CUF yatangaza `vita` kupigania eneo la kiuchumi katika bahari kuu

Naibu katibu Mkuu wa CUF Zanzibr,akiwahutubia wananchi katika Uwanja wa Gombani ya Kale kisiwani Pemba.

Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi mambo ya nje wa Chama cha CUF, Ismail Jussa Ladhu
Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kwamba kitapinga Umoja wa Mataifa (UN) kuiongezea Tanzania mipaka ya eneo la kiuchumi la bahari Kuu kabla ya kupatikana muafaka kati ya Serikali ya Muungano na Zanzibar.
Tamko hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi mambo ya nje wa Chama hicho, Ismail Jussa Ladhu, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliyofanyika katika uwanja wa Gombani ya Kale huko kisiwani Pemba.
Alisema Serikali ya Muungano imefanya makosa kuandaa kupeleka maombi ya kutaka kuongezewa mipaka ya eneo tengefu la kiuchumi la bahari kuu (EEZ) bila ya kushirikisha Zanzibar.
Jussa alisema wananchi wa Zanzibar wapo tayari kupoteza maisha lakini hawatokubali eneo la bahari Kuu la Zanzibar kuongezwa na kuwa sehemu ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Wananchi wa Pemba simameni kidete kutetea maslahi ya Zanzibar hata kama tutamalizika sote haiwezekani eneo la bahari Kuu la Zanzibar kuwa la muungano,” alisema Jussa.
Alifafanua kuwa Januari 16 mwaka huu Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alitangaza mpango wa Tanzania kuomba UN kuiongezea maili 150 sawa na kilometa 241.5 kutoka usawa wa mwambao wa Tanzania.
Profesa Tibaijuka alisema kazi ya kukamilisha andiko hilo ilianza mwaka 2007 na kugharimu Sh. Bilioni 5.2 na kushilikisha wataalamu kutoka sekta ya mbalimbali, ili iweze kulifanyia utafiti zaidi kuhusu rasilimali zilizoko chini ya bahari kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi.
Jussa alisema mpango huo umelenga kuiwezesha serikali ya Muungano kuongezewa eneo hilo ili kufanikisha mpango wake kufanya utafiti na uchimbaji wa mafuta wakati SMZ imekwishaliondoa kwenye orodha ya mambo ya muungano.
Hata hivyo, alisema mpango wa Tanzania kuongezewa eneo la maili 150 kutoka usawa wa bahari ya Hindi umefanyika bila ya kuishilikisha SMZ.
Jussa ambaye pia mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, alisema alipohoji suala hilo ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) alitakiwa na serikali kuwa na subira na kutoa nafasi kwa serikali ya SMZ kulifuatilia.
Alisema suala la mafuta na gesi asilia tayari SMZ imeamua tangu mwaka 2009 kuliondoa katika orodha ya mambo ya muungano na haikuwa muafaka kwa serikali kupeleka maombi hayo bila ya kupata baraka ya Zanzibar.
“Wenzetu wanataka kuchimba mafuta na gesi asilia ya Zanzibar kwa kutumia mlango wa nyuma hatukubali kwa maslahi ya Zanzibar na nchi yetu,” alisema Jussa.
Kuhusu kufukuzwa kwa viongozi wanne wa CUF akiwemo Mbunge wa Wawi Hamad Rashid Mohammed, alisema viongozi hao wamekwenda kinyume na misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1992.
Alisema CUF ilianzishwa kwa madhumuni makubwa ya kupingania haki za Zanzibar na wananchi wake ikiwemo mfumo wa Muungano.
Jussa alisema katika kupingania haki za Zanzibar ndiyo maana wapo watu wamepoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu ndiyo maana chama kimeamua kuwafukuza viongozi hao baada ya kwenda kinyume na misingi ya kuanzishwa kwake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa haki za Binadamu na mahusiano ya umma Salim Biman, alisema kwamba viongozi waliyofukuzwa ndani ya CUF waliweka maslahi binafsi mbele badala ya maslahi ya chama na wanachama wake.
Awali akisoma risala ya mikoa miwili ya wanachama wa CUF Kisiwani Pemba, Ayoub Yussuf Mgeni, alisema wanachama wanaunga mkono maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi kwa kuwatimu viongozi hao.
Alisema viongozi hao ni wasaliti kutokana na kitendo chao cha kutetea maslahi binafsi na kuwapaka matope viongozi wa kitaifa kwa kutaka kuwagawanya kwa mtazamo wa Uunguja, Upemba na Utanzania Bara.
Alisema CUF kimefanya kazi kubwa kupingania misingi ya haki za binadamu na utawala bora hadi kufanikiwa kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Novemba mwaka 2010.
Alisema tangu kundwa kwa serikali hiyo kesi za kisiasa, ubaguzi na ukikwaji haki za binadamu umeondoka kwa wananchi wa Zanzibar.
Aliongeza kuwa hatua kama hizo zinapaswa kuendelea kuchukuliwa kwa mwanachama yoyote anayetaka kuvuruga umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Zanzibar.
Mapema Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye pia Makamu wa kwanza wa Rais, alipokea maadamano ya amani ambayo yalinzia huko Machomanne kupitia Mkanjuni huku wanachama wakiwa wamebeba mabango ya kumshutumu Mbunge wa Wawi aliyevuliwa uanachama Hamad Rashid Mohammed.
Baadhi ya mabango yalisomeka ‘Tumekukuta Wawi na shuka kiunoni, tumekupeleka Dodoma na suti leo watusaliti’; ‘Tamaa imekuponza, siasa hukuweza rudi Wawi ukavue’ na lingine likisema ‘Hamad umepanda upepo utavuna dhuruba’

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s