Kuwamo kwenye serikali hakujanitoa kwenye dhamira – Maalim Seif

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amepinga vikali shutuma za baadhi ya watu kwamba tangu kuingia madarakani katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, yeye na chama chake wameacha kupigania maslahi ya Zanzibar kwenye Muungano.

Kiongozi huyo ambaye mwaka 1988 alifukuzwa kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuvuliwa nyadhifa zote serikalini na kuwekwa ndani kwa muda mrefu, kwa sababu ya kupingana na mfumo wa Muungano, amesema hawezi kamwe kuacha kuipigania Zanzibar.

“Wapo watu wanasema siku hizi Maalim kawa kimya…Hapana. Mwenyezi Mungu kanijaalia kuniondolea woga na khofu. CUF kuwemo ndani ya serikali haina maana kuwa tumesalimu amri. Tuna dhamira yetu na tunaiamini.”

Maalim Seif ametoa kauli hiyo mbele ya maelfu ya wananchi wa Zanzibar waliokusanyika kwenye uwanja wa Demokrasia, mjini Unguja, katika mkutano wa hadhara uliondaliwa na CUF hapo jana.

Akipigia mfano wa uongozi imara wa Zanzibar katika awamu ya kwanza, chini ya Marehemu Abeid Amani Karume, Maalim Seif alisema kwamba hivyo ndivyo anavyoamini na kwamba Zanzibar hivi sasa inapitia kipindi muhimu kinachohitaji mshikamano wa Wazanzibari wote.

“Siku moja mwaka 1971, Mwalimu Nyerere alimuita Karume, akaitikia kwa kusema kwamba kuwa anakuja na wanaume wake. Fedha zenu na karafuu zetu, polisi yenu, mambo ya nje tugawane 50 kwa 50. Lazima tufuate mfano wa Karume kuwa na msimamo. Tushikamane, tudai mambo yetu kwa kauli kwa sauti moja. Lakini tukikubali kugawiwa, wengine wakifikiri maslahi yao tu, tutapata shida.“

Maalim Seif ambaye alitumia mkutano wa jana kuzungumzia dhima ya wananchi wa Zanzibar kuelekea Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema kwamba chimbuko hasa la vuguvugu la Katiba hiyo ni chama chake, na hivyo Wazanzibari hawatakiwi kujitenga kando na mchakato unaoendelea.

Maalim Seif amesema miaka mitatu iliyopita vyama vya siasa na makundi ya kiraia walikaa chini ya uongozi wa mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, katika hoteli ya Peacock, jijini Dar es Salaam, na kuandaa rasimu ya katiba mpya.

“Katika kikao hicho, alichaguliwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba iliyoundwa kwa jina la Zero Draft, na mwenyekiti huyo nilikuwa mimi, Maalim Seif. Baada ya kuikamilisha, tulitaka kukabidhi rasimu hiyo kwa maandamano, lakini askari wengi wakamwagwa kuzuia maandamano hayo. Hata hivyo, CUF ilifanikiwa kuwasilisha ’draft’ kwa Waziri wa Katiba wa Muungano“. Maalim Seif aliuambia umati huo mkubwa, huku akirejelea msimamo wake katika suala la Katiba Mpya.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Ismail Jussa

Makamo huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema yeye na wenzake wamelivalia njuga suala hili na wanataka “ifikapo mwaka 2014 tuwe na Katiba Mpya“.

Akizungumzia kasoro zilizojitokeza wakati wa mswaada wa mwanzo uliotayarishwa na Serikali ya Muungano na ambazo zilipelekea Wazanzibari kuukataa jumla-jamala, Maalim Seif amesema yale yote ya msingi yaliyolalamikiwa na upande wa Zanzibar yamerekebishwa.

“Kati ya mambo 13, kumi yamekubaliwa kama walivyotaka wananchi wa Zanzibar na serikali yao. Kwa hili, serikali ilikuwa na iko bega kwa bega na wananchi“.

Kuhusiana na hadhi ya Zanzibar, ambacho kimekuwa kilio cha Wazanzibari kwa miaka kadhaa sasa, Maalim Seif amesema kuwa nchi ya Zanzibar na Tanzania zote ni sawa, na ndio maana hata Tume itakayoundwa kukusanya maoni ni lazima iwe na wajumbe sawa kutoka pande zote mbili za nchi, huku kila hatua ya kukusanya maoni hayo ikiwa na uwazi na sio usiri.

Hata hivyo, Maalim Seif amesema uamuzi wa mwisho utafanywa na wananchi kwa kupitia kura ya maoni, ambapo ameitaja Zanzibar kuwa kwake nchi ya kwanza kuanzisha utaratibu wa kura ya maoni, kama ilivyo historia ya nchi hiyo kutangulia katika kufanya mageuzi.

“Na mambo mengi mazuri yanaanza Zanzibar, halafu ndiyo yanakwenda Bara“.

Kwa mujibu wa sheria hiyo ya Katiba Mpya, ni lazima kwa zaidi ya asilimia 50 ya wananchi kutoka kila upande kukubaliana na Katiba hiyo, ili kuipa uhalali. Katika hilo, Maalim Seif amewataka wananchi wa Zanzibar kutokuwa na woga na kuwa huru kuzungumza juu ya masuala yote yanayohusu hatima ya taifa lao, ukiwemo Muungano wenyewe, na kuahidi kuwa “hakuna atakayeguswa“.

Makamo huyo wa Rais amesema Muungano una kasoro nyingi sana na lazima wananchi wa Zanzibar waseme vipi wanataka Muungano huu sasa uwe, likiwemo suala la kuiongoza Tanzania. Itakumbukwa kuwa hivi karibuni, Maalim Seif alitoa kauli ya kutaka uraisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lazima uwe ni wa kupokezana baina ya Tanzania Bara na Zanzibar, na isiwe kama ilivyo sasa, ambapo uwezekano wa kumpata rais kutoka Zanzibar ni finyu sana.

Suala jengine alilosema kuwa lina mapungufu makubwa ni uchumi, ambapo amesema si la Muungano, lakini linalazimishwa lionekane kuwa hivyo, na matokeo yake Zanzibar inadidimizwa kila uchao.

“Zanzibar lazime iwe huru kabisa katika mambo yote ya kiuchumi, kwa mfano mafuta yaondolewe katika Muungano. Na sisi Wazanzibari lazima tukazane kuhakikisha kuwa suala la mafuta lisiwe katika Muungano“.

Maalim Seif amesema lazima Zanzibar iwe na udhibiti wa sera zake za kiuchumi ikiwemo Kamati za Fedha na pia kuwa na Benki Kuu yake yenyewe. Vile vile katika masuala ya kodi, amesema ni lazima kwa Zanzibar kuwa na kodi za zake zenyewe, ambazo zitakuwa za chini.

Ukiwacha masuala ya kiuchumi, Maalim Seif alizungumzia pia suala la elimu, na kusema kuwa haiwezekani wanafunzi wa Zanzibar kufanya mitihani ya Tanzania, wakati mitaala inayotumika ni ya Tanzania Bara. Badala yake ametaka Zanzibar iwe na mitaala yake yenyewe.

Katika kufanikisha hayo, Maalim Seif alitumia mkutano wake wa jana, kuwataka Wazanzibari waweke pembeni tofauti zao za kisiasa.

“Lazima ndugu zangu tuwe na umoja. Maana hivi sasa wapo baadhi ya viongozi wanaopita mitaani kuhubiri kuwa sera ya CCM ni serikali mbili. Kauli kama hizi haziwezi kujenga nchi na kwa miaka mingi hatujafanikiwa“.

Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu, Sheria na Mawasiliano, Salim Bimani

Amesema yeye, kama Maalim Seif na kiongozi wa Wazanzibari, hana tatizo na hao wanaotetea mfumo wa serikali mbili, lakini zikiwa mbili, basi moja ya Zanzibar na Katiba yake na mambo yake yote, na ya pili ya Tanganyika na Katiba yake na mambo yake yote. “Halafu tutaamua yepi tunataka tushirikiane na kwa mfumo upi“.

Wakizungumza baada ya hotuba hiyo, wananchi mbalimbali waliomfuatilia Maalim Seif, wamesema wanaunga mkono kauli yake kuhusiana na hatima ya Zanzibar.

“Pongezi kwa Maalim (Seif) kwa points (hoja) zake nzuri. InshaAllah Wazanzibari natushirikiane hivyohivyo hadi tujue moja. Ila baadhi yetu ambao hatujawahi kuonja ladha ya uhuru tunasema chochote tutakachokipata ndani ya Katiba Mpya tutakichukua lakini lengo letu hasa ni kuuvunja Muungano huu, Afrika Mashariki inatutosha“. Amesema mmoja wa wananchi hao, Yahya Hamad.

Mapema, kabla ya Maalim Seif kuhutubia, Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu, Sheria na Mahusiano na Umma wa CUF, Salim Bimani, aliwataka wananchi wote wa Zanzibar ambao hawajapata vitambulisho vyao vya ukaazi (Zan-IDs), kwenda moja kwa moja kwa Mkurugenzi wa Vitambulisho Zanzibar, Mohammed Juma Ame, kuchukua.

“Kila ambaye amenyimwa kitambulisho, aripoti kwa mkurugenzi Mohamed Ame ili apewe. Bila vitambulisho, Wazanzibari watashindwa kutoa maamuzi mazito juu ya Katiba Mpya inayokuja.“ Alisema Bimani.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Ismail Jussa, alimuhakikishia Maalim Seif kwamba bado wana-CUF na Wazanzibari kwa ujumla wana imani naye.

Akirejelea taarifa za karibuni kwenye vyombo mbalimbali vya habari juu ya kufukuta kwa mgogoro ndani ya chama chake baina ya Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid, kwa upande mmoja, na Maalim Seif kwa upande mwengine, Jussa alisema kuwa hakuna mgogoro huo ndani ya CUF, na tafauti zilizopo zitamalizwa kwa utaratibu wa vikao vya kawaida vya Chama.

“Maalim Seif hawezi kujibu shutma kupitia vyombo vya habari. Mambo yote yatajibiwa katika vikao vya chama kwa sababu CUF ina taratibu zake hivyo haiwezi kuvunja taratibu kwa kujibizana kwenye vyombo vya habari“, alisema Jussa kabla ya kumkaribisha Maalim Seif jukwaani.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s