Tanzania daima acheni kuandika habari za “kupika” dhidi ya wenzenu wapinzani

Jana nimeshangazwa sana na kichwa cha habari cha gazeti linalomilikiwa na mhe. Freeman Mbowe(Tanzania Daima) kuwa wana taarifa kuwa Profesa Lipumba atakuwemo kwenye baraza la mawaziri la JK linalotegemewa kutangazwa hivi karibuni. Gazeti hili la propaganda za CHADEMA limekuwa likitumika ipasavyo katika mkakati maalum wa kuhakikisha CUF haiungwi mkono na watanzania.

Na hata habari husika imekuwa na malengo hayo hayo ya kuwafanya watanzania waamini kuwa CUF inafanya kazi bega kwa bega na CCM. Pamoja na kuwa mwandishi alimuuliza profesa Lipumba naye akashangazwa na habari hizo na mwandishi akaripoti upande wa Profesa Lipumba – ukweli unabakia kuwa lengo la kuiweka stori hiyo kama “lead story” ni mbinu tu za kuidhoofisha CUF. Mbona CUF ikifanya mkutano mkubwa Tabora stori hiyo haiwekwi mbele?

Kuna wakati fulani DR. SLAA aliwahi kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya CUF nami nikamjibu, Tanzania Daima wakanijia juu sana na kuandika stori ya kishabiki hadi unawashangaa. Mara zote ukiona Tanzania Daima inaitaja CUF ukurasa wa mbele maana yake ni kuwa kuna stori ya kutengenezwa na kupikwa inatangazwa kwa lengo la kuishughulikia CUF.

Unaweza kujiuliza maswali…..kwa nini mbowe hayumo kwenye baraza la Kikwete, Kwa nini Slaa hayumo? Kwa nini lipumba awemo kwenye baraza hilo? Stori zingine bwana…..wala hazisaidii ustawi wananchi. Tunatarajia gazeti la Tanzania Daima lisimamie propaganda za kuisaidia CHADEMA na siyo kuzua mambo ya uongo dhidi ya vyama vingine.

Mie natambua magazeti ya propaganda za vyama yapo, lakini “in a modern world” gazeti husika linapaswa kuendelea na kazi yake ya kuwadanganya wananchi kuwa chama ambacho gazeti linakiunga mkono ndiyo chama cha ukombozi wa kweli, gazeti hilo halianzi tu kuzua mambo yasiyokuwepo.

Uhuru na Tanzania daima ni magazeti ya propaganda, moja linamilikiwa na chama na lingine linamilikiwa na mwenye chama lakini yote yanafanya kazi moja, kutetea vyama husika kama ambavyo wahariri wameelekezwa(jambo hili siyo dhambi) – lakini uhuru na Tanzania Daima ni magazeti tofauti sana. Uhuru linamilikiwa na CCM na DOLA yake na linatetea wezi, wabadhirifu n.k. walioko ndani ya seikali na serikali yenyewe na linazua mambo ya uongo kila kukicha ili mradi serikali “MFU” ya CCM iendelee kupigiwa kura lakini Tanzania Daima linamilikiwa na mpinzani, unategemea alitumie gazeti lake kutangaza chama chake na kupambana na hoja za chama kilichoshindwa kuongoza dola (CCM).

Sasa unapokuta tena Tanzania daima, gazeti la mpinzani limeacha kazi ya kupambana na CCM linaanza ati kupika stori ili wananchi wasiwe na imani na viongozi wa vyama vingine vya upinzani na kuanza kupambana vyama vya upinzani vingine nadhani siyo busara. Hizi kazi za mambo ya kuzua, mambo ya udaku zinapaswa kufanya na magazeti pendwa, ambayo hayajihusishi sana na nani kaiba nini bali yanajihusisha na nani kanunua nini(hata kama fedha alizotumia ni za wizi). Tanzania Daima ni gazeti linaloheshimika pamoja na kusimamia propaganda za CHADEMA, lisianze kutumika kufanya kazi za kudhoofisha vyama vingine kimakusudi……tukumbuke muosha….huoshwa….

Na kuna wakati niliona kwenye “wall” ya rafiki yangu “Zitto Kabwe” akilalamika kuwa gazeti la mwenyekiti wake wa chama(Tanzania daima) linamchafua zitto kwa maslahi ya mwenyekiti wa chama chake. Nadhani wahariri wa Tanzania Daima wanapaswa kujipanga sana, kama kazi ya gazeti ni kupambana na kuhakikisha CHADEMA inaingia ikulu mliache lifanye kazi hiyo nanyi jijengeeni “status” kubwa mliyonayo, lakini mkiacha gazeti mnalolilihariri litumike kuzua mambo yasiyokuwepo dhidi ya kina Zitto Kabwe kwa maslahi ya Mbowe au mambo yasiyokuwepo dhidi ya Lipumba na CUF kwa maslahi ya CHADEMA Na viongozi wake kwa kweli hamtafanikiwa sana.

Bahati nzuri wahariri wote wa Tanzania daima ni weledi mno katika tasnia ya habari, Absalom Kibanda, Ansbert Ngurumo- Ni watu mnaoaminika mno na jamii, labda nyie hamjitambui. Chukueni jukumu la kuhakikisha Tanzania Daima inaendeleza propaganda za kumuwezesha mbowe na chama chake kufika Ikulu nasi CUF kama tuna magazeti ya kutusaidia kufika Ikulu yaendelee kufanya hivyo lakini tusiendelee na huu mchezo wa kushughulikiana kwa mambo ambayo hayapo kabisa, mambo ya kufikirika mno.

Lipumba hawezi na hataweza kufanya kazi chini ya serikali iliyoshindwa ya KIKWETE labda leo hii watanzania wapige kura na kuamua kuwa Lipumba kasaidie serikali. Tunapoongelea hizi serikali za pamoja hatuna maana kuwa CUF inaingia tu serikalini. Wenzetu Zanzibar waliamua kwa masanduku ya kura kutaka serikali ya pamoja. Lipumba na CUF hawawezi kutumika chini ya serikali ya Kikwete bila ridhaa ya watanzania, CUF tunafanya na tunaamini katika mambo yanayoamuliwa na wananchi wenyewe – kama tulivyofanya Zanzibar.

Sisi kama chama cha siasa tuna vyanzo vya habari vya kutosha kutoka serikalini na kwingineko, kutoka usalama wa taifa, ikulu na kila mahali. Hakuna wazo wala azimio lililofikiwa mahali popote wala kutolewa – iwe ikulu, usalama wa taifa na kwingineko kuwa ati Lipumba aingizwe kwenye baraza la mawaziri na wala hakuna mtu yeyote amewahi kumpigia Lipumba kumjuza juu ya suala hili.

Stori ya Tanzania daima ya jana ni ya kutengeneza na kupika kwa maslahi ya watu ambao mimi na wewe hatuwajui. Gazeti hili linaheshimika na kufahamika, liache kujidogoesha kwa kupika stori ili liuze nakala, andikeni vitu “real” na mtauza nakala bila mashaka yoyote.

Julius Mtatiro,
National Deputy Secretary General,
The Civic United Front – CUF Chama Cha Wananchi,
P.O BOX 10979,
+255(717) (787) 536 759 – juliusmtatiro@yahoo.com.
Dar es Salaam – Tanzania.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s