Maamuzi ya umma yataheshimiwa – Jussa

Mwakilishi wa Mji Mkongwe na Mjumbe wa Baraza Kuu CUF, Ismail Jussa.

Mwakilishi wa Mji Mkongwe na Mjumbe wa Baraza Kuu CUF, Ismail Jussa.

Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa CUF ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa, amesema katika mwaka 2012 Zanzibar ilipiga hatua muhimu iliyokuwa inasubiriwa kwa muda mrefu kwa kuwawezesha wananchi kutoa maoni yao juu ya muundo wa Muungano wanaoutaka baina yake na Tanganyika.

Akiwahutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika jioni ya leo (tarehe 1 Januari) katika viwanja vya Kwamzushi, Mtoni, wilaya ya Mjini Unguja, Jussa amesema kuwa Wazanzibari kudai mamlaka ya nchi yao si suala la Uhizbu kama wanavyosema baadhi ya watu, bali ni haki yao ya msingi. Ameongeza kuwa hilo ndilo litakaloiwezesha Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ya kujiamulia inachokitaka tafauti na hali ilivyo sasa.

Akibainisha kuhusu mambo yaliyoikandamiza Zanzibar ndani ya mfumo wa sasa wa Muungano, Jussa alisema ni  pamoja na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano kuyachukua mambo yasikuwa ya Muungano na kuyafanya kuwa ni ya Muungano. “Hilo limeidumaza nchi yetu kiuchumi zaidi na kuonekana kuwa  ni nchi maskini sana duniani,” alisisitiza mwakilishi huyo na miongoni mwa viongozi vijana wa CUF.

Akiyataja mambo hayo yaliyoingizwa kinyemela kwenye Muungano, alisema mojawapo ni masuala ya sarafu. Alisema kuwa hata jambo hilo lilipowekwa kwenye orodha ya mambo ya Muungano, Serikali ya  Zanzibar haikuwa na taarifa na ikalikataa kabisa, lakini kwa ubabe likalazimishwa kubakia humo.

Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu, Uenezi na Mahusiano na Umma, Salim Bimani.

Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu, Uenezi na Mahusiano na Umma, Salim Bimani.

Jussa ameeleza kwa kuwa kwake nchi ya visiwa, uchumi wa Zanzibar hutegemea zaidi bahari pamoja na utalii, lakini mambo hayo hayafaidishi Zanzibar kwani  upande wa pili wa Muungano huu umehodhi mamlaka ya bandari ndani ya Zanzibar pamoja na suala zima la utalii. “Hata ukienda kwenye ofisi za balozi za Tanzania nje ya nchi, wanayoitangaza  kiutalii ni Tanzania tu na sio Zanzibar.”

Akizungumzia elimu, Jussa alisema Zanzibar inakandamizwa sana na serikali ya Muungano akipigia mfano wa hivi karibuni ambapo tayari Wizara ya Elimu ya Tanzania ilishawazuia wanafunzi wa Zanzibar kutokufanya mitihani ya taifa ya Kidato cha Sita kwa madai eti hawana sifa, licha ya kuwa walishasoma miaka miwili na kujisajili kwenye mamlaka husika.

“Lakini kwa jitihada za (Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa CUF) Maalim Seif, mara baada ya kuliongelea jambo lile tu, ndio siku ya pili yake wizara ya Elimu Bara wakatoa tamko kuwa wanafunzi wote watafanya mtihani.”

Pamoja na yote, mwakilishi huyo wa Mji Mkongwe  Jussa aliwahakikishia Wazanzibari wote kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watahakikisha wanayalinda kwa hali yoyote maoni yao waliotoa ya kutaka Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa na ikitokezea upande wapili wa Muungano huu wakayakataa maoni yao, basi watawaambia kuwa sasa wabaki kuwa marafiki na majirani wema.

“Lakini hatutoendelea tena na Muungano huu.”

Kwa upande wake Mkurugeni wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF, Salim Bimani, amewataka wananchi wa Zanzibari hususani vijana kutokukubali kuchokozeka katika kipindi hichi muhimu cha kuipelekea nchi kuwa huru.

“Kuweni watulivu sana. Na pia fichueni vitendo viovu popote pale munapoviona kwa kutoa taarifa kunakohusika.”

Imeandikwa na Hamed Mazrui

Advertisements

2 thoughts on “Maamuzi ya umma yataheshimiwa – Jussa

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s