Baina ya ukombozi wa gesi na nchi, upi ni uzalendo zaidi?

gesibg

Wakaazi wa mikoa ya kusini ya Tanzania wakipigania gesi asilia inayozalishwa kwao kuwafaidisha kwanza wao.

Wahenga walisema ‘adhabu ya kaburi aijuae ni maiti’. Dunia imewahi kuishuhudia Tanzania ikipambana vikali na Uganda katika mwaka 1979 kwa madai ya kuvamiwa na sehemu ya nchi yake katika Mkoa wa Kagera kukaliwa kwa mabavu na Iddi Amin. Halkadhalika dunia imewahi kushuhudia mara kadhaa Tanzania ikikwaruzana na jirani yake mwengine, Malawi, kwa madai kwamba eneo lake la ziwa Nyasa limevamiwa na nchi hiyo. Halkadhalika tuimewahi kushuhudia jamii mbali mbali za watanzania wakiuwana na kuchinjana kwa kugombania raslimali kadhaa, kila mmoja akidai kudhulumiwa. Hili limejitokeza wazi katika mapambano kadhaa ya kugomania raslimali ya ardhi, raslimali za madini nk. Hivi sasa mapambano yamepambamoto katika raslimali ya gesi iliyoko katika Mkoa wa Mtwara.

Somo lililopo katika utangulizi hapo juu ni kwamba kumbe kila mmoja anathamini kitu chake na kukiona ni bora kuliko cha mwenzake, na bila shaka yuko tayari kwa lolote lakini kitu chake hicho kisimtoke mikononi mwake. Hii ndio maana Tanzania iliingia vitani na Uganda kuipigania Kagera, hii ndio maana Tanzania imekua ikitishia mara kadhaa ikilazimika itaingia vitani na Malawi kulinusuru ziwa Nyasa. Halkadhalika hii ndio maana watanzania wa jamii mbali mbali wamekua wakipigana wenyewe kwa wenyewe kama vile jamii za wafugaji dhidi ya wakulima. Wamekua wakipigana na wawekezaji katika maeneo yao kama vile mapambano ya wanavijiji dhidi wamiliki wa migodi. Hakadhalika wananchi wamekua wakipambana na serikali yao kukataa maamuzi ambayo kwa mtazamo wa wananchi wa maeneo hayo ni kuibiwa raslimali zao na badala yake ni kwenda kuwanufaisha wengine. Mfano wa haya ndio kama yanayojiri hivi sasa katika Mkoa wa Mtwara. Wananchi wa Mtwara wanaendelea kupambana na serikali huku watu kadhaa wakipoteza roho zao alimradi tu wanahakikisha raslimali yao ya gesi haitoki ndani ya Mtwara na badala yake inabaki Mtwara na inatumika kwa ajili ya maslahi na maendeleo ya watu wa Mtwara.

Wananachi wa Mtwara wakiandamana kupinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.

Wananachi wa Mtwara wakiandamana kupinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.

Maelezo yote hapo juu yanaonyesha jinsi watanganyika walivyokua wamechichipaa kwa ushujaa kupambana na mataifa jirani ili kulinda maeneo ya nchi yasivamiwe. Pia maelezo hayo yanaonyesha jinsi watanganyika wenyewe kwa wenyewe (jamii moja na nyengine) wanavyopambana kwa ushujaa ili kulinda maslahi ya sehemu zao, ardhi zao au raslimali za jamii zao husika zisichukuliwe na wengine. Sasa basi iweje iwe ni jambo dogo linaloonekana halina maana kwa wazanzibari kusimama kidete, kujanza munkari, mori na hamasa kupigania nchi yao iliyomezwa na kupokonywa mamlaka yake yote ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutawala? Hivi ni mtu gani mwenye akili yake asiyefahamu kama gesi haina thamani mbele ya nchi nzima? Mbele ya utamaduni wa taifa zima? Mbele thamani ya watu wa taifa zima?

Alipopambana Mzee Aboud Jumbe wakati ule wa Nyerere yaliitwa ni machafuko tu ya hali ya hewa Zanzibar yaliyolengwa kuuhatarisha Muungano, machafuko ambayo yalihitaji kudhibitiwa kwa kufukuzwa Mzee Jumbe katika kiti cha urais wa Zanzibar. Alipopambana Maalim Seif na wenzake wakati ule wa Nyerere ulionekana ni uchochezi uliolengwa kuigawa CCM na kuuhatarisha Muungano, uchochezi ambao ulihitaji kudhibitiwa kwa kufukuzwa Maalim Seif na wenzake katika chama na katika nyadhifa za serikali.

Wana CUF walipoandamana mwaka 2001, pale Unguja na Pemba enzi ya Benjamin Mkapa kudai pamoja na mambo mengine mabadiliko ya katiba ya Tanzania ili kutoa fursa ya muungano wa haki na usawa baina ya Tanganyika na Zanzibar walifanywa kama wahalifu tu na hivyo kuvamiwa na vikosi vyote vya ulinzi na salama na kumiminiwa risasi za moto na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 50, walemavu, wajane, mayatima na maelfu ya wakimbizi. Halkadhalika wazanzibari walipopambana na vyombo vya dola mara kadhaa katika mwaka wa 2011 chini ya harakati za taasisi za kiislamu kudai Muungano wa haki, hadhi na heshma ya Zanzibar kurejeshwa waliitwa wahuni, magaidi, Alshababb, Alqaida nk. Walivamiwa na polisi kupigwa, kuumizwa, kuwekwa vizuizini na kufunguliwa kesi wao na viongozi wao wa harakati hizo.

Hapa ndipo pale penye lengo la makala yangu hii. Lengo ni kuwauliza watawala wa Jamhuri ya Muungano na vibaraka wao walioko kule Zanzibar, kama wazanzibari wanaopigania nchi yao nzima iliyotekwa na majirani zao watanganyika ni wahuni, magaidi, Alshabab na Alqaida, jee hawa wanaopigania gesi tu isichukuliwe tena na serikali yao wenyewe tuwaite vipi? Kati ya hawa wazanzibari waliopigana kujibu na kupinga maonevu ya vyombo vya dola dhidi ya harakati zao, na wale waliojipanga wenyewe kuanzisha harakati za mapambano ya kupinga gesi yao isitoke nje ya Mtwara ni nani gaidi zaidi? alkaida zaidi? Muhuni zaidi? Au alshabab zaidi?

Askari wa kikosi cha FFU wakimpa kipigo mwananchi aliyekua amekaa umbali wa mita 200 kuwatambua wapiga kura mamluki

Askari wa kikosi cha FFU wakimpa kipigo mwananchi aliyekua amekaa umbali wa mita 200 kuwatambua wapiga kura mamluki

Wazanzibari tunasema kama ambavyo wana Mtwara wanayo sababu ya kupambana kulinda gesi yao isichukuliwe kwenda kuimarisha Dar es Salaam, Dodoma na Arusha basi wazanzibari wanazo zaidi sababu za kupigania nchi yao iliyohodhiwa na watanganyika na hatimae kuirejesha katika mikono yao hata kama wataendelea kuitwa magaidi, alshabab, alqaida, wahuni nk. Halkadhalika wataendelea na mapambano ya kuimezua nchi yao hata kama makombora yote makubwa ya Tanganyika yataelekezwa Zanzibar. Kama wana Mtwara wanayosababu ya kuipigania gesi yao ambayo bado imo katika matayarisho ya kuchukuliwa Dar es Salaam basi wazanzibari wanazo zaidi sababu za kupigania nchi yao iliyomezwa miaka 49 iliyopita na raslimali zake kadhaa kuibiwa na watu wake kuachwa maskini tokea miaka hiyo hadi leo.

Wanaoijuwa athari ya gesi ya Mtwara kwenda Dar es Salaam na kuwaacha watu wa Mtwara wakiendelea kuwa masiki ni watu wa Mtwara. Halkadhalika, waijuwao athari ya Zanzibar kumezwa na Tanganyika huku wazanzibari wakibakia wanyonge hawana maamuzi, hawana heshma ya nchi yao, hawana mamlaka ya nchi yao na uchumi wao ukizidi kufa ni wazanzibari. Adhabu ya kaburi aijuae ni maiti. Wazanzibari wamechoka kunyanyasika na wataendelea kupambana kuliko walivyowahi kupambana mpaka watakapoyatia mikononi mwao mamlaka kamili ya nchi yao. Jamhuri ya watu wa Zanzibar Kwanza!

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s