Waraka wa Hashil Seif kutoka Copenhagen: Tusisahau kuwa kama si Maalim Seif, Zanzibar isingefika ilipo leo

Hashil Seif Hashil

Matokeo ya hivi karibuni yaliyotokea kwenye chama cha CUF ambayo yameanzishwa na Mheshimiwa Hamad Rashid si jambo la kufurahisha hata kidogo. Hata hivyo, inajulikana wazi kabisa wako walioanza kupiga vikorombwe kwa furaha ya yanayotokea, kutoka pande zote mbili, yaani baadhi ya upande wa CUF na hata CCM.

Hebu tuanze kulichambua jambo hili kwa kitaalamu kabisa. Mheshimiwa Hamd Rashid anayo haki ya kukosowa chama chake. Suala linazuka mwanachama mwenye dukuduku lake kwenye chama chake anaweza kutoa mawazo yake namna gani? Wako wanaosema kuwa ni kwenda kwenye chama na kueleza yale mambo yanayomkereketa binafsi. Wako pia wanaosema kuwa Bwana Hamad Rashid hakupitia njia zitakiwazo kutoa dukuduku lake. Badala yake kaanza kuandika kwenye magazeti, jambo ambalo limewakasirisha baadhi ya wanachama wa CUF na hata Maalim Seif Sharif mwenyewe.

Pia wako wanaoeleza kuwa Mheshimiwa Hamd Rashid katumiliwa na CCM kufanya hivyo. Na pia huenda amepewa pesa. Lakini hizo ni shutuma ambazo bado hakuna aliyeweza kuzithibitisha!

Maalim Seif Sharif Hamad

Yafuatayo ni mawazo yangu binafsi ambayo ningaliomba muyachambue kwa kina. Kwanza nasaha zangu kwa Hamad Rashid: lazima afahamu wapi chama chake cha CUF kinakotoka. Pili hakuna asiyejua kuwa chaguzi zote zilizopita CUF wameshinda, lakini hawakuruhusiwa kuendesha serikali. Na hata hilo nina hakika Bwana Hamad Rashid analijua vilivyo na hakuna anayeweza kumfahamisha zaidi kuliko anavyofahamu binafsi.

Jengine, ambalo ni muhimu kabisa, kuwa leo baada ya pirika chungu nzima zilizotokea, serikali iliyopo ni ya CUF na CCM. Kufahamu zaidi ni kwamba, kama kuna kitu kinachoitwa `miujiza` basi yaliyotokea Zanzibar ni miujiza. Nani aliyefikiri kama tutaweza kuona kwa macho yetu siku moja CCM, hususan Serikali ya Zanzibar, kukubali kufanya serikali ya mseto na CUF? Mbona tunasahau upesi upesi?

Tutokako kulikuwa hakuna sheria. CCM Zanzibar wakijifanyia wayatakayo, na hakuna aliyekuwa akiweza kuwazuia. Musifikiri yaliyotokea baadhi ya CCM yamewafurahisha. Wako mpaka leo ambao wanafanya kampeni chini kwa chini kutaka turejea tulikotoka.

Hamad Rashid Mohammed

Yagujuu! Tulikotoka haiwezekani kurejea tena. Lakini ninalokuombeni, macho yetu yawe wazi kabisa kwa vitimbakwiri, ambao bado tunao Zanzibar. Nafikiri Mheshimiwa Hamad Rashid anayo haki ya kutoa maoni yake, lakini kwa maoni yangu njia alizoamua kupita si za halali.

Sifikiri kama Maalim Seif namna alivyochambuliwa na baadhi ya wanachama wa CUF ni sahihi kabisa. Sisemi kama namjua zaidi Maalim Seif, lakini aliwahi kuja kwenye kituo chetu cha Haki za Binaadamu kwa muda wa miezi mitatu kwa kufanya utafiti. Wanavyomueleza Maalim na ninavyomfahamu mimi, sifikrii kama dhana zao ni sahihi. Siamini hata siku moja kuwa Maalim Seif ana uchu wa madaraka.

Jengine ambalo ningalikuombeni mulichambue ni kuwa musisahau mchango wa Maalim Seif. Na kama si mchango wake, basi hapa tulipofika hivi leo, Wallahi tusingaliweza kufika. Musiwe munajaribu kumponda tu, bali pia yaangalieni aliyoyafanya.

Ukifanya utafiti, haitakiwi huhimili upate wowote ule
Mwiko, kutekenya machati; nakuendelea kupiga makelele
Ufyagio wa njukuti, umepitwa na wakati, ni jambo la kale

Wakatabahu
A luta continua/Venceremos
Hashil Seif Hashil (Copenhagen Denmark)

Advertisements

2 thoughts on “Waraka wa Hashil Seif kutoka Copenhagen: Tusisahau kuwa kama si Maalim Seif, Zanzibar isingefika ilipo leo

  1. Swadakta!kama kuna tatizo lolote lile linahusu chama ilikuwa lijadiliwe ndani ya chama alichokifanya Mh Hamad Rashid nikinyume na taratibu na mila zetu hapa zanzibar!pengine ingalikuwa vizuri zaidi kama alifuata taratibu za chama chake akaeleza alonayo akadai anachokiona amekikosa.Hivi sasa zanzibar iko katika wakati mgumu,hasasa na muhimu,bila ya mashirikiano na uwelewano,tujue hakika hatutafikia tunakotaka ambako ni muhimu zaidi kuliko maslahi ya binafsi.
    Mimi kwa upande wangu ambae sina chama chochote cha siasa nawaomba watu wa visiwa hivi, wawe macho ili wajuwe wakati huu na fursa hii inathamani kubwa juu ya maendeleo ya nchi yetu,ambayo katu hayatapatikana bila kufikia uhuru kamili.
    Mwisho nawambia raia wa zanzibar tushirkiane ili tuwe na nguvu,tusaidiane ili tuzidi kupendana.Huika uhuru wetu,huika uhuru wetu sisi tunakungojea!!

  2. hayo uliyoyanena ni sahihi, vyema viongozi wetu wafumbe macho na kumchomoa kidudu mtu, kwani maovu yake wanayajua au kwa kuwa wako kimya?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s