinganifu na kwa uadilifu;
i) Kuhakikisha kwamba kila kitendo cha mamlaka ya dola au cha kiongozi yeyote mwenye madaraka kina lengo la kuliletea Taifa manufaa kwa maana ya kuweka maslahi ya Taifa bila ya kujali maslahi binafsi:
j) Kwamba ni wajibu wa dola kumwandaa raia kielimu na kiujuzi ili kumwezesha kila mmoja kumudu kupata na kuendesha shughuli halali na kujipatia riziki yake ama kwa kuajiriwa au kwa kujiajiri;

k) Kwamba haki za binadamu zilizotamkwa na Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu la mwaka 1948 kuhusu haki za Binadamu na zilizotamkwa katika Mkataba wa Haki za Binadamu na za Jamii wa Umoja wa Afrika wa mwaka 1981 pamoja na mikataba au mikataba ya nyongeza iliyoundwa au itakayoundwa na Umoja wa Mataifa au umoja wa Afrika au Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa minajili ya kutunza, kuhifadhi na kutetea haki za binadamu au sehemu ya jamii kama vile wanawake, watoto, wazee na walemavu vitachukuliwa kuwa ni sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali zake.
l) Kila mmoja ana haki ya uhuru wa kutoa na kueleza maoni yake, kujiunga na chama cha siasa au taasisi na vyama vya kijamii ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli za chama au taasisi aliyojiunga kwa hiari yake mwenyewe.
m) Kwamba dola na vyombo vyake vyote vitatoa haki na fursa sawa kwa raia na wananchi wote wa Tanzania bila ya kujali jinsia, rangi, kabila, ukanda, dini, itikadi ya kisiasa wala hali ya mtu;
n) Kwamba aina zote za dhuluma, uonevu, vitisho, ukandamizaji,uhujumu wa uchumi, ufisadi, ubaguzi, upendeleo na rushwa zinakuwa mwiko na kukomeshwa kabisa;
o) Kwamba shughuli zote za uendeshaji wa mamlaka za dola zitafuata misingi ya uwazi, ukweli na uwajibikaji na kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litakagua na kudhibiti utendaji wa vyombo vya dola pamoja na kuridhia mikataba muhimu ya umma. Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na la Zanzibar yatafanya hivyo kwa mamlaka za Tanganyika na Zanzibar kila moja kwa eneo lake na kwa mambo yahusuyo serikali husika na si vinginevyo;
p) Kwamba serikali itazisaidia na kuziimarisha taasisi za kijamii ili ziweze kutoa huduma za kuharakisha shughuli za maendeleo ya wananchi na kukuza utamaduni wa kidemokrasia.

Katika utetekelezaji wa kazi na wajibu wake, mamlaka zote za dola zitakuwa na jukumu na wajibu wa kutii na kuzingatia maadili na misingi yote iliyotamkwa kwenye Sehemu hii ya katiba na misingi hii itakuwa chanzo cha sera na sheria za nchi.

3. HAKI ZA BINADAMU NA WAJIBU MUHIMU:

3.1. HAKI YA USAWA

a) Haki za binadamu ziendane na maadili ya kitanzania. Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa. Sheria zote kandamizi kama zile zinazohusiana na masuala ya ugaidi zipitiwe upya na au zifutwe, kila mtu anastahili heshima na kuthaminiwa utu wake na iwe ni marufuku kumtesa, kumtweza au kumdhalilisha mtu;
b) Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria;
c) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na Mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au inayotumika nchini kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake isipokuwa kama imefanyika hivyo ili kurekebisha athari mbaya ya ubaguzi wa jinsia au kundi lolote la watu;
d) Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya mamlaka ya nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria;
e) Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au na mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya Mamlaka ya Nchi;

3.2. HAKI YA ELIMU NA AFYA:

a) Kila mtu ana haki ya kuelimishwa. Elimu ya msingi itolewe bure na iwe ya lazima kwa kila mtoto. Elimu ya ufundi stadi iwe wazi kwa wote. Na elimu ya juu iwe wazi kwa wote kwa kutegemea sifa ya mtu. Serikali iwalipie watu wote wenye vipaji vya kuendelea na elimu ya juu bila ubaguzi wowote.
b) Elimu ya uraia itolewe katika ngazi zote za elimu kwa madhumuni ya kuendeleza maadili ya Taifa, kukuza mshikamano na umoja wa kitaifa na uelewa wa haki za binadamu na kuendeleza kuelewana, kuvumiliana na urafiki kati ya Watanzania wa kabila, rangi na dini mbalilmbali.
c) Kila Mtanzania ana haki ya kupata huduma za msingi za afya, kupata hali bora ya maisha yeye mwenyewe pamoja na familia yake na kupata chakula, mavazi, nyumba, matibabu na hifadhi za lazima kwa maisha yake. Pia ana haki ya kutunzwa wakati akiwa hana ajira kwa sababu ambazo haziko chini ya uwezo wake, wakati wa ugonjwa, wa kutojiweza, ujane, uzee au anapokosa riziki yake kwa kutoweza kujisaidia. Mafao yote haya yalingane na uwezo wa uchumi wa Taifa.

3.3. HAKI YA KUWA NA FAMILIA:

a) Kila mtu anayo haki ya kuwa na familia, kuoa na kuolewa kwa hiari bila kuwekewa pingamizi kutokana na rangi, kabila, dini, jinsia, itikadi au hali yake ya maisha;
b) Ndoa itafungwa kati ya mume na mke kwa hiari na familia itakuwa kitengo muhimu katika mfumo wa jamii kitakacholindwa na kustawishwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi;
c) Wanandoa watakuwa sawa na kufaidi haki sawa kwa mujibu wa katiba.
d) Watoto ni hazina na rasilimali kuu ya Taifa hivyo Mamlaka za dola na za kijamii zitahakikisha kuwa kila mtoto anapata ulinzi, hifadhi, lishe, tiba, malezi ya kimaadili na elimu bora.

3.4. HAKI YA KUMILIKI MALI
a) Kila mtu anayo haki ya kumiliki mali binafsi kwa njia halali ama peke yake au kwa ushirikiano na mtu yeyote mwingine;
b) Ni marufuku mtu yeyote ambaye anamiliki mali binafsi kwa halali kunyang’anywa au kutaifishiwa mali yake isipokuwa pale tu ambapo amelipwa fidia stahili na inayomridhisha, na kwamba sababu ya kumyang’anya au kutaifisha mali husika ni kwa maslahi ya juu ya umma na kwa mujibu wa sheria ;
c) Ikiwa mali inayotaifishwa ni makazi basi mamlaka ya dola itahakikisha kuwa aliyetaifishiwa makazi yake anapewa ardhi mbadala na muda wa kutosha kujenga makazi mbadala;
3.5. HAKI YA KUMILIKI ARDHI;

a) Ardhi ni mali ya Watanzania wote katika ujumla wao kama Taifa.
b) Raia wa Tanzania peke yao ndiyo watakuwa na haki za kumilikishwa ardhi.
c) Kila Mtanzania atakuwa na haki ya kumilikishwa ardhi anayoitumia peke yake kwa shughuli za uchumi na kijamii.
d) Kutakuwa na ardhi itakayosimamiwa na mamlaka za vijiji, halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji. Ardhi iliyobaki itamilikiwa na Serikali Kuu.
e) Ardhi ya Umma itakuwa chini ya udhamini wa Rais kwa niaba ya Raia wote kwa mujibu wa sheria.
f) Katiba itamke kuwepo kwa Tume ya Ardhi itakayosimamia ardhi ya umma, kutoa ushauri pamoja na kushughulikia masuala yote ya utoaji ardhi kwa wananchi na kuweka kumbukumbu ya masuala yote ya ardhi.

3.6. HAKI YA KUCHAGUA NA KUCHAGULIWA KUWA KIONGOZI:

a) Kila mwananchi aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki ya kupiga au kupigiwa kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania na wananchi kwa ngazi za vitongoji, vijiji, mitaa, kata na majimbo. Umri wa chini wa kugombea nafasi ya Urais uwe miaka 30
b) Bunge litunge sheria na kuweka masharti yanayolinda na kuwezesha utekelezaji wa haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi.
c) Pawepo haki kwa mwananchi mwenye sifa za kuchaguliwa kuwa kiongozi kugombea binafsi bila kushurutishwa kujiunga na chama chochote cha siasa.
d) Usifanyike uchaguzi wowote ule pasina kuhakikisha utaratibu wa uhakiki wa watu wote wenye sifa za kupiga kura kikatiba wameingizwa katika orodha halali ya wapiga kura katika Daftari la kudumu la wapiga kura.

3.7. HAKI YA KUKUSANYIKA NA KUANDAMANA:
Raia wanayo haki ya kukusanyika, kuandamana kwa amani na kufanya mikutano bila kizuizi na utakuwa wajibu wa Mamlaka ya dola kuhakikisha kuwa raia wanapokusanyika, kuandamana kwa amani au kufanya mkutano hawabugudhiwi na kunyanyaswa na vyombo vya usalama au mamlaka yoyote wa serikali.

3.8. UHURU WA KUJIAMULIA MAMBO:
a) Raia wa Tanzania kwa pamoja wanayo haki ya kujiamulia mambo yao wenyewe na kukubaliana katika mambo yanayohusu uhuru wa nchi, siasa na jinsi ya kujiletea maendeleo ya uchumi na utamaduni;
b) Raia wa Tanzania kwa pamoja wanayo haki ya kumiliki na kuvuna na pia wanao wajibu wa kuhifadhi rasilimali asili na utajiri wa nchi yao na ni marufuku kwa mtu yeyote au mamlaka ya dola au binafsi kuweka saini mkataba wowote unatwaa au kudhoofisha haki hii au kuruhusu umiliki na uvunaji wa rasilimali asili na utajiri wa nchi kuwa mikononi mwa watu wasio raia au mashirika ya nje pasipo na ubia wa raia wa Tanzania;
c) Watanzania wanayo haki ya kulinda na kuendeleza utamaduni wao pamoja na mifumo ya maisha, uchumi na mila bora zinazoendana na utamaduni wao;

d) Ni wajibu wa kila mwananchi kuachana na mila potofu ambazo zikiendelezwa zinawakandamiza wanawake, watoto, mtu yeyote au sehemu ya jamii kiafya , kimwili na kisaikolojia.
3.9. UHURU WA KUTOA MAWAZO, HABARI, TAARIFA NA MAONI;
a) Kila raia anayo haki ya kutoa mawazo, habari, taarifa na maoni bila kuingiliwa na mamlaka yoyote ile na sheria zote zinazokandamiza uhuru wa kutoa mawazo, taarifa, habari na maoni hazitakuwa na nafasi.
b) Vyombo vya habari vyote vinawajibika kwa jamii na taifa kwa ujumla kwa hivyo vinapaswa kurusha habari na taarifa ambazo jamii yetu inazihitaji ili kupata mustakabali mwema.
c) Vyombo vya habari vya serikali ni mali ya umma na vitawajibika kurusha taarifa na habari zake bila kuegemea upande wowote na kutoa fursa sawa kwa watumiaji wote.
d) Nyakati za matukio makubwa ya kitaifa kama vile chaguzi mbalimbali, kumbukumbu za kitaifa na matukio makubwa ya huzuni na furaha na masuala yote yenye maslahi kwa taifa yatapewa kipaumbele na vyombo vya habari vya serikali bila kujali yanatoka serikalini, taasisi za kijamii, vyama vya siasa n.k. matukio haya yataoneshwa kwa usawa bila kubagua.
3.10. HAKI YA KUPATA DHAMANA
a) Kila raia ana haki ya kupewa dhamana pale ambapo atakuwa anashikiliwa na vyombo vya dola na ni marufuku raia kushikiliwa bila sababu za msingi.
b) Haki ya dhamana inaweza kuondolewa pale tu ambapo raia anashikiliwa na vyombo vya dola kwa makosa ya uhaini, mauaji ya kukusudia na unyang’anyi wa kutumia silaha.

4. VYAMA VYA SIASA:

a) Vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu viwe na uwezo wa kikatiba wa kuungana kwa ajili ya kuunda chama kimoja kushiriki katika uchaguzi siku ishirini na moja (21) kabla ya tarehe iliyotangazwa na Tume ya uchaguzi kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni na vyama vilivyoungana visipoteze uasili na usajili wao wa kudumu.
b) Mtu yeyote asilazimishwe kujiunga na chama cha siasa au chama chochote cha siasa kukataliwa kusajiliwa kwa sababu tu ya itikadi au falsafa yake isipokuwa kama falsafa yake inapinga waziwazi maadili ya Taifa na misingi muhimu ya haki za binadamu;
c) Utaratibu wa vyama vya siasa kuweka wagombea katika uchaguzi wa viongozi wa ngazi zote za vyombo vya uwakilishi vya dola hautamlazimisha raia kuwa mwanachama wa chama cha siasa ili kupata sifa ya kuteuliwa kuwa mgombea.
d) Bunge litunge sheria na kuweka mipaka ya matumizi ya haki kwa baadhi ya watendaji wakuu wa vyombo vya dola ili kulinda uhuru, ubora wa utendaji wa wakuu hao na imani ya umma kwa ujumla kwa vyombo wanavyoviongoza.

5. TUME YA UCHAGUZI;

a) Kuwepo na Tume huru za Uchaguzi ambayo ni asasi huru ambayo haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali au kutoka chama chochote cha siasa, katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria. Tume itakuwa na wajumbe wafuatao watakaoteuliwa na Rais, kutokana na majina yatakayopendezwa kwake na sekta za jamii husika na hivyo pawepo na wajumbe wa tume wakiwemo;
i. Mjumbe mmoja kutoka kila chama cha Siasa chenye wabunge wa kuchaguliwa.
ii. Mjumbe mmoja anayewakilisha mashirika na taasisi zisizo za kiserikali zinazoshughulikia uongozi wa jamii;
iii. Mjumbe mmoja anayewakilisha taasisi za kidini za kiislamu.
iv. Mjumbe mmoja anayewakilisha taasisi za kidini za kikristo.
v. Mjumbe mmoja anayewakilisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa.
vi. Mjumbe mmoja anayewakilisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
vii. Mjumbe mmoja anayewakilisha walemavu.
viii. Mjumbe mmoja anayewakilisha wanawake.
ix. Mjumbe mmoja anayewakilisha vijana.
x. Mjumbe mmoja anayewakilisha wazee.
b) Tume ya Uchaguzi itachagua mwenyekiti na makamu mwenyekiti wake yenyewe na wajumbe wake watakula kiapo cha uaminifu mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufani kabla ya kuanza utekelezaji wa majukumu yake;
c) Wajumbe wote wa Tume, Mwenyekiti, Makamu na Makamishna wasiwe na wadhifa mwingine wowote kwenye vyombo vya umma.
d) Tume ya Uchaguzi itaajiri sekretarieti na watendaji wake na kuendesha shughuli za uchaguzi kwa uhuru bila vitisho wala ushawishi wa mtu, taasisi au mamlaka yoyote kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge;
e) Fedha za matumizi ya Tume ya Uchaguzi zitengwe moja kwa moja na Bunge kutoka kwenye Mfuko wa Hazina wa Taifa (Consolidated Fund)

f) Tume itakuwa na watendaji wake wenyewe mpaka katika kila halmashauri.
g) Majina yatakayopendekezwa kwa Rais yatatokana na watu ambao siyo viongozi wa chama chochote cha siasa, na uteuzi utakaofanywa na Rais sharti uthibitishwe na Bunge.
h) Wajumbe wa Tume Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwa kufuata kanuni kwamba endapo Mwenyekiti ni mtu anayetoka sehemu moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wake atakuwa ni mtu anayetoka sehemu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uchaguzi huo uwe umefanyika katika mkutano wa kwanza wa Tume ya Uchaguzi.
i) Tume ya Uchaguzi ya Taifa itasimamia chaguzi zote toka ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa, madiwani, wabunge na Rais.
j) Bunge litunge sheria ya Uchaguzi na kuweka masharti kuhusu mambo yafuatayo;
• Utaratibu endelevu na wa kudumu wa uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa wanachi unaofanywa nchini Tanzania;
• Utaratibu wa kudumu wa kutunza na kuhakiki wapiga kura waliomo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura;
• Utaratibu wa kumwezesha mpiga kura aliyejiandikisha sehemu moja kupiga kura sehemu nyingine au kuhamisha usajili wake wa kupiga kura;
• Kutaja wajibu na shughuli za tume za Uchaguzi na utaratibu wa kila uchaguzi ambao utaendeshwa na Tume hizo;
k) Uchaguzi unaofanywa na wananchi nchini Tanzania utafanyika katika vipindi vya mara kwa mara vilivyowekwa na sheria ya uchaguzi na katiba.
l) Uchaguzi utakaofanyika ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania utahusisha;
• Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
• Rais wa Tanganyika na Zanzibar,
• Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
• Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na la Zanzibar
• Madiwani na wenyeviti wa Serikali za Mitaa za Tanganyika na Zanzibar
m) Mambo mengine ya kuzingatia;
• Uchaguzi wa madiwani ujumuishwe katika serikali za mitaa.
• Rais ashitakiwe akiwa madarakani au akiwa nje ya madaraka.
• Matokeo ya uchaguzi yanaweza kuhojiwa mahakamani.
• Mtanzania yeyote anaweza kuchaguliwa kuwa Rais kwa vipindi visivyozidi viwili.

6. MFUMO WA UCHAGUZI:

a) Katiba mpya itamke kuwepo kwa mfumo wa uwiano wa kura kwa uchaguzi wa wabunge, madiwani na wajumbe wa serikali za vijiji na mitaa. Ikiwa kiti cha Mbunge yeyote aliyechaguliwa kuwakilisha jimbo la uchaguzi kitakuwa wazi kwa sababu nyingine yoyote isiyohusika na kuvunjwa kwa Bunge basi orodha ya chama alichokuwa mbunge aliyepoteza nafasi yake itatumiwa kujaza nafasi hiyo kwa kuzingatia jinsia ya mbunge aliyetoka. Ikiwa mbunge aliyetoka ni mwanamke litachukuliwa jina la mwanamke anayefuatia katika orodha na kadhalika kwa mwanaume. Ikiwa Mbunge aliyetoka alikuwa mgombea binafsi basi orodha ya chama kilichopata kura nyingi na kuwa cha pili katika eneo hilo itatumiwa kuteua mbunge. Ikiwa mgombea binafsi mwingine ndiye aliyekuwa wa pili basi yeye ndiye atakayeteuliwa kuwa mbunge.
b) Kila Chama kitaandaa orodha ya wagombea nafasi ya ubunge. Orodha hii itabadilishana majina kijinsia. La kwanza likiwa la mwanamke la pili litakuwa la mwanaume. Bunge litatunga sheria kugawa maeneo ya uchaguzi na vigezo vya kutumia kuamua idadi ya viti vya bunge katika kila eneo. Vyama vya siasa vitaandaa orodha ya wagombea wa ubunge katika kila eneo kufuata utaratibu wa kubadilishana majina kijinsia.
c) Mgombea uchaguzi katika kila eneo la uchaguzi atatakiwa atimize masharti yafuatayo:-
i. Awe amependekezwa na chama cha siasa kilichosajiliwa,
ii. Awe amepata uteuzi wa Tume ya Uchaguzi kwa kuwa na sifa ya kuwa mgombea
iii. Kama ni mgombea binafsi awe ametimiza masharti ya ugombea binafsi yaliyowekwa na Katiba na sheria ya uchaguzi;
d) Hapatakuwa na haja ya viti maalum vya wanawake kwani orodha za vyama zitakuwa na asilimia 50 wanawake na asilimia 50 wanaume. Chama kikipata wabunge 10, watano watakuwa wanawake.
e) Rais atatangazwa kushinda uchaguzi ikiwa atapata asilimia 50 + 1au zaidi ya kura zote. Ikiwa hakuna mgombea aliyepata asilimia 50+1 ya kura zote uchaguzi wa Rais utarudiwa na wagombea wawili walioongoza kwa kura watateuliwa kuwa wagombea katika uchaguzi wa marudio wa Rais.

7. MUUNDO WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA:
CUF inapendekeza uwepo wa muundo wa serikali Tatu. Serikali ya Jamhuri ya watu wa Tanganyika, serikali ya Jamhuri ya watu wa Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. CUF inapendekeza kuwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano pamoja na masuala mengine, katiba itayokuwa na mambo muhimu yafuatayo;
a) Itamke kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni MUUNGANO wa nchi mbili (2) zilizokuwa huru na kila nchi kuwa na mipaka yake.
b) Nchi hizo mbili zimeungana kwa mkataba wa Muungano (Articles of Union) wa 1964 ambao ndiyo sheria mama. Katika uandikaji wa katiba mpya Mkataba huu upitiwe upya kufikia muafaka wa mambo ya Muungano.
c) Katika Muungano huo mambo muhimu yaelezwe kama vile kutokuvunja Muungano, kwamba kila nchi ina haki sawa kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano na kwamba nchi hizo mbili kila moja itakuwa na Katiba yake ambayo itaelezea utaratibu wake wa kuendesha nchi yake kwa maslahi ya watu wake.
d) Katiba ya Jamhuri ya Muungano ielezee vipi Serikali ya Jamhuri ya Muungano itapatikana (Serikali Kuu, Bunge na Mahakama) na kuonesha dhahiri kuwa serikali ya Muungano itakuwa na uwakilishi sawa wa pande mbili za Muungano ili kuondoa manung’uniko ya upande wowote.
e) Mahakama ya Muungano itakuwa ni Mahakama ya Rufaa kama vile ilivyokuwa mahakama ya rufaa ya Afrika Mashariki hapo zamani. Kesi kuhusu uchaguzi wa Rais zitasikilizwa na Mahakama hii.
f) Katiba ya Jamhuri ya Muungano ielezee kuwepo kwa haki za binadamu na namna zitakavyolindwa na kama haki hizo zikivunjwa mtu anaweza kwenda Mahakamani kutafuta haki yake.
g) Katiba za nchi mbili hizi kila moja itaelezea utaratibu wa nchi husika kwa kadri ambavyo wananchi wa nchi husika wanataka kuendesha serikali zao. Ni vizuri baada ya kupitia Mkataba wa Muungano (Articles of Union) na kukubaliana upya mambo ya Muungano, Wananchi wa Tanzania Bara (Tanganyika) wangeandika katiba yao kuhusu mambo yasiyo ya Muungano na Wananchi wa Zanzibar wangepitia Katiba yao kuona kama inakidhi mahitaji ukizingatia makubaliano mapya ya mambo ya Muungano. Baada ya kuwa na Katiba hizo mbili, ndipo Katiba ya Jamhuri ya Muungano ingeandikwa kuzingatia mambo ya Muungano yaliyokubaliwa na pande mbili. Kwa mchakato wa sasa Zanzibar tayari ina katiba na kwa hiyo Tanganyika itabidi kuwa na “Interim constitution” itayoelezwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili Tanganyika iweze kuandaa katiba yake au kubadili iliyokuwa ya Tanzania na kuifanya kuwa ya Tanganyika kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Tanganyika au kwa kadri ambavyo wananchi watapenda iwe.
h) Kwa mambo ya Muungano Katiba ya Jamhuri itatamka wazi kuwa vyombo vya Muungano vitagawiwa kwa utaratibu utaokubalika ili kuonesha uwakilishi wa nchi zote mbili (Zanzibar na Tanganyika). Utaratibu huo uwekwe vizuri ili usivunjwe, na uwe ndani ya Katiba Mpya.

i) Nchi mbili hizi pale zinapozungumzia jambo la Muungano au si la Muungano lakini Serikali ya Jamhuri inahusika, basi uwakilishi ya nchi zote mbili katika suala hilo lazima upatikane.
j) Mhimili wenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma utakuwa ni Bunge la Muungano, Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar;
k) Katika kutekeleza majukumu ya serikali ya Muungano vyombo vya dola vya Muungano vitakuwa na kipaumbele cha kwanza kuliko vyombo vya dola vinavyotekeleza mamlaka ya Tanganyika na Zanzibar; ilimradi kwamba majukumu yaliyokabidhiwa kwa Tanganyika na Zanzibar hayatakabidhiwa na kutekelezwa na vyombo vya dola vya serikali ya Muungano. Majukumu yaliyokabidhiwa kwa serikali ya Muungano yanaweza kukabidhiwa kwa vyombo vya dola vyenye mamlaka vya Tanganyika na vya Zanzibar ili yatekelezwe na vyombo hivyo kwa niaba ya Serikali ya Muungano.
8. MAMBO YA MUUNGANO
Makubaliano/Mkataba wa Muungano(Articles of union) kwa pande zote mbili yapitiwe upya na masuala ya Muungano yanaweza kuwa ni pamoja na:
a) Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
b) Ulinzi na Usalama;
c) Polisi
d) Uraia.
e) Uhamiaji.
f) Utumishi katika Serikali ya Muungano.
g) Mamlaka ya juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari.
h) Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti) mabenki (pamoja na mabenki ya kuweka akiba) na shughuli zote za kibenki, fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha na mikopo ya nje.
i) Haki za Binadamu.

9. MUUNDO WA SERIKALI NA BARAZA LA MAWAZIRI

9.1. RAIS NA MADARAKA YAKE

a) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na Rais mtendaji ambaye atachaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais na Makamu wa Rais watagombea kwa pamoja. Ikiwa Rais anatoka upande mmoja wa Muungano Makamu wa Rais atoke upande wa pili wa muungano.
b) Rais atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

9.2. MUUNDO WA BARAZA LA MAWAZIRI NA MADARAKA YAKE:

a) Mawaziri hawatakuwa wabunge. Watateuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge.
b) Kutakuwepo na wizara zisizozidi 15, na ikitokea Rais anataka kuongeza wizara nyingine sharti apate ushauri na ithibati ya Bunge. Suala la idadi ya baraza la mawaziri lisiwe utashi wa Rais anayechaguliwa kushika nafasi hiyo pekee.
c) Wizara za Jamhuri ya Muungano ni pamoja na
i) Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
ii) Wizara ya Mambo ya Nje
iii) Wizara ya Mambo ya Ndani
iv) Wizara ya Fedha na Uchumi
v) Wizara ya Sheria na Katiba
vi) Wizara ya Utumishi wa Serikali ya Muungano

d) Wizara za Serikali za Tanganyika ni pamoja na
i) Wizara ya Fedha na Ucumi
ii) Wizara ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Misitu
iii) Wizara ya Biashara na Viwanda
iv) Wizara ya Nishati na Madini
v) Wizara ya Elimu, Michezo na Utamaduni
vi) Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
vii) Wizara ya Afya na huduma za jamii
viii) Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji
ix) Wizara ya Ajira na Hifadhi ya Jamii
x) Wizara ya Maji na Mazingira
xi) Wizara ya Miundombinu, Usafiri na Mawasiliano
xii) Wizara ya Habari na Utalii
xiii) Wizara ya Utumishi wa Serikali ya Tanganyika

(e) Waziri Mkuu haitakuwa nafasi ya kikatiba.

10. BUNGE NA MAMLAKA YAKE:

a) Bunge liwe mhimili huru wa dola na Rais asiwe sehemu ya Bunge
b) Bunge liwe chombo kikuu cha kutunga sheria. Serikali itapendekeza sheria mpya lakini lazima zijadiliwe na kupitishwa na Bunge.
c) Kabla ya sheria kuanza kutumika itabidi ikubaliwe na Rais kwa kuweka sahihi yake. Ikiwa Rais ataikataa sheria iliyopitishwa na Bunge, sheria hiyo haitahitaji idhini ikiwa baada ya kurudishwa Bungeni itaungwa mkono na theluthi 2 ya Wabunge wote.
d) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba mamlaka ya Bunge kujadili, kubadili au kupitisha mapendekezo ya bajeti ya serikali. Bunge lisimamie na kudhibiti mapato na matumizi ya serikali na litafanya hivyo kwa kujadili, kupitisha au kukataa mswada wowote au sehemu ya mswada unaohusu mambo yafuatayo:-
i. Kutoza kodi au kubadilisha kodi;
ii. Kuagiza kwamba malipo au matumizi ya fedha yafanywe kutokana na mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au kubadilisha kiwango hicho;
iii. Kufuta au kusamehe deni lolote linalotakiwa lilipwe kwa Serikali ya Muungano.
e) Pamoja na kazi zake nyingine zitakazotajwa katika katiba, Bunge litakuwa pia na wajibu wa kuidhinisha uteuzi utakaofanywa na Rais kwa vyeo vifuatavyo:-
i. Waziri au Naibu Waziri;
ii. Balozi;
iii. Gavana wa Benki Kuu;
iv. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
v. Mwanasheria Mkuu;
vi. Mkurugenzi wa Mashtaka;
vii. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
viii. Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Maadili
ix. Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ardhi
x. Makamishina wa Mamlaka zilizoundwa kwa mujibu wa sheria
xi. Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama
10.1. SPIKA NA NAIBU WA SPIKA

a) Pawepo na Spika wa Bunge ambaye atachaguliwa na Wabunge kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuwa wabunge ambaye atakuwa ndiye kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine vyote nje ya Bunge;
b) Waziri, Naibu Waziri, Mbunge au mtu mwenye madaraka ya aina nyingine yoyote itakayotajwa na Sheria itakayotugwa na Bunge hataweza kuchaguliwa kuwa Spika. Spika hatakuwa Mbunge.

11. MAMLAKA YA MAHAKAMA;

11.1. MASHAURI YA KATIBA (MAHAKAMA YA KATIBA);

a) Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na mamlaka ya mwanzo na ya asili kusikiliza mashauri yanayotokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
b) Endapo shauri la kikatiba litafunguliwa Mahakama Kuu ya Muungano kwa mujibu wa ibara hii, mahakama hiyo itaitwa “Mahakama Maalumu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” na itakuwa na mamlaka ya kulisikiliza na kutoa uamuzi wa usuluhishi au hukumu yenye nguvu ya kisheria juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba au sheria za nchi;
c) Pande zenye haki ya kufungua shauri la kikatiba mbele ya Mahakama Maalumu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni:-
i. Serikali ya Muungano;
ii. Serikali ya Tanganyika;
iii. Serikali ya Zanzibar;
iv. Raia wa Tanzania ikiwa ni pamoja ya taasisi zenye uhai wa kisheria ambazo pia zimesajiliwa na Watanzania na si raia wa kigeni.
11.2. MAMLAKA YA RUFAA
Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na mamlaka ya kusikiliza rufaa kutoka kwenye Mahakama Kuu ya Tanganyika na ya Zanzibar kuhusiana na mambo yote ya Muungano isipokuwa yale ambayo ina mamlaka ya asili na ya pekee ya kusikiliza mashauri yake kwa mara ya kwanza. Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kuweka masharti kuhusu utaratibu wa kupeleka shauri mbele ya Mahakama Kuu ya Muungano na uendeshaji wa shauri au kesi ya jinai pamoja na utaratibu wa rufaa kwenda Makama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilimradi kwamba sheria yoyote haitatungwa inayoweka vipengele vya kiufundi vinavyodhoofisha au kutwaa haki ya mlalamikaji au mtuhumiwa mbele ya sheria.
11.3. MAHAKAMA YA RUFANI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

a) Kutakuwa na Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayojulikana kwa kifupi kama “Mahakama ya Rufani”, ambayo mamlaka yake yatakuwa kama yatakavyoelezwa na katiba zote Tatu.
b) Mahakama ya Rufani itakuwa na mamlaka ya kusikiliza rufani yoyote kutoka Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama Maalumu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama kuu ya Tanganyika na Mahakama Kuu ya Zanzibar; Kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano itasikilizwa moja kwa moja na Mahakama ya Rufani.

11.4. TUME YA KUAJIRI YA MAHAKAMA YA MUUNGANO;
Kutakuwa na Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Muungano ambayo itakuwa na mamlaka ya kuajiri watumishi wote wa mahakama za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia mamlaka ya kupendekeza majina ya watu wanaostahili kuteuliwa kushika nafasi ya jaji wa Mahakama Kuu ya Muungano na Mahakama ya Rufani ya Muungano.

12. VYOMBO VYA DOLA VYA TANGANYIKA NA ZANZIBAR; (SERIKALI YA TANGANYIKA NA YA ZANZIBAR)

a) Kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika na ya Zanzibar ambazo zitakuwa na mamlaka mamlaka kamili katika Tanganyika na Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano.

b) Marais wa Tanganyika na Zanzibar watachaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanganyika na Katiba ya Zanzibar; Mfumo wa uchaguzi wa katiba zote tatu ufanane. Pawepo na Rais Mtendaji Tanganyika na Zanzibar
c) Serikali za Mitaa na Halmashauri zake zitaundwa katika kila wilaya kwa mujibu wa Katiba ya Tanganyika na Katiba ya Zanzibar; Kwa upande wa Tanganyika wilaya ziundwe upya kwa kuzingatia idadi ya watu, ukubwa wa eneo na mapato yanayoweza kukusanywa kuendesha halmashauri.
d) Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na la Zanzibar laweza kutunga sheria kuweka taratibu za uendeshaji wa Serikali za Mitaa na Halmashauri zake, isipokuwa masuala yanayohusiana na Muungano yatafanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

13. MABARAZA YA WAWAKILISHI
a) Kuwepo kwa mabaraza mawili ya wawakilishi, moja la Tanganyika na jingine la Zanzibar ambayo yatakuwa na mamlaka ya kutunga sheria kuhusu mambo yasiyo ya Muungano, kujadili, kusimamia na kudhibiti shughuli za Serikali za Tanganyika na Zanzibar;
b) Mabaraza ya wawakilishi yawe na wajumbe wanaolingana na idadi ya majimbo ya uchaguzi yatakayotangazwa na Tume za Uchaguzi za Tanganyika na Zanzibar;
c) Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watachaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanganyika na Katiba ya Zanzibar ambazo zitafuata mfumo wa uwiano wa kura kama ilivyoelezwa kwa uchaguzi wa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano.
15. MADARAKA YA UMMA NA SERIKALI ZA MITAA
a) Katiba ya Tanganyika na Zanzibar itamke uwepo wa Serikali za Mitaa. Katiba ieleze serikali za mitaa ni serikali zenye mamlaka kamili kwenye mambo yanayosimamiwa na serikali za mitaa na hazitaingiliwa katika maamuzi yake na serikali kuu. (TUNAPINGA KUWEPO KWA SERIKALI ZA MAJIMBO AU KANDA)
b) Serikali za mitaa zitakuwa na vyanzo vya mapato vya kuaminika na endelevu. Kwa upande wa Tanganyika alau asilimia 30 ya mapato ya serikali kuu yatapelekwa katika halmashauri kwa kuzingatia uwiano wa maendeleo.
c) Katiba ieleze kwamba serikali za mitaa zitawajibika kwanza kwa wananchi wa eneo lao. Halmashauri za serikali za mitaa zitakuwa na haki ya kuteua watendaji wa halmashauri zao na siyo kuteuliwa watendaji na serikali kuu.
d) Kuwepo kwa vyombo vya serikali za mitaa katika kila wilaya na miji na katika Jamhuri ya Muungano, ambavyo vitakuwa vya aina na majina yatakavyowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na la Zanzibar;
e) Baraza la Wawakilishi, litatunga sheria itakayofafanua utaratibu wa kuanzisha vyombo vya serikali za mitaa, miundo na wajumbe wake, njia za mapato na utaratibu wa utekelezaji wa shughuli za vyombo hivyo;
f) Madhumuni ya kuwapo serikali za mitaa ni madaraka kuwa mikononi mwa wananchi kwa hiyo vyombo vya serikali za mitaa vitaundwa na wananchi na vitakuwa na haki na mamlaka ya kupanga mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa jumla;
g) Shughuli na taratibu zote za uchaguzi wa serikali za mitaa zitafanywa na tume ya uchaguzi ya serikali ya Tanganyika na tume ya uchaguzi ya serikali ya Zanzibar;
h) Kila chombo cha serikali za mitaa, kwa kuzingatia masharti ya sheria iliyokianzisha, pamoja na masuala mengine kitahusika na shughuli zifuatazo:-
• Kutekeleza kazi za serikali za Mitaa katika eneo lake.
• Kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi.
• Kuimarisha demokrasia katika eneo lake na kuitumia demokrasia kuharakisha maendeleo ya wananchi.

16. USIMAMIZI WA MALIASILI NA RASILIMALI ZA TAIFA:

a) Katiba itamke kuwa maliasili ya madini na raslimali zote nchini ni mali ya umma na zitumike kwa manufaa ya Watanzania wote.
b) Bunge litapitia mikataba yote ya madini iandikwe upya ili kuhakikisha Taifa linanufaika na raslimali za nchi.
c) Kwa kuzingatia ukubwa wa mapato ya serikali kutoka sekta ya madini na hasa gesi, mafuta ya petroli, urani, dhahabu na mengineyo, Bunge litatunga sheria ya kugawa moja kwa moja kwa wananchi sehemu ya mapato hayo. Madhumuni ya utaratibu huu ni kupambana na umaskini na kushinikiza kuwepo kwa utawala bora katika sekta ya madini. Utafiti unaonyesha mgawo wa fedha taslimu kwa watu maskini hasa wanawake unaboresha elimu, lishe na afya za watoto wa familia maskini. Vile vile mgawo wa fedha unasaidia kuendeleza ujasiriamali wa wananchi wenye biashara ndogo ndogo. Kutumia utaratibu wa malipo ya elektoniki kupitia simu za mkononi au kadi za elektoniki kutasidia kusambaza huduma za kibenki kwa watu maskini. Kugawa mapato kwa wananchi kutahakikisha ushiriki wa karibu wa wananchi katika usimamizi na utawala wa maliasili.
d) Utafutaji, uvunaji na matumizi ya maliasili utafanywa kwa uangalifu na utalinda mazingira.
17. TUME YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
a) Maadili ya Taifa yatamkwe katika Katiba.
b) Kuwepo kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo itakuwa na mamlaka ya kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya katiba hii na sheria ya maadili ya Viongozi wa umma yanazingatiwa ipasavyo;
c) Maana ya kiongozi wa umma na masharti ya maadili ya viongozi wa umma itabidi vifasiriwe kwa mujibu wa masharti ya Katiba kuhusu Maadili ya Taifa, masharti ya Katiba kuhusu sifa za viongozi wa umma na masharti ya sheria ya maadili ya Viongozi wa Umma au masharti ya sheria nyingine yoyote itakayotungwa na Bunge;
d) Tume ya Maadili itakuwa na Kamishna wa Maadili na wafanyakazi wengine ambao idadi yao itatajwa na Sheria itakayotungwa na Bunge.
e) Bunge litatunga Sheria kufafanua na kuainisha misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma itakavyozingatiwa na watu wote wanaoshika nafasi za madaraka zitazotajwa na Bunge.
f) Misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaweza kuwa :-
i. Itafafanua nafasi za madaraka ambazo watu wenye kushika nafasi hizo watahusika nayo;
ii. Itawataka watu wanaoshika nafasi fulani za madaraka kutoa mara kwa mara maelezo rasmi kuhusu mapato, rasilimali na madeni yao;
iii. Itaelekeza taratibu, madaraka na desturi zitakazofuatwa ili kuhakikisha utekelezaji wa maadili;
iv. Itapiga marufuku rushwa, ufisadi na uhujumu wa uchumi wa Taifa katika shughuli za umma,
v. Itapiga marufuku mienendo na tabia inayopelekea kiongozi kuonekana hana uaminifu, anapendelea au inahatarisha maslahi ya ustawi wa jamii;

vi. Itafafanua adhabu zinazoweza kutolewa kwa kuvunja misingi ya Maadili.
vii. Itaweka masharti mengine yoyote yanayofaa au ambayo ni muhimu kwa madhumuni ya kukuza na kudumisha uaminifu, uwazi, kutopendelea na uadilifu katika shughuli za umma na kwa ajili ya kulinda fedha na mali nyinginezo za umma.

g) Bunge laweza kutunga sheria itakayoweka masharti ya mtu kufukuzwa au kuondolewa kazini kutokana na kuvunja maadili ya viongozi, bila ya kujali kama kazi hiyo ni ya kuchaguliwa au kuteuliwa.
17. TUME YA KUPAMBANA NA KUZUIA RUSHWA
a) Katiba ieleze kuwepo kwa Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa na kueleza kazi zake
b) Tume hii iwe na uhuru wa kupeleka kesi mahakamani bila idhini ya DPP
18. MDHIBITI NA MKAGUZI WA HESABU ZA SERIKALI
a) Katiba ieleze kuwepo kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na kazi zake.
b) Ofisi ya Mdhibiti iwe huru katika kufanya kazi zake.
c) Bunge litatunga sheria kuibana serikali kutekeleza mapendekezo ya Mdhibiti.

19. TUME YA TAIFA YA ARDHI
a) Katiba itamke kuwepo kwa Tume ya Taifa ya Ardhi itakayokuwa na mamlaka ya usimamizi wa ardhi ya umma kwa mujibu wa sheria itakayotungwa na Bunge.
b) Tume ya Ardhi itasimamia shughuli zote za umilikaji na ukodishaji wa ardhi kwa mujibu wa sheria
c) Tume itaweka kumbukumbu zote za ardhi ikiwa ni pamoja na hifadhi za taifa, ardhi ya vijiji, halmashauri, miji, manispaa, majiji na ardhi ya serikali kuu, umilikaji na ukodishaji wa ardhi.

20. ULINZI WA TAIFA NA VYOMBO VYA DOLA
20.1. ULINZI WA TAIFA
a) Ulinzi wa Taifa ni wajibu wa kila mwananchi na utapewa kipaumbele katika sera, sheria na shughuli za Mamlaka ya dola;
b) Mtu yeyote isipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatakuwa na haki ya kuweka saini kwenye mkataba wa kusalimu amri au kukubali kutekwa kwa nchi au wa sehemu yoyote ya nchi, kuridhia au kutambua kitendo cha uvamizi au mgawanyiko wa Tanzania;
c) Hakuna mtu au Mamlaka yoyote itakayokuwa na haki ya kuwazui raia wa Tanzania kupigana vita dhidi ya adui yeyote anayeshambulia nchi;
d) Uhaini ni jinai kuu dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kosa la uhaini na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atapewa adhabu ya kifo.
e) Uhaini maana yake ni kitendo cha mtu yeyote:-
i. Kumuua, au kujaribu kumuua au kula njama ya kumua Rais wa Jamhuri ya Muungano la Tanzania; au
ii. Kuanzisha vita au kusaidia adui katika vita dhidi ya Jamhuri ya Muungano la Tanzania.

21. WAJIBU WA KUTII NA KULINDA KATIBA
a) Kila mtu anao wajibu wa kufuata na kutii Katiba na sheria za nchi;
b) Kila mtu anayo haki kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Katiba kuchukua hatua za kuilinda Katiba na sheria za nchi;
c) kila mtu anayo haki ya kupinga kufutwa, kubadilishwa au kuvunjwa kwa Katiba kinyume na utaratibu uliowekwa na Katiba yenyewe.
d) kila mtu anao wajibu wa kuiheshimu mali ya mtu mwingine, kulinda mali asili, utajiri wa nchi, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi.
e) Kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, amani, mamlaka na umoja wa Taifa.

HAKI SAWA KWA WOTE

Tunaomba kuwasilisha,
Prof Ibrahim Haruna Lipumba

Advertisements

2 thoughts on “Katiba Mpya: Ufafanuzi wa Maoni ya CUF

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s