Operesheni Mchakamchaka 2015 yaanzia Arusha

Mwenyekiti wa CUF Taifa, Prof. Ibrahim Lipumba, akimkabidhi kadi ya Chama hicho aliyekuwa Diwani wa CHADEMA kata ya Ererai mjini Arusha, John Bayo, baada ya kuamua kukihama chama hicho.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF Taifa, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, amesema Tanzania inahitaji kuwa na viongozi wenye dira watakaoweza kuzitumia rasilimali za nchi kwa maslahi ya WaTanzania.

Profesa Lipumba ametoa changamoto hiyo katika viwanja vya Levolosi jijini Arusha, alipokuwa akizungumza na wanachama na wapenzi wa chama hicho, ikiwa ni sehemu ya operesheni mchakamchaka hadi 2015 iliyoandaliwa na chama hicho katika mikoa mbali mbali nchini.

Amesema Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi zikiwemo jiografia yake, bahari na madini ambazo bado hazijatumika vizuri kuwanufaisha Watanzania wanaoendelea kuishi katika hali ngumu ya kiuchumi.

“Tunahitaji viongozi wenye dira watakaoweza kuzisimamia rasilimali za Watanzania kwa maslahi ya Watanzania wenyewe”, alisema Profesa Lipumba na kuongeza
“Watanzania tumeshindwa kuzitumia rasilimali tulizonazo kwa maendeleo yetu, tunayo mazao mengi ya mboga mboga, tunayo madini mengi, bandari na kadhalika ambazo zote hizi zikitumika vizuri tunaweza kujikwamua kiuchumi”, alifafanua.

Wafuasi na wapenzi wa CUF Mkoa wa Arusha wakimshangilia Maalim Seif wakati akiwahutubia katika viwanja vya Levolosi jijini Arusha.

Amefahamisha kuwa Watanzania wanahitaji kujipanga kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo pamoja na maendeleo ya teknolojia, na kwamba iwapo kutakuwa na mipango imara kila Mtanzania anaweza kunufaika moja kwa moja na rasilimali za nchi.

Profesa Lipumba ametaja utajiri mwengine unaoizunguka Tanzania kuwa ni pamoja na vivutio vya utalii vikiwemo milima mikubwa kama vile Kilimanjaro na Meru, Visiwa vya Zanzibar pamoja na rasilimali za mafuta na gesi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad amewakebehi wale wanaobeza maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa Zanzibar, na kwamba maridhiano hayo yalikuwa ni maamuzi ya Wazanzibari wenyewe na haifai kuyabeza.

Amesema maridhiano hayo yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa yameifanya Zanzibar kuwa mfano wa kuigwa kwa Tanzania na nchi nyengine za Afrika Mashariki.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wanachama na wapenzi wa Chama hicho kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Levolosi jijini Arusha.

“Chama Cha CUF kina malengo ya kuwaunganisha Watanzania wote na ni chemchem ya amani, sio kama vyengine hivi vyenye sera za kuripua mabomu na siasa za kibaguzi”, alisema Maalim Seif na kuongeza,
“Siasa si lelemama wala si vurugu, bali viongozi wa kisiasa wanatakiwa washindane kwa hoja sio kuwabagua wananchi kwa misingi ya udini na ukabila, na wajue kuwa hili linavuruga umoja wa kitaifa” alifahamisha.

Aliwashukuru wananchi wa Arusha kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo, na kwamba kuanzia sasa Chama kitajikita katika Mkoa huo kuhakikisha kuwa kinawakomboa wananchi wa eneo hilo.

“Nasema hakuna mtu wala chama chenye hati miliki ya Mkoa huu, bali Mkoa huu ni wa wananchi wote wa Arusha, na kuanzia sasa tutajikita kisiasa katika mkoa huu hadi kieleweke”, alibainisha Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Amewataka wananchi wa Arusha kuwa makini na propaganda zinazoenzwa dhidi ya chama hicho kuwa ni chama cha kiislamu na waarabu, na kwamba propaganda hizo zina lengo la kuwagawa Watanzania badala ya kuwaunganisha.

Mapema akisoma risala ya wanachama wa CUF Wilaya ya Arusha, Katibu wa Chama hicho katika wilaya hiyo Hassan Zakaria Zani, amesema wananchi wa Arusha wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na siasa za vurugu.

Katika mkutano huo Prof. Lipumba alimkabidha kadi ya CUF aliyekuwa Diwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kata ya ERERAI Mkoani Arusha Bw. John Bayo, baada ya kuamua kukihama chama hicho, pamoja na wanachama wengine kutoka CHADEMA na CCM, sambamba na kukabidhi kadi kwa wanachama wapya walioamua kujiunga na CUF.

Mkuatano huo pia ulihudhuriwa na kuhutubiwa na viongozi kadhaa wa CUF wakiwemo Makamu mwenyekiti wa CUF Taifa Machano Khamis Ali na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Tanzania Bara, Julius Mtatiro.

Habari na Hassan Hamad, picha Salmin Said, OMKR

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s