Rafu za CCM, CHADEMA zaivuruga Mwanza

MIVUTANO ya kisiasa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Halmashauri ya Ilemela, sasa ni kikwazo cha maendeleo katika halmashauri hiyo mpya.

Wachunguzi wa mambo ya siasa wameielezea hali hiyo kuwa kielelezo cha ubinafsi wa baadhi ya wanasiasa kuthamini zaidi maslahi ya vyama vyao badala ya wananchi.

Baada ya uchaguzi ulioelezwa kujaa mizengwe na Diwani wa Kata ya Kitangiri, Henry Matata, kuchaguliwa kuwa Meya wa Manispaa hiyo na idadi ya madiwani iliyolalamikiwa kuwa haikidhi akidi ya theluthi mbili inayotakiwa ili kufanyika kwa uchaguzi huo, hali ya mambo imeendelea kuwa tete baada ya Meya huyo kuwafukuza madiwani watatu wa CHADEMA na wao kujiandaa kukata rufaa kutetea haki yao.

Viongozi wa CHADEMA kwenye maandamano Mwanza.

Viongozi wa CHADEMA kwenye maandamano Mwanza.

Mmoja wa madiwani waliofukuzwa, Dani Kahungu wa Kata ya Kirumba, amesema kuwa kinachofanyika katika halmashauri hiyo ni uhuni huku mamlaka zinazosimamia halmashauri hiyo zikionyesha uvumilivu wa kushangaza kwa matukio ya ukiukwaji wa haki unaoendelea, hali inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani iwapo wananchi watakosa uvumilivu wa yanayoendelea.

Amesema amepokea barua ya kuvuliwa udiwani iliyosainiwa na Meya Matata Desemba 11, mwaka huu, ikieleza kuwa amevuliwa wadhifa wa udiwani kwa kuwa amaeshindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo wakati kwa mujibu wa maelezo yake halmashauri hiyo imefanya vikao viwili.

“Kikao cha kwanza ni kile kilichofanyika Novemba 9 wakati nikiwa gerezani, kwa kesi ambayo nayo ni ya kisiasa, kwa hiyo hicho nilihesabiwa sipo na kikao cha pili ni kile kilichofanyika Novemba 14, kuchagua wenyeviti wa kamati, baada ya hapo kikao kingine cha kikalenda kilipaswa kufanyika Desemba 4, lakini hakikufanyika” alisema.

Siku hiyo, Desemba 4 madiwani wote wa CHADEMA walikwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Zuberi Mbyana na kuuliza kwa nini kikao hakijafanyika siku hiyo kwa mujibu wa ratiba hiyo, aliwajibu kuwa kamati ya huduma za jamii haijapeleka taarifa yake kwa hiyo kikao hakitafanyika, na wakatia saini kwa Mkurugenzi.

Anaeleza zaidi kuwa kimsingi halmashauri hiyo haijafanya vikao rasmi vinavyofika vitatu, badala yake imekaa vikao viwili tu, lakini anaongeza kuwa wakati wa kuhudhuria vikao au kutohudhuria walikuwa wanahusika madiwani wote wa CHADEMA, inashangaza kwa nini Meya huyo ameamua kuwafukuza madiwani watatu tu, na hapo ndiyo anapodhani kuna hujuma za kisiasa zinafanyika dhidi ya Chama chake.

“Kile kikao cha kwanza cha uchaguzi ambacho nilikuwa gerezani, madiwani wote wa CHADEMA walisusia uchaguzi huo, lakini hata kile cha kuunda kamati, kilichofuatia Matata (Meya) alikivunja ghafla baada ya sisi kuhoji uhalali wa yeye kuongoza kikao wakati hajachaguliwa kihalali, baada ya kuvunjika kikao hicho kihuni hatukujua nini kimeendelea, matokeo yake ndiyo hii barua ya kuvuliwa udiwani,” anaeeleza.

Anasema kuwa hizo ni njama za kisiasa zinazosimamiwa na washindani wao ili kuivuruga halmashauri hiyo kwa manufaa ya CCM huku mamlaka zinazohusika kusimamia taratibu za kuendesha halmashauri zikikaa kimya bila kuchukuliwa hatua hata kama kumekuwa na ukiukwaji wa wazi wa sheria za nchi.

Kahungu anaeleza kuwa kulitakiwa kuwe na kikao cha kufikia uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao ambacho hakikufanyika na kwamba uamuzi huo umefikiwa na Meya pekee kwa sababu zake binafsi tena bila kufuata taratibu.

Madiwani wengine waliosimamishwa ni pamoja na Marietha Chenyenge wa Ilemela na Abubakaar Kapela wa Nyamanoro. Kahungu anaeleza kuwa hawatakubali haki ya wananchi waliowachagua kupuuzwa kwa kiwango hicho.

Hata hivyo Meya Matata amezungumzia malalamiko hayo dhidi yake akisema halmashauri hiyo imekaa vikao sita, vikiwamo vya kamati ambavyo navyo vinahesabika kisheria na ikiwa diwani hajahudhuria vikao hivyo anachukuliwa hatua.

Kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa namba 8 ya mwaka 1982 kifungu cha 25 kifungu kidogo cha 5(a) kinasema kuwa diwani atavuliwa wadhifa huo ikiwa atashindwa kuhudhuria mikutano mitatu bila kuwapo sababu zozote za msingi wala taarifa.

Kifungu cha 69(1)(e) cha kanuni za kudumu za halmashauri ya Jiji la Mwanza kinasema kiti cha udiwani kitakuwa wazi ikiwa “Bila sababu zozote za kuridhisha au bila idhini au kibali cha maandishi cha mwenyekiti, mjumbe amekosa kuhudhuria mikutano mitatu ya kawaida, mikutano ya halmashauri au kamati ambazo yeye ni mjumbe.”

Akijibu tuhuma kuwa anatumia nafasi hiyo kama njia ya kuwakomoa madiwani wa CHADEMA kwa manufaa ya Chama tawala, Meya Matata anasema anachofanya ni kutimiza wajibu kisheria na kufuata kanuni.

“Tatizo hawa watu (CHADEMA) hawajui kuwa wanashughulika na mwanasheria, mimi ni mwanasheria ninaendesha mambo yangu kwa sheria na taratibu, wao hawajui kuwa hata vikao vya kamati vinahesabika, nataka nikuhakikishie tangu nimechaguliwa tumekaa vikao sita, hizo nyingine ni kelele tu,” alieleza.

Alipotakiwa kufafanua zaidi kuhusu idadi ya vikao walivyokaa kama ni viwili au sita na ni kikao gani kilikaa kufikia uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilemela, Zuberi Mbyana, ambaye pia ndiye katibu wa vikao vya Baraza la Madiwani alijibu kwa ufupi tu kwamba; “Nadhani Meya atakujibu vizuri sana”.

Mtumishi mmoja wa halmashauri hiyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini ameliambia gazeti hili kuwa malumbano hayo ya kisiasa yanachangia kupunguza kasi ya utekelezaji wa masuala ya maendeleo.

“Kwenye huu mvutano ndipo mambo ya ajabu yanafanyika, vikao vikikaa hakuna hata kimoja kilichojadili maendeleo ya watu kwa kina, badala yake malumbano ya kisiasa tu, huu mwanya unaweza kutumiwa na watumishi wasio waaminfu kufanya ufisadi wa ajabu kwa kuwa wanajua hakuna msimamizi makini,” anaeleza.

“Ukiwa huku ndani ndiyo utajua ubaya wa hizi siasa chafu, mambo mengi yanakwazwa kwa maslahi ya watu binafsi na vyama vyao, natamani siku moja wananchi waelezwe ukweli huu ili wawajue hawa wanasiasa, kwa kweli mambo yanayoendelea hapa yanatia aibu,” alisema.

Katika mvutano huo umekuwa ukitajwa ushawishi wa CCM kama moja ya mbinu za kukisambaratisha CHADEMA katika Jiji la Mwanza, ambacho katika Uchaguzi Mkuu uliopita kilinyakua majimbo mawili ya Ilemela na Nyamagana, na kuongoza iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kabla ya kugawanywa na kuzaa Halmashauri ya Ilemela.

Hali hiyo imekuwa ikihusishwa na ukweli kwamba Meya Matata pamoja na kuwa ni diwani kwa tiketi ya CHADEMA alichaguliwa kuwa Meya na madiwani wa CCM na CUF, huku CHADEMA wakisusia uchaguzi huo kwa sababu ya madiwani wao wawili kuwa rumande kwa kesi waliyoiita ya kisiasa.

Viongozi wa CCM hawakuwa tayari kulizungumzia hilo, ingawa kiongozi mmoja wa Chama hicho wilayani Ilemela alisema kama Chama hawajihusishi kwa lolote na mgogoro huo, kwa kuwa CHADEMA wanagombana wenyewe na hivyo hawahitaji kupoteza nguvu katika hilo.

“Hatuwezi kuingilia, hiyo ni faida kwetu hatuhitaji kupoteza nguvu au hata heshima ya chama kujihusisha na jambo ambalo matokeo yake ni yale yale kama tukiingia au tusipoingilia, sisi tuna Tanzania tu ili watu wajue tofauti kati ya nidhamu za Chama chetu na CHADEMA na ninaamini watu wameona,” alieleza kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji wa Chama hicho.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s