CUF yavitikisa CHADEMA, ADC

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake kitaendelea kutetea na kutekeleza sera yake ya kuwaunganisha watanzania popote walipo bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Amesema operesheni mchakamchaka hadi mwaka 2015 iliyozinduliwa na chama hicho hivi karibuni imekuwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo, na kwamba tayari imeanza kuleta mafanikio katika mikoa iliyoanza kutekelezwa ukiwemo mkoa wa Arusha.

Wafuasi na wapenzi wa CUF wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad wakati akiwahutubia katika viwanja vya Buguruni jijini Dar es Salaam.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika viwanja vya Buguruni jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa chama hicho kwenye mkutano maalum wa hadhara uliolenga kuwakaribisha wanachama wapya na kuwapokea wanachama walioamua kurejea CUF baada ya kukihama na kuhamia vyama vyengine.
Katika mkutano huo Maalim Seif aliwapokea na kuwapa kadi za chama hicho wanachama kadhaa walioamua kurejea chama hicho wakitokea chama cha ADC wakiongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa ulinzi na usalama wa ADC Bw. Al-Badawi.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa ulinzi na usalama wa ADC Bw. Al-Badawi akizungumza katika mkutano wa hadhara wa CUF baada ya kuamua kurejea CUF akitokea ADC. Kabla ya kwenda ADC na baadae kurejea CUF Al-Badawi alikuwa mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Temeke.

Kabla ya kujiunga na ADC, Bw. Al-Badawi alikuwa mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Temeke, na sasa ameamua kurejea CUF kwa kile alichokieleza kuwa ni ubabaishaji ndani ya chama hicho kipya kinachohusishwa na mbunge wa jimbo la Wawi Mhe. Hamad Rashid Mohd.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema Tanzania imekuwa ikipita katika kipindi kigumu cha migogoro na uvunjifu wa amani, mambo ambayo yanapaswa kupigwa vita ili kurejesha hali ya amani na kuvumiliana.
Amedai kuwa chanzo kikuu cha migogoro ya kijamii ikiwemo ya ardhi na mizozo ya kidini inatokana na kutokuwepo kwa mikakati imara ya kuendesha nchi, na kwamba viongozi wanapaswa kujifunza kutokana na migogoro hiyo, ili kuweka mikakati imara ya kuendesha nchi kwa uhakika.
“Nchi haiendeshwi kwa kuigiza, bali kwa kuwa na viongozi wenye dira ya mabadiliko kwa maendeleo ya wananchi”, alisisitiza Maalim Seif.
Amesema kutokana na viongozi kutokuwa na dira na mikakati imara ya kuendesha nchi, Watanzania wameshindwa kunufaika na rasilimali za nchi yao ambazo ni nyingi na zinaweza kuwabadilisha kiuchumi.
Amefafanua kuwa iwapo wananchi watanufaika moja kwa moja na rasilimali zao, wataweza kuzitunza na kuzilinda ili ziwe endelevu, na kwamba kinyume chake ni kuzihujumu rasilimali ambazo watahisi haziwanufaishi.
“Popote pasipo na haki hakuna amani, tunataka kila Mtanzania ajihisi kuwa ana haki sawa katika nchi hii, sio kuwa na raia wa madaraja, yaani daraja la kwanza, la pili na la tatu”, alifahamisha huku akishangaliwa na umati wa watu waliojitokeza kwenye mkutano huo.

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akimkabidhi shati la chama hicho kijana Joseph Christian ambaye alikuwa katibu mwenezi wa CHADEMA tawi la Chuo Kikuu Dodoma. Joseph amekihama CHADEMA na kujiunga na CUF kwenye mkutano wa hadhara huko Buguruni jijini Dar es Salaam.

Katika hatua nyengine, aliyekuwa katibu mwenezi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA katika tawi la Chuo Kikuu Dodoma bw. Joseph Christian amejiengua katika chama hicho na kujiunga na CUF.
Akizungumza katika mkutano huo bw. Joseph amesema ameamua kujiengua CHADEMA na kujiunga na CUF kwa madai kuwa chama hicho kimekuwa kikiendeshwa kwa misingi ya undugu na ukabila, na kuwatelekeza vijana wenye lengo la kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini.
Amewatahadhamisha vijana kuwa makini na sera za chama hicho na kuacha kukurupuka kuvamia sera za vyama wasivyovifahamu.
Nae Mwenyekiti wa ADC Wilaya ya Kinondoni Bw. Saburi Mtoro, ambaye pia ameamua kukihama chama hicho na kujiunga na CUF amemuahidi Katibu Mkuu wa CUF kuwa wanachama wote wa ADC katika Wilaya hiyo watajiunga na CUF.

Habari na Hassan Hamad, picha Salmin Said, OMKR

Advertisements

2 thoughts on “CUF yavitikisa CHADEMA, ADC

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s