Elimu ya Dini iimarishwe Madrasa – Maalim Seif

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Al-haj Maalim Seif Sharif Hamad amesema mafanikio yaliyopatikana katika chuo cha Madrasat Nuur Islamiya cha Ukutani Zanzibar ni neema kwa Wazanzibari wote na wanapaswa kuithamini na kuiendeleza neema hiyo.

Amesema Madrasa hiyo ina historia ndefu ya kutoa wanazuoni na wasomi mbali mbali wa dini ya kiislamu na kusambaa katika nchi tofauti duniani, ambao husaidia harakati za kuiendeleza dini ya kiislamu.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia katika mahafali ya 14 ya Madrasat Nuur Islamiyat ya ukutani yaliyofanyika Skuli ya Haile Sellassie mjini Zanzibar. Kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Othman Makungu na kushoto ni Mudir wa Madrasa hiyo ustadh Khalid Mohd Mrisho.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akihutubia katika mahafali ya 14 ya na Madrasa hiyo yaliyofanyika Skuli ya Haileselassie mjini Zanzibar.

Amesema madrasa hiyo ni chemchem ya elimu ya dini ya kiislamu kwa Zanzibar na Afrika Mashariki kwa ujumla, na imetoa wanazuoni wengi wanaotajikana duniani tangu kuanzishwa kwake na Marehemu Sheikh Abdallah Bakathir mwaka 1967.

Makamu wa Kwanza wa Rais amewapongeza walimu wa madrasa hiyo kwa kusimama kidete katika kuendeleza mema yaliyoachwa na muanzilishi wa madrasa hiyo na kuzitaka madrasa nyengine kuiga mfano huo katika kujenga jamii yenye maadili bora.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi zawadi kwa mwanafunzi bora wa madrasa hiyo (wanaume) ustadh Othman Omar Othman.

Katika hatua nyengine Maalim Seif ametoa wito kwa jamii kushirikiana katika malezi ya watoto ili kurejesha malezi bora ambayo kwa kiasi kikubwa yanaonekana kupotea, sambamba na kuwahimiza watoto kutafuta elimu bila ya kubagua elimu ya dini na ile ya dunia.

“ Mazoweya ya wenye nacho kuwasaidia wanaohitaji yamepotea, heshima ya watoto kwa wazazi na jamii kwa ujumla imepungua sana” alikumbusha Maalim Seif.

c. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi zawadi kwa mwanafunzi bora wa madrasa hiyo (wanawake) ustadhat Safia Abdalla Hamad.

Sambamba na hilo Maalim Seif amewataka wazazi na walezi kusimamia elimu ya mtoto wa kike kama ilivyo kwa watoto wa kiume, ili kusaidia kurejesha heshima na maendeleo kwa taifa.

“Kuna usemi kuwa unapomuelimisha mwanamke mmoja, unaelimisha jamii yote. Hivyo wazazi na walezi tujitahidi kuwaelimisha watoto wetu bila kubagua”, alisisitiza,

Katika risala ya wanafunzi hao iliyosomwa na mwanafunzi Abdulhalim Majid wamewaomba wazazi kuwa karibu zaidi na walimu, sambamba na kutoa kipaumbele kwa elimu ya akhera ambayo ni nuru katika maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Mapema akitoa nasaha zake kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mudiri wa madrasa hiyo ustadh Khalid Mohd Mrisho amesema lengo la kuandaa mahafali ni kuwashajiisha na kuwajengea ari zaidi wanafunzi, hali inayopelekea kuwa na ushindani mkubwa wa kimasomo.

Amefahamisha kuwa kwa sasa chuo hicho chenye wanafunzi 1300, kina mpango wa kuanzisha elimu ya Sekondari, ili kuwawezesha vijana kuielewa vyema dini yao, sambamba na kuwajengea uwezo katika masomo yao dunia.

Amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana lakini chuo hicho bado kinakabiliwa na matatizo ya ufinyu wa nafasi pamoja na vifaa vya kusomea vikiwemo kompyuta, hali inayowafanya kuchukua wanafunzi mara moja tu kwa mwaka.

Katika mahafali hayo Makamu wa Kwanza wa Rais ameahidi kuchangia shilingi milioni moja pamoja na komputa tatu kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya madrasa hiyo.

Mahafali hayo ya Madrasat Nuur Islamiya ya Ukutani Zanzibar, yamehudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo Jaji Mkuu Sheikh Omar Othman Makungu na Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Ngwali.

Hassan Hamad (OMKR).

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s