Wazanzibari tuungane – Maalim Seif

Maalim Seif Sharif Hamad

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema hana tatizo la wanaotetea serikali mbili lakini kuwepo na mfumo maalumu utakaokubalika na wananchi wote. Alisema wale wanaotetea mfumo wa Serikali mbili, kama ni hivyo yeye hana tatizo. Ila ziwepo Serikali mbili, moja ya Zanzibar na Katiba yake na mambo yake yote, na ya pili ya Tanganyika na Katiba yake na mambo yake yoye. “Halafu tutaamua yepi tunataka tushirikiane na kwa mfumo upi” alisisitiza Maalim Seif.
“Wazanzibari ni lazima waweke pembeni tofauti zao ya kisiasa. tuwe na umoja. Maana hivi sasa wapo baadhi ya viongozi wanaopita mitaani kuhubiri kuwa sera ya CCM ni serikali mbili. Kauli kama hizi haziwezi kujenga nchi na kwa miaka mingi hatujafanikiwa” alisisitiza Maalim Seif.
Maalim Seif amesisitiza baadhi ya mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kutoa maoni ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwataka viongozi na wananchi kuungana katika kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano.

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Salim Bimani

Amesema iwapo Wazanzibari wataungana na kuwa na sauti moja juu ya jambo hilo, kauli yao itakuwa na nguvu na upande wa pili wa Muungano utalazimika kuheshimu maamuzi hayo ya Wazanzibari.
“Viongozi na wananchi wote tushikamane na tuweni na kauli moja juu ya jambo hili, na kamwe tusikubali kugawanywa kwa maslahi ya nchi yetu”, alisema Maalim Seif.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo katika viwanja vya demokrasia Kibandamaiti mjini Zanzibar wakati akiwahutubia maelfu ya wanachama na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliotishwa na chama hicho, baada ya kumaliza kikao chao cha chama hicho cha ndani.
Maalim alisema kwa sasa wazanzibari washughulikie katika suala la katiba mpya tu kwani hiyo ndio ajenda muhimu kwa wazanzibari wote, kwani ni jembo pekee ambalo litakaloinusuru Zanzibar katika kupata haki zake ndani ya Jamhuri ya Muungano.
Alibainisha baadhi ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa na kuingizwa katika katiba mpya kuwa ni haja ya Zanzibar kuwa na benki kuu yake ikiwa ni nia moja wapo ya kudhibiti uchumi wake.
Uchumi alisema sio suala la Muungano, kwa hivyo lazima Zanzibar iwe huru kabisa katika mambo yote akitoa mfano suala la mafuta yatakayoshimbwa Zanzibar alisema yaondolewe katika Muungano.

Mamia ya wafuasi wa CUF wakisikiliza hotuba huko Kibandamaiti mjini Zanzibar

Alisema lazima wazanzibari wakazane kuhakikisha kuwa suala la mafuta lisiwe katika muungano. na lazima Zanzibar iwe na udhibiti wa sera zake za kiuchumi ikiwemo kamati za fedha, wazanzibari kuwa na sauti juu ya fedha, pamoja na kuwa na benki yetu kuu (Benki kuu).

Ambapo Maalim amesema Zanzibar ni lazima iwe na kodi za chini kama zamani ambapo Tanzania Bara walipoona suala hilo linafanyiwa kazi basi wakaona wivu, na kuanzisha kodi ya pamoja (harmonization).
Maalim Seif amefahamisha kuwa Zanzibar inastahiki pia kuwa na uwezo wa kuweka viwango vyake vya kodi, pamoja na kuwa na mitaala yake ya elimu inayoendana na mazingira ya Zanzibar kwa maslahi ya Wazanzibari.
Maalim Seif amesema suala la katiba yeye na wenzake wamelivalia njuga na matarajio yao ni kwamba ifikapo mwaka 2014 watanzania wawe wameshapata katiba mpya ambapo alisema serikali tayari imepitishwa mswada huo.
Aidha alisema kasoro zilizojitokeza, na kupelekea wazanzibari kukaa mwanzo na kupitia upya, kwani yote ya madai yao ya msingi yamerekebishwa na kati ya mambo 13, kumi yalikubaliwa.
Alisema serikali ya Zanzibar ilikuwa bega kwa bega na wananchi katika maoni juu ya katiba mpya na itafanya hivyo katika siku zinazofuata kwani lengo ni kupata katiba ambayo ina maslahi na wazanzibari wote.
Katika mkutano huo Maalim Seif alisema kuwa nchi ya Zanzibar na Tanzania zote ni sawa kimataifa. Hivyo anasema Tume itakayoundwa kukusanya maoni ni lazima iwe na wajumbe sawa kutoka pande zote mbili za nchi huku akisiistiza kila hatua ya kukusanya maoni lazima itafanywe kwa uwazi na sio kwa usiri.
Kwa kuzingatia kuwa Zanzibar ni nchi ya kwanza kuanzisha mfumo wa kura ya maoni hivyo maamuzi ya mwisho yatafanywa na wananchi kwa kura ya maoni juu ya mustakabali wa nchi yao katika katika mpya.
“Ni lazima asilia 50 au zaidi ya wananchi kutoka kila upande ndipo katiba ikubalike” alisema Maalim Seif.
Katika kuwatoa khofu wananchi amewataka wananchi kuondosha khofu wakati ukifika na wawe wazi katika kutoa maoni yao kuzungumza juu ya Muungano, kwani kufanya hivyo hakuna atakaeguswa au kuchukuliwa hatua yeyote kisheria kwani katiba iliyopo inaruhusu mtu kutoa maoni yake.
Aidha hakuacha kugusia suala la kasoro iliyopo katika mfumo wa sasa wa Muungano akitoa mfano wa suala la kuongoza Tanzania, ambapo Maalim Seif amesema tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uasisiwe ni rais mmoja tu amekuwa rais kutoka Zanzibar na marais wengine wote wamekuwa wakitoka upande wa Bara hivyo alisema lazima kuwe na mfumo wa kupokezana katika kuongoza Tanzania.
Wiki iliyopita Maalim Seif alielezea umuhimu wa kuwepo utaratibu maalum wa kikatiba utakaoruhusu nafasi ya Urais wa Muungano kutumikiwa kwa awamu kati ya Tanzania bara na Zanzibar, tofauti na utaratibu uliopo sasa ambao hautoi fursa kwa Wazanzibari kuitumikia nafasi hiyo kubwa kabisa ya uongozi nchini.
Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais alitumia fursa hiyo kutoa mkono wa pole kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na baadhi ya wananchi hasa wa mkoa wa Dar es Salaam kupoteza maisha yao, hali iliyosababishwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa.
Amesema mwisho mwa mwezi huu chama chake kimepanga kuzitembelea kambi wanazoishi watu walioathirika na kupoteza makaazi kutokana na mafuriko hayo kwa lengo la kutoa pole na mchango wake kwa waathirika hao.
Wakati huo huo Naibu Katibu mkuu wa CUF Zanzibar Mheshimiwa Ismail Jussa Ladhu amewataka wanachama wa chama hicho kupuuza uvumi juu ya mgogoro ndani ya Chama hicho, na kwamba chama hakina mgogoro na kiko imara wala hakiyumbi.
Amesema uvumi huo unaosambazwa kupitia vyombo vya habari umekuwa ukitolewa kwa malengo maalum ya kukivuruga chama, malengo ambayo amesema hayatofanikiwa.
Jussa amesema wanachama wa CUF bado wana imani kubwa na Maalim Seif na amemuomba wananchi kupuuza yanayozungumzwa kuwa Maalim Seif kachoka.
Nae Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Salim Bimani amesema bado serikali ya Muungano haijatoa fursa zinazostahiki kwa Zanzibar katika masuala ya kimataifa ikiwa ni pamoja na kuinyima nafasi za kibalozi nchi za nje.
Akizungumzia suala la vitambulisho Bimani amesema watu ambao hadi sasa wamenyimwa vitambulisho vya mzanzibari mkaazi wende wakaripoti kwa Mkurugenzi wa vitambulisho, Mohamed Juma Ame ili wapewe vitambulisho vyao kwa kuzingatia kwamba hiyo ni haki yao kwani bila vitambulisho wazanzibari watashindwa kutoa maamuzi mazito juu ya katiba mpya inayokuja.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s