Chokochoko ndani ya CUF zimalizwe haraka.

mwenyekiti wa CUF taifa, Professa Ibrahim Harouna Lipumba

Chama cha Wananchi, ama Citizen United Front (CUF), sio chama cha siasa cha Kiislamu wala si cha Waislamu. Kisingeweza kuwa hivyo na kikasajiliwa na kikaruhusiwa kutangaza sera zake nchi nzima, Bara na Visiwani, kwa vile sheria ya nchi hii imepiga marufuku kabisa vyama vya siasa vyenye mlengo wa kidni na kikabila. Sheria hii lakini huweza kupigwa chenga bila Serekali kuchukua hatua zozote.
Ni vigumu kutokuamini kuwa chama cha siasa cha United Democratic Party sio chama cha siasa cha Wanyantuzu. Huko nyuma kiongozi wake alipojaribu kujitosa katika kutafuta Urais wa nchi hii yeye alianzia kampeni yake huko nyumbani na wala haikufika sehemu nyingine nyingi za nchi. Kama hilo halitoshi basi mpaka sasa wabunge wake wametokea huko tu.

Katibu Mkuu wa CUF, maalim Seif Sharif Hamad

Hakika CUF pia kimekuwa kikisingiziwa kwa kiwango kikubwa sana kuwa kilikuwa ni chama cha Waislamu kiasi kwamba kilipigwa vita sana na makanisa na wafuasi wao katika chaguzi zote zilizopita. Shutuma hizo zilitokea kuwa nzito kiasi kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikatoa matamshi kukana kuwa CUF kilikuwa ni chama cha Waislamu.
Hii ilikuwa ni baada ya baadhi ya wananchi kuwajulisha watu kuwa CCM nayo ilikuwa ikiongozwa na viongozi wengi wakiwa Wakristo, (kwa hiyo ni cha Kikristo?). Hayo ya CCM hayakuweza kufuta mawazo ya wengi ambao walikuwa na nafasi ya kukihujumu CUF.

Ilikuwa ajabu kubwa katika bunge lilopita wakati mgombea urais wa chama hicho aliibuka na kura zilizompa nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu lakini CUF haikupata hata kiti kimoja katika Bunge.

Hii haiingi akilini mpaka pale inapotambulika kuwa kulikuwa na hujuma za hali ya juu sana. Kwa kuibuka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuungwa mkono kwa nguvu zote za makanisa, CUF kikawa kimefifia kwa kiwango kikubwa tu.

 

Makamo Mwenyekiti, Machano khamis Ali

Ni kweli kabisa kuwa Waislamu wengi kwa muda mrefu wamejitambulisha na CUF linapokuja kuzungumzia siasa za vyama vingi. Haikuwa hivyo kwa sababu ya udini hata kidogo. Wasomaji watakumbuka kuwa pale siasa za vyama vingi ilipoanza, ni NCCR-Mageuzi ndio waliokuwa ni tishio kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kilikuwa na mvutio wa aina yake kiasi kwamba kiliungwa mkono na wananchi wa kila aina hata Waislamu walikuwa katika mkondo huo.

Mambo mawili yaliwavunja nguvu Waislamu na kukiona NCCR-Mageuzi kuwa si rafiki wa Waislam.
La kwanza ni kule kumkaribisha kwa shangwe kubwa Mheshimiwa Augustine Mrema kuwa ndiye mwenyekiti na ambaye ndiye atakayesimama kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu.

Huyu Muheshimiwa huko nyuma akiwa Waziri wa mambo ya ndani kulikuwa na shutuma dhidi yake kuwa aliwanyanyasa sana Waislamu. Hivyo isingewezekana chama hicho ambacho kitakuwa kinaongozwa na Muheshimiwa huyo kuwa ni rafiki wa Waislamu.

naibu katibu mkuu wa CUF, Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu

Sababu ya pili inatokana na chuki juu ya Uislamu miongoni mwa viongozi wa Kikristo duniani. Bila shaka Waislamu watakumbuka wale waandishi wa wawili mke na mume walioandika kitabu kilichoitwa THE TWO HEADED DRAGON. Hawa waliwazushia viongozi waliohudhuria mkutano wa Waislamu kule Nigeria ati wao wamekubaliana kuifanya Afrika iwe nchi ya Kiislamu.

Hata pale ilipotambulika kuwa yaliyokuwemo katika vipeperushi vyao ni uwongo mtupu kulikuwa na viongozi wa NCCR-MAGEUZI ambao waliukubali uwongo huo na kuushabikia kwa nguvu zao zote. Hili liliwavunja nguvu baadhi ya Waislamu kiasi cha kuona kuwa NCCR-MAGEUZI hakiwezi kuwa chama chao.

Kuhangaika huko kwa mawazo ya Waislamu kunatokana na ukweli kwamba CCM (na TANU kabla yake) imekuwa mstari wa mbele katika kusimika dhulma dhidi ya Waislamu nchini humu.

 

Naibu katibu Mkuu Wa CUF (bara) Julius Mtatiro

Pengine itakuwa vigumu kutetea shutuma hizi kwa vile kwa muda mrefu na mpaka leo mna viongozi wengi wa Kiislamu humo CCM. Lakini mambo mawili ya kumbukwe. Kwanza kwa muda mrefu nchi hii ilitawaliwa na chama kimoja; hivyo wale waliokuwa na tamaa ya kuwa wanasiasa ilikuwa ni lazima wawe wana-CCM.

Ubinafsi badala ya kuwa muumini mkereketwa wa Kiislamu kuliweza kuwafanya wengine kushabikia CCM. Jambo la pili ni kuwa Waislamu wamedanganywa sana na hivyo kutumiwa katika kudumisha dhuluma dhidi yao.
Wao kwa mfano waliamini kabisa ile sera ya kutochanganya dini na siasa ambayo ilikuwa ikinadiwa kila siku. Lakini wakati huo huo Makanisa yakipendelewa na serakali ya CCM, chama ambacho hawa Waislamu walichokuwa wakikiunga mkono kwa hali na mali.

Hata pale walipoundiwa kinachoitwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) walikishabikia na pengine mpaka leo wanakishabikia ilihali kiliwekwa pale kuwa kikwazo cha maendeleo ya Waislamu.

Haya sasa yanajulikana kwa wazi kabisa miongoni mwa Waislamu wa nchi hii.
Ndipo hapo Waislamu wa nchi hii wakawa na tamaa kuwa labda Chama Cha Wananchi, Citizen United Front (CUF) kingeweza kuwa mkombozi wao.

Kweli kilikuwa kikishutumiwa kuwa viongozi wake takriban wote walikuwa ni Waislamu. Lakini hiyo haikuwa hoja ya maana kwa vile viongozi wengi sana wa juu wa CCM walikuwa ni Wakristo. Kiasi kwamba hata Bunge limejaa wao.

Waislamu walikishabikia CUF sio kwa sababu kuwa viongozi wake wengi walikuwa Waislamu ama kwamba kilikuwa chama cha Waislamu, ila tu baada ya kuwa vyama vingine vingi havikuonyesha viko tayari kupigana na dhulma dhidi yao, basi Waislamu wakaona hebu tujaribu hiki CUF.

Imani hii imo hadi leo katika mioyo ya Waislamu wengi wa nchi hii, hasa wale walio na maoni kuwa CCM na Serekali yake haijawa tayari kutoa haki kwa sawa kwa sawa kwa wananchi wote wote wa nchi hii. Kwa hoja hizi inaweza kabisa kukubalika kuwa Waislamu wengi wamekuwa wakikitegemea CUF kuwa wakombozi wa Waislamu.
Haijulikani kwa kiasi gani viongozi wa CUF wanafahamu dhima hiyo waliyopewa na Waislamu wa nchi hii. Wao ni wanasiasa katika nchi inayojiita ya kisekula na hilo ni lazima walionyeshe wazi wazi kama wanataka chama kisifutwe.

Bahati mbaya sana ni kuwa kama ilivyoelezwa huko nyuma, wale wenye uwezo mkubwa katika kuiendesha nchi hii wamekwisha kukipaka tope kuwa ni chama cha Waislamu hata kama si cha Kiislamu.
Pamoja na hayo yote ni bahati nzuri sana kuwa viongozi wengi wa juu wa CUF ni Waislamu. Ni lazima wawe wanafahamu dhulma inayopitishwa dhidi ya Waislamu; dhulma ambayo inaweza kurekebishwa kwa njia mbili tu

Njia moja ambayo Waislamu wengi wanaipendelea ni ile ya amani, yaani ya kisiasa. Na hapa ndipo chama cha kisiasa kama vile CUF kinaweza kuchukua majukumu hayo, na ndivyo wananchi wengi wanategemea hivyo.
Kwa sababu hizi linakuwa ni jambo la kusikitisha sana pale kunatokea mtafaruki mkubwa katika chama hicho. Mbaya zaidi ni kuwa mgogoro umo miongoni mwa viongozi wanaotegemewa kuonyesha njia iliyonyooka.

Viongozi hawa wakumbuke kuwa wao wamewabeba wananchi wengi sana wa nchi hii ili wawavushe salama kupita dimbwi refu la maji machafu!!!
_________________________________________
Chanzo Gazeti la Annuur

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s