Maalim Seif ‘aitikisa’ Tanga

  • Ataka wanachama wasikubali kuyumbishwa
  • Asema Tanga ni ngome ya CUF ambayo haiwezi kubomoka

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia katika mkutano wa hadhara kata ya Msambweni, Tanga.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wanachama na wapenzi wa Chama hicho katika Mkoa wa Tanga kuacha kuyumbishwa kwa mambo yasiyokuwa na msingi, na badala yake waungane katika kikiimarisha Chama hicho. Amesema Chama hicho kiko imara na kitaendelea kuimarika kutokana na uwezo wa viongozi wake ambao wamepata sifa kubwa duniani kutokana na umahiri wao wa masuala ya uchumi na siasa.

Maalim Seif ametoa changamoto hiyo katika eneo la Msambweni Tanga wakati akiwahutubia maelfu ya wanachana na wapenzi wa Chama hicho waliojitokeza kwa ajili ya kumsikiliza na kujua mwelekeo wa Chama hicho baada ya kupata misukosuko ya kuwatimua baadhi ya viongozi wake.

Amesema Chama hicho siku zote kimekuwa mstari wa mbele katika kusimamia misingi ya haki na usawa kwa wananchi wote, na kwamba hakitosita kufanya hivyo kwa kuangalia maslahi ya mtu binafsi.

Maalim Seif amewapongeza wananchi wa Tanga kwa kumpa mapokezi makubwa wakati akipowasili katika uwanja wa ndege wa Tanga, hali inayodhirisha uhai wa chama hicho katika mkoa huo na maeneo mbali mbali Tanzania bara na Visiwani.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, akionesha tunzo maalum aliyokabidhiwa na wazee wa Tanga kutoka na mchango wake kwa amani ya Zanzibar.

Amesema mapokezi yake ambayo yanathibitisha kuwa Tanga ni ngome ya CUF ambayo haiwezi kubomoka, na yale ya Prof. Lipumba yaliyofanyika Dar es Salaam tarehe 11 Machi 2012 yatakuwa dira ya kukiimarisha zaidi chama hicho na kasi hiyo itaendelezwa hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Maalim Seif amewakebehi wanaodai kuwa CUF ni CCM ‘B’ kwamba “wana wivu wa kisiasa” na wanaumwa na maendeleo ya chama hicho, na kuweka wazi kuwa CCM na CUF havijaungana na wala havitoungana ikizingatiwa kuwa kila chama kina sera zake.

Akiwasilisha salamu za Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, kwa wakaazi wa mkoa wa Tanga amewataka kusimama imara na kujipanga katika kutoa maoni ya katiba mpya ili kuhakikisha kuwa katiba inaweka wazi suala la maliasili kuwa rasilimali za Watanzania.

Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na maliasili nyingi zikiwemo dhahabu, almasi, Tanzanite, shaba na madini mengine kadhaa, lakini bado rasilimali hizo hazijawanufaisha wananchi kutokana na kutokuwepo utaratibu unaoeleweka juu ya mgawano wa rasilimali hizo.

Amesema Watanzania wanaweza kunufaika moja kwa moja na mgawano wa rasilimali hizo, hali ambayo itapunguza utegemezi wa chakula, mfumko wa bei na kupunguza umaskini kwa wananchi.

Katika salamu hizo Maalim Seif amesema Tanzania inahitaji uongozi wenye dira ya kuikomboa Tanzania kiuchumi, kwa kuweka mipango imara ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu na kuvutia wawekezaji wa sekta mbali mbali, jambo ambalo limekosekana kwa kipindi kirefu.

Katika mkutano huo Maalim Seif alikabidhiwa tunzo maalum kutoka kwa wazee wa Tanga kutokana na ujasiri wake wa kurejesha Amani Zanzibar.

Mkutano huo ulikwenda sambamba na kumtambulisha na kumnadi mgombea wa udiwani wa chama hicho kata ya Msambweni,  Abrahman Hassan Omar, ambapo amewataka wanachama kumchagua mgombea huyo ili aweze kusaidia kuwatatulia kero zao.

Nae mgombea udiwani wa CUF kata ya Msambweni,  Abrahman Hassan Omar, amesema haombi uongozi ili apate kuwa bwana mkubwa bali kuwatumikia wananchi wakati wote.

Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama hicho, Sheweji Mketo, amewatahadharisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya tarehe 1 Aprili 2012, huku akiwataka wananchi wasishawishike kwa chochote na waelewe kuwa siku hiyo itakuwa “April Fool”.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s