Ujerumani yaahidi kushirikiana na Zanzibar katika nyanja mbali mbali za Kiuchumi

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Bw. Klaus Peter Brandes alipofika ofisi kwake Migombani kwa ajili ya kubadilishana mawazo juu ya uhusiano wa Ujerumani na Zanzibar.

Ujerumani imeahidi kuendeleza ushirikiano wake na Zanzibar katika nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo kuendelea kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Zanzibar. Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Bw. Klaus Peter Brandes amesema nchi yake inajivunia uhusiano mzuri uliopo katika yake na Zanzibar, hali ambayo imeiwezesha nchi hiyo kufanya shughuli zake hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za afya katika hospitali, sambamba na kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka nchini ujerumani. Balozi Brandes ameeleza hayo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko ofisini kwake migombani. Katika hatua nyengine balozi Brandes ameiomba Zanzibar kuweka mikakati imara ya kukabiliana na tatizo la uharamia katika mwambao wa bahari ya hindi, ili kuondoa vikwazo vya kibiashara vinavyosababishwa na maharamia wa kisomali, hali ambayo pia inazorotesha shughuli za kiuchumi.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Bw. Klaus Peter Brandes mara baada ya mazungumzo ya viongozi hao huko Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Migombani mjini Zanzibar.

Nae Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad amesema tatizo la uharamia katika pwani ya Afrika Mashariki limekuwa likitishia shughuli za kibiashara na kuchangia kuongezeka kwa bei za bidhaa mbali mbali zikiwemo za vyakula. Amesema Zanzibar inalichukulia suala hilo kama changamoto kubwa kwa serikali, na kuiomba Ujerumani kusaidia juhudi za serikali katika kupambana na vitendo vya uharamia ikiwa ni pamoja na kusaidia kutoa mafunzo na mbinu bora za kukabiliana na vitendo hivyo kwa vikosi vya ulinzi. Wakati huo huo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alikutana na balozi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) nchini Tanzania Bw. Filiberto Ceriani Sebregondi na kuelezea mafanikio ya serikali ya umoja wa kitaifa hapa Zanzibar tangu kuanzishwa kwake mwaka mmoja uliopita. Amesema tangu kufikiwa kwa makubaliano hayo, mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuwepo amani na utulivu, sambamba na kurejesha mshikamano miongoni kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba. Amefahamisha kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na nia njema ya waanzilishi wa maridhiano pamoja na viongozi waliopo madarakani. Amesema kwa serikali inaimarisha uchumi wa nchi kwa kuendeleza shughuli mbali mbali za kiuchumi zikiwemo kilimo cha umwagiliaji ili kujiandaa kupunguza utegemezi wa kuagizia chakula kutoka nje.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) nchini Tanzania Bw. Filiberto Ceriani Sebregondi alipofika ofisini kwake Migombani jana. (Picha: Salimn Said, OMKR).

Maalim Seif ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya kuja kuwekeza miradi mbali mbali hapa nchini ikiwemo ya uvuvi na viwanda vidogo vidogo. Kwa upande wake, Balozi huyo wa Jumuiya ya Ulaya Tanzania Bw. Filiberto Ceriani Sebregondi, amesema katika kukuza mashiriano kati yake na Zanzibar, Jumuiya hiyo itaendelea kuunga mkono shughuli za kijamii pamoja na kuwajengea uwezo wananchi wa Zanzibar juu ya kuendeleza miradi ya kiuchumi. Amesema katika mipango yake, Jumuiya hiyo inakusudia kuzisaidia nchi zinazoendelea ikiwemo Zanzibar kwa kuangalia maeneo muhimu yaliyoainishwa na nchi hizo, sambamba na kuhimiza matumizi bora ya rasilimali za nchi husika. _________________________________________________________________

Chanzo;

Hassan Hamad (OMKR).

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s