Hotuba ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa hali ya siasa Zanzibar huko Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar – tarehe 13, februari, 2012

Mheshimiwa Mwenyekiti wa mkutano,

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala,

Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na serikali ya Mapinduzi Zanzibar,

Waheshimiwa Wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,

Waheshimiwa Mabalozi na Wana Diplomasia,

Waheshimiwa waalikwa wote, Mabibi na Mabwana.

Assalam Alaykum
Kwanza kabisa sinabudi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwa wazima wa afya nakuweza kukutana hapa leo kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya siasa na maendeleo ya nchi yetu. Tumshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kutuwezesha kufika salama katika ukumbi huu, hasa kwa vile miongoni mwetu wamo waliotoka mbali, kuja kujumuika nasi katika mkutano huu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kuufanya mkutano wetu huu na kumaliza kwa salama na amani na kile kitakachozungumzwa kiwe ni kwa manufaa na chenye maslahi kwa nchi yetu na watu wake. AMIN.

Kwangu mimi binafsi najiona ni mwenye bahati kubwa kwa kualikwa hapa Hoteli ya Bwawani kufungua rasmi mkutano ulioandaliwa kujadili kwa kina `Hali ya Siasa Zanzibar’, ambapo mada kuu ni UIMARISHAJI WA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR.

Nimeambiwa kwamba huu ni mkutano wa pili wa namna hii kuitishwa. Ninawapongeza waandaaji wa mkutano huu, yaani Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa kutualika sote kwa mara nyingine tena, kuja hapa kujadiliana kuhusu masuala muhimu yanayohusu siasa hapa Zanzibar. Napenda pia kuwashukuru waandaaji kwa kutenganisha sehemu mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusiana na mikutano hii ya hali ya siasa kwa sababu kwa muda mrefu kulikuwa na mkutano mmoja tu kwa ajili ya Tanzania nzima.

Kutokana na kuanzishwa kwa utaratibu huu wa sasa, Zanzibar ina nafasi kubwa ya kuangalia na kujadili siasa zake kama Zanzibar, jambo ambalo naamini litaleta manufaa zaidi kwa siasa katika visiwa vyetu. Katika kuthibitisha hilo, hata mada kuu ya mkutano wa mwaka huu ambayo ni “Uimarishaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar”, inalenga zaidi kupata mawazo na michango itakayozidi kuleta ufanisi katika utendaji wa serikali yetu, tukumbuke pia mafanikio ya Zanzibar ni maslahi ya Watanzania wote.

Kwa mtazamo wangu, Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ni imara. Mada ijikite katika kuimarisha zaidi mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hivyo naamini katika siku mbili hizi za mkutano huu, wajumbe watapata nafasi ya kuangalia, kurejea na kupendekeza namna ya kuufanya mfumo huo uwe madhubuti zaidi na kupendekeza pia jinsi ya kuendesha siasa hapa Zanzibar kwa manufaa ya wananchi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti,
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar imetokana na matakwa ya wananchi wenyewe wa visiwa hivi, baada ya kuona mfumo uliopita yaani mfumo tenganishi hauna faida kubwa katika kujenga umoja na kukuza maendeleo ya Wazanzibari. Na kama ilivyo katika mataifa mengine, mfumo wowote mpya unapoanzishwa huwa unakuja na changamoto mbali mbali,hivyo kuhitajika marekebisho ya hapa na pale, ili kuufanya uweze kufanikisha malengo yaliyokusudiwa tangu mwanzo. Uzuri ni kwamba Zanzibar ina fursa nzuri ya kuweza kujifunza kupitia sehemu nyingine za dunia, ambazozina serikali zenye mfumo wa aina hii.

Vile vile ni jambo la kutia moyo sana, kwetu sisi Wazanzibari, Watanzani na hata jumuiya ya Kimataifa kuona kwamba hapa Zanzibar katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa serikali shirikishi tunashuhudia faida nyingi. Faida kubwa moja wapo ni maelewano makubwa miongoni mwa wananchi wa Zanzibar. Sote ni mashahidi kwamba, kabla ya kuja kwa utaratibu huu tulikosa kuwa na maelewano, hali iliyokuwa imesababishwa kwa kiasi kikubwa na kutafautiana kwetu katika itikadi za kisiasa na kukosa mashauri ya pamoja katika kuendesha nchi yetu na kujiletea maendeleo.

Katika Zanzibar iliyo chini ya mfumo wa serikali shirikishi tunashuhudia wananchi wenye itikadi tafauti pamoja na viongozi wao, wakikaa pamoja wakishirikiana katika kila uwanja wa maisha na zaidi katika mambo ya kuwaletea maendeleo yao. Sina budi kukiri kwamba changamoto za hapa na pale zinatokea na hazitaacha kutokea, lakini kutokana na utaratibu tuliojiwekea kuweka maslahi ya wananchi wetu mbele, changamoto zinapojitokeza tunakaa pamoja kuzijadili na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka.

Viongozi na watendaji wa REDET, na takriban wajumbe wengi ninaowaona katika mkutano huu, nyote ni mashahidi juu ya hali ilivyokuwa Zanzibar, ambapo maelewano kama haya tunayo yazungumzia hii leo, ikiwemo watu kutoka vyama tafauti vya kisiasa kupanga mambo yao kwa pamoja na kujadiliana mustakabali wa Zanzibar na baadaye kutoa maamuzi yaliyojikita katika kuendeleza nchi na wananchi wote haikuwa rahisi. Kwa niaba yangu na serikali ya Mapinduzi Zanzibar nakupongezeni kwa dhati kwa namna mlivyoshirikiana na mnavyoendelea kushirikiana nasi na kutupa ushauri katika hatua zote, hadi kufikia hapa tulipo. Nakuombeni msichoke na muendeleze moyo huo huo, na mzidi kushirikiana nasi katika mambo haya yenye maslahi kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti na washiriki wa mkutano,
Mada kuu ya mkutano huu ni Hali ya Siasa Zanzibar, hivyo ni vyema nigusie japo kidogo yale yanayohusu mada hiyo.

Siasa ya Zanzibar inajumuisha mlolongo wa mambo mengi na kuweza kuizungumzia kwa kina na ufasaha inahitaji muda mwingi, na sio katika wasaa mdogo kama huu wa ufunguzi wa mkutano. Hata hivyo kwa kugusia japo kidogo nina imani kuwa sote tunakumbuka kwamba, baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010, Zanzibar iliunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kuundwa kwa serikali hiyo kulitokana na mabadiliko ya katiba yaliyoruhusu utaratibu huo mpya kutokana na kura ya maoni iliyopigwa tarehe 31 Julai 2010 kuamua iwapo tuwe na serikali ya namna hiyo au la.
Maamuzi hayo ya busara yalitokana na historia yetu ambayo imekuwa na matukio yasiyopendeza ya kuwa jamii yetu imegawika katika misingi ya kiitikadi na siasa za chuki, ushindani wa kisiasa usiokuwa na tija kwa wananchi wetu, na kutoaminiana baina ya watu wa pande zilizokuwa zinasigana. Hali hiyo ilikuwa ni ya kutisha ukiangalia tulikotoka kama jamii moja na sasa siasa zikaishia kututenganisha na kutufanya mahasimu. Ni dhahiri kuwa wananchi walio wengi walishachoshwa na hali hiyo. Hivyo wananchi walipotakiwa kufanya uamuzi kupitia kura ya maoni juu ya mfumo wa Serikali kuwa shirikishi au tenganishi thuluthi mbili walichagua mfumo shirikishi.

Hali hiyo imesababisha kwa sasa tuwe na maridhiano ambayo yameleta mafanikio kuliko ilivyokuwa kwa Muafaka I na II. Jambo la kupendeza zaidi ni kuwa maridhiano haya yalifanyika baina yetu sisi wenyewe bila shinikizo la nje. Sisi wenyewe Wazanzibari, Watanzania wenzetu wengi na Jumuia ya Kimataifa tumeridhika na utulivu tunaoushuhudia. Kabla ya maamuzi hayo hali ya siasa iliyokuwepo ilifanya shughuli nyingi za kiuchumi kwenda kwa kusuasua, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa jamii kwa ujumla.
Lakini sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa badala ya kupoteza muda mwingi kushughulikia kutatua migogoro, muda karibu wote unatumiwa kufikiria, kubuni na kupanga mipango ya maendeleo itakayo wanufaisha wananchi. Wawekezaji wa ndani na wa nje wamevutiwa na hali hiyo na wamo katika mazungumzo na taasisi husika kuwekeza nchini Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti na wajumbe wa mkutano,
Hayo yaliyotokea huko nyuma kabla ya kufikiwa kwa Maridhiano ya Wanzibari yaliendelea kutokea ingawa juhudi kubwa zilishafanywa na zilikuwa zinafanywa zilizolenga kuupatia suluhu ya kudumu mgogoro wa kisiasa Zanzibar. Zipo hatua zilizochukuliwa na serikali zote mbili, ile ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar kwa nia ya kufanikisha azma hiyo. Kwa bahati mbaya, matokeo yake hayakuwa mazuri kama ilivyotarajiwa jambo lililopelekea kujitokeza haja ya kuendeleza kazi hiyo, hadi leo hii ambapo tayari tunaSerikali ya Umoja wa Kitaifa.

Historia fupi ya Zanzibar inaonesha kuwa wakati wa kupigania uhuru palikuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa ambao uliwatenganisha wananchi katika makundi mawili makuu, kila kundi likiunga mkono chama au muungano wa vyama. Baada ya Mapinduzi ya Januari 1964, tukaingia katika mfumo wa chama kimoja cha siasa ambacho kiliendana na dhana ya chama kushika khatamu, yaani kuwa ndio chombo chenye maamuzi ya mwisho.

Mfumo huo uliendelea kwa takriban miaka ishirini na minane (1964 – 1992). Mwaka 1992 tukaingia katika mfumo wa vyama vingi. Kwa Zanzibar mfumo huu ulipelekea kuwepo kwa vyama viwili vikubwa vya siasa vyenye kulingana kwa kuungwa mkono na wananchi. Misuguano na mikwaruzano iliyokuwepo kabla ya Mapinduzi ikajirudia, saisa ikawa imejengeka juu ya utamaduni wa malumbano, chuki na hasama baina ya wafuasi wa vyama hivyo viwili vya CCM na CUF.
Hali ya mivutano ilikithiri hasa wakati wa uchaguzi hadi kupelekea watu kupoteza maisha, mali kuharibiwa na hata kwa mara ya kwanza Tanzania kuzalisha wakimbizi. Ndio maana juhudi hazikusita kuchukuliwa ili kuiepusha nchi na hasara zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti,
Chaguzi zilizofanyika baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ziligubikwa na kushutumiana kutokana na Tume zilizosimamia chaguzi hizo kutokuwa na uwazi wa kuridhisha. Kulijitokeza kasoro za wazi katika uandikishaji wa wapiga kura, uendeshaji wa mikutano ya kampeni, majaku katika kuhesabu kura na kutangaza matokeo. Hivyo basi Serikali ya Mapinduzibaada ya mashauriano na vyama vya CCM na CUF kupitia mazungumzo yaliyozaa miafaka miwili ya 1999 na 2001 ilichukua hatua zilizokusudiwa kusawazisha kasoro hizo.

Miongoni mwa hatua hizo ni ile ya kuanzishwa kwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (PVR). Sio kwamba kuwepo kwa Daftari kumemaliza matatizo yote ya wananchi wote kupata haki ya kupiga kura kwani bado malalamiko mengi yapo. Hata hivyo, naamini hii ni hatua muhimu ya kuelekea tunakokusudia na kuhakikisha kila Mzanzibari anapata haki yake ya kuiweka madarakani Serikali anayoiona itaweza kumsaidia kupambana na matatizo yake ya kimaisha.

Uchaguzi wa 2010 ulionesha maendeleo makubwa katika uwanja wa kampeni, vyama vyote vilitumia haki yao ya kufanya kampeni bila ya vizingiti. Kampeni zilikuwa za kiungwana. Pamoja na kuwa na hamasa, lakini kwa kiasi kikubwa hapakuwepo na malumbano, matusi wala kushambuliana. Kila mgombea na chama chake alijikita katika kutetea sera na ilani ya uchaguzi ya chama chake na kujenga hoja za kuwashawishi wananchi watoe kura zao kwa mgombea na chama chake.

Hata katika siku ya kupiga kura kama mizengwe ilikuwepo ilikuwa michache. Uhesabuji wa kura ulifanyika vituoni. Pengine shaka ilikuwepo katika sehemu za kujumuisha kura na kutangaza matokeo. Walijitokeza maafisa wa ZEC wachache waliojaribu kuchakachua matokeo. Pale mawakala wa vyama walipokuwa macho na kugundua hila hizo, taarifa zilitolewa kwa Tume ya Uchaguzi Makao Makuu na baadhi ya maafisa wa ZEC waliohusika walichukuliwa hatua papo hapo. Haya ni maendeleo mazuri na ni wajibu wote sote kuyaendeleza na kuyafanya kuwa bora zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti,
Eneo jengine ambalo limepata maendeleo ni uwakilishwaji wa wanawake katika vikao vya kufanya maamuzi na katika ngazi za juu za utendaji serikalini, katika Baraza la Wawakilishi, Bungeni, Mabaraza ya Miji na Halmashauri za Wilaya, uwakilishi wa wanawake umefikia au kupindukia asilimia thelathini (30%).Lengo ni kufikia malengo ya SADC ambapo uwakilishi wa wanawake unatakiwa usipingue asilimia khamsini (50%) katika Mabaraza ya Kutunga Sheria. Leo katika Zanzibar yetu kuna wanawake ambao ni Mawaziri, kuna Makatibu Wakuu wa Wizara, kuna wanawake wanaoongoza taasisi muhimu za serikali kama CAG na kadhalika. Ni nia ya Serikali ya Mapinduzikuwashirikisha wanawake wengi zaidi katika nyadhifa za uongozi wa nchi. Na hili linafanyika sio kwa upendeleo wa jinsia, bali kutokana na uwezo wa wanawake wenyewe.

Eneo jengine, ni kuruhusu vyombo huru vya habari. Hii ni moja ya sifa za nchi ambazo demokrasia inashamiri. Vyombo vya habari vimekuwa vikielezwa kuwa ni mhimili wa nne wa dola kutokana na umuhimu wake katika masuala ya kuwaelimisha wananchi kufahamu haki zao kupata taarifa na kusimamia uwajibikaji wa serikali. Ukweli na uwazi, vyote vikiwa ni vigezo muhimu vya viwango vya maendeleo vyombo vya habari vinawajibika kuvizingatia. Kwa mfano wakati wa chaguzi, vyombo vya habari huviunganisha vyama vya siasa na wagombea wake kwa upande mmoja na wapiga kura wao kwa upande mwingine. Aidha, hutumika pia kama jukwaa la kutangazia sera na ilani za vyama vya siasa, kwa kusaidia waangalizi wa chaguzi kufuatilia hali ya kampeni inavyokwenda pamoja na kutoa nafasi kwa wananchi kuwapima wagombea, sera na ahadi za vyama na hivyo kuwawezesha kufanya maamuzi kwa busara.

La tano, Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu miaka ya 1990, nchi yetu imekuwa ikiondoa vikwazo visivyokuwa vya lazima katika nyanja ya Asasi za Kiraia. Asasi hizi kwa sasa zinafanya kazi kwa uhuru mkubwa na zimekuwa zikichangia kwa namna moja au nyingine katika maendeleo ya wananchi wetu. Haki ya kuunda na kujiunga na vyama vya kiraia ni kiashiria kuwa mfumo uliopo wa kisiasa unafuata njia sahihi ya kuelekea kwenye demokrasia.

Mheshimiwa Mwenyekiti
Mara nyingi asasi hizi za kiraia katika jamii zinaundwa ili kushughulikia matatizo ya kawaida, vipaumbele vya kikundi, maadili na tamaduni. Juhudi zitokanazo na ushirikiano wao zinaweza kusaidia katika shughuli mbalimbali. Asasi hizi zimefanya kazi nyingi ikiwa ni pamoja na zile zinazohusu mchakato wa kujenga demokrasia nchini, hasa kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika michakato ya kisiasa na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Tafiti zimeonesha kuwa migogoro mingi baina ya dola na asasi za kiraia, chanzo cheke ni pale asasi zinapoona au kudhani kuwa wadau wao wanatengwa katika michakato ya ufanyaji maamuzi, na hasa maamuzi yale yanayoathiri ustawi wa maisha ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti na wajumbe wa mkutano
Kwa kifupi lengo kuu la juhudi zote hizo ni kuifanya Zanzibar kuwa ni nchi iliyopiga hatua kubwa katika kukuza demokrasia, kuheshimu haki za binaadamu na kujenga misingi ya utawala bora. Kwa maneno mengine kuiwezesha nchi yetu kuwa na,

1. Kiwango cha juu cha Demokrasia.
2. Serikali yenye mihimili mitatu inayofanya kazi zake kwa uhuru na kila mmoja kuhakikisha muhimili mwengine hauvuki mipaka yake (cheks and balances).
3. Wananchi wenye uelewa mkubwa, iliwaweze kushiriki katika kujadili na kufanya maamuzi juu ya mambo yao kwa maslahi yao na kwa nchi yao.
4. Haki za binaadamu zinaheshimiwa, zinalindwa na kuendelezwa.
5. Vyombo vya habari vinafanya kazi kwa uhuru, lakini kwa kuzingatia weledi na maadili yao.
6. Uhuru, haki na fursa sawa kwa raia wote.


Mheshimiwa Mwenyekiti na washiriki wa mkutano,

Kwa ujumla hali ya kisiasa ya Zanzibar hivi sasa ni shwari, na kama nilivyogusia hapo awali, wananchi wanafanya shughuli zao za kisiasa, kijamii na kimaendeleo bila ya bughudha yoyote ile. Haya ni maendeleo makubwa tukilinganisha na tulikotoka. Kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika mfumo wa vyama vingi ni hatua kubwa sana, ambayo inaonyesha upevu wa kisiasa ambao utaiwezesha nchi yetu isonge mbele kimaendeleo kwa kasi zaidi. Ile tabia ya kupingana kwa sababu tu za kisiasa imepungua sana na kuelekea kwisha kabisa, jambo ambalo litawezesha serikali kufanya maamuzi kwa haraka na ambayo yatakubalika kwa wananchi wa mirengo yote mikubwa na viongozi wao.
Kukubali kuachana na siasa za ‘mshindi kuchukua kila kitu’ na kuamua kukaa pamoja na kuunda serikali ambayo itapata mchango kutoka kila chama kilichohusishwa katika kuunda serikali hiyo ni suala muhimu, kwa vile linawashirikisha wengi kwa maslahi ya taifa na watu wake. Ile dhana tu ya ‘Umoja wa Kitaifa’ ni kitu cha kutia moyo.

Hivi sasa wawekezaji wanavutiwa na hali ya amani na utulivu ya Zanzibar, ambayo hujenga mazingira bora katika shughuli za uwekezaji na shughuli za kiuchumi kwa jumla. Wawekezaji hao wamekuwa wajijitokeza katika kuonesha nia ya kufungua miradi yao Unguja na Pemba.Hatua hii itachangia kwa kiasi kikubwa wananchi wetu kupata ajira na kuimarisha hali zao za kiuchumi.

Aidha, hivi sasa Wazanzibari wote wanachangia na kushiriki katika harakati za maendeleo ya nchi yao, miongoni mwao ni wale Wazanzibari ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi nje ya Zanzibar yaani ‘Diaspora’. Wazanzibari hao wamekuwa wakielezea kufurahishwa kwao na hali iliyopo ya umoja na maelewano. Baadhi yao wamekuwa wakifuatilia hatua zitakazowawezesha kutumia fursa hiyo kufungua miradi ya kiuchumi itakayowanufaisha wao na jamii nzima ya Wazanzibari. Pia wamekuwa wakijumuika kusaidia wanajamii wenzao hapa Zanzibar, kama vile kwa kuleta kama misaada, vifaa vya elimu, matibabu na fedha taslim kuchangia miradi ya kijamii.
Wako wale walioonesha utayari wao wa kuja kutumia taaluma zao katika kuitumikia nchi yao wakati wanapokuwa katika likizo zao. Hata wale ambao wamestaafu, lakini bado wana nguvu za kimwili na akili wameonesha hamu ya kuja kutumikia Zanzibar na watu wake. Haya yasingeweza hata kufikirika huko nyuma.

Hali hii inanikumbusha swali aliloulizwa mtaalamu mmoja wa nchi ya Liberia, kwa jina akiitwa Mr. Johnson, aliulizwa, ni vipi hali ya amani itakuza uchumi wa nchi hiyo, ambapo jawabu lake rahisi lilikuwa, ‘Nadhani ni pale mioyo ya wananchi wote wa Liberia itakapokuwa imejawa na mapenzi na hamu ya kuwepo amani katika nchi yao, hali hiyo itaepusha machafuko na wafanyabiashara watawekeza miradi itakayosaidia kukuza uchumi wa nchi’.

Majibu ya mtaalamu huyo wa Liberia pia ni darasa tosha kwa Zanzibar,ambayo inahitaji sana kuwa na amani na utulivu, ili iweze kujenga imani kwa wawekezaji na kuondokana na uchumi dhaifu unaosababisha wananchi wetu kukabiliwa na hali ngumu ya umasikini.

Kwa upande wa kijamii hivi sasa tunashuhudia ushirikiano mkubwa miongoni mwa wananchi wetu. Kwa mfano katika tukio la ajali ya kuzama kwa meli ya MV. SPICE ISLANDER, mwezi Septemba mwaka jana hapa Zanzibar, umoja na mshikamano ulioonyeshwa na Wazanzibari ulidhihirisha wazi namna wananchi walivyokuwa wamoja. Wengi wetu tumekuwa tukijiuliza, iwapo tukio lile lingetokea wakati ule ambapo hakuna maelewano miongoni mwetu hali ingekuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti na wajumbe wa mkutano,
Huwezi kuzungumzia hali ya kisiasa Zanzibar kwa ufasaha kabisa bila ya kugusia suala la Muungano wa Tanzania, na ndio maana utaona masuala ya Muungano kwa Zanzibar hupewa uzito na umuhimu wa kipekee na wananchi wetu. Hivi sasa wananchi wana shauku kubwa na hamu ya kutoa maoni yao juu ya Katiba mpya, wakiamini kwamba ndio njia mfuaka kumaliza malalamiko yao ya siku nyingi. Miongoni mwa hayo ni yale yanayogusa uchumi wa Zanzibar na siasa kwa ujumla. Utaona ni kwa jinsi gani Wazanzibari wanavyoguswa na suala hilo, pale walipoletewa rasimu ya awali ya mswada wa sheria ya kuweka utaratibu wa kukusanya maoni ya wananchi juu ya katiba mpya walivyojitokeza kwa wingi kuujadili na kufikia hatua ya kuukataa kwa sauti moja. Kwa Wazanzibari ambao wao wanayo katiba yao iliyo sawa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, suala kubwa kwao katika kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ni nafasi ya Zanzibar katika Muungano utakaotoa haki sawa kwa washiriki wa Muungano huo, bila ya kuwa na dhana ya mkubwa na mdogo au BIG BROTHER. Mambo gani yawe ya Muungano. Aina ya Muungano: Je uwe kama ulivyo sasa, uwe wa serikali tatu au uwe ni Muungano wa mkataba kwa mambo tutakayokubaliana, badala ya kuwa Muungano wa kufungana Kikatiba.

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, mimi mwenyebinafsi na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Idd pamoja na viongozi wengine serikalini, tumekuwa tukiwahimiza wananchi kufuatilia kwa makini mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, ili waweze kujipanga vizuri na wakati utakapofika waweze kutoa maoni yao juu ya katiba hiyo mpya wanayoitaka, ambayo wanahisi itakuwa yenye maslahi sawa kwao na Zanzibar na kwa wenza wa Tanganyika. Wananchi wanapaswa kuifanya kazi hiyo wakati utakapofika, bila ya woga, la muhimu watoe maoni yao kwa ustaarabu mkubwa na bila ya kuwatukana watu wengine.

Wakati wa kutoa maoni juu ya katiba mpya utakapofika wananchi kote nchini watapata fursa ya kipekee kuujadili Muungano wao na baadaye kutoa maamuzi yanayofaa, ili kumaliza migogoro, na manung’uko yasiyokwisha baina ya pande mbili zinazounda Muungano huo, malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa wingi na kutishia uimara wake, tangu muungano huo ulipoasisiwa mwaka 1964.

Mheshimiwa Mwenyekiti,
Naona niangalie kwa ufupi changamoto tulizonazo ambazo ni nyingi na zenye uzito wa aina yake. Kama ambavyo mnaelewa serikali za Umoja wa Kitaifa popote pale duniani hukabiliwa na changamoto nyingi na wahusika wasipokuwa makini wanaweza kuhisi kwamba mifumo ya serikali za aina hiyo sio hatua muafaka kufikia pale wanapotarajia. Hata hivyo kwa upande wa Zanzibar hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa bila ya mivutano katika kupata viongozi kutoka kwenye vyama husika au sera na miongozo inayopaswa kutumika katika kuendesha serikali yenyewe.

Mafanikio haya bila shaka yametokana na kufuata Katiba ya Zanzibar ya 1984 kama ilivyorekebishwa mwaka 2010. Hata pale zinapojitokeza changamoto za hapa na pale, tumekuwa tukikabiliana nazo kwa majadiliano ya uwazi na kupata maelewano na baadaye kuendelea mbele.Naamini chini ya utaratibu kama huo na kwa mashirikiano na pande nyengine na kwa kuthamini fikra za kitaalamu kama zile tunazotarajia kuzipata kupitia mkutano huu, tutaweza kusonga mbele zaidi na kufikia malengo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti na wajumbe wa mkutano,
Miongoni mwa changamoto tulizonazo ni ukweli kwamba hadi leo wapo baadhi ya viongozi na watu ambao hawafurahishwi na Maridhiano ya Wazanzibari.Watu hao ni wachache.Baadhi yao wamekuwa wakijaribu kutia fitna ili kuvuruga maelewano, kwa bahati mbaya yako magazeti machache yanayotolewa Tanzania Bara ambayo yamepania kuleta chochoko ili kuvuruga kuaminiana kuliko jengeka.Hata hivyo, kwa vile walio wengi wanaona umoja wetu huu unafaida kubwa zaidi, kuliko hasara watu hao hawatafanikiwa. Ni wajibu wetu sote kuendelea kuwaelimisha watu hao, ili nao baadaye waone umuhimu wa umoja wa Wazanzibari na waweke mbele maslahi ya wengi kuliko ya wachache, na kwa hakika watu wa aina hii wanapungua kila kukicha.

Changamoto nyengine tunayokabiliana nayo ni katika kukidhi matarajio makubwa ya wananchi juu ya serikali yao, pengine kuliko hali halisi ilivyo. Wananchi wengi walitarajia serikali yao itaweza kutatua kwa muda mfupi kero kubwa zinazowakabili katika maisha, kama vile mifumko ya bei za bidhaa muhimu na kuwepo hali ngumu ya maisha.

Serikali hii tokea ilipoanza kazi imekuwa ikichukua hatua kubwa kuhakikisha ugumu wa maisha ya Wazanzibari unapungua, na wananchi kote Unguja na Pemba wanapata nafuu katika maisha. Hata hivyo, uhaba wa fedha serikalini pamoja na hali isiyotarajiwa inayojitokeza ulimwenguni, kama vile kupanda kwa bei ya mafuta mara kwa mara, kushuka thamani ya shilingi dhidi ya dola, uharamia katika bahari yetu ya Afrika Mashariki, pamoja na majanga ya ukame na mafuriko katika nchi tunazo zitegemea zaidi kununua bidhaa za vyakula, baadhi ya wakati huchangia kutofikiwa malengo yetu.

Serikali inachukua juhudi kubwa kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi, kama tusemavyo Waswahili, ‘Kata pua uunge wajihi’, baadhi ya wakati tunalazimika kupunguza kodi za bidhaa zote muhimu, kwa kuzingatia hali za maisha ya wananchi wetu.

Tunalazimika kuchukua hatua hizo kwa kuzingatia kuwa, hali ngumu za kimaisha si jambo la mchezo na tayari tumepata fundisho kubwa kwa yale yanayotokea katika baadhi ya nchi, kama huko Mashariki ya Kati, ambapo kwa upande mwengine ugumu wa maisha umechangia hayo yanayotokea.

Kwa upande mwengine uhaba wa fedha unahusishwa pia na baadhi ya kasoro zinazojitokeza, ikiwemo kuchelewa kufanyiwa mapitio daftari la kudumu la wapiga kura Zanzibar, ambalo wananchi waliahidiwa lingefanyiwa mapitio hayo katika mwezi Oktoba wa kula mwaka, lakini hadi sasa kazi hiyo haijafanyika. Bado kuna tatizo la wananchi wasio kuwa haba kupambana na vikwazo katika kupata vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambavyo ndivyo sharti la lazima la kumuwezesha mwananchi kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Masheha kwa bahati mbaya, wanahusishwa kuwawekea vikwazo wananchi hao kupata vitambulishio hivyo.

Changamoto hizi zinafahamika na Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hatua za kuzimaliza zinajadiliwa.

Ukitulinganisha sisi Wazanzibari na wenzetu wa nchi nyengine zilizokumbwa na mgawanyiko wa raia wake, sisi tumeanza vizuri na tunaendeela vizuri. Ni matumaini yangu kuwa Zanzibar itaendelea kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyengine, ikiwemo Tanzania Bara, katika kuendeleza, amani utulivu, mshikamano na maelewano miongoni mwa wananchi wake.

Baada ya kusema hayo machache naomba kuwashukuru wote kwa uvumilivu wenu wa kunisikiliza kwa makini.

Basi niruhusuni nitamke wazi kuwa Mkutano wa Pili wa Hali ya Siasa Zanzibar nimeufungua Rasmi.

Mungu Ibariki Zanzibar

Mungu Ibariki Tanzania

AHSANTENI.

Advertisements

One thought on “Hotuba ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa hali ya siasa Zanzibar huko Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar – tarehe 13, februari, 2012

  1. Pingback: Mfumo tenganishi hauna nafasi tena Zanzibar -Maalim Seif « Haki Sawa kwa Wote

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s