Waliovuruga uchaguzi wa Bububu ni maadui wa Umoja wa Kitaifa

Askari wa kikosi cha FFU wakimpa kipigo mwananchi aliyekua amekaa umbali wa mita 200 kuwatambua wapiga kura mamluki

Sasa kuna kila aina ya sababu iliyo wazi kusema kwamba maridhiano ya wazanzibari na dhamira ya kuundwa kwa serikali ya Umoja wa kitaifa ilikuwa ni agenda  ya Maalim Seif Sharif Hamad na chama chake cha CUF kwa upande mmoja. Kwa upande wa pili wa CCM maridhiano hayo yanaonekana kubaki katika nyoyo za watu wachache nao ni waasisi wa maridhiano hayo Mzee Hassan Nassoro Moyo, Rais mstaafu Mhe Amani Abeid Karume, Waziri Mansoor Yussuf Himid, pamoja na wafuasi wao wachache walioweza kuifahamu na kuikubali kwa dhati agenda hii ya maridhiano.

Kundi kubwa lililoanzia serikalini halikuyapenda wala kuyakubali maridhiano hayo. Viongozi wengi chama na wa serikali hawakuyataka maridhiano hayo tokea yanaasisiwa. Viongozi hao walilazimika tu kutii mawazo na maamuzi ya rais Karume na si ridhaa na hiari zao.  Kwa maana hii agenda ya maridhiaano haikuwa ya CCM, viongozi wa CCM wala ya wana CCM. CCM walilazimika kuheshimu mawazo ya rais Amani Karume kwa kuwa alikuwa na msimamo usioyumba juu ya kuifanikisha agenda hiyo ili kunusuru amani na utulivu wa nchi kabla ya hajaondoka madarakani. Halkadhalika nafasi yake kubwa ya kisiasa na kiserikali aliyokua nayo kwa Zanzibar iliipelekea NEC kulazimika kuheshimu uwamuzi wake.

 

Pia kuna tetesi zilizotoka ndani ya vikao vya CCM kwamba agenda ya Amani Karume italazimika kuheshimiwa shingo upande na sio kukubaliwa  ili kunusuru “kuchafuka kwa hali ya hewa Zanzibar kwa mara nyengine”. Machafuko ya hali ya hewa Zanzibar yaliwahi kutokea katika  miaka ya 1980 pale Rais mstaafu wa awamu ya pili Mzee Aboud Jumbe alipojidhatiti kutaka kuleta mabadiliko makubwa ya mfumo wa Muungano kutoka serikali mbili kwenda serikali tatu. Jambo hilo lililoitwa kuchafuka kwa hali ya hewa Zanzibar lilipelekea kufukuzwa kiongozi huyo katika madaraka ya urais na katika madaraka makubwa ya chama cha CCM aliyokuwa nayo. Kwa kuwa agenda ya maridhiano Zanzibar  ilikubaliwa na kiongozi huyu mkuu wa seriakali ya Zanzibar ambae ni rais na ni kiongozi mwenye madaraka makubwa ndani ya CCM (makamo mwenyekiti) haikuwa rahisi hata kidogo kwa NEC kuipiga ngware agenda hiyo baada ya kufikiria na kujifunza kwa makini somo la kuchafuka kwa hali ya hewa la miaka ya 1980.

CCM imekuwa ikipinga wazi wazi kwa kauli na kwa vitendo maazimio yote ya miafaka iliyowahi kufanywa huko nyuma. Katika hali isiyo ya kawaida CCM pia ilipinga maazimio ya muafaka wa mwisho ambao ulipendekeza pamoja na mambo mengine kuundwa kwa serikali ya Umoja wa kitaifa Zanziabr kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Hii ni hatua ya mapema, muhimu na ya wazi wazi iliyobainisha kuwa chama hicho kamwe hakikuwa tayari kuingia katika maridhiano na serikali ya Umoja wa kitaifa. Viongozi kadhaa wa CCM walitamka bayana mara baada ya maridhiano hayo kwamba maridhiano hayakuwa halali kwani yalifanywa kwa siri na hayakuvishirikisha vikao vya CCM katika kufikiwa kwake. Mmoja wa viongozi wa CCM aliyetamka maneno kama hayo ni Nape Nnauye, ambae ni msemaji mkuu wa CCM wakati vyombo vya habari vilipotaka kauli ya CCM kuhusu maridhiano ya Rais Amani Karume na Maalim Seif.

Mawaziri, wawakilishi, wabunge na viongozi wa CCM walionyesha kuikubali agenda hiyo mbele ya uso wa Rais Amani Karume na kufanya unafiki wa hali ya juu katika kuipotosha na kuipinga agenda hiyo. Viongozi hao wa kisiasa walitumia nafasi zao kwa siri kufanya kampeni chafu ya kinafiki ya kupinga kuundwa kwa serikali ya Umoja wa kitaifa katika maeneo ambayo wana ushawishi wa kisiasa. Kiongozi mmoja mkuu wa serikali aliyedhihirisha mapema kuwa yeye hakuyakubali maridhiano hayo ni waziri Ali Juma Shamhuna, mwakilishi wa jimbo la Donge. Pamoja na maridhiano na kukubaliana kusameheana yaliyopita, waziri huyo alitayarisha jeshi la polisi na vikosi vya SMZ kuhakikisha chama cha CUF hakifanyi kampeni zake katika jimbo lake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010.

Wakuu wa wilaya na masheha nao walifanya kila wawezalo kuhakikisha agenda ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa haifanikiwa katika kura ya maoni. Mkuu wa wilaya ya kati kwa wakati huo aliitisha kikao cha masheha wa wilaya yake na kuwapa maagizo masheha hao wawahamasishe watu wao wapige kura ya HAPANA jambo ambalo lilimlazimisha rais Karume kumpkonya cheo mkuu huyo wa wilaya. Vita hivyo vya kuipinga serikali ya umoja wa kitaifa ndani ya CCM ilipelekea takriban asilimia 90 ya wana CCM kuipigia kura ya HAPANA agenda hiyo ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa katika kura ya maoni. Mambo pekee yaliyosaidia ushindi wa kura ya NDIO katika kura ile ya maoni kwa asilimia 66 ni haya yafuatayo: (1) wingi wa kimaumbile wa wana CUF ambao wote waliikubali agenda hiyo, (2) wana CCM wachache sana waliomfahamu na kuamua kumtii kwa moyo wote rais Karume waliweza kuongeza japo kidogo asilimia ya kura ya NDIO na (3) agizo la Rais Karume kwa tume ya uchaguzi kutothubutu kutumiwa na mtu yeyote kufanya hila na kuyachakachua matokeo ya kura hiyo ya maoni.

Pamoja na seriakali ya umoja wa kitaifa kuundwa kwa mafanikio makubwa na kuanza kufanya kazi zake vizuri haikuwemo katika miyo ya viongozi wengi wa CCM na wafuasi wao wengi kama ambavyo haikuwa wakati wa kuasisiwa kwake. Bila shaka viongozi hawa wanafanya kazi kubwa katika maeneo yao kuendelea kuwatia chuki wafuasi wao wasiipende serikali hiyo ya umoja wa kitaifa na waione ndio adui na kikwazo kwa chama chao. Dalili za wazi wazi za haya ni tabia ya kudumu ya maskani maarufu na muhimu za CCM hapa Zanzibar (KISONGE, KACHORORA na maskani ya Wazee Jang’ombe) kuchapisha mabango ya matusi dhidi ya chama cha CUF, viongozi wa CUF na watu wenye asili ya kisiwa cha Pemba huku viongozi wa chama chao na serikali inayoongozwa na chama chao ikitazama kama haioni tu bila ya kuchukua hatua yeyote dhidi ya vitendo hivyo.

Mikutano kadhaa ya hadhara imewahi kufanywa na viongozi na makada maarufu wa CCM ambayo inaashiria wazi CCM haiyaheshimu maridhiano wala serikali ya umoja wa kitaifa. Viongozi na makada hao wamekua wakupanda katika majukwaa na kutamka matusi ya wazi dhidi ya chama cha CUF na viongozi wa seriakali ya umoja wa kitaifa kutoka CUF akiwemo makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na Waziri wa katiba na sheria Abuu Bakar Khamis Bakari, wote wawili wakituhumiwa eti ndio wanaowalinda UAMSHO. Makada hao wamekuwa wakitangaza wazi kuwa majanjawiri wao bado wapo na silaha zao zikiwemo  nondo bado zipo na hwenda zikatumika wakati wowote kama zilivyokuwa zikitumika kabla ya kuja kwa maridhiano na serikali ya umoja wa kitaifa. Halkadhalika hakuna yote hayo yakitendwa hakuna mhusika aliyeonywa, aliyekemewa au aliyechukuliwa hatua kwa kumtukana kiongozi wa juu serikali, kuhatarisha amani ya nchi au kufanya uchochezi.

Katika muundo wa serikali mpya ya umoja wa kitaifa Zanzibar CCM ilihakikisha nafasi nyeti za utendaji wa shughuli kuu muhimu na ndogo ndogo za serikali sio tu zote zishikwe na CCM lakini pia wapewe viongozi wa CCM ambao hawakuyakubali maridhiano. Kufanya hivyo kutasaidia kwa kiwango kikubwa na hivyo kulinda maslahi ya chama chao dhidi ya nguvu yoyote ya kisiasa ambayo itajaribu kuhamisha nguvu za CCM na kuzipeleka katika serikali ya Umoja wa kitaifa. Viongozi hao wahakikishe pamoja na uwepo wa CUF katika serikali, serikali hiyo inabaki  kama vile ni ya chama kimoja tu cha CCM kwa kulinda misimamo na maslahi yote ya CCM ikiwemo ile inayopingana na uwepo wa serikali yenyewe ya umoja wa kitaifa. Viongozi hao ni Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Mwinyihaji Makame na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Mwinyihaji Makame ameshawahi kufanya vitimbi vingi tokea kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa akionyesha yupo katika nafasi hiyo kulinda maslahi ya chama chake na kuendeleza yale ya zamani ya uonevu na unyanyasaji hasa kwa wafuasi wa CUF. Mfano mzuri ni maamuzi yake ya kuyahamisha makontena ya Darajani yaliyopo hapo kisheria na kupingana uwamuzi wa mahakama na kukusudia kuanzisha ujenzi wa bustani katika eneo hilo. Kilichomo katika mawazo ya Mwinyihaji ni chuki dhidi ya wafanya biashara wale ambao takriban wengi na wafuasi wa CUF na watu wenye asili ya kisiwa cha Pemba. Lakini pia Mwinyihaji ana ajenda ya kuwatia chuki na hasira wafanyabiashara wale dhidi ya chama chao cha CUF ili waione na CUF kwa kuemo kwake katika serikali itakua imeshiriki uovu huo.

Uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu umeanika hadharani ukweli kwamba chama cha CCM hakiyataki wala hakiyaheshimu maridhiano ya November 9, 2009 na serikali ya umoja wa kitaifa. Inavyoonekana ni sawa na mtu aliyepewa mke au mume kwa lazima na wazazi wake lakini hana mapenzi hata kidogo bali anaishi nae kwa kukosa maamuzi ya kumuacha. Katika serikali ya umoja wa kitaifa ya Zanzibar, Rais Mstaafu Amani Karume amewalazimisha CCM kuingia katika ndoa ambayo hawana mapenzi nayo hata kidogo, jambo ambalo linaonekana wazi baada ya CCM kutumia ubabe kulazimisha maslahi yake katika ndoa hiyo.

Uchaguzi wa Bububu umekuja kuifichua siri hii nzito ambapo viongozi wa CCM wamejitia wenyewe mtegoni baada ya muda mrefu kukataa hoja kwamba wao si waumini wa dhati wa maridhiano na serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar. Kabla ya siku ya upigaji kura yalikuwepo matukio kadhaa ambayo yailtoa kila aina ya dalili ya kuwepo kwa harufu ya kuharibiwa kwa uchguzi na bila shaka kuzuka kwa vurugu ambapo bila shaka ni kukejeliwa kwa maridhiano na serikali ya uomoja wa kitaifa. Hapa lazima ifahamike kwamba tatizo la msingi la Zanzibar ni chaguzizisizoheshimiwa, chaguzi zinazokorogwa kwa kuvunjwa kwa makusudi sheria zinazosimamia chaguzi hizo ili kukipatia ushindi wa lazima chama cha CCM tokea uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa 1995 baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Akifunga kampeni CCM za uchaguzi huo wa Bububu Balozi Sefu Iddi alisema hadharani kwamba CUF wajue kabisa karamu ya Bububu ambayo italiwa siku ya kupiga kura si yao ni ya wenyewe CCM. Hakuishia hapo ila aliwapa maagizo wana CCM kutumia kila njia kuhakikisha CUF hawasogei na ndizi zao kutaka kula karamu ambayo sio yao. Balozi alikwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba mseto wa CCM na CUF umebakishwa juu kwa makusudi, utaendelea kubaki juu na kamwe hautaruhusiwa kufika chini mpka ngazi ya jimbo na shehia. Akimaanisha kwa kuwa jimbo hilo lina mbunge kutoka CCM hakuna ni lazima na mwakilishi atoke CCM. Aliwauliza wana CCM kama wako tayari kuruhusu mseto katika jimbo la Bububu nao wakamuahidi Balozi kwamba kamwe hawatauruhusu. Serikali ya umoja wa kitaifa imewekwa katika ngazi ya uwaziri pekee ili kuepusha kupunguza nguvu za kiutendaji za CCM katika ngazi zote. Pindipo CUF ikiachiwa kushinda katika jimbo la Bububu ni kuweka mchanganyiko wa CUF na CCM katika uongozi wa jimbo jambo ambalo Balozi Seif aliwaagiza wana CCM walizuie kwa nguvu zao zote.

Halkadhalika Balozi Seif ni muumini wa Mfumo wa sasa kandamizi wa Muungano na anaitumikia Tanganyika wazi wazi kuimaliza Zanzibar. Inavyosemekana hana mizizi mirefu na nasaba ya kizanzibari bali mizizi yake mirefu ni ya Tanganyika hivyo amewekwa katika nafasi hiyo ili kulinda muendelezo wa mamlaka ya Tanganyika juu ya Zanzibar. Balozi amekuwa akipambana na kufikia kuwatisha viongozi kadhaa wa CCM na hata Mzee Moyo ameshiriki kukiasisi cha cha CCM ili wasiunge mkono mabadiliko ya mfumo wa muungano kutoka muungano wa kikatika wa serikali mbili kwenda katika mfumo mpya wa muungano wa MKATABA. Balozi anafahamu wazi kuwa ushindi wa CUF katika jimbo hilo ni kuongezeka kwa sauti ya chama hicho ambacho ndio championi wa muungano wa MKATABA katika bunge la katiba ambalo litazaa mabadiliko ya mfumo na muundo wa muungano hapo baadae. Balozi akifahamu tayari CCM imeshapoteza nguvu kubwa katika kuulinda muungano wa serikali 2 baada ya baadhi ya wawakilishi wa CCM kuapa kuunga mkono MKATABA ameamua kutumia nguvu za ziada kulirejesha jimbo la Bububu katika CCM kwa lazima.

Zipo taarifa za uhakika kwamba tume ya uchaguzi ya Zanzibar imetumika kikamilifu kama ilivyozoea huko nyuma kuuharibu uchaguzi wa Bububu. Wataalamu wa wizi wa kura kutoka Tanganyika ambao ni Harbat Kiato na Aneth Angelo waliletwa Zanzibar na kupokewa na mwenyeji wao Mbunge wa jimbo la Kikwajuni Hamad Yussuf Massauni. Wataalamu hawa walikutanishwa na Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi Taifa Salim Kassim Masego, Makamo Mwenyekiti Saidi Bakari Jecha pamoja na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Bububu Bwana Suluhu. Mpango mkubwa ni kusaidia kutengeneza vipande feki vipya na vya haraka mno kwani vipande feki vilivyopo havikubaliani sura ya mpiga kura na picha iliomo katika kipande cha kupigia kura. Mpango huo ulifanikishwa na vipande hivyo feki vilizagaa na wapiga kura kadhaa waliokuwa na vipande hivyo walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi Bububu ambao wote waliachiwa bila hata ya kufunguliwa majalada.

Mengi yametokea siku ya kupiga kura lakini kwa kifupi ni matumizi ya nguvu za dola na ubabe ule ule wa zamani kuuvuruga uchaguzi. Wanamgambo maharamia waliounzwa uasi (janjawiri), Vyombo vya ulinzi ikiwemo polisi, majeshi na kikosi cha JKU ndio walioongoza operation ya kuuvamia uchaguzi ili kutengeneza ushindi wa CCM. Polisi wao waliwapa ulinzi JKU ili kuhakikishindwi kutekeleza majukumu yao waliopangiwa. JKU waliwapiga watu kwa matako ya bunduki, marungu na kuwatwanga risasi wale waliojaribu kukaa umbali wa mita 200 ili kuwabaini wapiga kura ambao si wakaazi wa jimbo la Bububu. Makamanda wa JKU bila hofu wala kificho walikuwa wakitoa amri kwa askari wao kupiga risasi. Halkadhalika askari wa JKU kutoka nje ya jimbo hilo na wengine walioletwa kutoka Pemba walishiriki kupiga kura zao Bububu.

Tume ya uchaguzi nayo iliifanyia kazi ya wazi CCM ili ishinde. Msimamizi wa uchaguzi Bwana Suluhu pamoja na kufanya kazi kubwa ya matayarisho ya  kuuchafua uchaguzi kabla ya siku ya kupiga kura pia alifanya kazi nzuri siku ya kupiga kura kuhakikisha azma ya ushindi wa CCM wa lazima inafanikiwa. Suluhu alikuwa akiwafuatilia waandishi wa habari wote wanaofuatilia kwa umakini matukio ambayo ni ushahidi wa wazi juu ya kuvurugwa kwa uchaguzi huo. Kila aliponuikuta mimi binafsi kama mwadishi wa kujitegemea (Freelance Journalist) katika eneo lenye matukio ya uvunjifu wa taratibu za uchaguzi alinifokea na kuniambia maneno  ya kunivunja moyo na kunitaka niondoke katika eneo hilo. Maneno yake yalikuwa haya “wewe tunakujua umetumwa na nani lakini tutakukamata tu”, “nasema wewe tumekupa press card sio ukae katika milango ya kituo cha kupigia kura, mbona kule ambako kura inapigwa hukai?” Ikikumbukwa mapambano makubwa siku ya upigaji kura yalihamia katika mageti ambapo wafuasi wa CUF na waangalizi walijipanga kuwatambua wapiga kura mamluki na kuwazuia wasiingie kituoni. Katika maeneo haya ndio vita vyote vikubwa vilitokea. Bwana Suluhu pia alitishia kunipokonya press card kwa kunimbia “wewe nimeshakuonya mara nyingi sasa nitakupokonya press card yangu”.

Wapiga kura kura mamluki awali walianza kuingia mmoja mmoja na wawili wawili wakiwa peke yao kama raia wenzao jambo ambalo lilidhibitiwa na wafuasi wa CUF waliokuwepo umbali wa mita 200 kwa ajili hiyo. CUF wanafahamu kuwa wapiga kura hao wanavyo vipande vya kupigia kura vya bandia lakini hawakujali vipande bali walijali ukaazi wa mpiga kura katika jimbo la Bububu. Walifanya hivi wakifahamu tume ya uchaguzi tayari imeshaandikisha, imeshatengeneza vipande vingi feki na kuwapatia wana CCM kutoka nje ya jimbo la Bububu kuja kushiriki kupiga kura jimboni hapo wakiwemo askari wa JKU. Baadhi ya wapiga kura mamluki waliozuiwa kuingia kituoni walikimbia na kuondoka na waliojaribu kuleta ubishi walipewa vipigo na raia waliokuwa na hasira kuvurugiwa uchaguzi wa jimbo lao. Waangalizi wa uchaguzi kutoka CUF ambao ni wawakilishi, wabunge na mawaziri wa CUF walikagua kadi moja moja ya kupigia kura katika mageti ya kuingilia kituoni na waliobainika kuwazuia kuingia kituoni. Hata hivyo vikosi vya KMKM walikuja milangoni na kupambana na wawakilishi na wabunge wa CUF na kutumia nguvu za silaha zao kuwapitisha. Kila muda ulivyokuwa ukienda ndivyo mamluki wa kutosha walivyokosa nafasi ya kupenya na hivyo idadi yao kuwa ndogo.

Baada ya hali kuwa mbaya kwa CCM ndipo amri za wakubwa zilipotoka rasmi ili nguvu yeyote inayohitajika itumike lakini lazima CCM ishinde uchaguzi. Hapo ndipo hata waziri Mwinyihaji alipolazimika kujakatika vituo vya kuoigia kura kuja kuwapanga askari wake. Hapa ndipo askari wa JWTZ, polisi na JKU walipoanza kuwapa ulinzi wapiga kura mamluki na kuwaingiza vituoni. Walifyatua risasi na kupiga mabomu ili kuzuia jaribio lolote la wana CUF la kuwazuia mamluki hao. Watu wasiojulikana waliovaa nguo za kiraia na kufunika nyuso zao waliwasili katika eneo la uchaguzi na magari wakiwa bunduki mikononi wakiwafyatulia watu risasi ili wasithubutu kuendelea kuwazuia mamluki. Hakuna aliyefahamu hawa ni walinzi wa aina gani. Walifanana na vikosi vya Alshabab lakini baadae ilifahamika kuwa ni majanjawiri waliopewa mafunzo ya kiaskari ya kushambulia watu.

Kwa kua CCM haikutaka mambo haya yawe wazi basi ilijitahidi kuwatisha, kuwapiga na hata kufikia kutaka kuwaua waandishi wa habari. Mimi binafsi nilitaka kuuliwa na JWTZ na kuthubutu kutamka mble ya mawaziri wawili kama wangeniua. Nikiwa nikitokea kituo cha SUZA A kuelekea kituo cha SUZA B kuendelea nakazi yangu niliukuta gari ya JWTZ aina ya defender (2069 JW 97) imesimama pembeni ya kituo cha kupigia kura. Nyuma ya gari hiyo ilikuwepo gari nyengine ya JWTZ aina ya canter ikiwa imebeba wapiga kura mamluki wasiopungua 150.  Defender hiyo iliyokuwa na askari wa jeshi la JWTZ wenye silaha za kivita iliwaescot wapiga kura mamluki kwa nguvu za klijeshi kuwaingiza katika eneo la kupigia kura cha SUZA B. Gari hizo zilipaki mbele ya kituo cha NTRC cha SUZA pembeni ya chumba cha kupigia kura na kuwashusha mamluki katika eneo hilo. Nikiwa mwandishi wa habari nilisogea na kupiga picha. Majeshi hao waliniokea na kunitaka nisimame nilipo huku wakinikimbiza na silaha zo lakini nilinusurika kifo baada ya kukimbilia kwa kamanda mmoja wa polisi ambae alichukua dhima ya kunitetea akishirikiana waziri Nassor Ahmed Mazrui na waziri Abuubakar Khamis Bakari ambao wote wawili walikuwepo eneo la tukio. Si peke yangu mwandishi niliyenyanyaswa na vyombo ya dola, Mwandishi mwengine wa Channel 10, Munir Zakaria nae alifanywa chambo na askari wa JKU. Walimpiga na kuharibu vifaa vyake na gari lake. Kosa lake pia ni kurekodi matukio ya uvunjifu wa taratibu za uchaguzi huo.

Vijana ambao walikuwa eneo la mita 200 wakilinda kura zao kwa kuwabaini wapiga kura mamluki na vijana ambao walikuwa katika shughuli zao na wala hawahusiki na uchaguzi walikamatwa na askari wa JKU. Vijana hao Waliteswa wakati wa kukamatwa. Wapo walioingizwa ndani ya tawi la CCM karibu na kambi ya KMKM na kuteswa kwa mashirikiano kati ya janjawiri na askari wa KMKMK. Waliwekwa ndani ya kambi ya KMKM kuanzia kiasi cha saa 6 mchana mpaka saa 4 usiku. Wakiwa ndani ya kambi ya KMKMK waliteswa  na kiasi cha askari 50 wanawake na wanaume. Walivuliwa nguo, walipokonywa pesa na simu zao Askari mmoja wa KMKM alitoa uchi wake na kukojoa katika mwili wa kijana mmoja. Vijana hao Walipelekwa rumande kiasi cha saa 4 usiku wa Jumapili na kubaki humo mpaka asubuhi ya Jumanne walipopelekwa mahakamani. Wakuu wa vituo vya polisi walikoshikiliwa walipewa amri ya kutotoa dhamana. Katika mahakama ya Mwanakwerekwe walisomewa mashtaka ya kumchoma askari kisu na kufanya vurugu na uvunjifu wa amani. Pamoja na kutimiza masharti yote ya dhamana ambayo yalisimamiwa na CUF chini ya mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu Mhe Salim Bimani, askari wakereketwa waliwatia katika gari kwa jazba za kisiasa na kuwapeleka tena rumande. Baada ya chama kufuatilia kwa makamanda wa Polisi chama kilifanikiwa kuwatoa rumande vijana hao kiasi cha saa 10 jioni.

Mwinyihaji Makame, waziri ambae vikosi vya SMZ viko chini ya wizara yake alifika mwenyewe binafsi kituoni na kuwapanga askari wake wa JKU kufanya mashambulizi na uharamia. Alijaribu kuwanyanyasa baadhi ya makamanda wa polisi ambao hawakutaka kujiingiza katika vitendo vya kuvuruga uchaguzi huo. Mpiga camera wake alijaribu kuwapiga picha askari polisi ambao walijaribu kuleta mazingira ya utulivu katika vituo. Mwinyihaji akiwa katika kituo cha kupigia kura katika skuli ya Bububu alitjibishana maneno makali na mmoja wa makamanda wa jeshi la polisi pale mpiga kamera wake alipojaribu kumpga picha. Baadhi ya maneno aliyoyatoa Mwinyihaji ni haya “ala! wewe hunijui mimi? Mimi ni waziri ofisi ya Rais unanifanyia dharau? Jamani munamsikia askari huyu anavyonijibu, nyinyi ni mashahidi asije akanilaumu”. Kamanda alimkunja mpiga picha wa ofisi ya rais na kumjibu hivi waziri “mimi huwezi kunipiga picha bila ya ridhaa yangu, wewe ni waziri ala! Wale pale mawaziri wenzako (akimuonyesha Waziri Mazrui) mbona hawajaja kutufanyia dharau kama zako hapa? Mimi sikuogopi hata kidogo fanya unavyoweza kufanya”.

Huu katu haukuwa uchaguzi, ulikuwa ni uhuni wa wazi ambao sio umefanikiwa kuwadhihirishia wazanzibari tu bali ulimwengu mzima kwamba maridhiano na seriakali ya umoja wa kitaifa haikutakiwa na CCM, bali Amani Karume alilazimisha ndoa kwa kutumia mamlaka yake makubwa alokuwa nayo wakati ule akiwa rais. Maalim wakati akiwafariji wahanga wa unyanyasaji wa KMKM na polisi siku ya uchaguzi wa Bububu amesema: “huu si uchaguzi ni uhuni na ushenzi uliofanyika na kamwe hatuwezi kuukubali. Tumeingia katika maridhiano ili tusirejee mambo ya aina hii wenzetu wanaturejesha nyuma upya. Haya yote yalifanywa na kuandaliwa na tume ya uchaguzi. Tunamwambia Dr Shein ahadi yake aliyoichukua Bwawani anaivunja. Watu wanapigwa risasi tena eti kwa sababu lazima CCM ishinde. Hatukubali hatukubali. Kama CCM haitaki maridhiano potelea mbali na tugawane mbao turudi tulikotoka. Sisi CUF tunatulia sio kwa sababu ni wanyonge au hatuna nguvu ni kwa sababu tunataka amani. Hebu na tugamwane mbao turudi kule kule tuone kama CCM waitawala nchi hii”.

Mimi mwandishi wa makala hii natoa ushauri wangu kwa Dr Shein kama ana ukweli juu ya serikali ya umoja wa kitaifa achukue hatua za haraka na taratibu za kisheria dhidi ya wale wote walioandaa mazingira na kushiriki kuuvuruga uchaguzi wa Bububu. Taratibu za kisheria pia zifuatwe na ziheshimiwe kuuhoji uchaguzi huo batili ulioipa ushindi CCM na urejewe mara moja kwa mazingira yanayostahiki. Bila ya hivyo ni kuirejesha Zanzibar katika tanuri la moto ambalo kwa wakati huu hwenda likawa na kuli nyingi zaidi na moto wake ukawaka zaidi kuliko lilivyowahi kuwaka huko nyuma.


Advertisements

One thought on “Waliovuruga uchaguzi wa Bububu ni maadui wa Umoja wa Kitaifa

  1. Naona hii inaonesha wazi kwmba viongoz wetu wa nchi wameridhik na huu upotoshaji wa viongozi wachache ktk serikali! Mpak saiv hatujapat kusikia sauti ya raisi kusema angalau kitu chchote ili kukemea au kusapot hali km hii! Unajua mwisho wake ni hatar tupu inanyemelea! Na yakija matatizo hayachaguwi km huyu mwana cuf au ccm! Hebu tuamkeni jaman saiv si wakat wa kulumbana tena tujengeni nchi yetu ili ipate maendeleo. Sisi tukilumbana na kupigana watanganyika ndo wanavotak ili wazid kututawala.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s