Rushwa lazima idhibitiwe- Maalim Seif

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na wajumbe kutoka nchi mbali mbali zinazojitathmini kiutawala bora Afrika kupitia mpango wa APRM waliofika ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kujadiliana nae. Wa pili kulia ni kiongozi wa ujumbe huo Akere T. Muna kutoka nchini Cameroon

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar inajiandaa kuanzisha Mamlaka madhubiti ya kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa, ikiwa ni hatua muafaka ya kukomesha vitendo hivyo vinavyodumaza dhana ya utawala Bora katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Maalim Seif alisema hatua hiyo inachukuliwa baada ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kupitisha mswada wa sheria ya kupambana na vitendo vya rushwa, vitendo ambavyo kwa kiasi kikubwa vinasababisha watu wengi kukosa haki zao pamoja na kuzorotesha maendeleo na uchumi wa nchi.

Alisema hayo huko ofisini kwake Migombani Zanzibar, alipokuwa na mazungumzo na ujumbe unaojumuisha watu kutoka nchi mbali mbali Barani Afrika, unaofanyia tathmni ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika (APRM) kwa upande wa Tanzania.

Maalim Seif alisema vitendo vya rushwa vipo Zanzibar katika sekta tafauti, lakini malalamiko mengi ya wananchi hivi sasa yanaelekezwa katika taasisi za kutoa haki kwa raia, zikiwemo mamlaka zinazosimamia ardhi, polisi na mahakama, hivyo ni wajibu wa serikali kuandaa mikakati ya kudhibiti tabia hiyo.

“Tunakusudia Zanzibar tuwe na Mamlaka ya kudhibiti rushwa yenye meno, tayari wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepitisha mswada wa sheria ya kudhiti rushwa, hatua inayofuata ni kuanzisha mamlaka hiyo, ambayo itafanya kazi kwa ufanisi”, alisema Maalim Seif.

Akizungumzia hali ya ukuzaji uchumi Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais alisema wananchi pamoja na wawekezaji wa ndani na kutoka nje, hivi sasa wanaitumia ipasavyo fursa iliyopo ya kuwepo hali amani na utulivu kuwekeza kiuchumi na kukuza maendeleo.

Maalim Seif alisema watu mbali mbali wamevutika na miradi kadhaa ya uwekezaji imefunguliwa na wawekezaji wengi wamevitika katika sekta ya utalii, kutokana na mandhari nzuri ya visiwa vya Unguja na Pemba, ikiwemo fukwe na utajiri wa historia yake.

Hata hivyo, alisema milango imefunguliwa katika sekta mbali mbali za uwekezaji, ikiwemo ya ujenzi wa miundo mbinu, uvuvi, kilimo pamoja na na sekta ya uzalishaji nishati ya umeme.

Alieleza, Zanzibar inahitaji sana wawekezaji katika sekta ya ujenzi na miundo mbinu kutokana na azma yake ya kujenga bandari mpya na ya kisasa, ambayo itakuwa kiungo muhimu katika eneo la Afrika Mashariki na Kati pamoja na kuendelea na juhudi zake za kupanua uwanja wake wa ndege, ili kuongeza fursa za kiuchumi zitokanazo na sekta hiyo.

Maalim Seif alisema serikali zinajitahidi kujadili na kuzipatia ufumbuzi kero mbali mbali za Muungano, licha ya kero nyingi bado kuendelea kujitokeza, ikiwemo katika masuala ya kifedha na maliasili.

Akijibu maswali aliyokuwa akiulizwa na wajumbe hao, alisema miongoni mwa yaliyopatiwa ufumbuzi ni kero kubwa iliyokuwa ikilalamikiwa na Zanzibar juu ya wafanyabiashara kutoka upande huo biashara kutoka Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, pale wanapopeleka bidhaa zao Tanzania Bara.

Alieleza kwamba miongoni mwa mambo yanayohitaji kushughulikiwa kwa haraka na pande mbili hizo ni suala la mafuta na gesi asilia, ambapo licha ya katiba kulieleza kuwa ni la Muungano, Zanzibar inaona suala hilo halipaswi kuwa la Muungano.

Alitaja maeneo mengine yanopewa umuhimu mkubwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa ni kukuza hali za wanawake kiuchumi na kupiga vita tabia ya ukatili na udhalilishwaji dhidi yao pamoja na watoto.

Alipongeza hatua ya kufanyiwa tathmini ya kina masuala ya utawala bora, kwa vile yanagusa mambo muhimu kwa wananchi, ikiwemo kisiasa, kiuchumi na maendeleo yao na kwamba serikali ya Mapinduzi Zanzibar itafarajika sana pale ripoti ya wataalamu hao itakapotolewa.

Maalim Seif alisema hiyo itakuwa fursa ya kipekee kwa Zanzibar kuifanyia kazi ripoti hiyo kwa kujikosoa, pale itakapoanishwa kuna kasoro, lakini pia kuendeleza yale yatakayo bainika kuwa ni mazuri na yenye faida kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Kiongozi wa ujumbe huo, Barriseter Akere T. Muna kutoka Cameroon alimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa ripoti yao itatolewa kwa nchi husika baada ya kumaliza tathmini yao, ili kuona mapungufu yao na maeneo waliyoweza kufanya vizuri katika dhana ya kudumisha utawala bora.

Habari na Hassan Hamad,

Picha na Salmin Said (OMKR).

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s